Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamoja
Muhtasari
- Wabunge wa Tanzania wajeruhiwa katika ajali ya gari
- Maelfu ya watu wanaukimbia mji wa Homs nchini Syria huku waasi wakizidi kusonga mbele
- Korea Kusini: Maafisa wakuu wa kijeshi wawekewa marufuku
- Waumini wakimbia shambulio la uchomaji moto katika sinagogi Australia
- Vurugu za magenge ya dawa za kulevya zaongezeka Mexico
- Vyama vikuu vya Korea Kusini vyafanya mazungumzo ya dharura
- Wanajeshi wawili wa Ivory coast waachiliwa huru baada ya kuzuiliwa Burkina Faso
- Gaza ina kiwango cha juu zaidi cha watoto waliokatwa viungo duniani – UN
- Emmanuel Macron kumteua Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa ndani ya siku chache
Naam,Natumai U buheri wa afya popote pale ulipo duniani kwa mwoyo mkunjufu na mikono miwili Hujambo na karibu katika matangazo yetu Afrika Leo Mchana ya moja kwa moja Jina langu ni Cantona Joseph
Wabunge wa Tanzania wajeruhiwa katika ajali ya gari,

Wabunge 16 wa bunge la Tanzania, maafisa sambamba na dereva wamejeruhiwa baada ya gari walilokua wakisafiria kwenda nchini Kenya kwa ajili ya michezo ya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ajali hiyo imetokea jijini Dodoma leo hii, baada ya moja ya gari la mizigo kugongana na basi la wabunge hao kutokana na kushindwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma George Katabazi amesema dereva wa gari lililosababisha ajali hiyo anashikiliwa licha ya kwamba ni majeruhi.
‘Tunamshikilia Juma Said Juma mmoja wapo wa majeruhi ambaye ndiye dereva aliyesabaisha ajali hiyo. Tunawataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoendelea kuonekana’ amesema Katabazi.

Taarifa iliyotolewa na bunge la Tanzania inasema majeruhi wote wamepelekwa katika hospitali mbalimbali za mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kwamba wanaendelea vizuri.
Michezo ya mabunge ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki inatarajiwa kuanza Desemba 7 2024 Mombasa Kenya, ikijumuisha wabunge mbalimbali kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki
‘Tunaweza kuona mwisho wa utawala wa Assad’ – mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa

Kuanguka kwa Homs mikononi mwa wapinzani wa Syria kunaweza kuashiria mwisho wa utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad, kulingana na mtaalamu.
Profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Shule ya Uchumi ya London, Fawaz Gerges, anaiambia BBC kuwa jiji hilo ni “kituo cha neva” cha serikali ya Assad na kukipoteza kwake kunaweza kuufanya mji mkuu, Damascus, kuwa “lengo rahisi”.
“Uwezo wa serikali umeshushwa kwa kiasi kikubwa, hilo linaonekana wazi,” Gerges anasema.
“Ikiwa vikosi vya Assad havitawazuia wapinzani kuchukua udhibiti wa Homs, nadhani tunaweza kuona mwisho wa utawala wa Assad katika wiki chache zijazo au miezi michache ijayo.”
Rais wa Syria asema nchi za Magharibi zinajaribu ‘kuchora upya ramani’
Rais wa Syria Bashar al-Assad ameapa “kuwaponda” waasi, akiwataja kama “magaidi” huku serikali yake ikijibu mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.
Katika mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Masoud Pezeshkian siku ya Jumatatu, Assad aliilaumu Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa mashambulizi hayo, akisema walikuwa wakijaribu “kuchora upya ramani” ya eneo hilo.
Pezeshkian alisisitizia Iran kusimama “imara pamoja na serikali ya Syria na watu”, na kuongeza kuwa kuhifadhi mamlaka ya Syria na uadilifu wa ardhi yake ndio msingi wa mkakati wake wa kikanda.
Wakati huo huo msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Urusi pia inafuatilia kwa makini hali ya mambo karibu na jiji la Aleppo na inachukulia mashambulizi yanayoendelea kama “shambulio dhidi ya uhuru wa Syria”.
Peskov alisema Urusi “ingependa kuona mamlaka ya Syria ikileta utulivu katika eneo hilo na kurejesha utaratibu wa kikatiba haraka iwezekanavyo”
Rais wa Korea Kusini aamuru kukamatwa kwa kiongozi wa chama chake

Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol aliamuru kukamatwa kwa kiongozi wa chama chake tawala Han Dong-hoon alipotangaza sheria ya kijeshi Jumanne usiku.
Orodha ya waliokamatwa pia imejumuisha kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic, Lee Jae-myung, pamoja na wabunge watatu wa upinzani, naibu mkurugenzi wa huduma ya kitaifa ya ujasusi amesema.
Rais alijaribu “kutumia fursa hii kuwakamata na kuwafuta kazi,” mkurugenzi Hong Jang-won alisema.
Haya yanajiri wakati vyama vya kisiasa nchini humo vikifanya mikutano ya dharura siku nzima ya Ijumaa, huku wabunge wakipanga kupiga kura ya kumshtaki Yoon.
Hoja hiyo ambayo imepangwa kujadiliwa Jumamosi, itapitishwa iwapo theluthi mbili ya wabunge wataipigia kura.
Upinzani una wabunge wengi katika bunge hilo lenye viti 300 lakini wanahitaji kuungwa mkono na angalau wabunge wanane wa chama tawala ili kupata kura 200 zinazohitajika ili hoja ya kumuondoa madarakani ipite.
Chakula pendwa cha Ivory Coast chapata hadhi ya urithi wa kitamaduni wa Umoja wa Mataifa

Chakula pendwa cha Ivory Coast, attiéké – kinachotengenezwa kwa unga wa muhogo – kimeongezwa rasmi kwenye orodha ya Unesco ya urithi wa kitamaduni.
Attiéké hutengenezwa kutokana na mizizi ya mihogo iliyosagwa na ni chakula pendwa kwa kiamsha kinywa, chakula cha mchana, na chakula cha jioni.
Kwa kawaida huliwa na samaki wa kukaanga. Kilianza maeneo ya pwani ya Ivory Coast karne nyingi zilizopita, lakini sasa kinajulikana kote Afrika Magharibi.
Mjumbe wa Unesco wa Ivory Coast, Ramata Ly-Bakayoko, alikiambia kikao cha 19 kuhusu umuhimu wa kulinda turathi za kitamaduni huko Paraguay.
Sake ya Kijapani, kinywaji cha kilevi kinachotengenezwa kutokana na nafaka, pia kimeongezwa kwenye orodha mwaka huu.
Shirika la haki za binadamu la Amnesty laishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina huko Gaza

Shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International limeishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza, jambo ambalo Israel inalikanusha vikali.
Kikundi hicho cha haki za binadamu chenye makao yake nchini Uingereza kilisema maudhui ya ripoti hiyo yametokana na “taarifa za udhalilishaji wa utu na mauaji ya halaiki” za maafisa wa Israeli, picha za kidijitali na ushuhuda wa mashahidi.
Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilielezea ripoti hiyo yenye kurasa 295 kama “ya uwongo kabisa na yenye msingi wa uongo”, wakati jeshi la Israel lilisema madai hayo “hayana msingi kabisa na yameshindwa kujibu ukweli wa operesheni” inayoikabili.
Wakati haya yakijiri, madaktari wa ndani wanasema kuwa Wapalestina 50 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza.
Idadi kubwa zaidi ya watu waliuawa katika kambi ya al-Mawasi ya watu waliokimbia makazi yao, ambapo Israel inasema ilikuwa ikiwalenga wapiganaji wa Hamas.
Waasi wa Syria wauteka mji mkuu wa pili muhimu baada ya jeshi kujiondoa

Waasi wa Syria wanasema wameudhibiti mji mkuu wa pili muhimu wa Hama, baada ya jeshi kuwaondoa wanajeshi wake huku kukiwa na mapigano makali.
Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu Hayat Tahrir al-Sham (HTS), Abu Mohammed al-Jawlani, alitangaza “ushindi” katika mji huo na kuapa kuwa “hakutakuwa na kisasi”.
Hapo awali, kamanda wa waasi alisema wapiganaji wa HTS na washirika wao waliteka gereza na kuwaachilia wafungwa, huku jeshi likisema kuwa limetuma wanajeshi tena “kulinda maisha ya raia na kuzuia mapigano ya mijini”.
Hama ni makazi ya watu milioni moja na iko kilomita 110 (maili 70) kusini mwa jiji la Aleppo, uliotekwa wiki iliyopita baada ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza kutoka ngome yao kaskazini-magharibi.
“Katika vita Jeshi la Uingereza linaweza kushindwa ndani ya miezi sita”

Katika tukio la vita vikubwa kama vile vya Ukraine, jeshi lililopo la Uingereza kwa nguvu zake za sasa litaangamizwa ndani ya miezi sita, hivyo ni muhimu kwa Uingereza kuunda kikosi kikubwa cha askari wa akiba. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Alistair Carnes.
“Katika vita vikubwa – sawa na ile vya Ukraine – jeshi letu, kulingana na kiwango cha sasa cha hasara nchini Ukraine, litapoteza ndani ya miezi sita,” amesema naibu waziri Ulinzi, akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi (RUSI) huko London.
Alistair Carnes, kanali mstaafu wa jeshi la majini, ameeleza kwamba anaamini Uingereza inahitaji kuongeza idadi ya askari wa akiba.
Novemba, Luteni Jenerali Rob Magowan, akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya House of Commons, alihakikisha kwamba jeshi liko tayari kupigana ikiwa litaamriwa, na hakuna mtu anayepaswa kufikiri kwamba ikiwa Urusi itashambulia nchi za NATO, basi Uingereza haitawasaidia.
Rais wa Korea Kusini Yoon atakiwa kuondoka chama chake

Rais Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini ambaye alitangaza sheria ya kijeshi ametakiwa kuondoka kwenye chama chake cha People’s Power Party.
Kiongozi wa chama hicho Han Dong-hoon aliwaambia waandishi wa habari “amemtaka rais huyo kujiuzulu” kutoka kwa chama.
Hata hivyo chama hicho kimedokeza kuwa hakitaunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani iliyoletwa na upinzani.
Yoon amekubali kujiuzulu kwa waziri wa ulinzi Kim Yong-hyun, ambaye inasemekana ndiye aliyependekeza sheria ya kijeshi kwa rais.
Kim aliomba radhi kwa baraza la mawaziri hapo jana na kujiuzulu.
Maandamano zaidi na mikutano ya hadhara inafanyika kote nchini humo hii leo huku rais – ambaye sasa anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye – akitarajiwa kuomba msamaha.
Bunge linatazamiwa kupiga kura ya kumuondoa Yoon madarakani.
Uwezekano wa Urusi kuishambulia moja kwa moja Uingereza na nchi za NATO ni mdogo – UK

Admirali Tony Radakin, afisa mkuu wa jeshi katika vikosi vya jeshi la Uingereza, ametoa hotuba yake ya kila mwaka katika kitengo cha watalaam RUSI na kusema, pamoja na mambo mengine, uwezo wa Urusi kutekeleza mashambulizi ya moja kwa moja au kuivamia Uingereza ikiwa nchi hizo mbili ziko vitani iko chini.
Mkuu huyo wa jeshi alisisitiza haja ya kuwa “wazi” kuhusu vitisho vinavyoikabili nchi hiyo.
Moscow inajua “jibu litakuwa kubwa,” Radakin aliendelea. Lakini ni muhimu “kuweka nguvu na kuendelea kuimarisha” kizuizi cha nyuklia, na serikali kadhaa za Uingereza zimewekeza sana katika nyambizi na makombora ambayo yanaunda nguvu ya nyuklia ya Uingereza.
Sehemu hiyo ni ya akiba yetu ambayo Urusi inafahamu zaidi na ambayo ina athari kubwa kwa Putin,” aliongeza.
Radakin alibainisha kuwa dunia inaingia katika “enzi ya tatu ya atomiki” ambapo idadi ya mamlaka yenye silaha za nyuklia itaongezeka.
Alisema, kuwa Urusi, China, Iran na Korea Kaskazini zitaongeza akiba zao za silaha za nyuklia au zitaendelea kujaribu kuzipata.
Kuhusu vita vya Ukraine, Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi alitaja kuonekana kwa maelfu ya wanajeshi wa Korea Kaskazini kwenye mipaka ya Ukraine kuwa tukio la kushangaza zaidi la mwaka.
Kulingana naye, “makumi ya maelfu zaidi yatafuata kama sehemu ya mapatano mapya.
Mamlaka ya Congo kutoa taarifa kuhusu ugonjwa usiojulikana

Wizara ya Afya ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inatazamiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ugonjwa usiojulikana ambao umeua takriban watu 79 katika jimbo la Kwango kusini-magharibi tangu Oktoba 24.
Wengi wa waliofariki ni watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 15.
Zaidi ya watu 300 walioambukizwa dalili za mafua ikiwa ni pamoja na: homa, maumivu ya kichwa, mafua pua na kikohozi, ugumu wa kupumua na upungufu wa damu.
Afisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika aliambia BBC kuwa “wametuma timu katika eneo la mbali kuchukua sampuli kwa uchunguzi wa maabara”.
Mamlaka nchini humo imewataka wakazi kuwa watulivu na waangalifu.
Waliwataka watu kunawa mikono kwa sabuni, kuepuka mikusanyiko ya watu wengi, na kuepuka kugusa miili ya marehemu bila wahudumu wa afya waliopata mafunzo.
Amnesty International yaishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza

Amnesty International imeshutumu taifa la Israel kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza kwenye ripoti iliyochapishwa siku ya Alhamisi, madai ambayo viongozi wa Israel wameyakanusha mara kwa mara.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza limesema limefikia hitimisho hilo baada ya miezi kadhaa ya kuchambua matukio na kauli za maafisa wa Israel.
Amnesty ilisema kiwango cha kuzingatiwa kisheria cha uhalifu huo kilifikiwa, katika uamuzi wake wa kwanza kama huo wakati wa mzozo mkali uliohusisha utumiaji wa silaha.
Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948, uliotungwa kufuatia mauaji ya halaiki ya Wayahudi katika Mauaji ya halaiki ya Nazi, unafafanua mauaji ya halaiki kama “vitendo vilivyofanywa kwa nia ya kuharibu, kwa ujumla au kwa sehemu, kikundi cha kitaifa, kikabila, ubaguzi au kidini”.
Israel imekanusha mara kwa mara shtaka lolote la mauaji ya halaiki, ikisema kuwa imeheshimu sheria za kimataifa na ina haki ya kujitetea baada ya shambulio la kuvuka mpaka la Hamas kutoka Gaza mnamo Oktoba 7, 2023 ambalo lilichochea vita.
Maafisa wa Israel hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao kuhusu ripoti ya Amnesty International.
Bei ya Bitcoin yazidi $100k

Bei ya Bitcoin kwa mara ya kwanza imepita zaidi ya $100,000, na kufikia rekodi mpya ya juu.
Kuongezeka kwa thamani ya sarafu ya kidigitali iliyo kubwa zaidi duniani kumechochewa na matumaini kwamba Rais mteule wa Marekani Donald Trump atapitisha sera ambazo zinapendelea mfumo wa sarafa za kidigitali.
Hatua hiyo ilifikiwa saa chache baada ya Trump kusema atamteua kamishna wa zamani wa Tume ya Usalama na Biashara Paul Atkins kusimamia udhibiti wa masoko ya hisa.
Hatua hiyo muhimu ya $100,000 ilichochea sherehe kwa wanaopedelea sarafu za kidigitali kote ulimwenguni.
Thamani ya Bitcoin inayobadilika-badilika mara kwa mara imevutia watu wengi, huku wanaoipendelea wakifurahia kwa kupita viwango vya awali vya bei.
Ushindi wa Trump katika uchaguzi wa mwezi uliopita ulikuwa kichocheo cha ongezeko la thamani ya Bitcoin hivi punde.
Rais mteule ameapa kuifanya Marekani kuwa “mji mkuu wa fedha ya kidigitali duniani” – mabadiliko ya ajabu ya hivi punde kutoka kwake ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo alikuwa anaita Bitcoin “utapeli.”
Israel inasema mwili wa mateka Itay Svirsky wapatikana Gaza

Jeshi la Israel linasema mwili wa mateka wa Israel anayeshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza umepatikana katika operesheni ya pamoja na idara ya usalama ya Shin Bet.
Taarifa ilisema Itay Svirsky, 38, ambaye alitekwa nyara kutoka Kibbutz Be’eri wakati wa shambulizi la Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli, “aliuawa akiwa utumwani na watekaji wake”.
Hamas ilisema mwezi Januari kwamba Svirsky na mateka mwingine, Yossi Sharabi, 53, waliuawa wakati wa mashambulizi ya anga ya Israeli.
Hapo awali, jeshi lilisema uchunguzi ulihitimisha kwamba maelezo ya kina ya vifo vya mateka wengine sita waliopatikana wamefariki kwenye handaki huko Gaza mnamo mwezi Agosti ni kwamba walipigwa risasi na Hamas “karibu” na wakati wa shambulio la anga la Israeli.
Wanajeshi walipata miili ya Yagev Buchshtab, 35, Alexander Dancyg, 76, Avraham Munder, 79, Yoram Metzger, 80, Chaim Peri, 79, na Nadav Popplewell, mwenye umri wa miaka 51, mwenye uraia mara mbili wa Uingereza na Israeli, pamoja na wapiganaji sita wa Hamas, katika eneo la kusini la Khan Younis.
Jeshi lilisema “kuna uwezekano mkubwa” vifo vya mateka vilihusiana na mashambulizi ya Februari kwenye eneo la chini ya ardhi lililolenga makamanda wa Hamas.
Ndege mzee zaidi duniani ataga yai akiwa na miaka 74

Ndege mzee zaidi duniani ametaga yai akiwa na umri wa takriban miaka 74, wanabiolojia wa Marekani wanasema.
Wisdom, ndege huyo alirekodiwa na Shirika la Huduma ya Samaki na Wanyamapori la Marekani (USFWS) katika Bahari ya Pasifiki pamoja na mwenzi wake wa hivi punde akitaga yai.
Ndege wa spishi hii kawaida huishi kwa miaka 12-40 tu, lakini Wisdom alitambulishwa mnamo 1956 alipokuwa na umri wa miaka mitano.
Mtoto wake wa mwisho alianguliwa mwaka wa 2021.
Inaaminika kwamba alikuwa na zaidi ya vifaranga 30 maishani mwake.
Shirika la USFWS lilisema kwenye mtandao wa X kwamba Wisdom alikuwa na mwenza wake mpya mwaka huu na kwamba mwenza wake wa awali Akeakamai hajaonekana kwa miaka kadhaa.
Serikali ya Ufaransa yaporomoka baada ya kura ya kutokuwa na imani

Serikali ya Ufaransa imeporomoka baada ya Waziri Mkuu Michel Barnier kuenguliwa katika kura ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge walipiga kura kwa wingi kumtaka aondoke, miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa na Rais Emmanuel Macron.
Viongozi wa upinzani walileta hoja hiyo baada ya Barnier kutumia madaraka maalum kupitisha bajeti yake ambayo haikuwa imepigiwa kura.
Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Ufaransa kuanguka kupitia kura ya kutokuwa na imani tangu mwaka 1962.
Hali hii inaongeza msukosuko wa kisiasa nchini Ufaransa, ambako tayari uchaguzi wa mapema uliofanyika msimu wa joto ulisababisha ukosefu wa wingi katika upande zote bungeni.
Wabunge walihitajika kupiga kura ya ndio au kutoshiriki, ambapo kura 288 zilihitajika ili pendekezo lipite. Jumla ya kura 331 zilipigwa kwa ajili ya pendekezo hilo.
Barnier sasa anapaswa kujiuzulu kwa serikali yake na bajeti iliyosababisha kuporomoka kwake imepitwa na wakati.
Hata hivyo, anatarajiwa kusalia kama Waziri Mkuu wa mpito hadi Macron apate mrithi wake.
Mrengo wa kushoto na wa kulia walipeleka mapendekezo ya kutokuwa na imani naye baada ya Barnier kulazimisha mageuzi ya usalama wa kijamii kwa kutumia amri ya rais, baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha.
Rais Macron, aliyerejea Ufaransa baada ya ziara rasmi Saudi Arabia, anatarajiwa kutoa hotuba ya kitaifa Alhamisi jioni.
Haathiriwi moja kwa moja na matokeo ya kura, kwani Ufaransa inampigia kura rais wake tofauti na serikali yake.
Macron alikuwa amesema hatajiuzulu vyovyote vile matokeo ya kura yatakavyokuwa.
Anatarajiwa kumteua waziri mkuu mpya haraka iwezekanavyo ili kuepusha aibu ya serikali isiyokuwapo – na zaidi, kwa sababu Rais mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuzuru Paris wikendi hii kwa ufunguzi wa kanisa kuu la Notre-Dame.
Waumini wakimbia shambulio la uchomaji moto katika sinagogi Australia

Waumini wamelazimika kulikimbia sinagogi la Australia baada ya kuchomwa moto katika kile ambacho waziri mkuu amelaani kuwa ni “kitendo cha chuki”.
Wazima moto waliitwa kwenye sinagogi la Adass Israel la Melbourne baada tu ya 04:00 saa za eneo siku ya Ijumaa (17:00 GMT Alhamisi), jengo likiwa linawaka moto.
Viongozi wa jumuiya wameviambia vyombo vya habari kuwa “watu wachache” walikuwa ndani wakati huo kwa ajili ya maombi ya asubuhi, na waliripoti kuona mabomu ya moto yakirushwa.
Mtu mmoja alijeruhiwa na moto huo umesababisha uharibifu mkubwa.
Polisi wanasema kuwa wanaamini moto huo uliwashwa kimakusudi lakini wanaendelea kuwa na “mawazo huru” wakitafuta nia ya utekelezaji kitendo hicho.
Vurugu za magenge ya dawa za kulevya zaongezeka Mexico

Watu zaidi ya 200 wameripotiwa kupotea katika jimbo lililokumbwa na vurugu la Sinaloa nchini Mexico ambapo makundi mawili hasimu ya genge la dawa za kulevya walianza vita vya umwagaji damu vya kudhibiti kundi lao la uhalifu karibu miezi mitatu iliyopita.
Vita hivyo vilizuka baada ya kukamatwa kwa Ismael “El Mayo” Zambada nchini Marekani.
Wafuasi wake wanaojiita “Los Mayos” au “La Mayiza”, wanadai kuwa kiongozi wao alisalitiwa na kijana wa genge la Sinaloa, Joaquin “El Chapo” Guzman, na wamegeuka wanachama wa kundi lakelinalojulikana kama ‘’Los Chapitos.’’
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum ametuma mkuu wa usalama , Omar García Harfuch, kwenda jimbo la Sinaloa ili kutuliza kadhia hiyo.
Ongezeko la mauaji na kupotea kwa watu huko Sinaloa kumezidi miezi ya kwanza ya Sheinbaum madarakani.
Awali, Afisa mkuu wa usalama wa Mexico, Omar García Harfuch, alitangaza kupitia mtandao wa X, kukamatwa kwa dawa aina ya fentanyl yenye thamani ya dola milioni 394 yenye uzito wa zaidi ya tani moja kutoka nyumba mbili huko Sinaloa.
Wanajeshi wawili wa Ivory coast waachiliwa huru baada ya kuzuiliwa Burkina Faso

Msemaji wa serikali ya Ivory Coast, Amadou Coulibaly, amesema maafisa wawili wa kijeshi waliokamatwa nchini Burkina Faso mwaka jana, wameachiliwa huru na kurejea nyumbani.
Ametangaza matukio hayo baada ya kufanya mkutano wa baraza la mawaziri.
Maafisa hao walikamatwa mnamo mwezi Septemba 2023, baada ya kuvuka mpaka wa Burkina Faso wakitafuta wachimbaji haramu wa dhahabu.
Coulibaly alisema walikabidhiwa mamlaka za Ivory Coast tarehe 29 Novemba, akitoa shukrani kwa Jamhuri ya Togo kusaidia katika mazungumzo ya wawili hao kuachiliwa huru.
Msemaji huyo wa Ivory coast pia alifafanua kuwa rais wa Togo Faure Gnassingbe alihusika binafsi katika majadiliano ya kuachiliwa kwao.
Uamuzi wa Burkina Faso kuwakamata maafisa hao ilikuwa ni ishara ya kuendelea kwa mivutano kati ya nchi hizo mbili tangu jeshi la Burkina Faso kuchukua madaraka mwaka 2022.
Mnamo mwezi Julai, kiongozi wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traore, alishutumu Ivory Coast na Benin, washirika wa karibu wa Ufaransa, kuhusika katika njama za kutikisa utulivu wa nchi yake.
Hii si mara ya kwanza wanajeshi ya Ivory Coast kuhusishwa na mivutano ya kidiplomasia na majirani zao.
Miaka miwili iliyopita, wanajeshi 49 wa Ivory Coast walikamatwa nchini Mali baada ya kujulikana kama “mamluki,” ingawa Ivory Coast ilisisitiza kuwa walikuwa sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa UN.
Haijulikani kama kuachiliwa kwa maafisa hao kutasaidia kuboresha uhusiano kati ya Ivory Coast na Burkina Faso ambao tayari umedorora.
Gaza ina kiwango cha juu zaidi cha watoto waliokatwa viungo duniani – UN

Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina la UNRWA, limetoa tathmini yake ya hivi punde kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Gaza sasa ina idadi kubwa zaidi ya watoto waliokatwa viungo kuliko sehemu nyingine yoyote ile duniani.
Akiitaja hali ya Gaza iliyokumbwa na vita kuwa “ya kuogofya na ya kutisha”, mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema hali zinazowakabili Wapalestina katika eneo hilo zinaweza kuwa “uhalifu mbaya zaidi wa kimataifa”.
Watu waliokimbia makazi yao huko Gaza wako katika hatari ya kukabiliwa na hali ya hewa ya baridi na mvua msimu huu wa baridi.
Kwa sababu ya ukosefu wa usalama, UNRWA imelazimika kusitisha uwasilishaji wa misaada tangu Desemba 1 kupitia kivuko cha mpaka cha Karem Abu Salem – mahali pa kuingizia misaada ya kibinadamu katika eneo la Palestina.
Watu zaidi ya milioni 1 huko Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya Israel na amri za kijeshi, na wengi wao wameyakimbia makazi yao mara kadhaa.
Wafanyakazi wa shirika la UNRWA pia ni miongoni mwa waliouawa tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas Oktoba 7, 2023.
Ni vituo saba tu kati ya 27 vya UNRWA vinavyofanya kazi.
Emmanuel Macron kumteua Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa ndani ya siku chache

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema atamteua waziri mkuu mpya ndani ya “siku chache”, baada ya Michel Barnier kujiuzulu kufuatia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.
Katika hotuba ya dakika 10 kwa taifa siku ya Alhamisi, alikataa shinikizo la upinzani kujiuzulu, na kuapa kusalia katika wadhifa wake”, hadi mwisho wa mamlaka” mnamo 2027.
Alimshukuru Barnier kwa kujitolea kwake wakati wa muda wake mfupi kama waziri mkuu, na kuwashutumu Wafaransa wa mrengo wa kulia na kushoto kwa kushirikiana kuiangusha serikali.
Wabunge wa Ufaransa walipiga kura kwa wingi kumuondoa Barnier siku ya Jumatano, miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa na Macron.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa serikali ya Ufaransa kupigiwa kura ya kuiangusha na bunge kwa zaidi ya miaka 60, hatua ambayo Macron aliitaja kuwa hatua ambayo “haijawahi kutokea”.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.