UNAYALINDAJE MACHO YAKO DHIDI YA MTEGO WA MACHO?

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Sina shaka picha uliyoiona hapo chini, ndiyo iliyovuta akili yako haraka kabla hata hujajua nini kinafuata.

Hii si ajali. Ni sayansi halisi ya namna akili ya binadamu ilivyojengwa: kupendelea habari za burudani kuliko maarifa, starehe kuliko changamoto, na vichekesho kuliko mada ngumu.

Lakini umewahi kujiuliza kwanini inakuwa hivyo? Kwanini mtu unakuwa mwepesi ku-like na ku-comment katika mambo mepesi?

Kwanini habari na picha zenye mwelekeo wa ngono husisimua haraka kuliko habari za siasa, kilimo ama mwenendo wa uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla?

Jibu lipo…..

Katika zama hizi za utandawazi imethibitika kirahisi kwamba akili ya mwanadamu huvutwa kirahisi kwenye habari nyepesi kama vile burudani, michezo na mapenzi.

Kwa asili, ubongo wa mwanadamu hupendelea kitu kinachoamsha hisia, chenye kutia shamra; kinachoibua furaha au ladha ya starehe kwa haraka.

Sababu? Mambo mepesi hayatumii nguvu nyingi za kufikiri. Hayachoshi. Huchangamsha dopamine (kemikali ya furaha). Lakini furaha hii huwa ya vipindi vifupi. Haidumu.

Kinyume chake, mada ngumu kama za uchumi, mafundisho thabiti ya kiroho, au mbinu za ujasiriamali; zinahitaji umakini, kuhoji, na muda wa kufikiri kwa kina; vitu ambavyo akili haina haraka navyo. Ingawa ndiyo mada zenye kutoa ufumbuzi wa kudumu katika maeneo mengi ya maisha yetu.

Ndiyo maana…

Ujumbe wa ngono hupata likes kuliko mafunzo ya biashara. Picha za kusisimua kama za huyo dada huleta msisimko wa haraka, kuliko picha za mkulima katika shamba la mpunga.

Habari za udaku au connection za kunyanduana, hupata shares nyingi na za haraka kuliko connection za kiimani na maonyo ya kiroho.

Vichekesho hupata views kuliko post za elimu ya saikolojia, mahusiano na kujitambua.

Habari za soka huchangamkiwa zaidi, lakini somo la uadilifu halijawahi kuwa na mashabiki wa kudumu.

Simulizi za mapenzi ya watu maarufu huvuta hisia za wengi, kuliko simulizi ya mafanikio ya mkulima mkubwa.

Ujumbe wa “Diamond aachana na Zuchu” utapata engagement kubwa kuliko ujumbe wa “Mkurugenzi wa Super Feo aeleza faida ya kilimo cha miti.”

Ingawa hiyo ndiyo asili ya akili ya binadamu, ukweli ni kwamba hii tabia ina gharama.

Endapo tusipoweka uwiano mzuri katika kile tunacholisha akili zetu kila siku, kuna madhara yatatokea sasa ama usoni.

1) Tutakuwa watumwa wa furaha za muda mfupi kwa vitu vinavyovutia na kufurahisha nafsi, na si vinavyotuvusha.

2) Tutalewa na kushiba taarifa za udaku na burudani, huku tukiendelea kulala na kuamka na njaa ya maarifa.

3) Tutachangamshwa kwa habari za michezo na burudani, lakini tukiwa tumekwama kitaaluma, kiroho na stadi za maisha.

4) Tutajua mengi kuhusu maisha ya watu maarufu, lakini tusijue lolote kuhusu maisha yetu wenyewe wala hatima yake.

5) Tutaamka tukiwa wepesi, lakini maisha yakizidi kuwa mzigo mzito.

Kuna suluhisho? Lipo;

1. Weka ratiba ya kujiongezea maarifa: Tengeneza muda kila siku wa kusoma kitu kizito: siasa, imani, historia, au saikolojia, walau kwa dakika 15. Tabia njema hujengeka taratibu kama ilivyo Kwa tabia mbaya.

2. Kata mkondo wa vichekesho, burudani na michezo. Ingawa habari za burudani ni muhimu katika kuchangamsha nafsi na kutuliza ‘mood’, ni muhimu kujiwekea uwiano mzuri wa muda wa burudani na muda wa kujiongezea maarifa ya maisha. Usipoteze muda mwingi kwenye mijadala ya soka au maisha ya mastaa.

3. Chagua marafiki wa maendeleo: Wafuate watu wanaokupa changamoto ya kufikiri na si marafiki wa kukuvutia pekee; utaivuruga akili yako. Aina ya marafiki waliokuzunguka inahusiana kwa karibu sana na mwenendo wako.

4. Sikiliza podcast zenye mafunzo: Ukiwa safarini au mapumzikoni. Ni vizuri kutenga muda wa kujaza akili yako kwa maudhui yenye kukuza akili.

5. Andika unachojifunza: Uandishi huimarisha kumbukumbu. Fanya kunukuu japo sentensi 3 tu kwa siku.

RAI:

Siyo kila kitu kinachokuvutia kinakuendeleza.

Si kila kinachokuchangamsha kinakuimarisha.

Na si kila kinachokuchosha kinakuumiza.

Wakati mwingine, maarifa huvaa ngozi ya taabu na mateso na usumbufu; lakini ndani yake kuna uhuru wa kweli; uhuru wa kudumu.

Jifunze kupenda yasiyopendwa.

Kwani ndani ya ugumu, ndipo kuna ukuaji na ukomavu wa kweli.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment