Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Boniface Kariuki, mchuuzi aliyekuwa anauza barakoa aliyepigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya jana Jumanne, 17/06/2025 katikati mwa jiji la Nairobi, yuko katika hali mahututi, hospitali ya taifa ya Kenyatta (KNH) imethibitisha.
Afisa Mtendaji Mkuu wa KNH William Sigilai ametoa taarifa na kusema, Kariuki alipelekwa hospitali ya kitaifa kutokana na aagizo la hospitali aliyokuwa amepelekwa awali, baada ya kupata jeraha kichwani kutokana na risasi aliyopigwa.
“Wakati anawasili katika kituo cha ajali na dharura, alionekana kuwa katika hali mbaya akiwa na jeraha upande wa kushoto wa kichwa chake, na kusababisha kutokwa na damu nyingi ushahidi kwamba alikuwa na jeraha baya,” alisema Sigilai.
Aliongeza kuwa uchunguzi wa CT scan kwenye ubongo ulithibitisha kuwa risasi ilikuwa ndani ya kichwa chake upande wa kushoto.
“Mgonjwa alitayarishwa kwa ajili ya upasuaji wa dharura. Karibu saa mbili na dakika hamsini usiku, timu ya wataalamu mbalimbali iliyoongozwa na daktari wa upasuaji wa ubongo Dkt. Sam Njiru ilimfanyia upasuaji iliodumu takriban saa mbili, Sigilai alisema.
KNH imethibitisha kuwa kitu kinachoaminika kuwa risasi kilitolewa na mwanamume huyo akapelekwa kwenye chumba cha wangonjwa mahuti kwa uangalizi zaidi.
Taarifa kuwa Kariuki yuko hai katika hali mahututi pia imethibitishwa na familia yake. Baba yake Jonah Kariuki Nyambura pia amezungumza na vyombo vya habari na kusema kuwa risasi hiyo ilikuwa ndani ya kichwa juu kidogo ya sikio.
Video inayoonyesha jinsi Boniface Kariuki alivyopigwa risasi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha ghadhabu miongoni mwa waandamanaji.
Ubalozi wa Uingereza Kenya washutumu Polisi kwa kuwashambulia waandamanaji

Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya, umesema umeghadhabishwa na matukio ya polisi kuwapiga risasi raia waliokuwa wameandamana.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Uingereza imesema maafisa wa polisi wanapaswa kuwapa raia imani, kuwa waaminifu na kuwalinda.
Uingereza ilionyesha kukasirishwa na utumiaji wa nguvu kupita kiasi katika maandamano.
“Tumefadhaishwa sana na vurugu dhidi ya raia wasio na silaha na waandamanaji hapo jana,” ujumbe huo ulisema.
“Tunaomba uchunguzi wa haraka, huru na wa uwazi kuhusu vitendo vya polisi,” Uingereza imesema.

Pia imewatakia afueni ya haraka wale waliojeruhiwa kwenye maandamano hayo.
Maafisa wawili waliompiga na mmoja wao kumfyatulia risasi mchuuzi aliyekuwa akiuza barakoa, walikamatwa hapo jana na wanazuiliwa katika kituo cha Capital Hill.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za kuwajibishwa, akidai kwamba wale waliowafyatulia risasi waandamanaji katika maandamano ya 17/06/2025 wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Mbunge huyo alilaani kile alichokiita “mauaji” baada ya kuwatembelea waathirika wa maandamano hayo walioazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).
Hii si Kenya tunayotaka. Hakuna Mkenya anayepaswa kuteswa kwa kueleza maoni yake au kwa kusimama kidete kwa ajili ya mustakabali wake wa baadaye”, Babu Owino alisema.
“Hatutashindwa. Hatutaacha kudai haki. Na hatutaacha kusimama na watu wa Kenya mpaka wale waliowajibika watakapochukuliwa hatua”, Owino alinukuliwa na Gazeti la The Star.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.