Mlango wa kwenda mbinguni.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni Sana tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.

Kila mwanadamu akifa huenda sehemu mojawapo Kati ya hizi mbili; Kuna mtu akifa huenda Paradiso na kuna mtu akifa huenda mbinguni.

Paradiso ni eneo la mbinguni ambako hukaa huko wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU tu.
Ndio maana pale msalabani kuna mtu mmoja alimwamini YESU na kusamehewa pale pale na kuambiwa siku hiyo hiyo atakuwa Peponi yaani Paradise kwenye Biblia ya kiingeleza, ikiwa na maana ya paradiso kwa kiswahili, hiyo iko Luka 23:43

Hata mtume Paulo katika Wafilipi 1:23 anatamani kwenda mbinguni aliko KRISTO, Biblia inasema “Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na KRISTO maana ni vizuri zaidi sana;”
Hivyo wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU wakiondoka duniani huenda mbinguni.

Lakini waliomkataa YESU KRISTO wao wakiondoka duniani huenda kuzimu.
Kuzimu hukaa huko waliomkataa YESU KRISTO na watenda dhambi wote.
Zaburi 9:17 “Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau MUNGU.”

Kuzimu wengine huita ahera, Wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU hawaendi ahera wala kuzimu bali huenda mbinguni aliko Mwokozi wao YESU KRISTO.

Najua kila mtu anatamani kwenda mbinguni yaani kwenda kwenye maisha ya uzima wa milele.

Sasa niko hapa kukufundisha juu ya mlango au lango la mbinguni na wenye sifa za kupita katika lango hilo la kuingia mbinguni.

Zaburi 118:20 “Lango hili ni la BWANA, Wenye haki ndio watakaoliingia.”

Lango la mbinguni ni YESU KRISTO na watu wenye haki tu ndio wataoingia mbinguni.

Narudia tena, Lango la mbinguni Ni kwa njia ya YESU KRISTO tu na wenye haki tu ndio watakaoingia.

Ndugu, Kama kweli unaihitaji mbingu basi hakika unamhitaji YESU KRISTO na Wokovu wake ulio wa thamani sana.

Ndugu, Kama kweli unauhitaji uzima wa milele basi hakika unamhitaji YESU KRISTO na sio vinginevyo.
Bwana YESU anasema katika Yohana 10:9,14 kwamba “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. …………. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;”

YESU KRISTO ndiye mlango wa binadamu kuingia mbinguni, maana yake ukimpokea YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wako mlango wa kuingia mbinguni unakuwa umefunguliwa kwako.

Ndugu, nakuomba usiabudu bila kuhakikisha utaingia mbinguni.

Ndugu usiabudu bila kuhakikisha kwamba utakwenda mbinguni, lango la mbinguni ni Bwana YESU KRISTO hivyo mpokee kama Mwokozi wako kisha anza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
1 Petro 1:15 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;”

Hakikisha unakuwa mwenye haki mbele za MUNGU kwa wewe kuamua kuokoka na kuishi maisha matakatifu.

Wakati mwingine ukiokoka unaweza ukaonekana wa kawaida kawaida mbele ya jamii ya watenda dhambi, unaweza ukaonekana kama kuna vitu umepungukiwa mbele ya jamii ya watenda dhambi maana wewe huna mchepuko, huibi wala huisaliti ndoa yako.
Watu wanaweza kukuona kuna vitu unapungukiwa kwa sababu tu wewe huendi disko, hunywi pombe wala huimbi nyimbo za kidunia, hupokei rushwa wala huwezi kwenda kwa waganga wa kienyeji hivyo watenda dhambi watakuona kama unapungukiwa Sana kwa sababu huambatani na starehe zao, lakini kwa sababu umeokolewa na Bwana YESU Biblia inasema katika Isaya 35:8 kwamba “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.”

Ndugu, uko kwenye njia ya mbinguni ndio maana walio katika njia ya jehanamu wanakuona umepungukiwa.
Ndugu usiogope kutengwa, kunyanyaswa wala kutukanwa kwa ajili ya KRISTO, Songa mbele na YESU KRISTO maana Biblia inasema kwamba thawabu yetu ni kubwa mbinguni.

Luka 6:22-23 ” Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo.”

Ndugu, kwa sababu umeliona lango la mbinguni ambalo ni YESU basi kaa ndani yake milele.
Usikubali kitu chochote kikutenge wewe na YESU KRISTO Mwokozi.
Warumi 8:35-39 ” Ni nani atakayetutenga na upendo wa KRISTO? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa MUNGU ulio katika KRISTO YESU Bwana wetu.”

Ndugu nakuomba hakikisha una YESU KRISTO siku zote za maisha yako.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment