UNFPA: Wengi wanasita kupata watoto kisa ukosefu wa fedha

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA ameonya kuhusu kushuka kwa viwango vya watoto wanaozaliwa duniani akisema ulimwengu unashuhudia kuporomoka kwa idadi ya watu.

Ripoti mpya ya UNFPA inasema watu wengi wanataka watoto wawili na zaidi lakini mamilioni ya watu duniani hawawezi kufikia matamanio yao ya kufanya hivyo.

Uchunguzi uliohusisha watu elfu kumi na nne kutoka mataifa kumi na nne ulionesha kuwa matatizo ya kifedha na kukosa mwenza anayefaa kuwa sababu kuu za watu kusita kupata watoto.

Mtu mmoja kati ya watano waliohojiwa wamesema bado hawajapata au hawatarajii kupata idadi ya watoto wanaotaka.

Nchi zilizohusishwa katika utafiti huo ni Korea Kusini, Thailand, Italy, Hungary, Ujerumani, Sweden, Brazil, Mexico, Marekani, India, Indonesia, Morocco, Afrika Kusini na Nigeria ambazo zote kwa jumla zina theluthi moja ya idadi ya watu duniani.

Waliohojiwa ni kutoka matabaka mbali mbali, wakiwemo vijana walio katika umri wa kuweza kuzaa au kuzalisha na waliopita umri wa kufanya hivyo.

Mkuu wa UNFPA Dr Natalia Kanem amesema ulimwengu hivi sasa unashuhudia kushuka kwa kiwango cha kuzaliana kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa kutokana na watu wengi kuhisi hawana uwezo wa kuanzisha familia wanazozitaka na kulitaja hilo kuwa tatizo linalotoa picha halisi ya mfumo wa familia duniani.

Dr Kanem anaongeza kusema alishangazwa na idadi ya waliohojiwa ambao walisema wana watoto wachache kinyume na mapenzi yao.

Katika mataifa yote 14 ambapo utafiti huu ulifanywa, asilimia 39 ya watu walisema ukosefu wa fedha au kuwa na uwezo mdogo kifedha ndiko kunawazuia wao kupata watoto.

Korea Kusini ikiandikisha idadi kubwa zaidi ya wanaosita kupata watoto kwa asilimia 58 na Sweden ikiwa na kiwango kidogo cha wanaohisi fedha ni tatizo ikiwa ni asilimia 19 tu ya wanaohisi hivyo.

Profesa Gietel Basten wa chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Hong Kong anasema kwa muda mrefu, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA, liliangazia pakubwa kuhusu wanawake walio na watoto wengi kuliko wanavyohitaji na mzigo mkubwa wa kuwashughulikia watoto wengi waliozaliwa bila ya kuwepo njia za mpango wa uzazi.

Licha ya hayo, UNFPA inatahadharisha kuhusu namna ya kushughulikia uchunguzi huu wa hivi punde wa watu kuzaa watoto wachache au kutotaka watoto kabisa.

Dr Kanem wa UNFPA anasema miaka arobaini iliyopita, China, Korea, Japan, Thailand na Uturuki zilikuwa na wasiwasi kuwa idadi ya watu wake iko juu mno lakini kuanzia mwaka 2015, mataifa hayo yameelekeza juhudi kutaka kuongeza idadi ya watu wake kwa kuhimiza watu kuzaa.

Mbali na gharama ya kulea na kutunza watoto, kutopata mwenza anayestahili kuzaa naye, UNFPA pia imegundua kuwa kikwazo kingine cha kutokuwa na muda wa kuzaa na kulea.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment