Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limechapisha ripoti siku ya Alhamisi likiishutumu Israel kwa “kufanya mauaji ya halaiki” dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita, likitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa “kutohusika” katika hilo.

“Mwezi baada ya mwezi, Israel imewachukulia Wapalestina wa Gaza kama kundi la watu wasio na ubinadamu, wasiostahili kuheshimiwa, ikionyesha nia yake ya kuwaangamiza kimwili,” amesema katibu mkuu wa shirika hilo, Agnès Callamard.
Ni kurasa 300, ambazo zimeandikwa. Haya ni matunda ya miezi 10 ya uchunguzi huko Gaza na uchambuzi wa hotuba za maafisa wa Israeli. Matokeo yake ni wazi kulingana na waandishi: Israel inafanya mauaji ya kimbari kwa Wapalestina. Shirika hili lisilo la kiserikali linasema limejikita kwa kufanya ripoti hiyo na vigezo vilivyoainishwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mauaji ya Kimbari.
“Tunachosema leo ni kwamba uhalifu wa mauaji ya halaiki sio hatari tena, lakini ukweli unaoendelea,” Tchérina Jerolon, mkuu wa kitengo cha masuala ya migogoro, uhamiaji, haki katika shirika la Amnesty International. Ushahidi wetu unaonyesha kwamba mamlaka ya Israel ilifanya vitendo vitatu kati ya vitano vilivyokatazwa na Mkataba wa Mauaji ya Kimbari: mauaji, madhara makubwa kwa uadilifu wa kimwili au kiakili na uanzishwaji wa hali ya maisha ambayo inakusudiwa kusababisha vifo vya polepole na vilivyohesabiwa vya wakazi wa Gaza.”
Katika ripoti hiyo, Amnesty International inaangazia “mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia […], matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi”, na vikwazo vya kuwasilisha misaada ya kibinadamu katika eneo hilo na asilimia 90 ya wakazi wake kulazmishwa kuhama makazi yao.
Tangu kuanza kwa vita vilivyoanzishwa kwa kulipiza kisasi na Israeli, watu 44,532 wameuawa huko Gaza, raia wengi, kulingana na data kutoka kwa Wizara ya Afya ya Hamas kwa Gaza, inayoonekana kuwa ya kuaminika na Umoja wa Mataifa. Israeli iliamuru mnamo mwezi Oktoba 2023 “kuzingirwa kamili” kwa eneo hilo, ambalo lina karibu wakaazi milioni 2.4, na kauli mbiu ifuatayo: “Hakuna umeme, hakuna maji, hakuna gesi”, na sasa inaweka vikwazo vikali katika utoaji wa misaada. Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na “utapiamlo, njaa na magonjwa”, kulingana na Amnesty International
Israel imekanusha mara kwa mara shutuma za “mauaji ya halaiki” dhidi yake, ikiishutumu Hamas kwa kutumia raia kama “ngao za binadamu”. Tangu shambulio la Hamas, Israel imeangazia haki yake ya kujilinda dhidi ya vuguvugu la Kiislamu la Palestina, ambalo imeapa kulitokomeza. “Lakini tuwe wazi: malengo ya kijeshi yanaweza kuambatana na nia ya mauaji ya kimbari,” Agnès Callamard amesema katika mkutano na waandishi wa habari huko Hague, nchini Uholanzi.
Ripoti ya Amnesty inatoa mfano wa mashambulizi 15 ya anga yaliyotekelezwa kati ya Oktoba 7, 2023 na Aprili 20, 2024, ambayo yaliua raia 334 wakiwemo watoto 141, na ambayo shirika hilo “halikupata ushahidi kwamba yalielekezwa kwa malengo ya kijeshi. Hati hiyo pia inataja wito kutoka kwa maafisa na wanajeshi wa Israel kwa “maangamizi, uharibifu, uchomaji moto au ‘kuangamizwa’ kwa Gaza.” Maoni ambayo yanasisitiza “sio tu kutokujali kwa utaratibu, lakini pia uundaji wa mazingira ambayo yanahimiza […] tabia kama hiyo”.
Kulingana na ripoti hiyo, hakuna vita vya hivi majuzi vilivyoua watoto wengi kwa muda mfupi. Sasa haiwezekani kwa jumuiya ya kimataifa kufumbia macho, anabainisha Tcherina Jerolon: “Alama zote ni nyekundu. Tunahitaji hatua madhubuti kukomesha mauaji ya kimbari yanayoendelea. Miongoni mwa hatua hizi ni haja ya kuwa na vikwazo vya jumla vya silaha zinazoingia Israel. “
“Serikali lazima ziache kujifanya kuwa hazina uwezo wa kukomesha uvamizi, ubaguzi wa rangi na mauaji ya kimbari huko Gaza,” Agnès Callamard amesema.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.