Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, ameeleza kwa masikitiko makubwa kuwa licha ya kutohukumiwa kosa lolote hadi sasa, amekuwa akiwekwa katika mazingira kama ya wafungwa wa kifo gerezani, jambo analoliona kuwa ni ukiukwaji wa haki zake za msingi.
Akizungumza leo Jumatatu, Juni 16, 2025, mbele ya Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu alifichua kuwa tangu Ijumaa Kuu, amekuwa akishikiliwa katika “special room” (chumba maalumu) ndani ya Gereza la Ukonga, sehemu maalum inayohifadhi wafungwa waliokwishahukumiwa kunyongwa.
“Gerezani, gereza la Ukonga kuna sehemu moja inaitwa special room (chumba maalumu), eneo maalum ambalo wanakaa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa, mimi ninakaa hiyo sehemu wanayokaa wanaosubiri kunyongwa (death row).
Sasa Mheshimiwa ukiwa death row maana yake ni nini?” alihoji Lissu mbele ya Mahakama. Akiendelea kueleza, Lissu alisema kuwa anafuatwa na kuongozwa na askari wawili kila anapotoka kuonana na mawakili au ndugu zake, hali sawa na ile ya wafungwa waliokwishahukumiwa kunyongwa, licha ya yeye bado kuwa mshitakiwa asiyehukumiwa.
“Ninalindwa muda wote, usiku na mchana, mimi sijahukumiwa kifo lakini ninakaa death row. Pamoja na kuwa death row, bado una haki kwa mfano, haki ya kuabudu”…alilalamika Lissu kuwa hapewi haki hiyo ya kuabudu.
Katika hatua nyingine ya kushtua, Lissu aliieleza Mahakama kuwa ameomba rasmi kuwaondoa mawakili wake na kuamua kujitetea mwenyewe katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Alisema sababu kuu ya uamuzi huo ni kutoruhusiwa kuzungumza na mawakili wake kwa faragha kwa zaidi ya siku 68 akiwa mahabusu. “Mawakili wangu walifanya kazi yao kwa ustadi na kwa moyo. Lakini kutokana na mazingira haya ya kutopewa nafasi ya faragha kuwasiliana nao, ninaichukua hii kesi mikononi mwangu. Kuanzia sasa mimi mwenyewe nitakabiliana na mawakili wa serikali,” alisema.
Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga alikubali ombi hilo, akisema Mahakama itamruhusu Lissu kujitetea mwenyewe hadi pale atakapowasilisha maombi ya kuwarejesha mawakili wake.
Kesi hiyo ya uhaini imeahirishwa hadi Julai 1, 2025, ambapo Lissu anatarajiwa kuendelea na utetezi wake binafsi dhidi ya mashtaka yanayomkabili, ikiwemo pia kesi nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.