Mwanasiasa wa Afrika Kusini alaaniwa kwa kumtembelea mchungaji anayetuhumiwa kwa ubakaji na ulaghai

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

fc
Maelezo ya picha,Floyd Shivambu alijiunga na MK mwaka jana

Afisa wa ngazi ya juu katika moja ya vyama vikubwa vya kisiasa nchini Afrika Kusini amelaaniwa kwa kumtembelea mchungaji aliyekimbilia Malawi baada ya kutuhumiwa kwa ubakaji na ulaghai.

Floyd Shivambu, katibu mkuu wa chama cha Umkhonto weSizwe (MK) cha Rais wa zamani Jacob Zuma, alituma picha katika mtandao wa X akihudhuria ibada ya Pasaka katika kanisa la Shepherd Bushiri.

Bw Bushiri, kutoka Malawi, alikuwa mmoja wa wahubiri maarufu kusini mwa Afrika alipokamatwa na kushtakiwa kwa ulaghai mwaka 2020.

Baada ya kuachiliwa kwa dhamana, alifanikiwa kukimbilia nchi yake katika mazingira yasiyoeleweka. Afrika Kusini imekuwa ikijaribu kumrejesha nchini humo tangu wakati huo.

Mwezi uliopita, mahakama nchini Malawi iliunga mkono ombi la kurejeshwa Afrika Kusini lakini Bushiri na mkewe Mary, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai, wamekata rufaa.

Bushiri ni milionea ambaye alianzisha makanisa katika nchi kadhaa za Afrika.

Anashutumiwa kwa kuwanyonya watu maskini ambao wana hamu ya kuboresha maisha yao kwa kuwauzia bidhaa ikiwa ni pamoja na “mafuta ya miujiza.”

Bushiri anayejiita Nabii anadai ameponya watu VVU, kuwafanya vipofu kuona tena, kubadilisha maisha ya watu maskini na na kudai alitembea hewani mara moja.

Bushiri pia ameshtakiwa kwa ubakaji. Yeye na mkewe wamekana kosa lolote.

Waziri wa Sheria na Maendeleo ya Katiba wa Afrika Kusini Mmamoloko Kubayi alisema ushirikiano wa Shivambu na Bushiri ni “kitendo cha wazi cha kutoheshimu mfumo wa sheria wa Afrika Kusini.”

Chama cha MK cha Shivambu pia kilitoa taarifa ya kujitenga na ziara yake, kikisema ameifanya ziara hiyo “yeye binafsi, bila ruhusa au chama kujua.”

Chama hicho kiliongeza “kinalaani aina zote za unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji wa jamii zilizo masiki, haswa waumini kwa Kikristo wasio na hatia, unaofanywa na watu ambao wanadanganya ili kujitajirisha au kukwepa haki.”

Katika chapisho kwenye X siku ya Jumamosi, Shivambu alimsifu Bushiri kwa “kazi yake nzuri.”

Chini ya uongozi wa Rais wa zamani Zuma, chama kipya kilichoundwa cha MK kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa mwaka jana – na ikawa sababu kwa chama tawala cha ANC kupoteza wingi wake kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 1994.

Shivambu alijiunga na chama hicho Agosti mwaka jana akitokea chama pinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) na baadaye kuteuliwa kuwa katibu mkuu – moja ya nyadhifa za juu za chama hicho.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment