Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza imethibitisha kuwa ilituma wanajeshi kuipigania Urusi dhidi ya Ukraine.
Katika ripoti ya shirika la habari la serikali KCNA, jeshi la Pyongyang lilidai kuwa wanajeshi wake walisaidia vikosi vya Urusi “kukomboa kikamilifu” eneo la mpaka wa Kursk, kulingana na agizo lililotolewa na kiongozi Kim Jong Un.
Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya Mkuu wa Majeshi wa Urusi Valery Gerasimov kusifia “ushujaa” wa wanajeshi wa Korea Kaskazini wakati wa mashambulio ya Urusi, mara ya kwanza Moscow imekiri hadharani kuhusika kwao.
Pia anadai Moscow ilipata tena udhibiti kamili wa eneo la Kursk magharibi mwa nchi hiyo – madai ambayo yamekanushwa na Ukraine.
Idara za ujasusi za Korea Kusini na Magharibi zimeripoti kwa muda mrefu kuwa Pyongyang ilituma maelfu ya wanajeshi wake Kursk mwaka jana.
Uamuzi wa kupeleka wanajeshi ni kwa mujibu wa mkataba wa ulinzi wa pande zote kati ya Pyongyang na Moscow, ilisema KCNA.
“Waliopigania haki wote ni mashujaa na wawakilishi wa heshima ya nchi yetu,” Kim alisema kulingana na KCNA.
Korea Kaskazini na Urusi zilionyesha “muungano na udugu” wao huko Kursk, na kuongeza kuwa “urafiki uliothibitishwa na damu” utachangia sana kupanua uhusiano “kwa kila njia”.
KCNA haikusema nini kitatokea kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini baada ya misheni yao huko Kursk kumalizika.
Ripoti kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini walikuwa wametumwa ziliibuka mwezi Oktoba, kufuatia kuimarika kwa uhusiano wa pande mbili kati ya Kim na Putin. Hii ni pamoja na kusainiwa kwa makubaliano ambapo kiongozi wa Urusi Vladimir Putin na Kim walikubaliana kusaidiana iwapo nchi zote mbili zinakabiliana na “uchokozi”.
Mnamo Januari, maafisa wa nchi za Magharibi waliambia BBC wanaamini kuwa wanajeshi 1,000 kati ya 11,000 waliotumwa kutoka Korea Kaskazini waliuawa kwa muda wa miezi mitatu.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.