Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama chake cha ACT Wazalendo.

Othman ameeleza kuwa atafuata taratibu zote za chama chake na kuwaomba wanachama wa ACT Wazalendo kumpa dhamana ya kuwania nafasi hiyo. Pia amesisitiza azma yake ya kuwahakikishia Wazanzibari maendeleo, uhuru wa kweli, na ustawi bora kwa taifa lao.
“Napenda kwa heshima kubwa kutumia fursa hii kutangaza rasmi kwamba nimekusudia, inshaAllah, itapofika wakati wa kuanza mchakato wa kutafuta wagombea katika chama changu, kwa kufuata taratibu zilizopo, kukiomba chama changu cha ACT Wazalendo kinibebeshe dhamana ya kukiwakilisha kwenye nafasi ya kuwania uongozi wa juu wa nchi yetu, Zanzibar,” alisema Othman siku ya Jumatano Januari 1, 2025.
Othman amesema kuwa ACT Wazalendo imejipanga kutoa uongozi thabiti utakaowaondoa Wazanzibari kutoka katika hali ngumu wanayokabiliana nayo sasa, kuelekea kwenye mustakabali wa maendeleo endelevu.
Othman amesisitiza kuwa lengo la kugombea ni kuleta maendeleo, uhuru wa kweli, na ustawi kwa Wazanzibari. Aliongeza kuwa chama chake kimejizatiti kuwakomboa wananchi wa Zanzibar kutoka katika hali ya dhiki na kuwaletea maisha bora.
“Muda ukifika, tutawaomba Wazanzibari watupe sisi ACT Wazalendo jukumu la kuwatoa hapa mahala dhalili walipo na tuwapeleke kwenye maendeleo, uhuru wa kweli, na ustawi,” amesema.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.