Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Maafisa wa polisi wanne nchini Kenya wamefunguliwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kufuatia kifo cha mtoto aliyekuwa na umri wa miezi sita, Samantha Pendo, aliyeuawa wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2017.
Maafisa hao—John Chengo Masha, Linah Kogey, Cyprine Wankio, na James Rono—wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya mauaji, ubakaji, na mateso dhidi ya raia, chini ya Sheria ya Uhalifu wa Kimataifa ya Kenya.
Watuhumiwa wote wanne walikana mashtaka hayo mbele ya mahakama na kuachiliwa kwa dhamana.
Awali, maafisa wa polisi 12 walikuwa wametambuliwa kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.
Hata hivyo, Idara ya Mashtaka ya Umma (ODPP) iliamua kutowafungulia mashtaka maafisa 8 wa ngazi za juu baada ya kupitia upya nyaraka za kesi hiyo—hatua ambayo imelaaniwa na mashirika zaidi ya thelathini ya haki za binadamu.
Mashirika hayo yamedai kuwa uamuzi huo ni wa makusudi ili kuwalinda wakuu wa usalama waliokuwa na mamlaka na wajibu wa kutoa maagizo kwa maafisa waliotekeleza operesheni hiyo ya umwagaji damu.
Mamlaka huru ya kusimamia Polisi nchini Kenya (IPOA), ambayo huchunguza malalamiko na uhalifu unaotekelezwa na polisi, haikuhusishwa kwenye uamuzi wa kutowashtaki maafisa hao waandamizi.
Kupitia taarifa yake, IPOA ilisema kuwa haijapewa sababu yoyote kuhusu kwa nini maafisa hao wakuu waliondolewa kwenye kesi hiyo.
Nayo mashirika ya haki za binadamu pia yameeleza wasiwasi kuhusu usalama wa waathiriwa na mashahidi ambao majina yao sasa yamewekwa wazi.
Kwa mujibu wa Amnesty International, hatua hiyo si tu kuwa inakiuka taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa, bali pia inaweza kuwaweka mashahidi hatarini.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.