Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vikosi vya usalama vya Msumbiji vimetuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi katika juhudi za kukabiliana na maandamano ya muda mrefu, hali iliyosababisha vifo vya mamia ya watu, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International.
Maandamano hayo yalizuka kufuatia ushindi wa Chama cha Ukombozi wa Msumbiji (FRELIMO), kilichoko madarakani kwa miongo kadhaa, na mgombea wake Daniel Chapo katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana.
Ripoti ya Amnesty inabainisha kuwa viongozi 10 wa upinzani waliuawa na vikosi vya usalama, huku watu zaidi ya 3,000 wakijeruhiwa kati ya mwezi Oktoba na Januari, wakiwemo watu 315 waliopata majeraha makubwa.
Takwimu hizi, zilizokusanywa na mashirika ya kiraia ya ndani, ni kubwa zaidi kuliko zile zilizotolewa na serikali, ambazo zilitangaza idadi ya waliofariki ni 96 pekee, wakiwemo maafisa 17 wa usalama.
Kwa mujibu wa Amnesty, ushahidi wa mashuhuda, simulizi za manusura pamoja na vielelezo vya picha na video vilivyothibitishwa, vinaonesha kuwa maafisa wa usalama walitumia risasi dhidi ya waandamanaji.
Tarehe 12 Desemba, mwanablogu mmoja alifyatuliwa risasi alipokuwa akiripoti maandamano mubashara. Mwezi Januari, watu kadhaa walipoteza maisha baada ya polisi kufyatua risasi kwa umati wa watu waliokuwa wakisubiri kwa amani kumpokea kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane.
Ripoti hiyo pia inatuhumu mamlaka za Msumbiji kwa kukamata kiholela waandamanaji na raia wasiohusika, wakiwemo watoto, na waliokamatwa kueleza misururu ya mateso wakiwa kizuizini.
Amnesty International imeitaka serikali ya Msumbiji kuanzisha uchunguzi huru, wa kina na wa uwazi kuhusu madai hayo, na kuhakikisha wote wanaohusika na ukatili huo wa kibinadamu wanawajibishwa kisheria.
Maandamano hayo yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya utawala wa FRELIMO tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Kireno mwaka 1975.
Tarehe 24 Oktoba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Daniel Chapo kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 71 ya kura, huku mgombea huru Venancio Mondlane akipata asilimia 20.
Mondlane alipinga matokeo hayo akidai kuwepo kwa wizi mkubwa wa kura, ikiwa ni Pamoja na masanduku kujazwa kura zisizo halali, na akatoa wito wa kura kuhesabiwa upya.
Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya ulibaini kasoro nyingi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Katika kile kilichoonekana kama jaribio la kudhibiti hali ya taharuki, polisi waliwashutumu waandamanaji kwa kuharibu mali na kutumia mabomu ya kutengeneza majumbani kuchoma majengo ya serikali.
Hata hivyo, mazungumzo ya ghafla yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi Machi kati ya Rais Mteule Daniel Chapo na Venancio Mondlane yameibua matumaini mapya ya kupatikana kwa suluhu ya kisiasa na kurejesha utulivu nchini humo.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.