Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamoja
Muhtasari
- Ukraine yakiri kumuua Jenerali wa kikosi cha nyuklia wa Urusi
- Jaji akataa hoja ya Trump ya kutaka atupilie mbali kesi aliyopatikana na hatia
- Wanadiplomasia wa Uingereza wakutana na kiongozi wa waasi mjini Damascus
- Tundu Lissu adai ‘wasiojulikana’ wanapanga njama za kumdhuru
- Wanajeshi wa Korea Kaskazini waliuawa wakipigana na Ukraine – Marekani
- Jenerali wa Urusi auawa katika mlipuko mjini Moscow
- Isabel dos Santos apinga vikwazo alivyowekewa Uingereza
- Watu wawili wauawa na mwanafunzi wa kike Marekani
- Athari za kimbunga huko Mayotte ni kama matokeo ya vita vya nyuklia – wakaazi
- Iran yasitisha sheria mpya yenye utata ya mavazi
- Assad asema hakuwa na nia ya kuondoka Syria – taarifa inadai
- Takribani watu 34 wamekufa Msumbiji kufuatia kimbunga Chido
- DR Congo inaituhumu Apple kwa kutumia madini yanayochimbwa katika maeneo ya mizozo
- Maafisa wa Urusi wailaumu Magharibi kwa mauaji ya Kirillov na kusema ni kitendo cha kigaidi
- Mwanafunzi wa darasa la pili apiga simu polisi kuripoti shambulio la shule
- Taarifa nyeti zavuja baada ya udukuzi wa mtandao wa simu Namibia
- Barua iliowasili baada ya miaka 100 kwa aliyeandikiwa
- Wahamiaji walizuiliwa kinyume cha sheria na Uingereza, jaji aeleza
- “Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yako katika hatua ya mwisho,” – mpatanishi
- Ronaldo kugombea urais wa shirikisho la sola la Brazil
Naam,Natumai U buheri wa afya popote pale ulipo duniani kwa mwoyo mkunjufu na mikono miwili Hujambo na karibu katika matangazo yetu Afrika Leo Jioni ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 17/12/2024 Jina langu ni Cantona Joseph,karibu.

Iran yasitisha sheria mpya yenye utata ya kanuni za mavazi

Baraza la Usalama la Taifa la Iran limesitisha utekelezaji wa “sheria ya hijabu na kutokuwa na mahusiano yoyote ya ngono kabla ya ndoa,” ambayo ilikuwa ianze kutekelezwa siku ya Ijumaa.
Rais Massoud Pezeshkian aliita sheria hiyo “yenye utata na inayohitaji marekebisho”, akiashiria nia yake ya kutathmini upya hatua zake.
Sheria mpya iliyopendekezwa – ambayo ingeleta adhabu kali zaidi kwa wanawake na wasichana kwa kutofunika nywele zao, kuonyesha mapaja au sehemu ya chini ya miguu – ilikuwa imekosolewa vikali na wanaharakati wanaotetea haki za kibinadamu.
Kanuni kali za mavazi zilizowekwa kwa wanawake na wasichana, ambazo zimechukuliwa kama kipaumbele cha usalama wa taifa na watawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa miongo kadhaa, zilisababisha maandamano siku za nyuma.
Chini ya sheria hiyo mpya, wahalifu wanaorudia makosa na yeyote aliyekejeli sheria hizo atakabiliwa na faini kubwa zaidi na kifungo cha muda mrefu cha hadi miaka 15 jela.
Pia inaamuru kwamba biashara ziripoti mtu yeyote anayekiuka sheria.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalionyesha wasiwasi wake.
Amnesty International ilisema mamlaka za Irani “zinatafuta kuimarisha mfumo wa ukandamizaji ambao tayari unakera wengi”.
Wakati wa uchaguzi wa rais mwezi Julai, mgombea wa wakati huo Pezeshkian alikosoa waziwazi jinsi wanawake wa Iran wanavyotendewa kuhusu suala la kuvaa hijabu.
Aliahidi kutoingilia maisha yao ya kibinafsi, msimamo ambao uliwagusa Wairani wengi, haswa kutoka kwa kizazi kipya kilichokatishwa tamaa na udhibiti mkali wa serikali.
Mvutano unaozingira vazi la Hijabu umeendelea kuwa mkubwa tangu maandamano ya nchi nzima mwaka 2022 yaliyochochewa na kifo cha Mahsa “Zhina” Amini, msichana wa Kikurdi aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kuzuiliwa kwa madai ya kukiuka kanuni za mavazi.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, vijana wengi wa kike wa Kiirani wamevua hijabu zao kwa ukaidi hadharani, wakipinga mamlaka ya serikali.
Athari za kimbunga huko Mayotte ni kama matokeo ya vita vya nyuklia – wakaazi

Wakaazi wa eneo laMayotte wamezungumza juu ya “athari za kimbunga” kibaya zaidi katika miaka 90 ambacho kilipiga eneo la Bahari ya Hindi ya Ufaransa.
Kimbunga Chido kiliwasili kwa kasi ya upepo zaidi ya 225km/h (140mph), katika maeneo yenye tambarare ambapo wengi wanaoishi huko wanakumbwa na lindi la umaskini.
“Hatujapata maji kwa siku tatu sasa,” mkazi mmoja wa mji mkuu wa Mamoudzou alisema. “Baadhi ya majirani zangu wana njaa na kiu,” mwingine alisema.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema atasafiri hadi Mayotte “katika siku zijazo”, huku akiahidi kusaidia raia wake, wafanyikazi wa umma na huduma za dharura zinazohusika katika juhudi za uokoaji.
Watu wawili wauawa na mwanafunzi wa kike kwa kupigwa risasi katika shule ya Kikristo Marekani

Mwanafunzi mmoja amefyatua risasi katika shule ya kibinafsi ya Kikristo katika jimbo la Wisconsin Marekani, na kujeruhi watu sita na kumuua mwalimu na mwanafunzi kijana.
Mkuu wa Polisi wa Madison Shon Barnes alimtaja mshambuliaji huyo Jumatatu usiku kuwa mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 15 katika shule hiyo.
Mamlaka inasema mshambuliaji huyo alikuwa shule ya Abundant Life Christian School kabla ya kufyatua risasi na alikutwa amefariki katika eneo la tukio.
Wanafunzi sita walijeruhiwa, wakiwemo wawili waliopata majeraha yanayo tishia maisha yao.
Mwanafunzi wa gredi ya pili alikuwa wa kwanza kupiga simu, kulingana na Mkuu wa Polisi Barnes.
“Leo ni siku ya huzuni sio tu kwa Madison, kwa nchi yetu yote,” Barnes alisema.
Aliongeza kuwa polisi hawajabaini sababu za tukio hilo la ufyatuaji risasi, na familia ya mshukiwa ilikuwa ikishirikiana na uchunguzi.
Alisema bado haijabainika jinsi mshambuliaji huyo alipata bunduki.
Hata hivyo, matukio ya ufyatuaji risasi kwa wingi na wanawake ni nadra na ufyatuaji risasi shuleni unaofanywa na washambuliaji wa kike ni vigumu sana kutokea.
Isabel dos Santos apinga vikwazo vya Uingereza alivyowekewa

Tajiri wa Angola Isabel dos Santos, aliyewahi kutajwa kuwa “mwanamke tajiri zaidi barani Afrika”, ameikashifu Uingereza kwa kumuwekea vikwazo, akiambia BBC kuwa hatua hiyo ilishangaza kwani hajapatikana na hatia ya “ufisadi wowote katika mahakama yoyote kwenye nchi yoyote”.
Mwezi uliopita, binti wa rais wa zamani wa Angola alielezewa na serikali ya Uingereza kama “anayetumia mamlaka yake kuiba rasilimali za nchi yao” na mali yake ikashikiliwa na kupigwa marufuku ya kusafiri kwa madai ya kupora mali kutoka kwa nchi ya Angola yenye utajiri wa mafuta.
Alisema serikali ya Angola ilikuwa nyuma ya kampeni ya kumharibia jina.
“Mwisho wa siku hili ni suala la kisiasa,” Dos Santos, 51, aliambia podikasti ya BBC Africa Daily kutoka makao yake huko Dubai.
“Hakukuwa na uchunguzi, ambapo mtu alikuja na kuchunguza na kuangalia ushahidi au kunitaka nifafanue. Hakukuwa na utaratibu,” alisema.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy alitangaza vikwazo kwa Dos Santos kama sehemu ya kampeni yake ya kukabiliana na “fedha chafu”.
Taarifa ya serikali ilidai kuwa “ametumia vibaya nafasi zake katika kampuni zinazoendeshwa na serikali kwa ubadhirifu wa angalau £350m [$442m], na kuinyima Angola rasilimali na ufadhili wa miradi ya maendeleo yanayohitajika sana”.
Msemaji wa mwanasheria mkuu wa Angola alisema hawatajadili maelezo yoyote ya kisheria yanayoendelea hadharani lakini akasema kwamba ushahidi wowote wa kuwa nyaraka zilighushiwa zinapaswa kuwasilishwa mahakamani.
Iwapo atarejea Angola, pia anaweza kukamatwa – kwa amri ya serikali, Interpol imetoa hati ya ombi la kukamatwa kwake, hata hivyo si hati ya kimataifa ya kukamatwa.
Dos Santos amesema baada ya miaka hii migumu na mali zake kuzuiliwa, sasa anataka watu wasikie upande wa simulizi yake “tata” “kwa matumaini ya kuanza kufafanua dhana potofu zilizopo”.
Jenerali wa Urusi auawa katika mlipuko mjini Moscow

Jenerali wa ngazi za juu katika jeshi la Urusi ameuawa katika mlipuko uliotokea mjini Moscow.
Luteni Jenerali Igor Kirillov, mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Nyuklia, Biolojia, Kemikali (NBC), alikuwa akiondoka kwenye makazi yake mapema Jumanne wakati kifaa kilichofichwa kwenye skuta kilipolipulika, Kamati ya Uchunguzi ya Urusi ilisema.
Iliongeza kuwa msaidizi wa Kirillov pia aliuawa.
Mnamo mwezi Oktoba, Uingereza iliweka vikwazo kwa Kirillov, ikisema alikuwa amesimamia matumizi ya silaha za kemikali nchini Ukraine na alikuwa kiungo muhimu kama “msemaji wa habari za Kremlin”.
Siku ya Jumatatu, idara ya siri ya Ukraine, SBU, ilimfungulia mashtaka bila kuwepo mahakamani, ikisema kwenye Telegram “alihusika na matumizi makubwa ya silaha za kemikali zilizopigwa marufuku”.
Kamati ya Uchunguzi, mamlaka kuu ya uchunguzi ya Urusi, ilisema “imefungua kesi ya jinai ya mauaji ya wanajeshi wawili”.
“Wataalam wa uchunguzi na huduma za uendeshaji wapo katika eneo la tukio,” ilisema.
“Hatua za uchunguzi na shughuli za upekuzi zinafanywa kwa lengo la kubaini hali zote za uhalifu.”
Wanajeshi wa Korea Kaskazini waliuawa wakipigana na Ukraine – Marekani

Wanajeshi wa Korea Kaskazini wameuawa wakipambana na vikosi vya Ukraine katika eneo la mpaka la Kursk nchini Urusi, Marekani imesema.
Haya yatakuwa majeruhi ya kwanza kuripotiwa tangu ilipojulikana mwezi Oktoba kwamba Korea Kaskazini ilituma takriban wanajeshi 10,000 ili kuimarisha juhudi za vita vya Urusi.
Shirika la kijasusi la kijeshi la Ukraine, GUR, limesema takriban wanajeshi 30 wa Korea Kaskazini wameuawa au kujeruhiwa katika mapigano mwishoni mwa juma.
BBC haijathibitisha madai hayo kwa uhuru.
Wanajeshi wa Korea Kaskazini – ambao hawana uzoefu wa vita – wanaaminika walitumia wiki zao za kwanza baada ya kutumwa Urusi katika mafunzo na kisha katika majukumu ya usaidizi.
Siku ya Jumamosi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Urusi imeanza kutumia “idadi kubwa” ya wanajeshi hao katika mashambulio yake huko Kursk, sehemu ambayo Ukraine imeiteka tangu ilipoanzisha uvamizi wa ghafla mwezi Agosti.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, katibu wa vyombo vya habari wa Pentagon Meja Jenerali Pat Ryder alisema kuwa Marekani inaamini kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini “wameshiriki katika mapigano huko Kursk pamoja na vikosi vya Urusi” na “wamepata hasara, wote wakiuawa na kujeruhiwa”.
Hakutoa idadi maalum, ingawa alisema wanajeshi hao walikuwa kwenye mapigano tangu “zaidi ya wiki moja iliyopita”.
Tundu Lissu adai ‘wasiojulikana’ wanapanga njama za kumdhuru

Naibu mwenyekiti wa Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA Tundu Lissu amedai kuwa ‘watu wasiojulikana’ wanapanga kumdhuru wakati ambapo chama hicho kinakaribia kufanya uchaguzi wa mwenyekiti.
Katika chapisho lake la mtandao wa X jana usiku, Lissu amesema kwamba ‘watu wasiojulikana’ wanapanga kumdhuru halafu badala yake wamsingizie mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kuwa ndiye aliyetekeleza shambulio dhidi yake.
Amesema kwamba watu hao wamekuwa wakitekeleza mauaji kwa watu wasio na hatia kisha, wanasingizia watu wengine ili waliohusika wasiwajibike na udhalimu walioufanya.
‘’Enyi watu wabaya mjulikanao kama watu wasiojulikana, nimezisikia njama zenu. Mnataka kuniumiza halafu mumsingizie Mwenyekiti wetu wa chama,’’ ameandika Lissu.
CHADEMA inaelekea kwenye kilele cha uchaguzi wa ndani wa chama hicho huku Lissu akitazamiwa kuchuana na Mbowe kwenye nafasi ya juu zaidi ya chama hicho, na tayari jambo hilo limezua gumzo na hata nyufa baina ya wafuasi wa kambi za Lissu na Mbowe.
‘’Ndivyo mlivyofanya wakati wa kifo cha marehemu Chacha Wangwe. Ndivyo mlivyofanya tena wakati mliponishambulia tarehe 7 Septemba 2017 na ndivyo mlivyofanya miezi michache iliopita mlipomteka nyara na kumuua Mzee Ali Mohamed kibao‘’, alisema Tundu Lissu katika chapisho hilo la mtandao wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter.
Mwaka 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya makazi yake mjini Dodoma alipokuwa akihudhuria vikao vya Bunge.
Lissu alilizimika kukimbizwa Nairobi, Kenya na baadae Ubelgiji kwa matibabu. Lissu amesalia na ulemavu wa kudumu kutokana na shambulio hilo.
Hakuna mtu aliyekamatwa wala kufunguliwa mashtaka kutokana na shambulio hilo huku Lissu mwenyewe akiilaumu serikali ya utawala wa hayati John Magufuli kwa kutekeleza shambulio hilo, tuhuma ambazo serikali ya Tanzania imezikanusha.
Lissu alisalia ughaibuni baada ya matibabu yake kwa kuhofia usalama wake na alirejea Tanzania mwaka 2020 kugombea urais na Magufuli.
Mara baada ya uchaguzi Lissu alikimbia tena Tanzania huku akitoa shutuma kuwa kuna mipango ya kushambuliwa tena.
Lissu alirejea Tanzania baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani na alisema kuwa amepatiwa hakikisho la usalama wake.
Wanadiplomasia wa Uingereza wakutana na kiongozi wa waasi mjini Damascus

Wanadiplomasia wa Uingereza wamefanya mazungumzo na kiongozi wa kundi la waasi la Syria Hayat Tahrir al-Sham (HTS), kufuatia kumwondoa madarakani rais Bashar al-Assad zaidi ya wiki moja iliyopita.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na idara ya operesheni za kijeshi za kundi hilo zilionyesha kiongozi wa HTS Ahmad al-Sharaa – ambaye zamani alijulikana kama Mohammed al-Golani – akikutana na maafisa wakuu katika mji mkuu wa Syria, Damascus.
Miongoni mwa waliopigwa picha pamoja naye ni Ann Snow, mwakilishi maalum wa Uingereza kwa Syria.
HTS ilisema wajumbe walijadili “matukio ya hivi punde” nchini Syria.
Al-Sharaa pia alifanya mahojiano na gazeti la Times ambapo alitoa wito kwa nchi za Magharibi kuondoa vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi ya Syria chini ya utawala wa Assad – ikiwa ni pamoja na kutambuliwa kwa HTS kama shirika la kigaidi.
“Wanapaswa kuondoa vikwazo vyote, ambavyo viliwekwa kwa mhusika na mwathiriwa – mhusika hayupo tena kwa sasa. Suala hili haliko kwa ajili ya mazungumzo,” alisema.
Jaji akataa hoja ya Trump ya kutaka atupilie mbali kesi aliyopatikana na hatia

Jaji wa mahakama ya New York ameamua kuwa hatia aliyopatikana nayo Donald Trump katika kesi ya kutoa pesa za kutunza siri ni halali, amekataa hoja ya rais mteule kwamba hatia hiyo inapaswa kutupiliwa mbali kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Marekani juu ya kinga aliyonayo.
Mwezi Julai, mahakama ya juu ya nchi hiyo iliamua kwamba marais wana kinga dhidi ya mashtaka ya jinai kwa maamuzi rasmi wanayochukua wakiwa madarakani.
Lakini siku ya Jumatatu, Jaji katika jiji la Manhattan jimboni New York, Juan Merchan – ambaye aliongoza kesi ya Trump – aliwaunga mkono waendesha mashitaka, akisema hukumu juu ya makosa 34 ya uhalifu iko kwenye maamuzi ya Trump yasiyo rasmi.
Uamuzi huo wa kutiwa hatia, ikiwa utadumu utamuweka Trump katika historia ya kuwa mhalifu wa kwanza kuhudumu katika Ikulu ya White House.
Katika uamuzi wake wa kurasa 41, Jaji Merchan alikataa hoja za Trump, akisema ushahidi ulioonyeshwa kwenye kesi hii ulihusu “mienendo isiyo rasmi,” aliandika.
Jaji alibainisha kuwa katika uamuzi wa Mahakama ya Juu imegundua kuwa “si kila kitu anachofanya rais ni rasmi,” hata kama kinafanywa kutoka Ikulu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, msemaji wa Trump, Steven Cheung, alikosoa uamuzi huo na kuutaja kuwa “ukiukaji wa moja kwa moja wa uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu kinga ya rais.”
Mwezi Mei, jaji wa New York alimpata Trump na hatia ya kughushi rekodi za biashara.
Hatia hiyo ilitokana na jaribio la Trump la kuficha malipo yaliyofanywa na wakili wake wa zamani, Michael Cohen, ambaye mwaka 2016 alimlipa nyota wa filamu za ngono ili asitoboe siri ya kufanya ngono na Trump.
Trump amekana makosa yote.
“Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yako katika hatua ya mwisho,” – mpatanishi

Baada ya miezi kadhaa ya mkwamo, kuna dalili mpya kwamba Israel na Hamas wanaweza kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuwaachilia huru mateka.
Afisa mkuu wa Palestina anayehusika katika mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja aliambia BBC, mazungumzo yako katika “hatua ya mwisho.”
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, pia amesema makubaliano yako karibu zaidi kuliko hapo awali.
Katika wiki za hivi karibuni, Marekani, Qatar na Misri zimerudisha juhudi zao za upatanishi – zikiripoti utayari mkubwa wa pande zote mbili baada ya vita vya zaidi ya mwaka.
Afisa huyo wa Palestina alielezea kuna mpango wa awamu tatu ambao utashuhudia raia na wanajeshi wanawake wanaoshikiliwa mateka huko Gaza wakiachiliwa huru katika siku 45 za kwanza, na vikosi vya Israel vikijiondoa katikati ya miji, barabara ya pwani na ukanda wa kimkakati kwenye mpaka na Misri.
Kutakuwa na utaratibu kwa watu wa Gaza waliokimbia makazi yao kuweza kurejea kaskazini mwa eneo hilo, amesema afisa huyo.
Hatua ya pili itashuhudia mateka waliosalia wakiachiliwa na wanajeshi kuondolewa kabla ya hatua ya tatu kumaliza vita. Kati ya mateka 96 ambao bado wanashikiliwa huko Gaza, Israel inaamini 62 bado wako hai.
Mpango huo unaonekana kutegemea mpango ambao Rais wa Marekani Joe Biden alioutoa tarehe 31 Mei.
Ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani mwezi Novemba umetoa msukumo mpya kwa juhudi za kidiplomasia.
Katika mkutano na wanahabari siku ya Jumatatu, alionya tena kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yanapaswa kufikiwa kabla ya kuchukua madaraka.
Wahamiaji walizuiliwa kinyume cha sheria na Uingereza, jaji aeleza

Wahamiaji wa jamii ya Sri Lankan Tamil walizuiliwa kinyume cha sheria kwa miaka mingi katika eneo la milki ya Uingereza la Diego Garcia, jaji ameamua.
Mwaka 2021, makumi ya watu hao walikuwa watu wa kwanza kupata hifadhi kwenye kisiwa cha Bahari ya Hindi, ambacho ni eneo la siri la jeshi la Uingereza na Marekani.
Walizuiliwa kwa miaka mingi katika kambi ndogo iliyozungushiwa uzio, kabla ya kupelekwa nchini Uingereza mapema mwezi huu katika kile ambacho serikali ilieleza ni uamuzi kwa maslahi ya ustawi wao.
Wakiwa katika kisiwani hicho, Watamil, wakiwemo watoto 16, waliwekwa katika mahema ya kijeshi katika kambi yenye uzio, ambayo ilikuwa inalindwa kila wakati na kampuni ya ulinzi ya binafsi ya G4S.
“Ni kama gereza la wazi – hatukuruhusiwa kutoka nje, tulikuwa tukiishi kwenye uzio na kwenye hema,” mwanamke mmoja aliambia BBC baada ya kupelekwa nchini Uingereza akiwa na mumewe na watoto wawili mwezi huu.
Kulikuwa na mgomo wa kula mara nyingi na matukio mengi ya kujidhuru na kujaribu kujiua ili kukabiliana na hali ngumu katika kambi hiyo, ambapo baadhi ya watu walihamishiwa Rwanda kwa matibabu.
Pia kulikuwa na kesi na madai ya unyanyasaji wa kijinsia na bugudha ndani ya kambi kutoka kwa wahamiaji wengine, zikiwemo kesi dhidi ya watoto
Margaret Obi, kaimu jaji wa mahakama kuu ya Biot, amesema katika uamuzi wake siku ya Jumatatu kwamba kambi hiyo ni gereza na “imekuwa gereza tangu mwanzo.”
BBC imeelezwa kuwa kambi hiyo sasa imefungwa lakini wanaume wawili walio na hatia ya uhalifu na mwingine anayechunguzwa wamesalia huko Diego Garcia.
Uingereza ilichukua udhibiti wa Visiwa vya Chagos kutoka koloni yake ya wakati huo, Mauritius, 1965 na kuwafurusha wakazi wake zaidi ya watu 1,000 ili kujenga kambi za jeshi.
Hukumu hiyo inakuja baada ya Uingereza kukubali mapema mwaka huu kukabidhi visiwa hivyo kwa Mauritius. Chini ya mkataba huo, ambao bado haujatiwa saini, Diego Garcia itabaki kuwa na kambi ya kijeshi ya Uingereza-Marekani lakini Mauritius itawajibika kwa wahamiaji wowote watakao kuja.
Barua ya posta yapelekwa Uingereza kimakosa badala ya Australia

Mwanaume mmoja amepigwa na butwaa baada ya barua kufika kwenye mlango wake ambayo ilipaswa kuwasilishwa umbali wa zaidi ya maili 10,500 huko Australia.
Keith Georgiou kutoka Penarth, Vale of Glamorgan, Wales, Uingereza, alipoichukua barua hiyo, alitambua ilipaswa kutumwa kwenda anwani huko Penrith, katika jimbo la New South Wales, Australia.
Kampuni ya kutuma barua za posta ya Royal Mail inasema makosa ya namna hiyo ni nadra lakini hutokea.
Bw Georgious alipokea barua hiyo mwishoni mwa juma. “Jinsi ilivyofika Penarth badala ya kufika Australia ni kichekesho,” amesema mzee huyo wa miaka 60.
Jambo la kushangaza ni kwamba si mara ya kwanza kwa Georgiou kupokea barua ambayo ilipaswa kwenda Australia, lakini amesema hii ya wiki hii ni ya ajabu, kutokana na habari kwamba hivi karibuni kampuni hiyo ilipigwa faini ya pauni milioni 10.5 kwa kosa kama hilo.
Georgiou ameituma barua hiyo tena – na kuandika kinotisi juu yake kuiarifu Royal Mail juu ya kosa hilo.
“Natumai haitarudi hapa!” amesema.
Royal Mail imesema: “Tunawasilisha hadi barua milioni 35 kwa siku. Inaonekana katika tukio hili barua iliyoelekezwa kwenda Penrith imesomwa kimakosa kama Penarth.”
Taarifa nyeti zavuja baada ya udukuzi wa mtandao wa simu Namibia

Kampuni ya simu inayomilikiwa na serikali ya Namibia imeshambuliwa na wadukuzi waliotaka kikombozi na kusababisha uvujaji wa taarifa nyeti za wateja, ikiwa ni pamoja na taarifa kuhusu maafisa wakuu wa serikali.
Telecom Namibia inasema taarifa hizo zimevujishwa baada ya kukataa kuzungumza na kundi la wadukuzi wanaojulikana kama Hunters International.
Kampuni hiyo inasema kwa sasa inachunguza jinsi udukuzi huo ulivyotokea.
Rais anayemaliza muda wake Nangolo Mbumba amelaani udukuzi huo.
Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba wadukuzi waliiba karibu taarifa 500,000 ikiwa ni pamoja na taarifa binafsi na za kifedha za wizara, maafisa wakuu wa serikali na wateja wengine wa kampuni.
Katika taarifa ya Jumatatu, Telecom Namibia ilisema iligundua Ijumaa iliyopita kwamba baadhi ya taarifa za wateja wake zimevujishwa kwenye mtandao.
Mtendaji mkuu wa kampuni, Stanley Shanapinda alisema wadukuzi hao waliziweka hadharani taarifa walizoiba baada ya Telecom Namibia kusema haiko tayari kujadiliana nao kuhusu fidia iliyotakiwa.
Taarifa nyeti za mteja, ni pamoja na maelezo ya kitambulisho binafsi, anwani, na taarifa za benki zinasemekana kuvuja na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kampuni hiyo imewataka wateja kubadilisha nywila kwenye simu zao binafsi na kuepuka kuhamisha pesa katika mazingira ya kutiliwa shaka.
Mwanafunzi wa darasa la pili apiga simu polisi kuripoti shambulio la shule

Polisi katika jimbo la Wisconsin nchini Marekani wanasema simu ya dharura waliyopokea kutokana na shambulio la risasi katika shule siku ya Jumatatu ilitoka kwa mtoto asiyezidi umri wa miaka saba au minane.
Mwanafunzi na mwalimu walipigwa risasi na kufa na wengine sita kujeruhiwa katika shule binafsi ya Kikristo na msichana wa miaka 15, aliyetajwa na mamlaka kama Natalie Rupnow. Mshambulizi huyo ambaye alisoma shule hiyo pia alikutwa amefariki akiwa na bastola.
Mkuu wa polisi katika jiji la Madison, Shon Barnes amesema mtoto aliyepiga simu polisi anasoma darasa la pili.
Nia ya mshambuliaji huyo bado haijabainika. Waathiriwa bado hawajatajwa majina, na pia mtoto ambaye alitoa taarifa kwa polisi.
Mshambulizi huyo anaaminika kufariki kutokana na kujipiga risasi. Hakuna maafisa waliofyatua risasi.
Shule hiyo, ambayo ina wanafunzi wapatao 400 kutoka chekechea hadi sekondari, bado imefungwa wakati huu wa uchunguzi.
Maafisa wa Urusi wailaumu Magharibi kwa mauaji ya Kirillov na kusema ni kitendo cha kigaidi

Maafisa wa Urusi wamezishutumu nchi za Magharibi kwa kupanga mauaji ya Luteni Jenerali Igor Kirillov, wakisema ni kutokana na jukumu lake la “kufichua uhalifu wa Waanglo-Saxon.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Jimbo la Duma, Andrei Kartapolov, ameapa kuwatafuta na kuwaadhibu “wale waliohusika kuandaa na kutekeleza” mauaji ya Kirillov “bila kujali ni nani au wako wapi.”
Kwenye Telegram, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova ameandika, Kirillov “alitumia miaka mingi kufichua uhalifu wa Waanglo-Saxons.”
Jenerali mstaafu wa jeshi Andrei Gurulyov anasema, Kirillov ni mtu “aliyeelewa na kufuatilia shughuli zote za uhalifu za Marekani na satelaiti zake, ikiwa ni pamoja na maabara zao za uhalifu na silaha za kemikali na za kibaiolojia.”
Uingereza ilimtaja Kirillov mwezi Oktoba, ikimwita “msemaji muhimu wa habari za Kremlin, akieneza uwongo ili kuficha tabia hatari za Urusi.”
Kamati ya uchunguzi ya Urusi imeelezea mauaji ya Luteni Jenerali Kirillov kuwa ni “kitendo cha kigaidi.”
Msemaji Svetlana Petrenko anasema: “Tukio hilo limeainishwa kama kitendo cha kigaidi, mauaji, usafirishaji haramu wa silaha.”
Tazama: video fupi Jenerali wa Urusi auawa kwa bomu katika jengo la makazi la Moscow

Jenerali wa Urusi anayesimamia vikosi vya ulinzi wa nyuklia nchini humo ameuawa katika mlipuko uliotokea mjini Moscow.
Luteni Jenerali Igor Kirillov alikuwa akitoka kwenye makazi siku ya Jumanne wakati kifaa kilichofichwa kwenye skuta kilipozimika.
Bomu hilo lilitekelezwa kwa mbali na lilikuwa na takriban gramu 300 za vilipuzi, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimeripoti.
DR Congo inaituhumu Apple kwa kutumia madini yanayochimbwa katika maeneo ya mizozo

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imewasilisha malalamiko ya uhalifu nchini Ufaransa na Ubelgiji dhidi ya kampuni tanzu ya kampuni kubwa ya teknolojia ya Apple, ikiituhumu kutumia madini yanayochimbwa katika maeneo ya migogoro.
Wakifanya kazi kwa niaba ya serikali ya Congo, mawakili wamedai Apple inashiriki katika uhalifu unaofanywa na makundi yenye silaha ambayo yanadhibiti baadhi ya migodi mashariki mwa DR Congo.
Katika ukaguzi wake wa 2023 wa suala hilo, Apple ilisema inafuatilia chanzo cha madini hayo na kuboresha hatua za kufuatilia.
Mamlaka nchini Ufaransa na Ubelgiji sasa zitaangalia iwapo kuna ushahidi wa kutosha kuchukua hatua za kisheria.
Katika taarifa ya mawakili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanadai kuwa madini ya bati, tantalum na tungsten huchukuliwa kutoka maeneo yenye migogoro na kisha “hutakatishwa kupitia minyororo ya kimataifa ya ugavi.”
“Shughuli hizi zimechochea ghasia na migogoro kwa kufadhili wanamgambo na vikundi vya kigaidi na zimechangia ajira za kulazimishwa za watoto na uharibifu wa mazingira.”
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni chanzo kikuu cha uchimbaji wa madini na hilo limechochea vita huko kwa miongo kadhaa.
Mashirika ya haki za binadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakidai kuwa kiasi kikubwa cha madini kutoka kwenye migodi halali, pamoja na migodi inavyoendeshwa na makundi yenye silaha, husafirishwa hadi nchi jirani ya Rwanda na kuishia kwenye simu na kompyuta zetu.
Takribani watu 34 wamefariki Msumbiji kufuatia kimbunga Chido

Takriban watu 34 wamekufa kufuatia “dhoruba kali zaidi kuwahi kurekodiwa” kaskazini mwa Msumbiji, imesema Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Majanga (INGD).
Kimbunga Chido kilitua Msumbiji siku ya Jumapili, baada ya kusababisha uharibifu katika eneo la Bahari ya Hindi na kisiwa cha Mayotte.
Mamia wanahofiwa kufariki huko Mayotte – na watu kadhaa – ikiwa ni pamoja na zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 200 wa Msalaba Mwekundu – wanadhaniwa kupotea.
INGD inaonya kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka. Zaidi ya familia 34,000 za Msumbiji zimepoteza makazi yao, baada ya kimbunga cha upepo wa kasi ya karibu kilomita 260 kwa saa kupiga.
Shule, vituo vya afya na boti za uvuvi vimeharibiwa. Wengi wa waliouawa na Chido waligongwa na vitu vilivyokuwa vikianguka, kama vile kuta, amesema msemaji wa INGD Paulo Tomas.
Umeme na mawasiliano pia vimeathirika – kampuni ya umeme inayomilikiwa na serikali ya Electricidade de Moçambique (EDM) imetangaza kuwa karibu wateja 200,000 hawana nishati hiyo.
Mwaka jana Msumbiji ilipigwa na Kimbunga Freddy, mojawapo ya dhoruba zilizodumu kwa muda mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa katika kizio cha Kusini cha dunia, kama si dunia nzima.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani lilisema zaidi ya 180 nchini humo walikufa.
KIPENGA CHA MICHEZO.
Ronaldo kugombea urais wa shirikisho la soka Brazil

Gwiji wa Brazil, Ronaldo Luís Nazário de Limaametangaza atawania kiti cha urais katika chama cha soka cha nchi hiyo na anataka “kurudisha heshima” ya timu ya taifa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 48, atagombea kuchukua nafasi ya rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) Ednaldo Rodrigues.
Brazil, ambayo ina rekodi ya kushinda mara tano Kombe la Dunia, ilishinda kombe hilo mara ya mwisho mwaka 2002 na haijasonga mbele zaidi ya hatua ya robo fainali tangu wakati huo.
“Miongoni mwa mamia ya mambo yanayonipa motisha kuwa mgombea wa urais wa CBF ni kurejesha heshima ambayo timu ya taifa imekuwa nayo siku zote na hakuna mtu mwingine aliye nayo leo,” amesema.
Muhula wa Rodrigues utaendelea hadi Machi 2026 na uchaguzi wa urais lazima ufanyike katika miezi 12 kabla ya wakati huo.
Ronaldo, mshindi wa Kombe la Dunia mwaka 1994 na 2002, anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa kombe la dunia nyuma ya Miroslav Klose wa Ujerumani aliyefunga mabao 15 katika mechi 19 alizocheza.
Maisha ya soka ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid yalidumu kwa miaka 17 na kujumuisha mataji mawili ya Copa America na medali ya shaba ya Olimpiki.
Brazil wameshinda Copa America mara moja tangu Ronaldo alipostaafu kimataifa mwaka 2011 na kutolewa nje ya Kombe la Dunia la 2022 na Croatia katika robo fainali.
Je wajua ? Fahamu watu 14 wenye utajiri mkubwa zaidi duniani- Forbes

3 Aprili 2024
Katika orodha ya Forbes ya mwaka jana, kulikuwa na vigogo sita pekee waliokuwa wamevunja rekodi ya kuwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 100 za Marekani.
Jambo jipya ni kwamba katika orodha ya mwaka huu, iliyochapishwa Jumanne hii, kuna wanachama 14 wa klabu ya kipekee ambayo ni wale tu walio na thamani ya takribani tarakimu 12 huingia.
Tajiri wa Mexico Carlos Slim, mtu tajiri zaidi katika Amerika ya Kusini, hakuweza kuingia katika kundi la kipekee la wale wanaoitwa “kundi la wenye utajiri wa dola bilioni 100, kwa sababu utajiri wake ulikuwa dola za Marekani milioni 93,000.
Wakati huu, hata hivyo, alifanya hivyo.
Ili kupata wazo la ukubwa wa utajiri wa Dola za Marekani bilioni 100, angalia tu ukubwa wa Pato la Taifa la nchi (GDP), yaani, jumla ya bidhaa na huduma zote ambazo taifa huzalisha katika nchi fulani.
Kwa hivyo, utajiri wa kila mmoja wa hawa watu 14 ni mkubwa kuliko Pato la Taifa la nchi kama vile Panama, Uruguay, Costa Rica au Bolivia.
Chase Peterson-Withorn, mhariri mkuu wa utajiri katika Forbes, alisema umekuwa mwaka “wa kushangaza” kwa watu tajiri zaidi duniani.
“Hata wakati wa kutokuwa na uhakika wa kifedha kwa wengi, matajiri wakubwa wanaendelea kufanikiwa,” alibainisha.
Forbes walisema kutakuwa na rekodi ya mabilionea 2,781 mnamo 2024, 141 zaidi ya mwaka uliopita na 26 zaidi ya rekodi ya hapo awali mnamo 2021.
Wasomi hao ni matajiri zaidi kuliko hapo awali na wanajilimbikizia utajiri wa Dola za Marekani trilioni 14.2 .
Hii ndio orodha ya “Klabu 14”, kikundi cha kipekee zaidi cha matajiri kwenye sayari, kulingana na Forbes.
1. Bernard Arnault (Ufaransa)
Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 233
Kwa mwaka wa pili mfululizo Arnault ndiye mtu tajiri zaidi duniani. Utajiri wa Arnault ulikua 10% mnamo 2023 umekuwa mwaka mwingine wa rekodi kwa kampuni yake ya kifahari, LVMH, mmiliki wa Louis Vuitton, Christian Dior na Sephora.
2. Elon Musk (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 195
Kadiri nafasi inavyobadilika kila mara, Musk ameshinda na kupoteza jina la “tajiri zaidi duniani” mara kadhaa, kadiri tathmini ya SpaceX, Tesla na mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter) inavyobadilika.
3. Jeff Bezos (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 194
Bezos ni tajiri zaidi mwaka huu kutokana na utendaji mzuri wa soko la hisa la Amazon.
4. Mark Zuckerberg (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 177
Kwa mkurugenzi mtendaji wa Meta, hali iikuwa mbaya. Baada ya hisa za kampuni hiyo kubwa ya mitandao ya kijamii kushuka kwa 75% kutoka kiwango chake cha juu zaidi mnamo 2021, imeongezeka karibu mara tatu katika mwaka uliopita.
5. Larry Ellison (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 141,000
Katika kipindi cha mwaka jana, hisa za kampuni ya teknolojia ya Oracle ziliongezeka zaidi ya 30%, na kuongeza bahati yake. Ingawa alijiuzulu kama Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ellison bado ni rais, afisa mkuu wa teknolojia na mbia wake mkubwa zaidi.
6. Warren Buffett (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 133.
Akichukuliwa kuwa mmoja wa wawekezaji waliofanikiwa zaidi wakati wote, Buffett anaendesha Berkshire Hathaway, muungano ambao una makampuni kadhaa, ikiwa ni pamoja na kampuni ya bima ya Geico, mtengenezaji wa betri Duracell na mnyororo wa mgahawa wa Dairy Queen.
Hisa za Berkshire ziko katika viwango vya rekodi hadi 30% kutoka mwaka jana.
7. Bill Gates (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 128.
Mwanzilishi mwenza wa Microsoft alikuwa mtu tajiri zaidi ulimwenguni kwa miaka 18 kati ya 23 katika kipindi cha 1995 hadi 2017.
Licha ya utajiri wake mkubwa, Gates ameshuka kwenye orodha hiyo kutokana na ushindani mkali katika sekta ya teknolojia, talaka iliyomgharimu mwaka wa 2021, na michango yake kwa mashirika ya misaada, kulingana na Forbes.
Steve Ballmer (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 121.
Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Microsoft aliongoza kampuni kutoka 2000 hadi 2014, baada ya dot-com. Baada ya kustaafu kutoka Microsoft, Ballmer alinunua timu ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Clippers ya NBA (Chama cha Kikapu cha Kitaifa), ambayo thamani yake imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Hivi sasa ni timu ya tano yenye thamani kubwa katika NBA.
9. Mukesh Ambani (India)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 116.
Utajiri wa Ambani umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa hisa za kampuni yake ya Reliance Industries. Kampuni hiyo ina maslahi katika kemikali za petroli, mafuta na gesi, mawasiliano ya simu, rejareja na huduma za kifedha.
10. Larry Page (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani milioni 114,000.
Mwanzilishi mwenza na mjumbe wa bodi ya Alphabet, kampuni kuu ya Google. Pamoja na Sergey Brin, wanabaki kuwa wanahisa wakubwa wa kampuni kubwa ya teknolojia.
11. Sergey Brin (Urusi/Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 110.
Mwanzilishi mwenza na mjumbe wa bodi ya Alfabeti. Brin alijiuzulu kama rais wa kampuni hiyo mnamo Desemba 2019, lakini bado ana hisa nyingi katika kampuni pamoja na Larry Page.
12. Michael Bloomberg (Marekani)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 106.
Mwanzilishi mwenza wa habari za kifedha na kampuni ya vyombo vya habari Bloomberg LP. Kwa sasa anamiliki 88% ya biashara. Alikuwa meya wa jiji la New York kwa miaka 12.
13. Amancio Ortega (Hispania)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 103.
Mafaniki yake yaliongezeka mwaka jana kutokana na ongezeko la 43% la hisa za kampuni yake ya nguo, Inditex, ambayo inasimamia chapa ya Zara. Pia mali isiyohamishika ni pamoja na vifaa, makazi na mali za ofisi kimsingi huko Ulaya na Marekani.
14. Carlos Slim (Mexico)

Thamani halisi: Dola za Marekani bilioni 102.
Mfanyabiashara huyo alikuwa mtu tajiri zaidi duniani na bado anabaki kuwa tajiri zaidi katika Amerika ya Kusini. Utajiri wake ulikua mwaka jana kutokana na ongezeko la pesa ya Mexico na kupanda kwa bei ya hisa ya 60% ya kampuni yake ya viwanda, Grupo Carso.
Slim na familia yake wanamiliki América Móvil, kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano ya simu huko Amerika ya Kusini.
Katika miaka kumi iliyopita, utajiri wa wanachama wa klabu hiyo uliongezeka kwa 255%, ongezeko kubwa zaidi kuliko la bilionea wa kawaida.
Kwa sababu bahati nyingi huwekezwa katika masoko ya fedha, mali hupanda na kushuka kila mara.
Hivi ndivyo Bill Gates alifikia kwa ufupi alama ya “mabilionea mia” mnamo 1999, kabla ya utajiri wake kushuka kwa karibu nusu wakati wa shida ya dot-com.
Hakuna aliyeweza kuvunja rekodi hiyo tena kwa takriban miongo miwili, hata wakati soko lilikuwa likipata pesa nyingi, kabla tu ya Mdororo Mkuu wa Uchumi wa 2008-2009.
Hadithi iliendelea hivi, hadi Jeff Bezos hatimaye alivunja alama tena mwaka wa 2017, na kuwa mwanachama wa pili wa klabu ya tajiri na dola za Marekani bilioni 100, kutokana na kupanda kwa thamani ya soko la Amazon.
Na ilikuwa hadi 2021 ambapo Bezos hakuwa peke yake juu, wakati Elon Musk, Bernard Arnault na Bill Gates pia walifika kileleni.
Siku hizi, pamoja na kuongezeka kwa utajiri mkubwa ulimwenguni kote, kujiunga na kilabu kunazidi kuwa kawaida.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.