Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Zaidi ya wanawake 500 wamebakwa na wanamgambo wa Sudani tangu kuanza kwa vita dhidi ya jeshi mnamo mwezi Aprili 2023, afisa wa serikali amesema siku ya Jumanne Januari 7, 2025.

Sulaima Ishaq al-Khalifa, mkuu wa kitengo cha serikali cha kupambana na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto, amesema mamlaka imerekodi kesi 554 za ubakaji zilizofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kati ya mwezi Aprili 2023 na Desemba 2024. Ameongeza, hata hivyo kwamba takwimu hizi zinawakilisha sehemu tu – karibu “asilimia mbili”, kulingana na yeye – ya idadi ya kweli ya mashambulizi.
“Baadhi ya maeneo yametengwa kabisa, mawasiliano yametatizika na wanawake wengi huepuka kuripoti unyanyasaji wa kijinsia kwa kuhofia unyanyapaa wa kijamii,” amesema. Khalifa amesema mamlaka imeidhinisha utoaji mimba 36 kati ya mwezi Septemba 2023 na Aprili 2024 katika mji mkuu wa Khartoum, Kordofan kusini, na Darfur magharibi, kwa idhini ya kisheria kutoka kwa waendesha mashtaka.
Vitendo kumi vpya vya Uutoaji mimba vilifanyika hivi karibuni katika jimbo la mashariki la Kassala kwa wanawake waliofurushwa kutoka al-Jazeera, ambapo raia wameripoti mfululizo wa mashambulizi ya RSF katika miezi ya hivi karibuni. Nchini Sudani, utoaji mimba unaruhusiwa katika visa vya ubakaji au wakati ujauzito unaleta hatari kwa mama. Kwa zaidi ya miezi 20, nchi hiyo imekumbwa na mzozo wa madaraka kati ya mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdane Daglo, kiongozi wa RSF.
Vita hivyo vimeua makumi ya maelfu, vimewahamisha watu milioni 12 na kuunda kile ambacho Umoja wa Mataifa unakielezea kuwa moja ya maafa mabaya zaidi ya kibinadamu katika historia ya hivi karibuni. Siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema RSF “imefanya mauaji ya halaiki” nchini Sudan, na kuwashutumu wanajeshi hao kwa ukatili ikiwa ni pamoja na “kuwalenga kwa makusudi wanawake na wasichana wa baadhi ya makabila kwa ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia.
Mwezi Oktoba, Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli ulishutumu RSF na wanamgambo washirika kwa “kuenea kwa unyanyasaji wa kingono na kijinsia, ubakaji, utumwa wa kingono, utekaji nyara, uandikishaji na matumizi ya ‘watoto katika uhasama’. Ujumbe huo pia uliandika baadhi ya kesi zinazohusisha wanajeshi na makundi washirika, lakini iliamua kwamba unyanyasaji mwingi wa kingono ulifanywa na RSF. RSF haikujibu ombi la kutoa maoni kutoka kwa shirika la habari la AFP.
Mnamo mwezi Oktoba, walipuuzia mahitimisho ya Umoja wa Mataifa kama “propaganda kwenye mitandao ya kijamii”. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Mohamad Mokhtar, mwanachama wa RSF, amesema wanamgambo hao walirekodi kisa kimoja pekee cha ubakaji katika maeneo wanayodhibiti, na kuongeza kuwa walifanya “uchunguzi wa kimatibabu” kwa wanawake ili kuthibitisha madai ya ubakaji.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.