Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Nchi 17 zikiwemo Saudi Arabia, Qatar na Misri zimeitaka Hamas kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa unaolenga kufufua suluhu la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina.
Azimio la New York, lililotayarishwa na Ufaransa na Saudi Arabia, waliokuwa mwenyekiti wa mkutano huo, na kuidhinishwa na nchi nyingine 15 (ikiwa ni pamoja na Brazil, Canada, Uturuki, Jordan, Qatar, Misri na Uingereza), pamoja na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Nchi za Kiarabu, lilitoa wito wa kusitishwa kwa vita katika Ukanda wa Gaza ili kupata “suluhisho la haki, la amani na la kudumu la mzozo.”
Tamko hilo limethibitisha dhamira ya nchi hizo kuchukua hatua madhubuti, za muda na zisizoweza kutenguliwa katika utatuzi wa amani wa suala la Palestina na utekelezaji wa suluhisho la serikali mbili.
Katika muktadha huo, nchi hizo zimesisitiza kuwa, “utawala na udumishaji wa utulivu na usalama katika ardhi zote za Palestina ni lazima liwe jukumu la kipekee la Mamlaka ya Ndani ya Palestina, kwa uungaji mkono ufaao,” na kwamba “Israel lazima ijiondoe katika Ukanda wa Gaza… na Hamas inapaswa kukomesha udhibiti wake Gaza na kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.”
Wakati huo huo, nchi 17 zilitoa wito wa kupatikana kwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo katika Ukanda wa Gaza, ambao unatishiwa na njaa, na kukataa “matumizi ya njaa kama njia ya vita.”
Pia walionesha kuunga mkono “kutumwa kwa ujumbe wa kimataifa wa muda ili kuweka utulivu” huko Gaza.
Tetemeko la ardhi mashariki ya mbali ya Urusi lasababisha Tsunami Japan na Hawaii

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.8 katika kipimo cha Richter limekumba Rasi ya Kamchatka Mashariki ya Mbali ya Urusi siku ya Jumatano, na kuharibu majengo na kusababisha tsunami ya hadi mita 4 (futi 13).
Watu kadhaa wamejeruhiwa katika eneo hilo la Urusi, huku sehemu kubwa ya bahari ya mashariki mwa Japan – iliyoathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi na tsunami mnamo 2011 – ikiwaamuru wakaazi kuhama.
Wafanyikazi katika kiwanda cha nyuklia cha Fukushima – kilichoharibiwa na tsunami ya 2011 – wamehamishwa.
Nchini Marekani, maafisa wa Hawaii na California wametoa wito kwa umma kukaa mbali na fuo na maeneo ya chini.
Mataifa ya China, Ufilipino, Indonesia, New Zealand, Peru na Mexico zimetoa tahadhari za tsunami.
Kwengineko huduma za umeme zimesambaratika baada ya gridi ya umeme katika eneo la Sakhalin nchini Urus kuharibiwa na tetemeko a ardhi, shirika la habari la RIA linaripoti, likimnukuu gavana wa eneo hilo.
Eneo la Sakhalin limetangaza hali ya dharura katika visiwa vya Kuril kaskazini, huku video zikionyesha mawimbi ya tsunami yakiuvamia mji huo wa bandari
Mamlaka inasema watu wote katika eneo hilo wamehamishwa sehemu salama.
Zaidi ya watu 60,000 waliuawa Gaza kwa shambulio la Israel- Hamas

Zaidi ya watu 60,000 wameuawa kutokana na kampeni ya kijeshi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 2023, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema.
Ilisema Jumatatu idadi ya vifo ilifikia takribani 60,034, pamoja na watoto 18,592 na wanawake 9,782.
Takribani watu 112 waliuawa katika muda wa saa 24 kabla ya Jumanne asubuhi, na watu 22 waliuawa walipokuwa wakijaribu kupata msaada, wizara hiyo ilisema.
Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi ya usiku na asubuhi dhidi ya nyumba, vyanzo vya hospitali na mashuhuda waliiambia BBC.
Israel ilianza mashambulizi yake kujibu mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.
Uingereza kulitambua taifa la Palestina Israel isipotimiza masharti

Uingereza italitambua taifa la Palestina mwezi Septemba endapo Israel haitachukua “hatua madhubuti za kukomesha hali ya kutisha inayoshuhudiwa Gaza,” Waziri Mkuu Sir Keir Starmer amesema.
Starmer pia amesema Israel sharti ifikie matakwa mengine ikiwa ni pamoja na kukubali kusitishwa kwa mapigano, kujitolea kufikiwa kwa amani na utulivu wa muda mrefu ambayo inatoa suluhu ya mzozo wa nchi mbili, na kuruhusu Umoja wa Mataifa kurejelea upya usambazaji wa misaada, la sivyo Uingereza itachukua hatua dhidi yake kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Septemba.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema hatua hiyo “inatunza ugaidi wa kutisha wa Hamas”.
Serikali ya Uingereza iliwahi kusema kutambuliwa kwa Palestina kunapaswa kuzingatiwa wakati kunaweza kuwa na athari kubwa, kama sehemu ya mchakato wa amani.
Hata hivyo Wazi Mkuu huyo amekuwa akishinikizwa na wabunge ikiwa ni pamoja na wale kutoka kwa chama chake kuchukua hatua hiyo haraka iwezekanavyo.
Wiki iliyopita Ufaransa pia ilitangaza kulitambua rasmi taifa la Palestina mwezi Septemba – taifa la kwanza la G7 la nchi tajiri zaidi duniani kufanya hivyo.
Katika taarifa kwa waandishi wa habari baada ya kufanya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri, Sir Keir alisema anatangaza mpango huo kwa sababu ya “hali isiyovumilika” huko Gaza na wasiwasi kwamba “uwezekano wa kufikiwa kwa suluhisho la serikali mbili unapungua”.
Aliwaambia waandishi wa habari kwamba lengo la Uingereza la kuwa na “Israel salama na taifa huru la Palestina” linakabiliwa na “shinikizo kubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali”.
Starmer pia aliongeza kuwa “lengo kuu” lilikuwa kuboresha hali katika eneo la Gaza, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba misaada inawafikia raia wanaokabiliwa na hali ngumu.
Akielezea hatua ambazo Uingereza ilitaka serikali ya Israel kuchukua, Sir Keir pia alisema inapaswa kuweka wazi hakutakuwa na mpango wa kugawanywa kwa eneo la katika Ukingo wa Magharibi.
Serikali ya sasa ya Israel inapinga mpango wa kuelekea suluhu ya mataifa mawili na kuna uwezekano mkubwa isikubali masharti hayo.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.