AFRIKA LEO MCHANA -03-12-2024

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Erdogan: Uturuki inafuatilia kwa ukaribu yanayoendelea Syria

“Ni hamu yetu kuona kuwa utawala wa Syria unahifadhiwa na kulingana na mahitaji ya watu wa Syria,” alisema Rais Recep Tayyip Erdogan. / Picha: AA   

Rais wa Uturuki amesema kuwa Ankara inafanya kila liwezekanalo kumaliza mapigano katika ukanda wake.

Uturuki inafuatilia kwa karibu yanayoendelea Syria na kuwa inachukua hatua madhubuti kusitisha mapigano kati ya utawala wa Bashar al Assad na vikundi vyenye silaha nchini humo, amesema Rais Recep Tayyip Erdogan amesema.

“Tunafuatilia kwa karibu yanayojiri huko Syria” alisema Erdogan katika mkutano wa wanahabari akiwa na kiongozi mwenzake Jakov Milatovic wa Montenegro, katika mji mkuu wa Ankara nchini Uturuki siku ya Jumatatu.

Kulingana na Erdogan, Ankara inafuatilia kwa karibu kile kinachoendelea Syria kama ilivyo kipaumbele chake cha usalama na kuwa inachukua hatua madhubuti kuepusha madhara zaidi.

“Ni hamu yetu kuona kuwa utawala wa Syria unahifadhiwa na kulingana na mahitaji ya watu wa Syria,” alisema Rais Recep Tayyip Erdogan.

Alisisitiza kuwa Ankara iko tayari kumaliza kila aina ya mapigano katika kanda yake.

Mapigano yalizuka tarehe 27 Novemba kati ya wanajeshi wa utawala wa Assad na makundi yanayopinga serikali katika eneo la mashambani la Aleppo kaskazini mwa Syria, na kuashiria kuongezeka tena kwa mapigano hayo baada ya kipindi cha utulivu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoikumba Syria tangu mwaka 2011.

Wanajeshi waliochoka wa Ukraine nchini Urusi waambiwa wavumilie wakimsubiri Trump

Wanajeshi wa Ukraine

“Hali inazidi kuwa mbaya kila siku.” “Hatuoni mbele. Ardhi yetu haipo hapa.”

Takribani miezi minne baada ya wanajeshi wa Ukraine kuanzisha mashambulizi katika eneo la Kursk nchini Urusi, ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wanajeshi wanaopigana huko unatoa picha mbaya ya vita ambavyo hawavielewi vizuri na wanahofia kuwa wanaweza kushindwa.

Tumekuwa tukiwasiliana, kupitia Telegram, na wanajeshi kadhaa wanaohudumu Kursk, mmoja wao ameondoka hivi karibuni. Tumekubali kutomtambua yeyote kati yao.

Hakuna jina katika makala haya na ni makala halisi.

Wanazungumza juu ya hali mbaya ya hewa na ukosefu wa usingizi wa kudumu unaosababishwa na mabomu ya mara kwa mara ya Urusi, ambayo ni pamoja na matumizi ya mabomu ya kutisha ya 3,000kg.

Pia wako katika mafungo, huku majeshi ya Urusi yakichukua tena eneo lao polepole.

“Mtindo huu utaendelea,” Pavlo aliandika mnamo 26 Novemba. “Ni suala la muda tu.”

Pavlo alizungumza kuhusu uchovu mkubwa, ukosefu wa silaha na kuwasili kwa vitengo, vilivyoundwa kwa kiasi kikubwa na wanaume wa makamo, walioletwa moja kwa moja kutoka kwa pande nyingine bila wakati mdogo au bila kupumzika katikati.

Kusikia askari wakilalamika, kuhusu maofisa wao wakuu, amri na ukosefu wa vifaa, si kawaida. Askari mara nyingi hufanya nini katika hali ngumu?

Chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa adui na majira ya baridi yakianza, itakuwa jambo la kushangaza kusikia matumaini mengi.

Lakini ujumbe ambao tumepokea unakaribia kuwa mbaya, ukieleza kuwa motisha ni tatizo.

Baadhi walihoji ikiwa mojawapo ya malengo ya awali ya operesheni hiyo, kuwaelekeza wanajeshi wa Urusi kutoka eneo la mashariki mwa Ukraine, lilifanya kazi.

Maagizo sasa, walisema, yalikuwa ya kusalia kwenye eneo hili dogo la ardhi ya Urusi hadi rais mpya wa Marekani, na sera mpya, atakapowasili katika Ikulu ya White House mwishoni mwa Januari.

“Kazi kuu inayotukabili ni kuvumilia zaidi hadi kuapishwa kwa Trump na kuanza kwa mazungumzo,” Pavlo alisema.

“Nina hakika kwamba [Putin] anataka kutuondoa ifikapo tarehe 20 Januari,” alisema.

“Ni muhimu sana kwake kuonesha kwamba anadhibiti hali hiyo. Lakini hadhibiti hali hiyo.”

Katika juhudi za kuisaidia Ukraine kuzuia mashambulizi ya Urusi huko Kursk, Marekani, Uingereza na Ufaransa zote zimeiruhusu Kyiv kutumia silaha za masafa marefu kulenga shabaha ndani ya Urusi.

“Hakuna mtu anayekaa kwenye mtaro wa baridi na kuombea makombora,” Pavlo alisema.

“Tunaishi na kupigana hapa. Na makombora yanaruka mahali pengine.”

Mnamo Oktoba pekee, Urusi iliweza kuchukua takribani kilomita za mraba 500 za eneo la Ukraine, idadi kubwa zaidi iliyochukuliwa tangu siku za mwanzo za uvamizi kamili wa 2022.

Kinyume chake, Ukraine tayari imepoteza karibu 40% ya eneo ambalo liliteka eneo la Kursk mnamo Agosti.

“Jambo kuu sio kukamata lakini kushikilia,” Vadym alisema, “na tunapambana na hilo.”

Vikosi vya Urusi vimechukua hatua kwa hatua eneo la Kursk tangu Ukraine ilipoiteka mwezi Agosti

Licha ya hasara, Vadym anafikiri kampeni ya Kursk bado ni muhimu.

“Iliweza kugeuza baadhi ya vikosi vya [Urusi] kutoka mikoa ya Zaporizhzhia na Kharkiv,” alisema.

Lakini baadhi ya wanajeshi tuliozungumza nao walisema walihisi kuwa walikuwa mahali pasipofaa, kwamba ilikuwa muhimu zaidi kuwa upande wa mashariki wa Ukraine, badala ya kukalia sehemu ya Urusi.

“Sehemu yetu inapaswa kuwa huko [mashariki mwa Ukraine], sio hapa katika ardhi ya mtu mwingine,” Pavlo alisema. “Hatuhitaji misitu hii ya Kursk.

Na licha ya wiki kadhaa za ripoti kueleza kwamba wanajeshi 10,000 wa Korea Kaskazini wamepelekwa Kursk kujiunga na uvamizi wa Urusi, wanajeshi ambao tumekuwa tukiwasiliana nao bado hawajakutana nao.

“Sijaona au kusikia chochote kuhusu Wakorea, wakiwa hai au wamekufa,” Vadym alijibu tulipouliza kuhusu ripoti hizo.

Jeshi la Ukraine limetoa rekodi ambazo linasema kuwa ni njia za mawasiliano ya redio ya Korea Kaskazini.

Wanajeshi walisema walikuwa wameambiwa wamkamate angalau mfungwa mmoja wa Korea Kaskazini, ikiwezekana na nyaraka.

Walizungumza juu zawasi ya ndege zisizo na rubani au likizo ya ziada, kutolewa kwa mtu yeyote ambaye amefanikiwa kumkamata mwanajeshi wa Korea Kaskazini.

“Ni vigumu sana kupata Mkorea katika msitu wa Kursk,” Pavlo alisema kwa kejeli. “Hasa kama hayupo.”

Morali inaonekana iko chini miongoni  mwa askari Ukraine

Kuanzia Oktoba 2023 hadi Julai mwaka huu, vikosi vya Ukraine vilijaribu kushikilia daraja dogo huko Krynky, kwenye ukingo wa kushoto wa Mto Dnipro, takribani maili 25 (40km) juu ya mto kutoka mji uliokombolewa wa Kherson.

Operesheni hiyo ilikuwa ya gharama kubwa. Kiasi cha wanajeshi 1,000 wa Ukraine wanakisiwa kuuawa au kutoweka.

Wachambuzi wa kijeshi wanasisitiza kwamba pamoja na shida zote, kampeni ya Kursk inaendelea kuwa jukumu muhimu.

“Ni eneo pekee ambalo tunadumisha mpango huo,” Serhiy Kuzan, wa Kituo cha Usalama na Ushirikiano cha Kiukreni, aliniambia.

Alikiri kwamba vikosi vya Kiukreni vinakabiliwa na “hali ngumu sana” huko Kursk, lakini alisema Urusi ilikuwa ikitumia rasilimali nyingi kuwaondoa, rasilimali ambazo ingependelea kutumia mahali pengine.

Rais wa Marekani Joe Biden amekutana na mwenzake wa Angola

.

Joe Biden amekutana na rais wa Angola, Joao Lourenco, leo Jumanne ikiwa ni ziara yake ya kwanza na ya pekee barani Afrika kama rais wa Marekani.

Anatarajiwa kuzungumzia mkopo wa Marekani kwa mradi wa reli mpya ya kilomita elfu moja na mia tatu.

Mradi huo unaonekana kama jaribio la kushindana na China ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kanda hiyo – hasa katika sekta ya madini.

Beijing ilitia saini makubaliano na Tanzania na Zambia mwezi Septemba kwenye mradi wa reli kuelekea pwani ya mashariki ya Afrika.

Hii ni ziara ya kwanza kabisa nchini Angola kufanywa na rais wa Marekani. Wakati wa vita baridi, ilikuwa mshirika wa Urusi na Cuba.

Hata hivyo, kwa sasa Angola ina washirika mbalimbali ikiwa ni pamoja na wapinzani kama Marekani na China.

Makampuni ya mafuta ya Marekani yamekuwa Angola kwa miaka mingi lakini sasa Joe Biden anawekeza katika reli kusaidia kuuza nje madini yanayohitajika ikiwa ni mabaadiliko kutoka kwa fueli ya visukuku.

Jambo ambalo bado halijajulikana ni iwapo Donald Trump ataupa kipaumbele mradi huo huo au atajiondoa huku China ikiongeza ushawishi wake katika eneo hilo.

Gari jipya la Jaguar linalotumia umeme lazua gumzo

.

Kampuni ya kutengeneza magari ya kifahari ya Jaguar imezindua gari lake jipya la umeme, chini ya wiki mbili baada ya kutolewa kwa video ya kuwatia hamu iliyozua mjada mkali mtandaoni.

Kuzinduliwa kwa gari aina ya Type 00 kulizua hisia tofauti kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku wengine wakishangilia muundo wake na wengine wakikejeli uzinduzi huo.

Mwezi uliopita, wakosoaji wengi walisema kuwa video ya matangazo ya modeli hiyo mpya haifanani na gari halisi – lakini kampuni hiyo pia ilisifiwa na wengine kwa ujasiri wake.

Wakati wa hafla ya uzinduzi huko Miami, Mkurugenzi Mtendaji wa Ubunifu wa Jaguar, Gerry McGovern, alisema anafurahi kuona mwelekeo mpya wa kampuni unavyoibua hisia mseto.

Aliandika kwa mtandao wa kijamii, “Jaguar haitaki kupendwa na kila mtu,” alisema.

Hata hivyo, mchambuzi Karl Brauer, alikuwa na mashaka kuhusu utambulisho mpya wa kampuni akihoji ikiwa kweli itafanikiwa.

“Kampuni ya Jaguar inaonekana “kuachana na malengo ya zamani kwa matumaini ya kupata mafanikio siku za usoni,” aliambia BBC.

“Sidhani kama hatua hii waliochukua itafanikiwa”.

Guinea yaanza siku tatu za maombolezo ya kitaifa

Maelezo ya video,Mashabiki wakipanda juu ya kuta kwa hofu baada ya mechi ya soka

Raia wa Guinea leo wataanza kuadhimisha siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kufuatia vifo vya takriban watu 56 katika mkanyagano uliotokea uwanjani kwenye mji wa N’Zerekore Kusini-mashariki.

Waziri Mkuu Amadou Oury Bah ambaye alitembelea eneo la tukio Jumatatu jioni, alisema bendera za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kuashiria kipindi cha maombolezo rasmi.

Mvutano ulizuka wakati wa mechi ya kandanda Jumapili, kufuatia uamuzi wa kutatanisha wa mwamuzi.

Walioshuhudia walisema mashabiki walio na ghadhabu walirusha mawe, na kusababisha hofu na msongamano na mkanyagano katika uwanja huo.

Mashindano ya kandanda yaliandaliwa kwa heshima ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Mamady Doumbouya, lakini upinzani ulikashifu serikali ya kijeshi kwa kutumia michezo kisiasa.

Walidai kuwa mashindano hayo yalikuwa ni mbinu ya kupendelea uwezekano wa Jenerali Doumbouya kugombea wakati wa uchaguzi ambao haujatangazwa.

Katika taarifa yake Rais alitangaza kuwa uchunguzi utaanzishwa ili kubaini chanzo cha mkasa huo huku akiwataka wananchi kuwa watulivu.

Namibia kupata rais wa kwanza Mwanamke

.

Namibia inajiandaa kupata rais wake wa kwanza mwanamke huku thuluthi mbili ya kura za uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita zikihesabiwa mapema hii leo na kumuweka mgombea wa chama tawala cha SWAPO kifua mbele katika uchaguzi ambao upinzani mkuu tayari umeupinga wakidai umekumbwa na udanganyifu.

Makamu wa rais Netumbo Nandi-Ndaitwah kutoka chama tawala ambacho kimeiongoza taifa hilo tangu ipate uhuru miaka 34 iliyopita, alikuwa amepata zaidi ya asilimia 54 ya kura, kulingana na hesabu ya tume ya uchaguzi ni karibu asilimia 66 ya kura zilizopigwa.

Kiongozi wa upinzani Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for change (IPC), ameachwa mbali na asilimia 28 ya kura.

Itula, mwenye umri wa miaka 67, amesema kulikuwa na “mapungufu mengi” na kwamba haijalishi matokeo yatakuwaje, “IPC haitakubali matokeo ya uchaguzi huu.”

Alisema, “Sheria ya utawala imeshindwa kabisa na hatuwezi kuita uchaguzi huu kuwa huru, haki, na wa halali kwa vyovyote vile.”

Uchaguzi wa tarehe 27 Novemba ulilazimika kuahirishwa mara mbili kutokana na matatizo ya kiufundi na ya usafiri, ikiwa ni pamoja na upungufu wa karatasi za kupigia kura, hali iliyosababisha foleni ndefu ambapo baadhi ya wapiga kura walilazimika kukata tamaa baada ya kusubiri kwa saa 12.

Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 72, anaweza kulazimika kwenda kwenye duru ya pili ya uchaguzi ikiwa hatapata zaidi ya asilimia 50 ya kura wakati matokeo yote yatakapotangazwa.

Ikiwa atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hii yenye watu takribani milioni tatu, inayojulikana kwa ukame na mazingira ya hali ya hewa ya jangwa.

Matokeo yaliyotangazwa mapema Jumanne yalikuwa ya majimbo 79 kati ya 121, ikiwa ni pamoja na karibu majimbo yote ya mji mkuu Windhoek. Kwa jumla, wapiga kura milioni 1.5 walisajiliwa, asilimia 73 walipiga kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.

Netumbo Nandi-Ndaitwah akitangazwa mshindi rasmi wa urais atakuwa rais wa tatu mwanamke barani Afrika.

Hakimu aachilia huru mvulana, 15, aliyeshtakiwa kunajisi msichana wa umri wa miaka 18

Msichana aliyelazimishiwa tendo la ngono. Picha|Maktaba

MWANAFUNZI wa Darasa la Saba mwenye umri wa miaka 15 katika shule moja ya msingi jijini Elodret atakumbuka jinsi alivyozuiliwa katika rumande ya watoto kwa miezi minne kwa madai ya kunajisi msichana anayekaribia kutimiza umri wa miaka 18.

B.K alilazimika kuacha masomo yake kwa muda wa miezi minne kwa kuwa alikuwa kizuizini akisubiri uchunguzi wa tuhuma za unajisi.

Kesi yake ilivutia mawakili wawili wakuu kutoka Eldoret ambao walijitolea kumpa huduma za uwakilishi wa bure walipogundua kuwa mvulana huyo alikuwa mwathiriwa wa sheria ya kingono yenye utata ya 2006.

Kutokana na kesi hiyo, mawakili Nathan Oburu na Samuel Ondieki wamefufua mjadala mkali wa kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho au la, haswa kwa kupunguzwa kwa umri wa idhini ya kujamiiana kutoka 18 hadi 16.

Huku akipinga kuzuiliwa zaidi kwa mtoto huyo, wakili Oburu alitetea mteja wake kwa kusema kuwa msichana huyo ndiye aliyepswa kushtakiwa kwa kumnajisi mvulana husika.

“Mshukiwa katika kesi hii ni mdogo zaidi kuliko mlalamishi, ikiwa kuna lolote msichana huyo ndiye aliyepaswa kushtakiwa kwa kumnajisi mteja wangu,” Bw Oburu aliambia Hakimu Mkuu wa Eldoret Peter Areri.

Msimamo sawa ulishikiliwa na wakili mwenzake maoni yake yakiungwa mkono na mwenzake Samuel Ondieki aliyeiomba mahakama kumwachilia mtoto huyo bila masharti yoyote.

“Kwa kuzingatia kwamba mvulana aliye mbele yako ana umri wa miaka 16 tu wakati mlalamishi anakaribia miaka 18. Mahakama inafaa kumwachilia mvulana huyu baada ya kuteseka rumande kwa zaidi ya miezi minne,” akasema Bw Ondieki.

Akitoa uamuzi wake, hakimu Areri alisema kuwa kukamatwa na kuzuiliwa kwa mvulana huyo ni kinyume cha sheria.

“Kukamatwa na kuzuiliwa kwa mshukiwa hakukuwa halali. Uko huru nenda nyumbani,” aliamuru Bw Areri.

Sababu za wanaharakati kutaka Kihika atupwe gerezani

Gavana wa Nakuru Susan Kihika. Picha|Maktaba

KUNDI moja la wanaharakati linataka korti iamuru Gavana wa Nakuru Susan Kihika atupwe ndani miezi sita kuhusiana na uchafuzi wa Ziwa Nakuru.

Shirika la Baboon Project Kenya liliambia Jaji Anthony Ombwayo kuwa Bi Kihika na Meneja Mkurugenzi wa huduma za usafi James Ng’ang’a, walipuuza amri ya korti iliyotolewa Septemba 2024.

Kundi hilo linasema uchafu wa viwanda hutupwa kila kuchao katika ziwa licha ya kuwepo kwa amri ya kusitisha tabia hii.

“Licha ya kujua kuna amri ya korti, washtakiwa na maafisa wao, maajenti na watumishi wamedinda kuiheshimu. Wameendelea kumwaga takataka, kemikali ya sumu na uchafu wa viwanda ziwani,” Wakili Kirui Kiprotich aliambia korti.

Kupitia Katibu wa Kaunti, Bw Samuel Mwaura, Bi Kihika alipinga kesi hiyo akisema si jukumu lake kusimamia Shirika la Huduma ya Maji ya Nakuru.

“Ninapinga kuwepo katika rufaa hii. Mlalamishi hajathibitisha na hawezi kuthibitisha kuwa Gavana amekosa kuheshimu mahakama,” Bw Mwaura akasema katika kesi ambayo itaamuliwa Januari 31.

Katika uamuzi wa Septemba 24, Jaji Ombwayo alibaini kuwa kuna ripoti iliyoangazia kudorora kwa usafi wa maji kwa sababu ya uchafuzi wa Ziwa Nakuru.

Hali hii imetokana na majitaka, maji ya mvua yanayosomba uchafu hadi majini na taka za viwanda.

“Korti hii imeamua kuwa rufaa hii ina usahihi kwa sababu washtakiwa (serikali ya kaunti) ina jukumu kubwa katika usimamizi na utunzaji wa mazingira (Ziwa Nakuru), jukumu ambalo wamepuuza,” jaji wa  Mahakama ya Mazingira na Ardhi alisema.Jaji huyo alitoa amri ya kulazimisha serikali ya kaunti na shirika la maji kutafuta suluhu mbadala ya kutupa kemikali ya sumu na uchafu wa viwanda.

Walinda mazingira walisema wachafuzi hawa wanafanya hivi kwa makusudi na wanaendelea kuchafua ziwa hilo, kitendo ambacho kinahatarisha afya ya wanyamapori.

Mkurugenzi wa kundi hilo Simon Gichohi Mbuthia anaamini serikali ya Kaunti ya Nakuru ina jukumu kubwa kufuata ilani na ripoti kuhusu uchafuzi wa ziwa.

Alitaja ilani mbalimbali pamoja na ripoti ya Taasisi ya Maji na Uvuvi nchini iliyobaini kuwa kuna sumu na uchafu mwingi katika ziwa Nakuru.

Maswali serikali ikirejesha sheria ya upakiaji viazi iliyopingwa vikali awali

Mwanamke akikalia gunia kubwa la viazi akisafirishwa na bodaboda. Serikali inataka sheria irudi ambapo viazi vitapakiwa kwenye magunia ya kilo 50 pekee. Picha|Maktaba

WIZARA ya Kilimo itaanza kutekeleza Sheria ya Viazi Ulaya ya 2019 ambayo inaweka kikomo cha upakiaji wa viazi kuwa kilo 50.

Utekelezaji huu ulisitishwa miaka mitatu iliyopita baada ya kuibuka kwa pingamizi.

Meneja wa Baraza la Kitaifa la Ukuzaji Viazi Henry Chemjor amesema uamuzi wa usitishaji huo mnamo 2021 ulitokana na vikao vya kusikiliza malalamishi ya wakulima na changamoto nyingine.

“Tumeanza mazungumzo na Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) na washirika wengine kupiga jeki utekelezaji,” akasema Bw Chemjor.

Tayari AFA imetoa mafunzo kwa zaidi ya wakaguzi 250 wa mimea kusaidia katika msako wa wanaokiuka kanuni kwa kurefusha magunia hivyo kuwapunja wakulima.

Magunia makubwa yaliyopakiwa viazi kinyume cha sheria shambani Narok.

Katika kanuni hiyo, wakulima, wanabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wanahitajiwa kujisajili na serikali za kaunti; la sivyo watozwe faini ya Sh5 milioni ama kifungo cha miaka mitatu jela.

Bw Chemjor alizungumza katika soko la Katheri, Kaunti ya Meru katika warsha ya mafunzo ya wakulima kuhusu kilimo cha viazi.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Korea Kusini, KOPIA.

Baraza la viazi limekuwa likitoa hamasa kwa wakulima ili kuwawezesha wakumbatie kanuni hii.

Afisa Mkuu wa Kilimo, Kaunti ya Meru, James Mutia alisema utekelezaji wa sheria hii utakumbwa na changamoto iwapo wakulima hawatajifunza mbinu za kisasa za kuhifadhi mazao.

Vibarua wapakia magunia ya viazi kwenye trekta Narok.

Bila mbinu hizi, wakulima hulazimika kuuza viazi baada ya kuvuna kwa bei ambayo inaamuliwa na madalali.

“Hata tukiwaambia Wakulima wauze viazi kwa magunia ya kilo 50 na hali hawajui kuhifadhi, watalazimika kuuza kwa mnunuzi yeyote ama mavuno yaharibike,” akasema Bw Mutia.

Mkurugenzi wa KOPIA Kenya Ji Gang Kim anasema, takriban asilimia 20 ya viazi ambavyo huvunwa Meru huharibika ama kupotea kila mwaka kwa sababu ya usimamizi mbaya wa mavuno.

Hii ina maana kuwa, angalau tani 815,000 za viazi huharibika baada ya mavuno.

Mshirikishi wa KOPIA eneo la Meru, Julius Gitonga alisema wamekita maghala katika maeneo ya Katheri na Murungurune ambapo wakulima watahifadhi viazi kwa angalau mwezi mmoja baada ya mavuno.

Vibarua wakivuna viazi ulaya Narok.

Makachero wachunguza mkulima wa miraa kuzikwa kisiri na binamu zake

Utepe wa polisi katika eneo la mkasa. Picha|Maktaba

MAKACHERO wanaendelea kufanya uchunguzi kuhusu kisa ambacho mkulima wa miraa aliuawa na mwili wake ukapatikana umezikwa kwenye kaburi la kina kifupi katika kijiji cha Kivwe, Kaunti ya Embu.

Mkulima huyo Apodia Njuki Njoka, 32, alitoweka mnamo Novemba 24 lakini mnamo Disemba 2, mwili wake ambao ulikuwa na majeraha mabaya ulipatikana umezikwa kwenye boma la binamu wake wawili.

Wanakijiji ambao walikuwa na hamaki waliwafurusha binamu hao kutoka nyumba zao na kudai walihusika na mauti hayo kisha kumvamia mmoja wao.

Mmoja wao aliokolewa na polisi na akakimbizwa hadi Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Siakago kabla ya kuhamishwa hadi hospitali ya rufaa ya Embu akiwa katika hali mbaya kiafya.

Kwa mujibu wa familia, marehemu Njoka alitoweka nyumbani wiki moja iliyopita. Familia yake ilianza kumtafuta kwenye vichaka na maeneo jirani lakini hawakumpata.

Mnamo Jumapili, baada ya kupigwa jeki na wakazi, familia hiyo ilipata kaburi ambalo ndilo lilikuwa limechimbwa na wakashuku Bw Njoka alikuwa amezikwa hapo.

Hapo ndipo waliwafurusha binamu hao kutoka nyumba zao wakawaangushia kipigo kikali na kutisha kuwaua wasipowaambia wakitaka ukweli.

Kuona mambo yanawaendea vibaya, ndugu hao walifunguka na kusema walimzika Bw Njoka kwenye kaburi hilo na wakakiri kuwa walihusika na mauaji yake.

Wakazi waliendelea kuwapiga na kuwajeruhi vibaya huku wakilaani mauaji hayo. Polisi kutoka Siakago walifika na kuwaokoa wawili hao kisha kuwapeleka katika Hospitali ya Siakago ambapo mmoja wao aliaga dunia.

Inahofiwa kuwa Bw Njoka aliuawa na kuzikwa kisiri kutokana na mzozo wa shamba.

Phrisnah Wanjue, dadake marehemu  alisema kuwa nduguye aliuawa kwa njia ya kikatili na akasisitiza kuwa lazima wapate haki.

“Tunashuku aliuawa kwa sababu alikuwa na shamba kubwa la miraa karibu na boma la washukiwa ambao walikuwa wakilimezea mate. Walitaka kuchukua shamba hilo kiharamu ndiposa walikuwa wakitaka kulichukua,” akasema Bi Wanjue.

Mauti ya Bw Njoka, baba wa watoto wanne, wote wakiwa mapacha kumeiacha familia, wakazi na marafiki zake wakiwa na mshtuko.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mbeere Kaskazini Eric Yego alisema makachero wanaendelea kuchunguza mauti hayo na kutoa wito kwa familia wake wawe watulivu na wanakijiji wadumishe amani.

“DCI wamechukua usukani na wanasuburi mwili huo ufukuliwe kisha hapa ndipo watafahamu jinsi ambavyo marehemu aliuawa. Hili ni suala ambalo lipo mikononi mwetu na tunatoa wito kuwe na utulivu,” akasema Bw Yego.

Ikiwa umekuza pamba nzuri na nyeupe ilete tutanunua pesa nzuri, kiwanda chatangaza

Mkulima akivuna pamba eneo la Keiyo Kaskazini, Elgeyo Marakwet. Kiwanda cha nguo Thika kinasema kina soko tayari kwa pamba katika juhudi za kufufua biashara ya nguo nchini

KIWANDA cha kutengeneza nguo cha Thika, kimewahimiza wakulima hapa nchini kurejelea kilimo cha pamba kwa wingi.

Meneja wake mkuu wa maendeleo, Bw Hesbon Olweny’, alisema tayari wamezuru kaunti ya za Siaya, Homabay, Machakos,  na Busia kuwarai wakulima warejelee kilimo cha pamba kwa wingi.

Chini ya miaka miwili  sasa, kiwanda hicho kimetumia zaidi ya Sh70 milioni kwa kuinua kilimo cha pamba huku kikiwapa wakulima vifaa vya kilimo na mbegu za upanzi.

Meneja huyo amepongeza serikali kwa kuwa na ushirikiano wa karibu nao kwa kuhakikisha ukuzaji wa pamba umefufuliwa katika maeneo tofauti nchini.

Kiwanda hicho kinaendeleza kauli mbiu ya “Nunua Kenya, Jenga Kenya” ili Wakenya wazidi kununua bidhaa zao za hapa nchini na kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi ambazo zinalemaza viwanda vya humu nchini.

Wakulima wamehakikishiwa soko la haraka ambapo kiwanda hicho kiko tayari kununua pamba kuanzia Sh78 kwa kila kilo kutoka Sh52 za hapo awali.

Vilevile, kiwanda hicho kina mipango ya kufufua viwanda vya pamba vilivyofungwa hapo awali. Viwanda vya Madiany’ katika Kaunti ya Siaya na Luanda – Samia, Kaunti ya Busia ni kati ya vilivyofufuliwa.

Meneja huyo alieleza kuhusu ujio wa nguo za mitumba nchini ambayo ilisababisha viwanda vingi vya kushona nguo kufungwa hapa nchini.

KIPENGA CHA MICHEZO

Guardiola: Sina ‘stress’, ninachojua ni kwamba Man City itafufuka na kuumiza upinzani

Mkufunzi wa Manchester City Pep Guardiola akizungumza kabla ya mechi. Picha|Reuters

LONDON, UINGEREZA

NYAKATI zimekuwa ngumu kwa Manchester City chini ya Pep Guardiola, lakini kumekuwa na hisia kwamba wataamka na watakuwa sawa huko mbele.

Mashine ya City inaonekana imevunjika, udhibiti ambao umewaendesha kwa muda mrefu haupo, umekwenda. Walipata kipigo kingine, cha sita katika mechi saba za mashindano yote. Ni wazi sasa kwamba, itakuwa ni vigumu kwao kutetea taji.

Umati wa mashabiki wa Liverpool ulimjulisha Guardiola kwamba, atatimuliwa asubuhi, jambo ambalo lilimfanya kuwakumbusha kwa kuinua vidole sita kuashiria kiasi cha mataji ya Ligi ya Premia ambayo ameshinda tangia alipofika Etihad mwaka 2016.

Ushindi huo mkubwa wa Liverpool wa 2-0 dhidi City Jumapili usiku ugani Anfield, ulifungua mwanya wa alama tisa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mabao hayo yakitiwa kimiani na wing’a Cody Gakpo na kiungo Mohammed Salah dakika ya 12 na 78 kupitia penalti mtawalia.

Kipigo cha City kimewafanya kuporomoka hadi nafasi ya tano chini ya Brighton & Hove Albion wakiwa na alama sawa (23).

Baada ya mechi 13, ‘Kompyuta bora’ ya Opta inaipa Liverpool nafasi ya 85.1% ya kunyanyua taji lao la 20 la EPL la hivi maajuzi wakiwa wameshinda taji hilo msimu wa 2019/20 chini ya kocha wa zamani Jurgen Klopp.

“Ni nafasi nzuri kuwamo,” alisema kocha wa mpya wa Liverpool Arne Slot baada ya mechi hiyo.

“Nyinyi mnajua zaidi kuliko mimi kwamba Arsenal na City wanaweza kushinda kila mechi kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu. Chelsea wanaweza kushinda kila mechi. Inaifanya EPL kuwa ya kuvutia sana.”

“Msimu uliopita kulikuwa na tofauti kubwa ya pointi kati ya Arsenal na City na bado waliweza kurejea mchezoni na kutwaa ubingwa.”

Arsenal ambao walimaliza nafasi ya pili nyuma ya City kwa misimu miwili iliyopita, pamoja na Chelsea wanafanya vyema zaidi msimu huu kuliko ilivyotarajiwa chini ya Enzo Maresca – wanashika nafasi ya tatu na alama sawa (23).

Lakini je, kushinda mataji sita ya kunamfanya Guardiola aepuke kufutwa?

Guardiola pia alikiri kwamba huenda “anastahili kufukuzwa” baada ya mechi yake ya saba mfululizo bila ushindi.

“Matokeo yatatusaidia kuona zaidi, lazima niwaone wachezaji wakirudi na kuwa bora zaidi kimwili, ni ngumu katikati ya msimu kwa sababu hatuwezi kubadilika, ni jambo lingine na hatuwezi kutarajia zaidi ya hili.

Guardiola alisema anahitaji kutafuta suluhu ili kuwa imara.

“Lazima nitafute suluhu la kuwa imara, nyuma hasa. Wachezaji hawa wamenipa nafasi ya kuishi labda miaka bora zaidi ya maisha yangu.

“Ninachoweza kufanya ni kuwa hapa kujaribu kutafuta suluhu. Katika wakati mwafaka klabu itafanya uamuzi kuhusu kile kinachohitajika kuruhusu klabu hii kuwa bado ipo.”

Bingwa wa dunia Dubois kuzichapa na Parker nchini Saudi

Muingereza Daniel Dubois atatetea taji lake la uzito wa juu duniani dhidi ya bingwa wa zamani Joseph Parker nchini Saudi Arabia mnamo tarehe 22 Februari.

Dubois, 27, alitetea mkanda wake wa kwanza wa IBF kwa kuzichapa na Anthony Joshua mnamo mwezi Septemba.

Parker wa New Zealand, 32, alishikilia taji la WBO kati ya 2016 na 2018 kabla ya kupoteza kwa Joshua.

Pia huko mjini Riyadh, Artur Beterbiev atatetea taji lake la uzito wa light-heavy katika pambano la marudiano na Mrusi mwenzake Dmitry Bivol.

Mchezaji wa London ambaye hajashindwa Hamzah Sheeraz atatetea taji lake la kwanza la dunia dhidi ya bingwa wa uzito wa kati wa WBC Carlos Adames, huku Waingereza wa uzani wa light-heavy, Joshua Buatsi na Callum Smith wakizichapa ulingoni kuwania taji la muda la WBO la Buatsi.

Shakur Stevenson atatetea mkanda wake wa WBC uzani mwepesi dhidi ya Floyd Schofield huku Zhilei Zhang akipambana na Agit Kabayel kuwania taji la muda la WBC uzani wa juu.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment