Wanajeshi kadhaa wauawa Kaskazini mwa Benin

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mamlaka nchini Benin zimesema kuwa wanajeshi kadhaa wameuawa katika shambulio lililotokea kaskazini mwa nchi, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu uasi wa Kiislamu katika baadhi ya maeneo ya Afrika Magharibi.

Kamanda Mkuu wa jeshi hilo, Kanali Faizou Gomina, ambaye alitangaza tukio hilo Alhamisi, hakutoa idadi kamili ya wanajeshi waliouawa.

Hata hivyo, alikiri kwamba jeshi lilipata hasara kubwa katika tukio hilo.

“Tumepigwa pigo kubwa sana,” alisema Kanali Gomina katika taarifa, akifichua kuwa “eneo lililoshambuliwa jana lilikuwa miongoni mwa maeneo yenye ulinzi mkubwa zaidi katika Operesheni MIRADOR.”

Hakutaja mahali halisi pa shambulio hilo, lakini ripoti zinasema lilitokea karibu na mpaka wa Benin na Niger na Burkina Faso — mataifa ambayo pia yanakabiliana na mashambulizi endelevu kutoka kwa makundi ya kigaidi.

Licha ya kuwa vikosi hivyo vilikuwa na silaha za kisasa, ndege zisizo na rubani, na vifaa vya kuripoti matukio ya uhalifu, bado vilishindwa kukabiliana na ghadhabu ya washambuliaji wao.

“Vifaa pekee haviwezi kutosha kushinda,” alikiri Kanali Gomina, akisisitiza kwa makamanda wa kijeshi kuandaa upya vikosi vyao na kuboresha mikakati ya kimapigano ili kukabiliana na vitisho vya kiusalama.

“Amkeni, maafisa na wakuu wa vitengo vya kiusalama. Tuna vita vya kushinda,” aliongeza.

Eneo la kaskazini mwa Benin linaendelea kuwa hatarini, huku mashambulizi kutoka kwa magaidi wanaohusishwa na Dola la Kiislamu na Al-Qaeda yakisemekana kuongezeka katika eneo hilo kwa miaka ya hivi karibuni.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment