Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamojaMuhtasari
- Mjadala wazuka Kenya kuhusu chanjo ya mifugo
- Urusi yamkamata mshukiwa wa mauaji ya jenerali Igor Kirillov
- Honda na Nissan zafanya mazungumzo ya kuungana
- Njama ya mauaji ya Papa ilitibuliwa na ujasusi wa Uingereza
- Mauaji ya Jenerali yaashiria kuwa hali sio shwari Urusi
- NATO yachukua uratibu wa misaada kwa Ukraine badala ya Marekani
- Trump ashtaki gazeti kwa ‘kuingilia uchaguzi’
- Facebook imezuia ufikiaji wa habari katika maeneo ya Palestina
- Makaburi ya halaiki Syria: Waokoaji wanatafuta na kuwataja waliofariki
Naam,Natumai U buheri wa afya popote pale ulipo duniani kwa mwoyo mkunjufu na mikono miwili Hujambo na karibu katika matangazo yetu Afrika Leo Asubui ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 18/12/2024 Jina langu ni Cantona Joseph,karibu
Honda na Nissan zafanya mazungumzo ya kuungana

Kampuni za magari za Honda na Nissan zimeripotiwa kufanya mazungumzo ya uwezekano wa kuungana ili kuzisaidia kushindana dhidi ya watengenezaji wa magari ya umeme (EV), hasa nchini China.
Mnamo mwezi Machi, kampuni hizo mbili za kutengeneza magari za Japani zilikubali kushirikiana kimkakati katika utengenezaji wa magari yanayotumia umeme.
Makampuni yote mawili yaliitikia wito na kutoa taarifa sawa kwa BBC, ambayo ilisema: “Kama ilivyotangazwa Machi mwaka huu, Honda na Nissan wanaangalia uwezekano wa ushirikiano wa siku zijazo, kutumia vilivyo uwezo wa kila mmoja wao.”
Hatua hii inawadia wakati kampuni nyingi za magari zinajitahidi kukabiliana na ushindani unaokua kadiri tasnia inavyobadilika kutoka kwa magari ya petroli na dizeli hadi ya umeme, huku uzalishaji ukiongezeka nchini China.
Honda na Nissan, watengenezaji nambari mbili na nambari tatu wa magari nchini Japani nyuma ya Toyota, zimekuwa zikipoteza sehemu ya soko nchini China, ambayo ilichangia karibu 70% ya mauzo ya magari yanayotumia umeme duniani mwezi wa Novemba.
Urusi yamkamata mshukiwa wa mauaji ya jenerali Igor Kirillov

Idara ya usalama ya Urusi imesema mwanamume mwenye umri wa miaka 29 kutoka Uzbekistan amezuiliwa kwa mauaji ya jenerali mkuu Igor Kirillov na msaidizi wake huko Moscow.
Luteni Jenerali Igor Kirillov, mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Nyuklia, Biolojia, Kemikali, alikuwa nje ya makazi mapema Jumanne wakati kilipuzi kilichofichwa kwenye skuta kilipolipulika kwa mbali.
Idara ya usalama ya Urusi ilisema mshukiwa alisajiliwa na ujasusi wa Ukraine, kulingana na vyombo vya habari vya serikali.
Chanzo cha habari cha Ukraine kiliiambia BBC Jumanne kwamba mauaji hayo yalipangwa na idara ya usalama ya Ukraine.
Chanzo cha usalama cha Ukraine kilisema Kirillov – ambaye alikuwa mkuu wa silaha za kemikali wa Urusi – “alilengwa kimaksudi” na kilidai kuwa alitekeleza uhalifu wa kivita.
Jumatatu, siku moja kabla ya mauaji hayo, Ukraine ilimshtaki Kirillov, 54, bila kuwepo mahakamani, ikisema “alihusika na matumizi makubwa ya silaha za kemikali zilizopigwa marufuku”.
Kitengo cha mahusiano ya umma cha Shirika la Ujasusi la Urusi kilisema Jumatano kwamba kijana mwenye umri wa miaka 29 “anashukiwa kufanya shambulio la kigaidi”.
Taarifa ilisema wakati wa “mahojiano alieleza kwamba aliajiriwa na huduma maalum za Ukraine”.
Mjadala wazuka Kenya kuhusu chanjo ya mifugo

Rais William Ruto amewakejeli wanaopinga mpango wa chanjo ya mifugo uliopangwa kuanza Januari, 2025.
Rais Ruto amesema kuwa mpango huo utaimarisha wakulima ili kuendana na viwango vya kimataifa wakati wa kuuza bidhaa za nyama na ngozi nje ya nchi.
Ruto amewataka wanasiasa wanaopinga mpango huo kuacha kueneza propaganda.
“Chanjo inatolewa hata kwa binadamu. Ikiwa sio hatari kuwachanja watu kwa nini iwe hatari kuwachanja wanyama?”, William Ruto ameuliza.
Hata hivyo, kuna baadhi ya wafugaji ambao wanapinga chanjo ya hiyo wakidai kuwa hawakupewa taarifa mapema huku wakiitaka serikali kutoa maelezo kamili kuhusu zoezi hilo.
Chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa kwa ng’ombe milioni 20 dhidi ya Ugonjwa wa Miguu na Midomo na kondoo na mbuzi milioni 50 kote nchini Kenya.
Njama ya mauaji ya Papa ilitibuliwa na ujasusi wa Uingereza

Njama ya kumuua Papa Francis wakati wa safari yake nchini Iraq ilizuiwa kufuatia taarifa kutoka kwa vyombo vya habari vya Uingereza, kulingana na wasifu wake ujao.
Papa anasema kwamba , baada ya kutua Baghdad mnamo Machi 2021, aliambiwa kuhusu tukio ambalo alipangwa kuonekana lilikuwa likilengwa na washambuliaji wawili wa kujitoa mhanga.
Washambuliaji wote wawili walinaswa na kuuawa, alisema katika sehemu zilizochapishwa na gazeti la Italia Corriere della Ser.
Ziara hiyo, ambayo ilifanyika kwa muda wa siku tatu wakati wa janga la corona, lilikuwa la kwanza kuwahi kufanywa na papa nchini Iraq na lilishuhudia operesheni kali ya usalama.
Miaka iliyopita Iraq ilishuhudia kuongezeka kwa ghasia za kimadhehebu na mapigano kati ya Waislamu wa Shia na Sunni pamoja na mateso ya dini ndogo.
Jumuiya ya Wakristo nchini humo ilikuwa imepungua kwa kiasi kikubwa, baada ya kulengwa hasa na kundi la Islamic State na wafuasi wengine wa itikadi kali za Kisunni.
Katika sehemu za wasifu wake, Papa anasema “karibu kila mtu alinishauri dhidi ya” ziara hiyo lakini alihisi “alipaswa kuifanya”.
Anasema njama hiyo ilifichuliwa na ujasusi wa Uingereza, ambao walionya polisi wa Iraq, na wao kwa upande wao walimweleza maelezo yake ya usalama mara tu alipowasili.
“Mwanamke aliyejaa vilipuzi, kijana mlipuaji wa kujitoa mhanga, alikuwa akielekea Mosul kujilipua wakati wa ziara ya papa,” anasema. “Na gari pia lilikuwa limeondoka kwa kasi kubwa kwa nia hiyo hiyo.”
Papa anaongeza kuwa alimuuliza afisa wa usalama siku iliyofuata nini kilikuwa kiliwapata washambuliaji hao.
“[Rasmi] alijibu kwa unyonge: ‘Hawapo tena’. Polisi wa Iraq walikuwa wamewakamata na kuwalipua,” aliandika.
Kitabu hicho kinachoitwa Hope, kinatarajiwa kuchapishwa tarehe 14 Januari. Vatikani haikujibu mara moja ombi la maoni, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Mauaji ya Jenerali yaashiria kuwa hali sio shwari Urusi

Wakati Luteni Jenerali Igor Kirillov na msaidizi wake Ilya Polikarpov walipouawa kwa bomu lililokuwa limefichwa kwenye skuta ya umeme, ukweli wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine ulionekana dhahiri mbele ya macho yao kwa raia wake.
Angalau kwa wale Warusi waliokuwa karibu na eneo la uhalifu.
“Ni jambo moja kufahamu juu ya hili katika vyombo vya habari, utahisi liko mbali, lakini linapotokea karibu na wewe, hilo ni suala tofauti kabisa na la kutisha,” Liza amesema kwa BBC. Anaishi jengo moja kutoka eneo la mlipuko huo.
“Hadi sasa, [vita] vilikuwa ni kana kwamba vinatokea mbali – sasa mtu sasa mtu amekufa, hapa, unaweza kuhisi athari zake.
“Wasiwasi wangu umeongezeka kupita kiasi. Kila sauti unayosikia inakushtua – unajiuliza kama ni ndege isiyo na rubani au kitu kimetokea kwenye eneo la ujenzi,” Liza anasema.
Mtazamo huu wa vita vya Urusi nchini Ukraine kama kitu cha mbali – hilo nimelisikia mara nyingi hapa. Ninapata maana kwamba, kwa idadi kubwa ya watu, ni vita wanayoiona tu kwenye televisheni zao au kwenye simu zao za mkononi. Vita vya kweli.
Inashangaza, kwa kweli, ukizingatia idadi kubwa ya waliokufa na waliojeruhiwa.
Lakini kuuawa kwa jenerali wa Urusi huko Moscow: hii ni tahadhari; ushahidi kwamba vita hii ni ya kweli iko karibu sana na nyumbani.
Je mauaji hayo yatachukuliwa kama tahadhari na mamlaka ya Urusi?
Pengine haitakuwa hivyo. Kuna dalili kidogo sana kwamba Urusi itabadili mwelekeo wake, badala yake ni ina uwezekano mkubwa wa kuzidisha vita.
Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev alisema “wachunguzi lazima wapate wauaji nchini Urusi.” Aliongeza: “Lazima tufanye kila kitu ili kumaliza vibaraka wao ambao wako Kyiv.”
Kutoka kwa Rais Vladimir Putin hisia za raia bado hazijaonekana hadharani hadi sasa kutokana na mauaji ya jenerali na msaidizi wake.
Lakini kiongozi wa Kremlin amesema mara nyingi kabla ya hapo, ikikabiliwa na vitisho vya usalama, wakati wowote ule Urusi “itajibu”.
Kulingana na ahadi hiyo, kuna uwezekano wa kulipiza kisasi.
NATO yachukua uratibu wa misaada kwa Ukraine badala ya Marekani

Muungano wa Atlantiki ya Kaskazini – NATO imechukua uratibu wa misaada ya kijeshi ya Magharibi kwa Ukraine kama ilivyopangwa, Reuters iliripoti, ikinukuu chanzo.
Hatua hiyo inaonekana kama ya kulinda mfumo wa msaada kwa Ukraine kabla ya Donald Trump kurejea Ikulu ya White House.
Hata hivyo, wanadiplomasia wanasema kwamba kukabidhi NATO jukumu hilo kunaweza kuwa na athari ndogo, ikizingatiwa kwamba Marekani chini ya Trump bado inaweza kuwa pigo kubwa kwa Ukraine kwa kusitisha uungaji mkono wake.
Ni mamlaka kuu ya muungano huo na inaipatia Kyiv silaha zake nyingi.
Trump amesema anataka kumaliza vita nchini Ukraine haraka iwezekanavyo, lakini bado hajabainisha ni kwa namna gani hasa anakusudia kufanya hivyo.
Wakati huo huo, kwa muda mrefu amekosoa kiwango cha msaada wa kifedha na kijeshi wa Marekani kwa Ukraine, Reuters inabainisha.
Ujumbe huo mpya wa NATO una makao yake makuu katika kambi ya kijeshi ya Marekani huko Wiesbaden, mji mkuu wa jimbo la Ujerumani la Hesse.
Siku za nyuma, vifaa vya kijeshi vya Magharibi kwa Kyiv viliratibiwa na Kundi la Mawasiliano linaloongozwa na Marekani kuhusu Ulinzi wa Ukraine, au Ramstein, muungano wa baadhi ya nchi 50 zilizopewa jina la kituo cha anga cha Marekani nchini Ujerumani ambako mkutano wa kwanza wa kundi hilo ulifanyika.
Trump ashtaki gazeti kwa ‘kuingilia uchaguzi’

Rais mteule Donald Trump ameshtaki gazeti la Des Moines Register, pamoja na kampuni yake mama na mchanganuzi wake wa zamani, kwa “kuingilia kati uchaguzi” juu ya kura ya maoni iliyochapishwa siku chache kabla ya uchaguzi wa rais wa 2024.
Kura ya maoni ya Novemba 2 ilipendekeza mgombeaji wa chama cha Democratic Kamala Harris angeshinda jimbo la Iowa, lenye watu wengi wa chama cha Republican.
Trump aliwasilisha kesi hiyo mpya baada ya kushinda kesi dhidi ya shirika la habari la ABC News kwa kumchafulia jina akifidiwa $15m (£12m), juu ya mtangazaji aliyesema uwongo kuwa Trump alipatikana na hatia ya ubakaji mwaka jana.
Mtazamo wa mara kwa mara wa Trump kwa vyombo vya habari vya Marekani unarejelea kampeni yake ya kwanza ya urais, na anatarajiwa kuendelea hadi muhula wake wa pili.
Alitangaza mipango yake ya kushtaki jarida hilo lenye makao yake makuu Iowa wakati wa mkutano na wanahabari siku ya Jumatatu ambapo aliviita vyombo vya habari kuwa “vifisadi”. Kesi hiyo iliwasilishwa katika Kaunti ya Polk, Iowa, baadaye asubuhi hiyo.
Katika uchaguzi huo chini ya wiki moja baadaye, Trump aliongoza katika jimbo la Iowa kwa pointi 13.
“Kwa maoni yangu, ulikuwa udanganyifu na ulikuwa uingiliaji wa uchaguzi,” Trump alisema.
“Ninahisi lazima nifanye hivi,” aliongeza. “Inagharimu pesa nyingi lakini inabidi tunyooshe vyombo vya habari.”
Facebook imezuia ufikiaji wa habari katika maeneo ya Palestina

Facebook imezuia pakubwa uwezo wa vyombo vya habari vya Palestina kufikia hadhira wakati wa vita vya Israel-Gaza, kulingana na utafiti wa BBC.
Katika uchanganuzi wa kina wa data ya Facebook, tuligundua kuwa ushiriki wa watazamaji katika vyomba vya habari vya Palestina – huko Gaza na Ukingo wa Magharibi – ulishuka kwa kasi tangu Oktoba 2023.
BBC pia imeona nyaraka zilizovuja zinazoonyesha kuwa Instagram – jukwaa jingine linalomilikiwa na Meta – liliongeza udhibiti wake wa maoni ya watumiaji wa Palestina baada ya Oktoba 2023.
Hata hivyo, Meta – mmiliki wa Facebook – imesema kwamba madai kuwa ilikandamiza sauti fulani kwa makusudi ni “uongo usio na msingi”.
Tangu kuanza kwa vita vya Israel na Gaza, ni waandishi wachache tu wa nje wameruhusiwa kuingia katika eneo la pwani la Palestina la Gaza kutoka nje, na waliweza tu kufanya hivyo wakisindikizwa na jeshi la Israel.
Akaunti za Facebook za vyombo vya habari kama vile Televisheni ya Palestina, shirika la habari la Wafa na Palestinian Al-Watan News – ambazo zinafanya kazi nje ya eneo la Ukingo wa Magharibi – zimekuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa wengi ulimwenguni.
Makaburi ya halaiki Syria: Waokoaji wanatafuta na kuwataja waliofariki

Raia wa Syria wamegundua makaburi ya halaika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Damascus.
Chini ya kilomita 10 (maili sita) kutoka katikati mwa jiji lenye shughuli nyingi la Damascus, katika kitongoji cha kaskazini-magharibi cha Adra, sehemu kame ya ardhi imezibwa kwa kuta za saruji.
Unapoingia eneo hilo, upande wa kushoto, timu ya waokoaji kutoka shirika la kibinadamu la White Helmet wanaonekana wakitafuta makaburi ya halaiki.
Siku chache zilizopita, video zimetumwa mtandaoni kuhusu makaburi ya halaiki ambapo utawala wa Bashar al-Assad ulizika wale walioteswa hadi kufa katika magereza yenye sifa mbaya nchini Syria.
Huko Adra, shirika la White Helmet lilipata shimo ndogo ambapo mifuko kadhaa mikubwa ya rangi nyeupe ya plastiki ilijazwa na mabaki ya miili.
Ujumbe unasema: “Miili saba, kaburi la nane, haijulikani.”
Timu ilikuwa ikitoa mabaki, mafuvu na mifupa, ambayo walikusanya.
Sampuli za DNA ziliwekwa kando katika mifuko ya rangi nyeusi ya kubeba mwili kwa ajili ya ukusanyaji taarifa na kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Ismael Abdullah, mmoja wa waokoaji, anasema wanamengi yanayowasikitisha.
“Maelfu ya watu hawajulikani walipo. Itachukua muda – mwingi sana – angalau kupata yaliyo karibu na ukweli kuhusu kile kilichowatokea,” anasema.
“Leo, baada ya kupigiwa simu kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa makaburi ya halaiki hapa, tumepata mabaki ya raia saba.”
Anaongeza kuwa taratibu zote muhimu zilitekelezwa “hivyo hapo baadaye tunaweza kuwabaini watu hao waliouawa”. Timu hiyo ni miongoni mwa idadi ndogo iliyofunzwa kukusanya taarifa na ushahidi wa kihalifu utakaotumiwa mahakamani.
Zaidi ya watu 100,000 wanadhaniwa kutoweka nchini Syria tangu 2011.
Katika wiki moja iliyopita, kundi la waasi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) – ambalo lilimuondoa Assad madarakani baada ya zaidi ya miaka 50 ya utawala wa familia yake – limefungua magereza na vituo vya kuzuia watu kote nchini Syria.
Kundi la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema makaburi hayo yanapaswa kulindwa na kuchunguzwa.
Katika eneo jingine la mji wa Qutayfah, kaskazini-magharibi mwa Damascus, jopo la dharura linasema maelfu ya miili inaaminika kuzikwa katika makaburi tofauti ya halaiki.
Mkaazi mmoja wa eneo hilo, ambaye alishuhudia miili ikizikwa katika miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, anasema ilikuwa imejaa kwenye makontena ya friji yaliyoletwa na vikosi vya usalama.
Ardhi ilitapakaa miili – na kisha eneo husika lingesawazishwa na tingatinga, aliambia BBC.
Video zilizohakikiwa zinavyoelezea jinsi kifo cha Igor Kirillov kilivyotokea

Maelezo kuhusu taarifa
- Author,Matt Murphy, Richard Irvine-Brown, Thomas Spencer & Joshua Cheetham
- Nafasi,BBC Verify
- Saa 4 zilizopita
BBC Verify imekuwa ikichambua video na picha kutoka mitandao ya kijamii kutoka Moscow ili kujaribu kupata uhalisia wa picha wazi zaidi ya mlipuko uliomuua Jenerali Luteni Igor Kirillov wa Urusi na msaidizi wake.
Vyanzo vya habari Ukraine vinasema walifanya shambulio dhidi ya kamanda huyo wa juu, ambaye ni mkuu wa vikosi vya nyuklia, biolojia na kemikali (NBC} , nchini Urusi tangu 2017.
Alikuwa amewekewa vikwazo na Uingereza mwezi Oktoba na akakosolewa kama “kasuku katika habari za kupotosha kuhusu Kremlin”.
Jenerali Luteni Kirillov alikuwa akiondoka katika jengo la kisasa la ghorofa katika sehemu ya kusini-mashariki ya Moscow mapema Jumanne wakati kifaa kilichofichwa kwenye skuta iliyoegeshwa kililipuka, kulingana na Kamati ya Uchunguzi ya Urusi – ambayo ni sawa kimamlaka na FBI ya Marekani.
Picha zilizothibitishwa na BBC Verify zinaonyesha watu wawili wakitoka kwenye jengo kabla ya mlipuko karibu na mlango.
Mavazi yao yana rangi ileile na yale ya maiti zilizopigwa picha baada ya mlipuko.
Skuta inaonekana ikiwa imeegeshwa kando ya mlango.
Hakuna kinachoonekana baada ya mlipuko, na picha zilizobaki zimefunikwa na vifusi kutoka kwa mlipuko.

Vyanzo vya habari mjini Kiev vinasema Ukraine imemuua jenerali wa Urusi Igor Kirillov, ambaye aliuawa katika mlipuko mjini Moscow mapema Jumanne
Katika video nyingine zilizochambuliwa na BBC Verify, mabaki ya skuta ya umeme yanaonekana yakiwa yameanguka kati ya vifusi na maiti mbili na mlango ulioharibiwa.
Picha ya karibu ya skuta, iliyothibitishwa kwa kulinganisha na vifusi, inaonyesha kuwa iko katika hali nzuri – isipokuwa sehemu ya usukani ambayo haionekani.
Wataalamu kutoka Janes – shirika la uchunguzi la binafsi linalotumia vyanzo wazi – waliliambia BBC Verify kwamba picha zinaonyesha kuwa mlipuko ulisababishwa na kilipuzi kilichotengenezwa kwa mkono (IED), badala ya silaha za kawaida.
“Kutoka kwa picha zilizopo za skuta, inaonekana kuwa bado iko kamili, hivyo athari inaonekana kuwa ni mivunjiko badala ya mlipuko mkubwa,” alisema msemaji wa shirika hilo.
IED ni aina ya bomu “lililotengenezwa nyumbani” ambalo linaweza kuwa la aina mbalimbali na mara nyingi linatengenezwa na vifaa rahisi vinavyoweza kupatikana – kama vile misumari, kioo au vipande vya chuma – kulingana na Idara ya Usalama ya Marekani.
David Heathcote, meneja wa ujasusi kutoka kwa wachambuzi wa usalama McKenzie Intelligence, pia alikubali kuwa kifaa hicho kilionekana kuwa IED.
“IED zinaweza kutengenezwa kwa makusudi ili kuonekana kama kitu cha kila siku ambacho hakionekani kuwa cha ajabu,” aliiambia BBC Verify. “Katika kisa hiki inaonekana kuwa kifaa kilifichwa ndani ya skuta, pengine kama kilipuzi kinachotumiwa na jeshi (lakini sio lazima) Semtex, badala ya kilipuzi cha kutengezewa nyumbani.”
Aliongeza kuwa shambulio hilo linaonyesha “nguvu ya hali ya juu na linaweza kuwa limetayarishwa kwa miezi kadhaa,” jambo ambalo lingehitaji “angalizo kubwa la mtu anayelengwa kabla ya shambulio.”
Vyombo vya habari vya Urusi vimekuwa vikiripoti kuwa bomu lilikuwa limefungwa kwenye usukani wa skuta.

Pia vyanzo vimeripoti, wakinukuu vyanzo vya vyombo vya usalama, kwamba mlipuko ulitengenezwa kwa kutumia njia ya kudhibiti kwa mbali.
Heathcote alikubaliana na tathmini hiyo, akisema kuwa ishara ya redio kutoka kwa simu au kifaa cha gari ingeweza kuwa kigezo cha mlipuko.
“Aliyetekeleza shambulizi atalazimika kuweka macho kwenye kifaa na atabonyeza kitufe ili kuanzisha mlipuko wakati mlengwa halali yupo karibu,” aliiambia BBC Verify. “Ukaribu wa shambulio na kifaa unategemea ukaribu wa transimita inayotumika.”
Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilisema mwanzoni kuwa Kifaa hicho kililipuka kwa mbali na kilikuwa na milipuko yenye uzito wa gramu 300, kisha baadaye kurekebisha takwimu hiyo hadi kilo 1, wakinukuu data kutoka kwa vyombo vya usalama.
Aliyeshuhudia mlipuko huo ameonyesha vyombo vya habari vya Urusi picha za kile alichosema ni vifusi vya mlipuko vilivyokuwa vimeanguka kwenye ghorofa yake inayozunguka mtaa wa tukio.
BBC Verify inaonyesha hizi kwa wataalamu wa silaha ili kusaidia kubaini kama vinaweza kuwa vimetoka kwa kifaa hicho.
Kwa mujibu wa wawekezaji, jengo la ghorofa alikouawa Jenerali Luteni Kirillov ni jipya na lilimalizika mwaka 2019.
Ghorofa hizo ni za kiwango cha juu, na baadhi zinapatikana kwa takribani paundi 153,540 mtandaoni.
Katika video zilizothibitishwa na BBC, kundi dogo linaonekana likikusanyika karibu na maiti, ambazo ziko kwenye eneo lililojaa theluji.
Magari ya huduma za dharura pia yanaonekana kwenye video.
Video zote mbili zilirekodiwa kwenye mtaa ukielekea kaskazini kuelekea Ryazansky Prospekt, Moscow, na kuibuka kwenye mitandao ya kijamii asubuhi ya Jumanne.
Zinaonyesha uharibifu katika mlango wa jengo, ikiwa ni pamoja na matofali kutawanyika na milango iliyofunguka, umbali kidogo kutoka kwa maiti.
Video nyingine imeonyesha mng’ao mkali kidogo kutoka kwenye kamera.
Nguvu ya mlipuko ilivunja theluji kutoka kwa magari yaliyoegeshwa karibu na jengo hilo.
Takriban ghorofa 10 nyingine kwenye mtaa huo wa mkasa zimeathiriwa na mlipuko, haya ni kwa mujibu wa mtandao wa Telegram wa Urusi Mash.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.