Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Takriban Wapalestina 18 wameuawa baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel kulenga kitengo cha polisi cha Hamas kilichojaribu kudhibiti soko katika mji wa Deir al-Balah katikati mwa Gaza, madaktari wameiambia BBC.
Walioshuhudia tukio hilo walisema ndege zisizo na rubani za Israel ziliwafyatulia risasi vikosi vya Hamas, waliokuwa wamevalia kiraia na kuvaa barakoa, ambao walikuwa wakikabiliana na wachuuzi wanaowatuhumu kwa upandishaji wa bei na kuuza bidhaa zilizoporwa kutoka kwa malori ya misaada.
Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Hamas ililaani shambulizi hilo, ikiishutumu Israel kwa kufanya “uhalifu mwingine dhidi ya kitengo cha polisi kilichopewa jukumu la kudumisha utulivu wa umma”.
Iran yawakamata na kuwanyongwa washukiwa kufuatia mzozo wa Israel

Mamlaka ya Iran imewakamata na kuwanyonga watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na mashirika ya kijasusi ya Israel, kutokana na vita vya hivi majuzi kati ya nchi hizo mbili.
Hatua hiyo inawadia baada ya kile maafisa wanaelezea kama kuingiliwa kwa huduma za usalama wa Iran na maajenti wa Israel.
Mamlaka zinashuku habari zilizotolewa kwa Israel zilihusika katika msururu wa mauaji ya hali ya juu wakati wa mzozo huo.
Haya yalijumuisha mauaji yaliyolengwa ya makamanda wakuu kutoka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na wanasayansi wa nyuklia, ambayo Iran inayataja kuwa yanahusishwa na watendaji wa shirika la kijasusi la Israel la Mossad wanaofanya kazi ndani ya nchi.
Wakitikiswa na ukubwa na usahihi wa mauaji haya, mamlaka zimekuwa zikimlenga mtu yeyote anayeshukiwa kufanya kazi na ujasusi wa kigeni, ikisema ni kwa ajili ya usalama wa taifa.
Wakati wa mzozo huo wa siku 12, viongozi wa Iran waliwanyonga watu watatu waliotuhumiwa kuifanyia Israel ujasusi.
Siku ya Jumatano – siku moja tu baada ya kusitishwa kwa mapigano – watu watatu zaidi walinyongwa kwa mashtaka sawa.
Maafisa wametangaza kukamatwa kwa mamia ya washukiwa kote nchini kwa tuhuma za ujasusi.
Televisheni ya taifa imerusha hewani madai ya kukiri makosa kwa wafungwa kadhaa, wakikubali kushirikiana na ujasusi wa Israel.
Mashirika ya haki za binadamu na wanaharakati wameelezea hofu yao juu ya matukio ya hivi punde, wakitaja mazoea ya muda mrefu ya Iran ya kulazimisha na kuendesha kesi zisizo za haki.
Kuna wasiwasi kwamba unyongaji zaidi unaweza kufuata. Wizara ya Ujasusi ya Iran inadai kuwa iko katika “vita visivyoisha” dhidi ya kile inachokiita mitandao ya kijasusi ya Magharibi na Israel – ikiwa ni pamoja na CIA, Mossad, na MI6.
‘Iran itajibu mapigo tena ikishambuliwa’- Ayatollah

Iran itajibu mashambulizi yoyote ya siku za usoni ya Marekani kwa kushambulia kambi za kijeshi za nchi hiyo Mashariki ya Kati, Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei alisema Alhamisi, katika hotuba yake ya kwanza kwenye televisheni tangu kufikiwa kwa usitishaji vita kati ya Iran na Israel.
“Jamhuri ya Kiislamu iliishangaza Marekani peupe. Ilishambulia moja ya kambi muhimu za Marekani katika kanda,” Khamenei alisema.
Khamenei alisisitiza kuwa Marekani “haijapata mafanikio yoyote” kutokana na mashambulizi yake dhidi ya vituo vya Iran vya nyuklia.
Ayatollah Ali Khamenei alisema mashambulizi hayo “hayakufanikisha lolote la maana” kutatiza mpango wa nyuklia wa Iran, na alielezea kulipiza kisasi dhidi ya kituo cha anga cha Marekani huko Qatar kama “pigo kubwa”.
Iran haitajisalimisha
Katika hotuba zake zilizorekodiwa awali, zilizosambazwa kwenye televisheni ya serikali, Khamenei aliahidi kwamba Iran haitajisalimisha licha ya wito wa Marekani.
“Rais wa Marekani Donald Trump aliweka wazi kuwa Wamarekani hawatataka kingine chochote zaidi ya kujisalimisha… tukio kama hilo halitatokea kamwe, “Khamenei alisema.
Alipoulizwa ikiwa Marekani itashambulia tena Iran ikiendeleza mpango wake wa kurutubisha nyuklia, Trump alijibu “ndio”.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema taarifa za kijasusi zilizokusanywa na Marekani na Israel zilionyesha kuwa operesheni hiyo “iliharibu mpango wa nyuklia kwa kiasi kikubwa, na kuurudisha nyuma kwa miaka”.
Tehran kwa miongo kadhaa imekuwa ikikanusha shutuma za viongozi wa Magharibi kwamba inatafuta silaha za nyuklia.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.