Ni ‘Siku ngumu kwetu’ – Ureno yamuomboleza Jota katika Euro 2025

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Maelezo ya picha,Mashabiki walishika mabango uwanjani kumuenzi Jota

“Bila shaka, kama tungekuwa na uwezekano wa kubadilisha kilichotokea, tungebadilisha kila kitu kwa uhakika. Lakini hii ni siku ngumu kwetu.”

Kocha wa Ureno Francisco Neto alijiunga na kumuenzi Diogo Jota huku maelfu ya mashabiki pia wakitoa heshima zao wakati wa mechi ya ufunguzi ya Euro 2025 dhidi ya Uhispania.

Mshambulizi wa Liverpool Jota na kaka yake, Andre Silva, wote walifariki mapema Alhamisi asubuhi wakati gari la Lamborghini walimokuwa wakisafiria lilipopata ajali katika jimbo la Zamora nchini Uhispania.

Mashabiki waliimba kwa hisia wimbo wa taifa wa Ureno kutoka moyoni na kisha kusalia kimya kwa dakika moja kabla ya kuanza kwa mchezo huo, ambapo picha ya Jota yenye rangi nyeusi na nyeupe ilionyeshwa kwenye skrini kubwa za uwanja huko Bern.

“Ilikuwa siku ngumu sana kucheza soka, kwa sababu maisha haya ni zaidi ya mchezo, zaidi ya soka,” alisema mshambuliaji wa Ureno Jessica Silva.

“Bila shaka kila mtu ana huzuni. Hili ni jambo zito, moyo wangu ni mzito – mambo muhimu zaidi kuliko kucheza mchezo.”

Mashabiki wa Ureno walishikilia mabango yenye ujumbe wa kumuenzi mchezaji huyo ambaye pia anaombolezwa huko Liverpool, huku wachezaji wote wakiwa wamevalia vitambaa vyeusi mkononi.

Licha ya kuwa na uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki wao katika muda wote wa dakika 90, Ureno iliangukia kwenye kichapo cha 5-0 mjini Bern huku mabingwa wa dunia na washindi wa michuano hiyo Uhispania wakianza harakati zao za kuwania taji la kwanza la Uropa.

Akizungumza katika mkutano wake na wanahabari baada ya mechi, kocha Neto, ambaye alionekana kuzuia machozi wakati wa kimya cha dakika moja, alimuelezea Jota kama mfuasi aliyejitolea wa timu ya taifa ya wanawake.

“Diogo aliifuatilia timu yetu kwasababu aliipenda nchi,” alisema Neto, ambaye alieleza kuwa alikutana na Jota mara ya kwanza alipokuwa mkufunzi katika kiwango cha wachezaji walio chini ya miaka 19.

“Diogo siku zote nilipozungumza naye alijua matokeo, alifuata timu, baadhi ya wachezaji na huu ndio utamaduni tulionao Ureno.

“Leo ni siku ya huzuni sana kwasababu wawili kati yetu wamepoteza maisha. Ni vijana sana. Sio siku nzuri.”

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment