Daktari ambaye watoto wake tisa waliuawa katika shambulizi la Israel huko Gaza afariki dunia

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Daktari wa Kipalestina ambaye watoto wake waliuawa katika shambulizi la anga la Israel huko Gaza tarehe 23 Mei amefariki kutokana na majeraha aliyoyapata katika shambulio hilo hilo, maafisa wa afya wanasema.

Dk Hamdi al-Najjar alikuwa tu ameingia baada ya kumpeleka mkewe, Dk Alaa al-Najjar, katika Hospitali ya Nasser, ambapo wanandoa hao walifanya kazi, wakati nyumba yao huko Khan Younis iliposhambuliwa. Watoto wao tisa waliuawa, huku wa 10 akijeruhiwa vibaya.

Hamdi alitibiwa hospitalini kutokana na majeraha ya ubongo na ya ndani lakini alifariki Jumamosi. Alaa na mtoto wao Adam mwenye umri wa miaka 11, ambaye amesalia hospitalini, ndio manusura pekee wa familia hiyo.

Katika taarifa, Israel ilisema “ndege ilishambulia washukiwa kadhaa waliotambuliwa na vikosi vya IDF kama wakifanya kazi katika jengo karibu na wanajeshi katika eneo la Khan Younis, eneo hatari la mapigano ambalo watu walikuwa wamehamishwa hapo awali, kwa ajili ya ulinzi wao. Madai ya raia kudhurika yanapitiwa upya.”

Dk Milena Angelova-Chee, daktari kutoka Bulgaria anayefanya kazi katika hospitali ya Nasser, aliambia BBC wiki iliyopita kwamba Hamdi alipata majeraha mabaya kwenye ubongo, mapafu, mkono wa kulia na figo katika shambulio hilo.

Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza kujibu shambulio la Hamas kuvuka mpaka tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Takriban watu 54,418 wameuawa huko Gaza wakati wa vita, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment