Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wamezungumza kwa takriban saa moja katika chumba kilichojaa waandishi wa habari katika klabu ya gofu ya Trump ya Scotland huko Turnberry.
Wawili hao wamezungumzia masuala ikiwa ni pamoja na suala la Ukraine ambapo Trump ameweka makataa ya siku 10-12 kwa Urusi kufikia makubaliano ya Ukraine, hatua hiyo ikiwa imepunguza nusu ya makataa yake ya awali ya siku 50.
Trump alisema ikiwa Urusi haitafikia makubaliano kwa muda huo, anaweza kuweka vikwazo na ushuru wa ziada.
Waziri Mkuu Starmer na Trump pia wamekubaliana kwamba msaada unahitaji kuingia Gaza na wanahitaji kusitishwa kwa mapigano, huku Starmer akielezea picha za njaa kama hali “isiyovumilika”.
Trump alisema imekuwa “vigumu” kufikia makubaliano na Hamas, na ni vigumu pia kwa mateka kusalia utumwani.
Wakimbizi wa kambi ya Kakuma waandamana kupinga kupunguzwa kwa mgao wa chakula

Makabiliano yamezuka kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga kupunguzwa kwa mgao wa chakula cha msaada katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.
Jengo la shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limechomwa moto.
Inaripotiwa kuwa makabiliano hayo ya leo katika kambi ya wakimbizi yametokana na tangazo la Umoja wa Mataifa kuwa ni wakimbizi kadhaa tu watakaokuwa wakipokea misaada kufuatia kupunguzwa kwa bajeti ya WFP.
Mnamo mwezi Mei, WFP ilionya kuwa huenda ikalazimika kusitisha kwa kiasi kikubwa misaada kwa wakimbizi zaidi ya laki tatu wa kambi ya Kakuma baada ya ufadhili kupungua.
Mwezi uliopita, BBC ilitembelea kambi hiyo ambapo ilishuhudia maghala matupu na shehena ya mwisho ya chakula cha msaada ikitolewa.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limethibitisha kuwa moja ya maghala yake yamechomwa moto leo katika makazi ya Kalobeyei huko Kakuka lakini haijaeleza nani amehusika na mkasa huo, taarifa ikisema WFP inachunguza mazingira yaliyosababisha mkasa huo na kuwa inatathmini uharibifu na hasara iliyotokana na moto huo.
Serikali ya Marekani imekuwa ikitoa zaidi ya asilimia 70 ya fedha kwa ajili ya misaada inayotolewa Kakuma ikiwemo pesa taslimu zinazopewa wakimbizi kukimu mahitaji yao ya msingi lakini hatua ya serikali ya Rais Donald Trump ya kupunguza bajeti kwa miradi na misaada ya kigeni imeathiri pakubwa utoaji wa misaada katika kambi za waikimbizi.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani mwezi uliopita iliiambia BBC kuwa Marekani haiwezi kuulisha ulimwengu pekee yake na kuyataka mataifa mengine yaliyo na uwezo kuongeza mgao wao wa misaada ya kigeni.
Kambi ya Kakuma inawahifadhi wakimbizi kutoka takriban mataifa 23 ya Afrika na Mashariki ya Kati.
Mateka 35 wauawa nchini Nigeria kwa kushindwa kulipa fidia

Ripoti zinasema kuwa watu wenye silaha wamewaua watu wasiopungua 35 waliowateka nyara kutoka kijiji cha Banga katika jimbo la Zamfara kaskazini magharibi mwa Nigeria, baada ya familia za mateka hao kushindwa kutimiza mahitaji ya fidia.
Vyombo vya habari vya eneo hilo vimewanukuu wakazi wakisema kuwa wanamgambo hao wameteka watu 53 kutoka eneo hilo na kudai naira milioni moja (karibu dola 655) kwa kila mmoja. Waathiriwa walitekwa nyara zaidi ya miezi minne iliyopita.
Kulingana na ripoti, watu 18 walioweza kulipa fidia yao waliachiliwa. Watekwa waliobaki ambao hawangeweza kulipa fidia waliuawa.
Wale walioachiliwa waliwasili katika kijiji chao cha Banga katika eneo la Kaura-Namoda, na kuwajulisha familia za waliofiwa kwamba walilazimishwa kushuhudia mauaji ya mateka wengine, mmoja baada ya mwingine.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa baraza la serikali ya Kauran Namoda, Mannir Haidara Kaura, aliiambia BBC kwamba idadi ya watu waliotekwa nyara ni watu 56 na kwamba wanawake 18 waliachiliwa baadaye.
Hata hivyo, afisa wa serikali ya eneo hilo aliongeza jambo jingine – alisema kwamba familia za waathirika wote zililipa fidia iliyodaiwa, lakini watu hao wenye silaha, wanaojulikana katika eneo hilo kama majambazi, waliwaachilia huru watu 18 tu na “kuua” mateka waliobaki.
Aliongeza kuwa waathiriwa 18 waliotolewa wamepelekwa hospitalini kwa matibabu.
Utekaji nyara kwa fidia imekuwa jambo la kawaida nchini Nigeria na serikali inachukulia kitendo cha malipo kwa wateka nyara kuwa uhalifu.
Mmarekani aliyemuua mvulana wa kipalestina afariki gerezani

Mwenye nyumba huko Illinois aliyepatikana na hatia ya kumuua mpangaji wake Mpalestina mwenye asili ya Marekani amefariki akiwa kizuizini.
Joseph Czuba alihukumiwa kifungo cha miaka 53 jela mwezi Mei kwa mauaji ya Wadea al-Fayoume pamoja na kumjeruhi vibaya na kujaribu kumuua mamake Hanaan Shaheen mnamo 2023.
Polisi wanasema kuwa mwenye nyumba aliwalenga wawili hao kwa imani yao ya Kiislamu muda mfupi baada ya kuanza kwa vita vya Israel na Gaza.
Alikufa katika Kituo cha Marekebisho cha Illinois siku ya Alhamisi, kulingana na Ofisi ya Sheriff ya Will County.
Czuba alikuwa ametumikia chini ya miezi mitatu ya kifungo chake cha miongo kadhaa alipofariki kwa sababu ambayo bado haijajulikana akiwa na umri wa miaka 73.
Familia iliyoathirika ilikuwa inakodi vyumba takriban maili 40 (64km) kutoka Chicago, wakati shambulio hilo lilipotokea. Polisi wanasema Czuba alimdunga kisu al-Fayoume mara 26. Mwanamume huyo baadaye alikufa hospitalini.
Czuba alipatikana na hatia ya makosa mawili ya uhalifu wa chuki, kosa moja la mauaji ya daraja la kwanza, moja la kujaribu kuua na mawili ya unyanyasaji mbaya.
Mamake alitoa ushahidi mahakamani kwamba Czuba pia alimshambulia kwa kisu kabla ya kwenda kwa mwanawe, akimwambia “wewe, kama Muislamu, lazima ufe”, Reuters iliripoti.
Hakuhudhuria mazishi ya mwanawe kwani alikuwa akipokea matibabu hospitalini kutokana na majeraha aliyoyapata katika shambulio hilo.
Watu ‘wanakabiliwa na kifo’ wakitafuta msaada, Raia wa Gaza aiambia BBC

Waandishi wa kujitegemea wa BBC huko kaskazini mwa Gaza wamekutana na Wagaza baada ya kufanikiwa kupata mfuko wa unga kutoka kwa lori la misaada.
Salah Mkhesi alikuwa miongoni mwa waliojaribu kupata msaada siku ya Jumapili.
“Tuko hapa kupata msaada kwa ajili ya familia zetu. Watu wanakuja hapa wakikabiliwa na kifo,” alisema. “Watoto watalala bila kula au kunywa maji. Hali hii itaendelea hadi lini? Tutafutie suluhu.”
Misaada imekuwa ikiingia katika eneo hilo kupitia malori na pia inadondoshwa angani kutoka kwa ndege.
Alipoulizwa kuhusu misaada inayodondoshwa alisema “nimekataa” kabisa.
“Ninaikataa kwa sababu ni hatari. Inaua watu. Naikataa kabisa.”
Matukio ya machafuko mwishoni mwa juma wakati misaada ilipoingia Gaza
Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amezungumzia matatizo ya kupata msaada huko Gaza.
Picha kutoka eneo la Gaza mwishoni mwa juma zilionyesha matukio ya ghasia huku watu wakitembea kwenye hali ya joto wakiwa wamebeba misaada.
Alama ya kiganja yapatikana Misri baada ya miaka 4,000

Alama ya kiganja yenye umri wa miaka 4,000 imepatikana kwenye kaburi la kale la Misri lililotolewa na wasimamizi wanaojiandaa kwa maonyesho.
Ugunduzi huo ulifanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Cambridge kuhusu “nyumba ya roho”, aina ya mfano wa udongo katika umbo la jengo, ambalo hupatikana kwenye mazishi.
Mhifadhi Helen Strudwick alisema alama kamili ya mkono, ambayo ni ya 2055 hadi 1650BC, ilikuwa “ugunduzi wa nadra na wa kusisimua”.
Alama hiyo itaonyeshwa kama sehemu ya maonyesho ya Chuo Kikuu cha Made katika Misri ya Kale kwenye Jumba la Makumbusho la Fitzwilliam litakapofunguliwa rasmi tarehe 3 Oktoba.
Netanyahu: ‘Hakuna njaa huko Gaza’

Israel haifanyi kampeni ya njaa huko Gaza, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema, na kuyataja madai hayo kuwa “uongo wa wazi.”
“Hakuna sera ya njaa huko Gaza na hakuna njaa huko Gaza,” aliuambia mkutano wa Wakristo huko Jerusalem siku ya Jumapili.
Aliongeza kuwa Israel “imewezesha kiasi kinachohitajika na sheria ya kimataifa kuingia” na kusema Hamas “huiba msaada huu wa kibinadamu na kisha kuishutumu Israel kwa kutoitoa”.
Umoja wa Mataifa unasema Israel inafanya kuwa vigumu kupata msaada Gaza kwa sababu ya vikwazo vya ukiritimba na hatua za kijeshi.
Mashirika ya kimataifa, likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), yanasema kuna tatizo kubwa la uhaba wa chakula na utapiamlo katika Ukanda wa Gaza.
Hamas inakanusha kuwa imekuwa ikiiba misaada kutoka kwa vituo vya kukusanya.
Ripoti ya hivi majuzi ya ndani ya USAID ilisema hakuna ushahidi wa uporaji wa kimfumo wa Hamas wa vifaa vinavyofadhiliwa na Marekani.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.