Israel inapanga kuwapeleka Wagaza wote katika eneo moja la Rafah

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

f
Maelezo ya picha,Wagaza wengi wamehamishwa zaidi ya mara wakati wa vita

Waziri wa ulinzi wa Israel anasema amewaagiza wanajeshi wake kuandaa mpango wa kuwahamisha Wapalestina wote walioko Gaza na kuwapeleka katika kambi iliyoko kusini mwa eneo hilo, zinasema ripoti za vyombo vya habari vya Israel.

Israel Katz aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kuwa anataka kuanzisha “eneo la kibinadamu” kwenye magofu ya mji wa Rafah ili kuwahifadhi Wapalestina wapatao 600,000 – na kisha wakazi wote milioni 2.1.

Anasema lengo ni kuwaingiza watu katika mji huo baada ya kuwahakiki kwa usalama ili kuhakikisha wapiganaji wa Hamas hawaingii, na hawataruhusiwa kuondoka.

Ikiwa hali itaruhusu, aliongeza, ujenzi utaanza wakati wa usitishaji mapigano wa siku 60 ambao Israel na Hamas wanajaribu kujadiliana.

Mwanasheria mmoja wa haki za binadamu wa Israel alilaani na kusema ni “mpango wa uhalifu dhidi ya ubinadamu.”

“Uhamisho huu wa watu hadi kusini mwa Ukanda wa Gaza unahusu maandalizi ya kufuwakuzwa nje ya ukanda huo,” Michael Sfard aliliambia gazeti la Guardian la Uingereza.

Umoja wa Mataifa pia hapo awali umeonya kwamba uhamisho au uondoaji wa nguvu wa wakazi wa eneo ni kinyume cha sheria za kimataifa za kibinadamu na ni “sawa na kuifuta jamii hiyo.”

Bado hakuna kauli kutoka Mamlaka ya Palestina au Hamas.

Siku ya Jumatatu, wakati wa mkutano katika Ikulu ya White House, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alizungumza kuhusu pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba Marekani iichukue Gaza baada ya vita na kuwapa makazi ya kudumu wakazi wake mahali pengine.

“Tunafanya kazi na Marekani kutafuta nchi ambazo siku zote zinasema zinataka kuwapa Wapalestina maisha bora ya baadaye,” alisema Netanyahu.

Mwezi Machi, mataifa ya Kiarabu yaliunga mkono mpango wa dola bilioni 53 (£39bn) kutoka Misri kwenda kwa Trump wa ujenzi wa Gaza ambao ungewaruhusu Wapalestina wanaoishi kusalia katika eneo hilo.

Pia walisisitiza kwamba “wanakataa aina yoyote ya uhamishaji WaPalestina”, wakielezea ni “ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu na kuwafuta Wapalestina.”

Mamlaka ya Palestina na Hamas pia ziliunga mkono mpango huo wa Misri, lakini Marekani na Israel zilisema umeshindwa kushughulikia hali halisi ya Gaza.

Wapalestina wanaogopa kutokea tena Nakba – neno la Kiarabu lenye maana ya “janga” – pale maelfu walipokimbia au kufukuzwa katika nyumba zao kabla na wakati wa vita vya kuundwa kwa Taifa la Israel mwaka 1948.

Wengi wa wakimbizi hao waliishia Gaza, ambapo wao na vizazi vyao ni robo tatu ya wakazi. Wakimbizi wengine 900,000 waliosajiliwa wanaishi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, wengine milioni 3.4 wanaishi Jordan, Syria na Lebanon, kulingana na UN.

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na 251 walichukuliwa mateka.

Zaidi ya watu 57,500 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Idadi kubwa ya wakazi wa Gaza pia wamehamishwa mara kadhaa. Zaidi ya 90% ya nyumba zimeharibiwa. Mifumo ya afya, maji, usafi wa mazingira vimeharibiwa na kuna uhaba wa chakula, mafuta, dawa na malazi.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment