Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Urusi ilidungua ndege ya Malaysia Airlines, MH17, mashariki mwa Ukraine mnamo Julai 2014, shirika la Umoja wa Mataifa la usafiri wa anga limesema.
Watu wote 298 waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya abiria walifariki dunia ndege hiyo ilipodunguliwa na kombora lililotengenezwa Urusi.
Kremlin daima imekuwa ikikanusha kuhusika na ajali hiyo.
Siku ya Jumatatu, Baraza la Umoja wa Mataifa la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) lilipiga kura na kuamua kwamba Urusi ilishindwa kutekeleza majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa ya anga, ambayo inazitaka nchi “kujizuia kutumia silaha dhidi ya ndege za kiraia zilizoangani”.
Ndege ya shirika la ndege la Malaysia MH17 ilikuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur ilipoanguka katika eneo la Donbas nchini Ukraine, wakati wa mzozo kati ya waasi wanaoiunga mkono Urusi na wanajeshi wa Ukraine.
Wengi wa abiria na wafanyakazi,196, walikuwa wanatoka Uholanzi.
Pia kulikuwa na watu 38 kutoka Australia, raia 10 wa Uingereza, pamoja na raia wa Ubelgiji na Malaysia.
Kesi hiyo kwa Umoja wa Mataifa iliwasilishwa mwaka 2022 na serikali za Australia na Uholanzi, ambazo zote zimefurahishwa na uamuzi huo.
“Tunatoa wito kwa Urusi hatimaye kukabiliana na wajibu wake kwa kitendo hiki cha kutisha cha vurugu na kulipa fidia kwa tabia yake mbaya”, alisema waziri wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong katika taarifa.
Mnamo 2022, mahakama ya Uholanzi ilitoa uamuzi wa kwamba kikundi kinachodhibitiwa na Urusi kiliangusha ndege hiyo na Warusi wawili na raia wa Ukraine anayeunga mkono Moscow walipatikana na hatia ya mauaji bila kuwepo.
Watatu hao wote walihukumiwa kifungo cha maisha jela, hata hivyo, kwa kuwa hawakurudishwa, hawajatumikia kifungo.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.