Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Waasi 10 wenye itikadi kali za Kiislamu wa Al Shabab wameuawa katika shambulizi la anga kusini mwa Somalia, mamlaka ya kijeshi ya Marekani imetangaza siku ya Jumanne Januari 7, 2025.

Shambulio hilo lilifanyika mnamo Desemba 31 huko Beer Xaani, karibu kilomita 35 kutoka mji wa bandari wa Kismayo, kamandi ya jeshi la Marekani kwa Afrika (Africom) imesema katika taarifa. Shambulio hilo lilitekelezwa “kwa ombi” la serikali ya Somalia, kulingana na Africom.
“Tathmini ya awali baada ya shambulio” ilionyesha kuwa operesheni ya anga iliua wanachama kumi wa Al Shabab, bila kuwadhuru raia, inabainisha mamlaka ya Marekani. Vituo muhimu vya magaidi viliharibiwa wakati wa operesheni hiyo, Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii ya Somalia pia imeripoti kwenye X.
Africom inahakikisha kwamba “itaendelea kutathmini matokeo ya mashambulizi haya ya anga na itatoa taarifa za ziada ikibidi”.
Wakihusishwa na Al-Qaeda, Al Shabab wamekuwa wakipigana na serikali ya shirikisho ya Somalia, ikiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, kwa zaidi ya miaka kumi na tano kuanzisha sheria za Kiislamu katika nchi hii, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani. Baada ya kufukuzwa nje ya miji mikuu mwaka 2011-2012, wamesalia imara katika maeneo makubwa ya vijijini, ambapo wanaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya usalama na ya kiraia.
Mwaka jana, Al Shabab ilifanya mashambulizi mengi katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya nchi, huku serikali ikiendelea na mashambulizi yake yenye lengo la kuwaangamiza wanajihadi.
Washington imewekeza kwa kiasi kikubwa kwa miongo kadhaa katika vita dhidi ya uasi. Wakati wa muhula wake wa urais, Donald Trump alitangaza kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Somalia, uamuzi uliotenguliwa na mrithi wake Joe Biden.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.