BBC iligundua nini kuhusu maandamano ya mwaka jana?

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Maandamano ya leo lengo lake ni kuwakumbuka waliouawa tarehe 25 Juni 2024, wakati waandamanaji walipovamia bunge kutaka kusitishwa kwa nyongeza ya kodi.

Mwezi Aprili, filamu ya BBC Africa Eye’s Blood Parliament, ilifichua jinsi vikosi vya usalama vilivyokabiliana kikatili maandamano hayo.

Kwa kutumia data huria na maudhui, uchambuzi wa BBC wa zaidi ya picha 5,000 uliwatambua maafisa wa usalama waliovalia sare – polisi na askari – ambao walifyatua risasi na kuua waandamanaji watatu wasiokuwa na silaha bungeni.

Amnesty International na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) zilisema maafisa waliotambuliwa katika filamu hiyo wanapaswa “kukabiliwa na sheria”.

Wakenya walielezea hasira zao mtandaoni, wakiishinikiza serikali kuwawajibisha maafisa wa usalama .

Rais Ruto amewahi kuwatetea polisi dhidi ya shutuma za ukatili.

Polisi pia wamekanusha mara kwa mara kuhusika na mauaji hayo.

Maandamano Kenya: Watu kadhaa wameripotiwa kupigwa risasi

g
Maelezo ya picha,Watu kadhaa wanasemekana kukimbizwa hospitalini

Tumepokea ripoti za watu kupigwa risasi, ikiwa ni pamoja na mmoja aliyeripotiwa kuuawa huko Machakos, mji ulio umbali wa kilomita 60 kutoka mji mkuu.

Watu kadhaa pia wanasemekana kukimbizwa katika hospitali kuu katika mji mkuu wakiwa na majeraha ya risasi baada ya kudaiwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano yanayoendelea, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.

Citizen TV, ambayo inaripoti kuwa takriban watu 10 walikuwa wamepigwa risasi, imechapisha video, ikionyesha wagonjwa wakiingizwa kwenye Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, jijini Nairobi.

Katika klipu hiyo, mwanamume mmoja anamwambia mtangazaji kwamba polisi wameanza kuwafyatulia risasi, na kwamba mmoja wa wafanyakazi wenzake alikuwa amepigwa risasi.

Maandamano Kenya: Rais Ruto yuko wapi?

g

Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa Rais William Ruto yuko katika Kaunti ya Kilifi pwani ya Kenya ambako anahudhuria mazishi ya baba wa Gavana wa Kilifi Gideon Mungaro.

Ziara ya Ruto inajiri katika siku ambayo maandamano ya vijana wanaofahamika kama Gen Z yamezuka katika maeneo kadhaa ya nchi, ukiwemo mji mkuu, Nairobi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga pia ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliohudhuria mazishi hayo mnamo yanayofanyika leo Jumatano.

Raila amekuwa Pwani kwa siku mbili zilizopita, akihudhuria hafla tofauti, zikiwemo hafla za kaunti, ambapo Jumanne aliwaonya waandamanaji wa Gen Z dhidi ya kuzua vurugu.

Mapema Jumatano asubuhi, Rais Ruto alisafiri kwa ndege hadi Kilifi baada ya kumkaribisha mjumbe maalum wa Mtukufu Mwanamfalme Rahim Al Hussaini Aga Khan, Sultan Ali Allana, katika Ikulu ya Nairobi.

Polisi wameonekana kushika doria na kupambana na waandamanaji katika mji mkuu Nairobi na miji mingine mikuu huku Wakenya wakiingia barabarani kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2024 ambayo yalisababisha vifo vya watu kadhaa na kuzua ghadhabu kote nchini kutokana na ukatili wa polisi.

Kenya yaamuru vyombo vya habari kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano -ripoti

Citizen TV/YouTube

Serikali ya Kenya imeamuru vituo vyote vya televisheni na redio kusitisha mara moja matangazo ya moja kwa moja ya maandamano hayo, ripoti zinasema.

“Atakayekiuka agizo hili atachukuliwa hatua za kisheria,” Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imesema katika taarifa iliyonukuliwa na runinga ya Citizen.

Baadhi ya vituo vya televisheni sasa vimeacha kuripoti moja kwa moja na badala yake kufanya mahojiano na wachambuzi.

Maandamano hayo yameenea kote nchini huku polisi zaidi wakitumwa kuyadhibiti.

Katika taarifa iliyotumwa kwa “Vituo vyote vya Televisheni na Redio,” Mamlaka ilisema kuwa kutangaza maandamano hayo moja kwa moja kunakiuka kanuni za Katiba ya Kenya, haswa Vifungu 33(2) na 34(1), pamoja na Kifungu cha 46I cha Sheria ya Habari na Mawasiliano ya Kenya ya 1998.

“Matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya Juni 25, 2025 ni kinyume na Ibara ya 33(2) na 34(1) ya Katiba ya Kenya,” inasomeka agizo hilo lililotiwa saini na David Mugonyi, EBS, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo ya mawasiliano.

Mamlaka haikuelezea adhabu zinazoweza kutolewa kwa watakaokiuka agizo hilo, lakini ilisisitiza kuwa amri hiyo izingatiwe kikamilifu.

Mara ya kwanza ambapo serikali ya Kenya ilikatiza vyombo vya Habari kupeperusha matangazo mubashara ilikuwa Januari 30 2018, alipokuwa akijiapisha Raila Odinga kama ‘Rais wa watu’ .

Kabla ya Mamlaka ya mawasiliano CA kuzima matangazo , barua ilikuwa imetumwa kwa wamiliki wa vituo hivyo vya Habari nchini Kenya kuhusiana na kile kilitajwa kama taarifa za kuzua taharuki ndani na nje ya nchi.

Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani wakati huo Fred Matiangi alitoa onyo kali akivitaka vyombo hivyo kudumisha uzalendo wa kitaifa na kuacha kuzua utata.

Mwaka 2024, serikali tena ilitishia kuzima matangazo ya moja kwa moja wakisema kwamba habari hizo za moja kwa moja zinaweka wasiwasi kwa sio tu raia nchini bali pia kimataifa.

Maandamano ya 2024 yalitangazwa moja kwa moja kwenye vyombo vyote vya habari nchini hadi pale polisi walipoanza kuwafyatulia risasi waandamanaji waliovunja ua wa bungee.

Na tena leo, serikali imeziandikia vyombo vya habari kuzima matangazo mubashara kw akuwa hali ilikuwa inaanza kuwa ngumu mjnini.

Katika miaka ya awali serikali mbali mbali pia zilipiga marufuku matangazo ya aina hiyo hasaa mnamo 2008 wakati wa vita vya baada ya uchaguzi ambapo watu zaidi ya elfu moja walipoteza maisha yao.

Maandamano Kenya: Polisi wakabiliana na waandamanaji katika barabara kuu ya Thika Road jijini Nairobi

Polisi wanakabiliana na makundi ya vijana waandamanaji katika barabara kuu ya Thika Road jijini Nairobi.

Vijana hao wanaotembea kwa kwa miguu kuelekea katikati mwa jiji la Nairobi huku baadhi yao wakiwa wameshika bendera, wamezuiawa kusonga mbele baada ya polisi kuwatupia mabomu ya kutoa machozi, huku moshi mkubwa ukionekana kufuka juu kwenye sehemu mbali mbali za barabara hiyo.

Pia wamelazimika kupiga risasi hewani kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakiwatupia mawe.

Magari ya polisi yamewekwa kwenye maeneo mbali mbali ya barabara hiyo kuwazuia watu kuingia katikati ya mji.

Helikopta za polisi pia zinashuhudiwa kufanya doria juu ya maeneo yenye makundi ya waandamanaji, kwa kile kinachoonekena kuwa zinatumika kubaini maeneo yenye makundi ya waandamanaji.

Maandamano Kenya: Wakaazi wa Kisii, Nyeri, Githurai wajiunga na maandamano

Wakaazi wa kaunti ya Kisii nao pia wamefurika barabarani kuungana na wenzao walioko maeneo mengine nchini katika maandamano ya kudai haki kwa wale waliopoteza maisha katika maandamano ya Juni 25 mwaka jana.

Vijana hao wamechoma magurudumu na kufunga barabara ya mji huo.

Mwito wao ni ule ule tu kuwa hawana imani na uongozi wa serikali ya rais William Ruto.

Makabiliano makali yashuhudiwa Githurai

Mapambanao makali yanaendelea baina ya polisi na waandamanaji katika eneo la Githurai.

Waandamanaji wamefunga barabara ya kuelekea mjini baada ya kuweka mawe huku polisi wakijaribu kuwadhibiti wasivuke kuingia kati kati ya mji.

Waandamamanji hao wanapambana na polisi kwa kuwarushia mawe nao polisi wakijibu kwa kutumia vitoa machozi.

Maandamano Kenya: Hali ilivyo jijini Nairobi kupitia picha

.

Maandamano Kenya: Polisi wakabiliana na waandamanaji

.

Polisi nchini Kenya wanakabiliana na waandamanaji katika maeneo kadhaa ya Jiji Kuu la Nairobi.

Katika eneo la Katikati mwa mji, waandamanaji wanaonekana wakicheza mpira huku wengine wakirusha mawe barabarani, nao polisi wakirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya.

Idadi ya polisi wanaokabiiana na vijana imeongezeka katika barabara ya Moi, ambapo wanarusha mabomu ya kutoa machozi huku wakilazimika pia kuwamwagia maji ya rangi nyekundu inayowasha mwili.

Vijana wamewasha moto katikati ya barabara huku wakijaza mawe barabarani na matairi ya gari pia yamewashwa moto.

Hali kwa sasa ni ya mguu niponye huku eneo zima likijaa moshi.

Katika upande wa pili wa mjii polisi wanaonekana wakiwatuliza vijana ambao wamekusanyika mjini, baadhi wakiwa wamevalia bendera ya kenya mwilini .

Katika mtaa wa Kitengele uliopo viungani mwa mji wa Nairobi, polisi wamewarushia baadhi ya waandamanaji mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya.

Viongozi wa Upinzani Kenya waweka maua bungeni kuwakumbuka vijana wa Gen Z waliouawa

Kiongozi wa chama cha Wiper nchini Kenya Kalonzo Musyoka amewaongoza viongozi wa upinzani jijini Nairobi kuwakumbuka vijana wa Gen Z waliofariki Juni 25, kabla ya hafla iliyopangwa ya kuweka shada la maua.

Viongozi hao wa upinzani walitembea hadi Barabara ya Bunge kuweka shada la maua na kuwasha mishumaa kwa heshima ya waandamanaji wa Gen Z waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya 2024.

Akihutubia wanahabari, Kalonzo amesema hatua hiyo ni kutoa heshima kwa vijana waliouawa.

“Leo, tunataka tu kuwakumbuka vijana hawa. Tunanuia kuwawekea mashada ya maua,” Kalonzo alisema.

“Hata kama tutanyimwa kuingia Bungeni leo, siku hii lazima iadhimishwe ipasavyo kama sikukuu ya kitaifa katika siku zijazo.”

Viongozi hao walifanikiwa kuweka mashada ya maua kwenye uzio wa waya za seng’enge kwa vile polisi walikuwa wamezingira Bunge.

Maandamano Kenya: Jaji Mkuu mstaafu Kenya aandamana

.

Aliyekuwa Jaji Mkuu nchini Kenya David Maraga amejiunga na maandamanao ya Gen z jijini Nairobi hii leo akilaani ukatili wa maafisa wa polisi dhidi ya vijana.

“Vijana hawa wana amani na tutashirikiana nao kufanya maandamano ya amani. Tunataka katiba iheshimiwe, tunataka maisha ya binadamu kuheshimiwa, inasikitisha kuona vijana wamezuiwa kufanya maandamano kuelekea bungeni ,mbali na mihemko tunayoina hapa leo,hakuna ghasia za aina yoyote,” alisema Maraga akiwa katika maandamano katikati ya jiji la Nairobi.

Maraga alihudumu kama Jaji Mkuu kutoka Oktoba 2016 mpaka alipostaafu Januari 2021. Toka alipotoka madarakani Maraga amekuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu ni kisiasa, na hata mwezi uliopita alihudhuria kesi ya Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema, Tundu Lissu jijini Dar Es Salaam.

Mwezi Aprili mwaka huu, Maraga alitangaza rasmi nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027 nchini Kenya.

Maandamano Kenya: Inspekta jenerali wa polisi Douglas Kanja atoa onyo

.
Maelezo ya picha,Inspekta jenerali wa Polisi Kenya Douglas Kanja

Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya Douglas Kanja amewaonya waandamanaji kuepuka maeneo yaliyohifadhiwa wakati wa maandamano ya jumatano ambayo yanawaheshimu waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha mwaka jana.

Katika kikao na wanahabari kilichodumu kwa chini ya dakika kumi, IG Kanja alibainisha kuwa maafisa wa polisi watachukua hatua kwa mujibu wa sheria kulinda maisha na mali.

Aliwataka waandamanaji kuandamana kwa mujibu wa sheria huku akiongezea kwamba maafisa wake watakuwa tayari kwa lolote lile.

Haya yanajiri huku mkuu wa polisi wa Nairobi George Seda akiwa amewahakikishia wananchi kwamba vyombo vya usalama viko tayari kuimarisha usalama wakati wa maandamano ya Jumatano.

Maandamano Kenya: Vijana wajitokeza barabarani katika maeneo mbalimbali

.

Vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya wamejitokeza katika kumbukumbu ya waliofariki mwaka jana kwenye maandamano yaliyotikisa Kenya.

Mjini Nairobi, vijana wamejitokeza katika barabara ya Moi Avenue wakiwa wamebeba bendera za taifa.

.

Mjini Mombasa, hali kama hiyo imeshuhudiwa, vijana wanaonekana wamebeba bendera za taifa la Kenya, firimbi, makaratasi na mabango yenye picha za waliofariki.

Pia kuna walioonekana katika barabara ya Moi Avenue Mombasa wakiwa wamebeba mishumaa iliyowashwa na kufanya maombi.

Katika maeneo ya Makueni, moto umewashwa barabarani huku polisi wakionekana kutuliza hali.

.

Katika barabara ya Muindi Mbingu mjini Nairobi, vijana wamejitokeza katika maandamano hayo huku wakiwa wanaimba nyimbo.

.

Polisi watawanya waandamanaji katika barabara ya Kenyatta jijini Nairobi.

Maeneo ya Kitengela mjini Nairobi, Kisii, Nakuru na Mombasa maandamano yanaendelea.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment