Jordan yaipiga marufuku Muslim Brotherhood

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

ghb
Maelezo ya picha,Siku ya Jumatano Polisi walivamia ofisi za Islamic Action Front, tawi la kisiasa la Muslim Brotherhood

Serikali ya Jordan imepiga marufuku kundi la Muslim Brotherhood wiki moja baada ya kusema, wanachama wa kundi hilo la Kiislamu wamekamatwa kwa tuhuma za kupanga mashambulizi ya roketi na ndege zisizo na rubani.

Waziri wa Mambo ya Ndani Mazen al-Faraya aliuambia mkutano na waandishi wa habari, ofisi zote za Brotherhood zitafungwa na kunyang’anywa mali zao, na shughuli zao zozote zitachukuliwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Hakuna kauli ya mara moja kutoka Muslim Brotherhood, ambayo ilikanusha uhusiano wowote na madai ya njama za mashambulizi.

Haijabainika ni vipi marufuku hiyo itaathiri chama cha kisiasa cha kundi hilo, Islamic Action Front (IAF) ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani bungeni. Makao makuu yake yalivamiwa na polisi kufuatia tangazo la Faraya.

Katibu Mkuu wa IAF, Wael Saqqa, amesisitiza kuwa chama hicho cha kisiasa ni huru, akieleza kuwa “hakina uhusiano na shirika jingine lolote.”

Mwaka 2020, mahakama kuu ya Jordan iliamua kuivunja Muslim Brotherhood kwa sababu haikuwa imekamilisha taratibu zake za kisheria.

Hata hivyo, kundi hilo liliendelea na shughuli zake za kisiasa na nyinginezo, na IAF ilishiriki katika uchaguzi wa ubunge wa mwaka jana, na kushinda viti 31 kati ya 138.

Wiki iliyopita, Idara ya Ujasusi ya Jordan ilisema imewakamata watu 16 wanaoshukiwa kupanga mashambulizi yenye lengo la “kulenga usalama wa taifa, kuzusha machafuko na hujuma.”

Wakituhumiwa kumiliki vilipuzi na silaha, utengenezaji wa roketi, ufichaji wa roketi moja ambayo iko tayari kurushwa, mradi wa kutengeneza ndege zisizo na rubani, na mafunzo ya watu nchini Jordan na nje ya nchi.

Faraya alidai wakati wa mkutano wa wanahabari Jumatano kwamba wanachama wa Brotherhood “wanafanya shughuli zao nyuma ya pazia na kushiriki katika shughuli ambazo zinaweza kudhoofisha utulivu na usalama.”

“Mamlaka imegundua “mabomu na bunduki zilizosafirishwa katika miji ya Jordan na kuhifadhiwa katika maeneo ya makazi,” pamoja na vifaa vya utengenezaji wa roketi na mafunzo na shughuli za kuajiri,” amedai.

Pia alisema wanachama wa Brotherhood walijaribu kuondoa na kuharibu hati kutoka katika makao yao makuu “katika juhudi za kuficha shughuli zao na uhusiano unaotiliwa shaka.”

Kundi hilo limekanusha kuhusika, wala halielewi kuhusu madai ya njama ya mashambulizi na kusisitiza kuwa “linafanya kazi kwa njia ya amani.”

Muslim Brotherhood ilianzishwa nchini Misri karibu miaka 100 iliyopita na ina matawi kote ulimwenguni. Moja ya malengo yake ni kuunda dola ya inayojiendesha kwa sheria za Kiislamu.

Kundi hilo limepigwa marufuku nchini Misri na nchi kadhaa za Kiarabu, ambazo serikali zao zinaliona kuwa tishio.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment