Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamoja
Muhtasari
- India na Bangladesh zazozana kuhusu kukamatwa kwa mtawa wa Kihindu
- Marekani kuanzisha juhudi mpya za mapatano Gaza
- Trump amteua mshauri wa kibiashara baada ya kuzitishia nchi washirika kuziwekea ushuru wa juu
- Mwendesha mashtaka wa ICC aomba hati ya kukamatwa kiongozi wa Myanmar
- Polisi aliyempiga ajuza wa miaka 95 bastola ya shoti apatikana na hatia ya mauaji
- Wanachama wawili wa Chadema wauawa, mmoja kwa risasi
- Nchi kadhaa zataka kusitishwa mapigano Gaza baada ya mapatano ya Lebanon
- Manusura wa tano wa boti iliyozama katika bahari ya Shamu wapatikana
- Maelfu ya watu waanza kurejea makwao baada ya usitishaji mapigano kati ya Israel na Hezbollah
- Urusi na Ukraine Mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi waathiriwa na shambulio la Ukraine
- Tanzania Mkurugenzi Mteule wa WHO, Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile aaga dunia
- Uchaguzi Tanzania Watanzania wapiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa
- Tunachokijua kuhusu mpango wa Israel na Hezbollah wa kusitisha mapigano
- Israel na Hezbollah Mpango wa Israel, Hezbollah kusitisha mapigano waanza baada ya shambulio jipya Beirut
India na Bangladesh zazozana kuhusu kukamatwa kwa mtawa wa Kihindu

Kukamatwa kwa mtawa wa Kihindu nchini Bangladesh kumezua vita vipya vya maneno na jirani yake India kuhusu hali ya jamii ya wachache nchini humo.
Chinmoy Krishna Das, msemaji wa shirika la Wahindu lenye makao yake Bangladesh, alikamatwa wiki hii kwa tuhuma za uchochezi, na kusababisha vurugu zilizopelekea kifo cha mtu mmoja.
India ilitoa taarifa ikielezea “wasiwasi mkubwa” juu ya kukamatwa kwake na kuitaka Bangladesh kuhakikisha usalama “wa Wahindu na jamii nyingine za walio wachache.”
Bangladesh ilijibu saa chache baadaye, ikielezea “kusikitishwa kwake juu ya kueleweka vibaya na baadhi ya watu kuhusu kukamatwa kwake.”
Uhusiano kati ya majirani hao, ambao kwa kawaida wamekuwa na uhusiano wa kindugu, umekuwa wa vita baridi tangu waziri mkuu wa zamani Sheikh Hasina kuondolewa madarakani mwezi Agosti baada ya maandamano ya wanafunzi ya wiki kadhaa.
Tangu wakati huo, amekuwa akikaa India, na kutoa changamoto kwa diplomasia kati ya nchi hizo.
Wakati wa uongozi wa Hasina wa miaka 15, Bangladesh ilikuwa mshirika wa kimkakati na mshirika muhimu kwa usalama wa India, hasa katika majimbo ya kaskazini-mashariki.
Tangu kuondolewa kwake madarakani, India mara kwa mara imeelezea wasiwasi kuhusu usalama wa Wahindu walio wachache nchini Bangladesh, madai ambayo Bangladesh inayakanusha.
Wahindu ndio walio wachache zaidi katika nchi ya Bangladesh yenye Waislamu wengi, ambao ni takribani 8% tu ya wakazi.
Marekani kuanzisha juhudi mpya za mapatano Gaza

Rais Joe Biden amesema Marekani itaanzisha juhudi nyingine kwa kushirikiana na serikali za kikanda ili kufikia usitishwaji mapigano huko Gaza, ikijumuisha kuachiliwa kwa mateka na kuondolewa kwa Hamas mamlakani.
Matamshi yake huko X yanakuja saa chache baada ya kusitishwa kwa mapigano nchini Lebanon kati ya Israel na Hezbollah, na kumaliza kwa vita vya karibu miezi 14.
“Katika siku zijazo, Marekani itafanya juhudi nyingine kwa kushirikiana na Uturuki, Misri, Qatar, Israeli na nchi nyingine kufikia usitishaji wa mapigano huko Gaza na mateka kuachiliwa na kumalizika kwa vita bila Hamas kuwepo madarakani,” aliandika Biden kwenye X. .
Hamas imesema inatumai kupata makubaliano kama hayo huko Gaza lakini inaendelea kukataa matakwa ya Israel, ya kujisalimisha.
Israel ilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 44,000 wameuawa na zaidi ya 104,000 wamejeruhiwa huko Gaza tangu mashambulizi hayo yalipoanza, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Trump amteua mshauri wa kibiashara baada ya kuzitishia nchi washirika kuziwekea ushuru wa juu

Rais mteule wa Marekani Donald Trump anasema Jamieson Greer atakuwa mshauri wa sera kibiashara atakapo chukua madaraka tarehe 20 Januari 2025.
Tangazo hilo linakuja baada ya Trump kutishia kuweka ushuru mpya – kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China, Canada na Mexico ili kudhibiti mtiririko haramu wa watu na dawa za kulevya kuingia Marekani.
Greer, mwanasheria wa biashara, alikuwepo katika muhula wa kwanza wa urais wa Trump – na alichukua jukumu muhimu katika kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa kutoka China.
Ni sera ya muda mrefu ya Trump ili kuhimiza wateja kununua bidhaa za ndani za Marekani kwa kufanya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kuwa ghali.
Mwendesha mashtaka wa ICC aomba hati ya kukamatwa kiongozi wa Myanmar

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), anasema ameomba hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Min Aung Hlaing kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu alioufanya dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Karim Khan amesema kuna sababu za kuridhisha za kuamini kuwa Min Aung Hlaing alihusika na utekelezaji wa jinai kwa kuwatesa na kuwafukuza Warohingya hadi nchi jirani ya Bangladesh.
Maelfu ya Warohingya waliikimbia Myanmar mwaka 2017 ili kuepuka mashambulizi ambayo Umoja wa Mataifa umeyataja kuwa mauaji ya halaiki yaliyoanzishwa na jeshi la Burma.
Lakini serikali ya Myanmar imekanusha hilo, ikisema ilikuwa ikiendesha operesheni dhidi ya wanamgambo wa Rohingya.
Mashambulizi dhidi ya Warohingya yalianza mwaka 2017, baada ya wanamgambo wa Rohingya kushambulia vituo zaidi ya 30 vya polisi nchini Myanmar.
Warohingya wanasema askari walijibu mashambulizi hayo kwa kuchoma vijiji vyao, kuwashambulia na kuua raia.
Takribani Rohingya 6,700, ikiwa ni pamoja na watoto wasiopungua 730 walio na umri wa chini ya miaka mitano, waliuawa katika mwezi mmoja baada ya ghasia kuanza, kulingana na shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF).
Amnesty International inasema jeshi la Myanmar pia liliwabaka na kuwadhalilisha wanawake na wasichana wa Rohingya.
Ghasia za kutisha dhidi ya Warohingya zilisababisha malalamiko ya kimataifa, lakini kiongozi wa wakati huo wa Burma, Aung San Suu Kyi alikataa kuwafungulia mashitaka majenerali wake.
Myanmar haijajiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, hivyo kufungua kesi dhidi ya jeshi awali ilionekana kuwa haiwezekani.
Hata hivyo, waendesha mashitaka wa ICC baadaye walisema baadhi ya makosa ya jinai, hasa kufukuzwa nchini, yalitokea Bangladesh – ambayo imejiunga na mahakama – na kulikuwa na sababu za kufunguliwa mashitaka.
Baada ya miaka mitano ya uchunguzi, mwendesha mashtaka mkuu anasema ana ushahidi wa kutosha kuomba hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Min Aung Hlaing.
Polisi aliyempiga bastola ya shoti ajuza wa miaka 95 apatikana na hatia ya mauaji

Afisa wa polisi aliyempiga shoti kupitia bastola mwanamke mwenye umri wa miaka 95, aliyekuwa na dalili ya tatizo la akili katika nyumba ya kutunza wazee nchini Australia amepatikana na hatia ya mauaji.
Kristian White, 34, alitumia silaha yake dhidi ya Clare Nowland baada ya ajuza huyo kukutwa akirandaranda na kisu kidogo cha jikoni tarehe 17 Mei 2023.
Kifo chake wiki moja baadaye kilisababisha malalamiko ya umma, lakini White – afisa wa ngazi ya juu wa polisi – alisema mahakamani kwamba matumizi yake ya nguvu yalikuwa halali na sawa kwa tishio lililokuwepo.
Hata hivyo, waendesha mashtaka, walisema Bi Nowland – ambaye alitegemea mkongojo kutembea akiwa na uzito wa chini ya kilo 48 – hakuwa hatari na afisa huyo “asiyekuwa na subira” alipuuza wajibu wake wa kumhudumia ajuza huyo.
Maafisa wa polisi walimwomba mara kadhaa adondoshe kisu chake. Muda mfupi kabla ya kupigwa shoti, kanda za video zilionyesha mwanamke huyo akitembea kusonga mbele polepole – mita 1 kwa muda wa dakika moja – kabla ya kusimama na kuinua kisu chake.
White alimuonya Bi Nowland kabla ya kufyatua bastola ya shoti, akiwa umbali wa mita 1.5 hadi 2. Alianguka na kufikia kichwa chake, na kusababisha ubongo kuvuja damu.
Mwendesha mashtaka alisema White alitumia silaha yake dakika tatu tu baada ya kumfikia mwanamke huyo: “Alikuwa amekasirika, hana subira, hakuwa tayari kusubiri.”
Familia ya Bi Nowland, iliyokuwa mahakamani kusikiliza uamuzi wa hakimu, iliwashukuru waendesha mashtaka na hakimu.
White, ambaye atasalia nje kwa dhamana, atahukumiwa baadaye.
Wanachama wawili wa Chadema wauawa, mmoja kwa risasi

Jeshi la Polisi nchini Tanzania, linamshikilia Askari Magereza kwa tuhuma za kusababisha Kifo cha George Juma (41), aliyekuwa Mgombea katika Kitongoji cha Stendi, Kata ya Mkwese, Jimbo la Manyoni Mashariki kupitia Chadema katika Uchaguzi unaoendelea wa Serikali za Mitaa.
Taarifa ya Polisi inasema marehemu alijeruhiwa na risasi katika purukushani zilizotokea, baada ya wafuasi wa Chadema kuwavamia wafuasi wa chama tawala CCM waliokuwa katika kikao cha ndani na hivyo Askari Magereza katika kituo cha karibu walipigiwa simu.
Taarifa hiyo inasema, walipofika eneo hilo walishambuliwa kwa mawe ambapo walipiga risasi hewani ili kuwazuia wafuasi wa Chadema, na katika purukushani hizo, risasi moja ilimpata Marehemu George Juma.
Lakini taarifa ya Polisi inakinzana na ile ya Chadema, ambapo chama hicho kikuu cha upinzani kinasema mwanachama wake alivamiwa nyumbani kwake na watu waliofahamika kuwa makada wa CCM, ndipo ukatokea mzozo na Polisi walifika nyumbani kwake na kumpiga risasi ndugu George Juma Mohamed na kufariki dunia .
Katika tukio jingine mwanachama na kiongozi wa Chadema katika Mji wa Tunduma, Steven Chalamila ameripotiwa kushambuliwa kwa mapanga na kuuawa.
Vyombo vya habari vya ndani nchini Tanzania, vikinukuu taarifa ya Chadema, vinasema mauaji hayo yamefanyika nyumbani kwa mwanachama huyo usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024.
Ingawa Jeshi la Polisi bado halijatoa taarifa rasmi juu ya tukio hili.
Matukio haya yanakuja wakati Tanzania ikianza uchaguzi wa serikali za mitaa siku ya leo, kuwachagua viongozi wao wa mashinani.
Nchi kadhaa zataka kusitishwa mapigano Gaza baada ya mapatano ya Lebanon

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon yalihusisha pande kadhaa za kimataifa; yalisimamiwa na Marekani, huku Ufaransa ikitarajiwa kusaidia kufuatilia makubaliano hayo.
Asubuhi ya leo, Uturuki imeunga mkono kuanzishwa kwa “amani ya kudumu” nchini Lebanon. Katika chapisho kwenye X, wizara yake ya mambo ya nje inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa “kutoa shinikizo” kwa Israel “kutoa fidia kwa uharibifu uliosababisha nchini Lebanon.”
Iran, ambayo inaiunga mkono Hezbollah, inasema inakaribisha habari za kumalizika kwa “mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon.”
Wakati usitishaji mapigano ukianza nchini Lebanon, mapigano yanaendelea kusini ya Gaza. Hii imeifanya Jordan – ambayo inapakana Israel upande wa Mashariki – kutoa wito wa juhudi kubwa zaidi za kimataifa ili kumaliza vita huko Gaza.
Pia Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, anasema mpango huo lazima uwe “suluhisho la kudumu” nchini Lebanon, na kuongeza kuwa lazima kuwe na “maendeleo ya haraka” kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Manusura watano wapatikana siku moja baada ya boti kuzama Bahari ya Shamu

Timua ya uokoaji kutoka Misri imepata miili minne na manusura watano siku ya Jumanne wakati wa msako katika Bahari ya Shamu baada ya boti ya watalii iliyokuwa imebeba watu 44 kuzama siku ya Jumatatu.
Jumla ya watu 33 wameokolewa kufikia sasa lakini saba bado hawajapatikana kufikia Jumanne jioni.
Boti hiyo ya kisasa ilikuwa imebeba watalii 31 na wafanyakazi 13, kabla ya kupigwa na wimbi kubwa karibu na mji wa Marsa Alam na kusababisha kupinduka.
Boti hiyo ilizama ndani ya dakika tano hadi saba tangu kuondoka, kwa mujibu wa gavana wa Bahari ya Shamu, Maj-Gen Amr Hanafi. Anasema baadhi ya watu walishindwa kutoka kwenye vyumba vyao.
Jumla ya watu 28 waliokolewa na wanajeshi na boti ya watalii iliyokuwa ikipita saa chache baada ya boti hiyo kuzama.
Boti hiyo yenye urefu wa mita 44 (futi 144) iliondoka kwenye bandari karibu na Marsa Alam siku ya Jumapili kwa safari ya siku tano ya kupiga mbizi.
Wananchi wa Namibia wapiga kura wakati chama tawala kikijaribu kuongeza tena utawala wa miaka 34
Chanzo cha picha,AFPUpigaji kura unaendelea nchini Namibia katika uchaguzi ambao unaweza kuwa wenye ushindani mkubwa tangu uhuru wake baada ya kutawaliwa na wazungu miaka 34 iliyopita.
Netumbo Nandi-Ndaitwah anatafuta kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.Anapeperusha bendera ya Chama tawala cha (Swapo), kuchukua nafasi ya Hage Geingob, ambaye alifariki Februari baada ya kukaa madarakani kwa miaka tisa.Lakini ukosefu mkubwa wa ajira, umasikini, ukosefu wa usawa na madai ya ufisadi yameondoa uungwaji mkono kwa chama.
Mpinzani mkuu wa Nandi, Ndaitwah ni Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for Change (IPC), pamoja na wagombea wengine 14.Vyombo vya habari vya ndani vilionesha misururu mirefu iliyokuwa tayari shuleni na vituo vingine vya kupigia kura huku upigaji kura ukianza Jumatano asubuhi.
Mshirikishe mwenzako, Wananchi wa Namibia wapiga kura wakati chama tawala kikijaribu kuongeza tena utawala wa miaka 34
Maelfu ya watu waanza kurejea makwao baada ya usitishaji mapigano kati ya Israel na Hezbollah

Vikosi vya Israel bado viko sehemu za kusini, huku kuondoka kwao kukitarajiwa kuwa kwa taratibu wakati wa usitishaji mapigano wa siku 60.
Jeshi la Lebanon, linalotarajiwa kuongeza uwepo wake kusini na wanajeshi 5,000 wa ziada, lilisema linachukua “hatua zinazohitajika” kukamilisha hilo.

Maelfu ya watu wameanza kurejea makwao, saa chache baada ya kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah kuanza kutekelezwa.
Kuna msongamano wa magari kwenye barabara kuu kati ya Beirut na kusini, na magari yamejaa familia, mifuko, masanduku na magodoro.
Tumeona bendera nyingi za Hezbollah zikipeperushwa kwenye madirisha.
Watu wengine, wanapoona kamera yetu, wanatabasamu na kutoa ishara ya “V” ya ushindi.
Hatua hii inafanyika wakati mamlaka ya Israel na Lebanon zikionya watu wasirejee sasa.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi waathiriwa na shambulio la Ukraine

Urusi imesema kuwa mfumo muhimu wa ulinzi wa anga na kambi ya anga katika eneo la Kursk ilipigwa na Ukraine kwa makombora ya Atacms yanayotolewa na Marekani.
Taarifa ya wizara ya ulinzi, ambayo ilitishia kulipiza kisasi, imekuja siku moja baada ya Ukraine kusema ilikuwa imefikia malengo katika eneo hilo.
Wakati huohuo jeshi la anga la Ukraine lilisema Urusi ilirusha droni 188 katika shambulio moja Jumatatu usiku, na kuharibu miundombinu muhimu.
Mvutano umekuwa mkubwa tangu Marekani iliporipotiwa kuruhusu Ukraine kutumia makombora ya Atacms kwenye shabaha ndani ya Urusi wiki iliyopita, ili kujibu hatua ya Urusi kupeleka wanajeshi wa Korea Kaskazini.
Wiki hiyo ilimalizika kwa Urusi kutumia kombora jipya la masafa ya kati la Oreshnik kwenye mji wa Dnipro nchini Ukraine.
Mashambulizi ya kwanza yaliyoripotiwa kufanywa na Atacms katika eneo la Urusi yaliripotiwa Jumanne, wakati Urusi iliposema kuwa vipande vilivyoanguka vilisababisha moto katika kituo cha kijeshi.
Mkurugenzi Mteule wa WHO, Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile aaga dunia

Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile ameaga dunia.
Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ametangaza taarifa za kifo chake kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 27, nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
”Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile. Kwa niaba ya Wabunge ninatoa pole kwa familia, wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote.” Alisema Spika Tulia.
Naye Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote.
Dkt Ndugulile pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya ya Bunge la Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa (IPU) Advisory Group Health na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH).
Dk. Ndugulile aliwahi kuwa naibu waziri wa Afya wa Tanzania kati ya 2017-2020, pia aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari 2020-2021.
Pia alifanya kazi kama mkurugenzi katika Wizara ya Afya Tanzania anayeshughulikia huduma za uchunguzi na pia meneja wa programu mwanzilishi wa Huduma ya Kitaifa ya Usambazaji Damu mwaka 2006.
Kati ya 2007-2010, aliwahi kuwa Mshauri Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini akitoa msaada wa kiufundi kwa nchi nyingine nyingi kama vile Angola, Msumbiji, Tanzania na Rwanda.
Watanzania wapiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa

Watanzania hii leo wanapiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Wapiga kura wanapiga jumla ya kura sita; Wajumbe kundi la wanawake 2, Wajumbe kundi mchanganyiko 3, na Mwenyekiti wa Mtaa 1.







Tunachokijua kuhusu mpango wa Israel na Hezbollah wa kusitisha mapigano

- Mpango huo unajumuisha “kuondoka kwa awamu” kwa wanajeshi wa Israeli kutoka Lebanon katika kipindi cha siku 60 zijazo.
- Jeshi la Lebanon litasaidia kushika doria katika eneo karibu na Blue Line huku jeshi la Israel likielekea kusini na Hezbollah kuelekea kaskazini.
- Marekani na Ufaransa zitajiunga na utaratibu uliopo wa Utatu, ambao kwa sasa unajumuisha jeshi la Lebanon, jeshi la Israel na Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (Unifil), kusaidia kutekeleza makubaliano katika eneo hili.
- Malalamiko yote ya uwezekano wa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yataelekezwa Marekani.
- Hakutakuwa na wanajeshi wa Marekani ardhini nchini Lebanon, lakini vikosi vya Marekani na Ufaransa vitasaidia jeshi la Lebanon kupitia mafunzo na kusaidia mawasiliano.
- Marekani, Ufaransa na nchi nyingine pia zitatoa msaada wa kiufundi na kifedha kwa wanajeshi wa Lebanon kupitia Kamati ya Kijeshi ya Kijeshi, au MTC.
- Mpango huo unatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia ukuaji wa uchumi na miundombinu kusini mwa Lebanon katika juhudi za kuweka mazingira yanayoweza kusababisha “kusitishwa kwa mapigano kuwa kwa kudumu”.
Mpango wa Israel, Hezbollah kusitisha mapigano waanza baada ya shambulio jipya Beirut

Mpango wa makubaliano ya Israel na Hezbollah kusitisha mapigano uliotangazwa siku ya Jumanne lazima sasa kutekelezwa.
Iwapo makubaliano hayo yatadumu, yatamaliza vita vya zaidi ya mwaka mmoja kati ya Israel na kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran.
Mapigano hayo yaliongezeka sana mwezi Septemba, wakati Israel ilipozidisha mashambulizi ya mabomu na kuanzisha uvamizi mdogo wa ardhini.
Kama ukumbusho, chini ya masharti ya usitishaji vita, vikosi vya Israeli vitaondoka Lebanon ndani ya siku 60, wakati vikosi vya Hezbollah vitachukuliwa na vikosi vya jeshi la Lebanon kusini mwa nchi katika kipindi hicho.
“Kuumaliza utawala wa Khamenei ni chaguo pekee la Israeli katika mgogoro wake na Iran” – Yedioth Ahronoth

Katika uchanganuzi wa magazeti ya leo, tutajadili makala kadhaa, ikiwa ni pamoja na moja ambayo inasema kuwa chaguo pekee kwa Israeli katika mgogoro wake na Iran ni kuumaliza utawala wa Khamenei, na makala nyingine inahusu fursa inayopatikana kwa Iran na nchi za Kiarabu kuunda mfumo mpya, rahisi zaidi na endelevu wa kikanda, na hatimaye makala kuhusu mgawanyiko wa muungano wa Magharibi baada ya Mahakama ya kimataifa ya uhalifu kutoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu.
Tunaanza na gazeti la Israeli Yedioth Ahronoth na makala ya maoni iliyoandikwa na Jacob Nagel na Mark Dubowitz yenye kichwa cha habari “Chaguo la Pekee la Israeli Kuhusu Iran ni kukomesha Utawala wa Khamenei.” Mwandishi anaanza kwa kurejelea kauli ya awali ya kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei, ambapo alitabiri uharibifu wa mwisho wa Israeli ifikapo mwaka 2040.
Mwandishi anasema kwamba wakati Khamenei anapotangaza kwamba mpango wake ni kuiangamiza Israel wakati huo, bila shaka anafanya kila awezalo kufikia azma hii, kwa msaada wa wafuasi wa Iran nyumbani na nje ya nchi, na lazima tushughulikie suala hilo kwa umakini.
Mwandishi anaongeza kuwa Israel haipaswi kuridhika na mkakati wa kuzuia kushambuliwa kama lengo lake, badala yake inapaswa kubadilisha mkakati wake kabisa na kuhama kutoka ulinzi hadi mashambulizi ya vitendo, ili lengo la Israeli liwe kumaliza utawala wa Khamenei ifikapo mwaka 2030.
Mwandishi anaamini kuwa utawala wa Iran ndio mfadhili mkuu wa ugaidi duniani, na kuyumbisha Mashariki ya Kati, ikitamani kumiliki silaha za nyuklia, akibainisha kuwa Tehran imejihami na kuongoza kile anachokiita “makundi ya kigaidi”, kama vile Hezbollah, Hamas, na Islamic Jihad kwa miongo kadhaa, kwa lengo la kuunda eneo la vita karibu na Israeli.
Mwandishi anasema kuwa kuiruhusu Iran kuendelea kuchochea mzozo huo sio suluhisho, na kutochukua hatua sio mkakati mzuri kwa Israel katika kukabiliana na tisho la Iran, na Israeli haipaswi kuendelea kuepuka vitisho vya Khamenei, badala yake inafaa kuondoa chanzo cha vitisho hivi.
Mwandishi anasema kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya kijeshi dhidi ya Hezbollah na Hamas, na uharibifu wa ulinzi wa anga wa Iran, inathibitisha kuwa jeshi la Israeli lina uwezo wa kumshinda mpinzani wa kisasa kama huyo, kwa kutumia akili sahihi, teknolojia ya hali ya juu, na operesheni sahihi za anga, na kwamba utaalam huu unaweza kuelekezwa kimkakati kuelekea kulenga maeneo ya nyuklia ya Iran.

Bango linalomuonesha kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei limewekwa karibu na kombora la masafa marefu katika uwanja wa Baharestan mjini Tehran.
Mwandishi anaamini kwamba kwa kuchaguliwa kwa Donald Trump kama rais wa Marekani, operesheni ya pamoja ya Israeli na Marekani haiwezekani na iwapo itawezekana itaongeza sana fursa mafanikio, kwa kushirikiana na uendeshaji wa Israeli na mifumo ya kiteknolojia na nguvu za mashambulizi za Marekani na vikosi maalum, pamoja na diplomasia
Kwa maoni ya mwandishi, vita vya kiuchumi, bado ni moja ya zana zenye nguvu zaidi dhidi ya Iran, baada ya vikwazo vya awali kama sehemu ya kampeni ya shinikizo viliharibu vibaya mapato ya mafuta ya Iran na kupunguza uwezo wake wa kufadhili mtandao wake wa kivita wa nje.
Mwandishi anaamini kuwa juhudi za kidiplomasia zinapaswa kuzingatia kuimarisha ushirikiano na nchi za Kiarabu, kusaini makubaliano ya amani na Saudi Arabia, na kujenga ushirikiano mpya, hasa kwa kuwa mashambulizi ya Iran, hasa kwa msaada wa Urusi, na vitisho vinavyoendelea kwa washirika wa Marekani katika Ghuba, vimeunda fursa mpya za kuunda ushirikiano dhidi ya Iran.
Mwandishi anaamini kwamba ushirikiano huu lazima ufanye kazi sio tu kuizuia Iran, lakini pia kudhoofisha na kumaliza utawala wake, wakati wa kuimarisha juhudi za kuvuruga ratiba ya nyuklia ya Iran, kuwalenga wanasayansi wake wa nyuklia na viongozi wa jeshi la mapinduzi la Iran, kutumia vita vya kielektroniki vya Israeli, na kuzingatia vipengele muhimu vya udhaifu katika utawala wake.
Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kusema kuwa Israel haipaswi kusubiri hadi 2040 wakati Khamenei anapanga kuiangamiza. Kama hilo ndilo lengo lake, basi jukumu la Israel ni kuuangusha utawala wake.
Ushindi ndio chaguo pekee, na hii inamaanisha kuhakikisha kuwa utawala wa Khamenei unakuwa kitu cha zamani, muda mrefu kabla ya ratiba yake kukaribia tarehe yake ya mwisho.
“Utaratibu Mpya wa Mkoa”

Tukiangazia gazeti la Asharq Al-Awsat lenye makao yake London na kipande cha maoni kilichoandikwa na Nadim Koteich chenye kichwa “Fursa ya Irani na ya Waarabu kwa mfumo mpya wa kikanda,” mwandishi anaanza kwa kuhoji: Je, mahusiano ya Irani na nchi za Kiarabu yana fursa mpya katikati ya matukio ya kijiografia na kuharakisha mabadiliko ya ndani na nje? Anaona fursa adimu ya kurekebisha uhusiano wa kikanda na kwenda zaidi ya muktadha unaosababisha kuendelea kwa migogoro na usawa.
Mwandishi anasema kwa bahati nzuri, au kutokana na ufahamu wa kisiasa, mabadiliko katika uhusiano wa Iran na Saudi Arabia mnamo Machi 2023 yalitarajia kungekuwa na vita vya Gaza kwa karibu miezi 6, kupitia upatanishi wa China ambao ulimaliza mgawanyiko wa miaka mingi na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Riyadh na Tehran.
Mwandishi anaongeza kuwa baada ya vita vya Gaza, mkutano kati ya rais wa Milki za Kiarabu (UAE), uliofanyika kando ya mkutano wa kilele wa BRICS mnamo Oktoba 2024, na mwenzake wa Iran, Masoud Pezeshkian, huko Kazan, Urusi, uliashiria hatua ya kushangaza ya kidiplomasia katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Vile vile, Bahrain, ambayo imekumbwa na mvutano wa muda mrefu na Iran, ilianza mazungumzo na jirani yake mnamo Juni 2024 kwa lengo la kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kuimarisha uwazi wa kisiasa kati ya mataifa ya Ghuba na Iran.
Oktoba 2024 tukio lisilo la kawaida, lilishuhudiwa pia mwezi Oktoba 2024 kwani ilitangazwa kuwa Saudi Arabia itashiriki katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika bahari ya Shamu pamoja na Iran, Oman na Urusi.
Baadaye, ujumbe wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Saudi Arabia ukiongozwa na mkuu wa majeshi ya Saudi Arabia uliitembelea Iran na kukutana na maafisa wa kijeshi wa Iran, husasn mkuu wa majeshi ya Iran.
Mwandishi anaamini kwamba mikutano hii inapata umuhimu zaidi kwa kuzingatia kuzorota kwa sheria za ushirikiano kati ya Iran na Israeli, na harakati zao kuelekea uwezekano wa mapambano ya moja kwa moja ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili, baada ya mfululizo wa mashambulizi makali.
Kubashiri kwao pia kumewezekana zaidi kutokana na mashambulizi ambayo yamesababishwa na washirika wa Iran katika eneo hilo, Hamas na Hezbollah.
Mwandishi anaamini kuwa kudhoofisha makundi haya mawili, na kutumia uwezo wa Iran wa kutumia makundi haya mawili ya ushawishi wa kisiasa na kijeshi katika eneo hilo, kuna uwezo wa kuisukuma Iran kuimarisha uhusiano wake na nchi za Kiarabu na kukabiliana na mabadiliko ya mienendo ya kikanda.
Mwandishi anaamini kwamba kurudi kwa Donald Trump katika ikulu ya White House, ingawa inaonekana kuwa sababu ya kuongezeka kwa mvutano na Iran, kunafungua fursa za uhusiano katika mahusiano mema na Iran. Katika wakati ambapo mataifa ya Ghuba, hasa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, yanatafuta kuepuka kuhusika katika kuzidisha uhasama kwa eneo lolote linalohusiana na sera za Marekani dhidi ya Iran, kwa njia ambayo inatishia miradi yao mikubwa ya maendeleo.
Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kusema kuwa kupitishwa kwa sera za kuongeza nguvu dhidi ya China kutasababisha mataifa ya Ghuba kuongeza mara mbili dau lao juu ya kuimarisha ushirikiano wao na kuimarisha usalama wa kikanda, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mazungumzo na Iran.
Anaamini kuwa eneo hilo linakabiliwa na fursa ya ushirikiano ambao huenda sio zaidi ya kutuliza tu mvutano wa nchi mbili, bali ni pia fursa ya kuanzisha mfumo mpya wa utawala wa kikanda ambao ni rahisi zaidi na endelevu.
“Janga kwa Israel na tatizo kwa muungano wa mataifa ya magharibi”

Tunahitimisha uchanganuzi wetu na gazeti la Uingereza, la Financial Times, na kipande cha maoni kilichoandikwa na Gideon Rachman chenye kichwa cha habari “Israeli itagawanya muungano wa Magharibi.”
Mwandishi anaanza kwa kusema kwamba kutolewa kwa waranti ya Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita dhidi ya waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Galant kwa mashtaka ya kufanya uhalifu wa kivita ni janga kwa Israeli, na pia inaleta shida kubwa kwa muungano wa Magharibi.
Israel ina uungwaji mkono kamili wa pande zote mbili nchini Marekani, na inataka kuondoa mashtaka ya ICC dhidi ya waziri mkuu wake na waziri wa zamani wa ulinzi, lakini serikali nyingi katika Umoja wa Ulaya, pamoja na Uingereza, Australia na Canada, zina uwezekano wa kuheshimu mashtaka hayo na zitasita kumkamata Netanyahu ikiwa atakanyaga ardhi yao. Mwandishi anasema.
Mwandishi anaamini kuwa utawala wa Trump utashinikiza vikwazo dhidi ya mwendesha mashtaka na wafanyakazi wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, na pia kuna mazungumzo katika duru za Republican kuhusu kuilenga mahakama, labda kwa kutishia kuziadhibu nchi zinazofadhili. Japan, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ni wafadhili wakuu wanne wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).
Si Israel wala Marekani zinazoonekana kuwa na nia ya kujihusisha na mashtaka hayo, ambayo yanajumuisha shutuma kwamba Israel iliua raia na kutumia “njaa kama njia ya vita.” Badala yake, Trump anakubaliana na madai ya Netanyahu kwamba ICC ina chuki dhidi ya Wayahudi. Kwa upande mwingine, ukweli kwamba mahakama pia imemshtaki Rais wa Urusi Vladimir Putin, Hamas na viongozi kadhaa wa Afrika watapuuzwa, na lengo litakuwa ni kuitangaza mahakama hiyo na wasaidizi wake wa Ulaya kama kuwa wenye chuki dhidi ya Wayahudi.
Mwandishi anasema kwamba baadhi ya nchi za EU, kama vile Ujerumani, zimejitolea kwa Israeli kwa uhakika kwamba zinaweza kukiuka Mahakama ya kimataifa ya uhalifu licha ya kutambua uhalali wake, lakini azma ya nchi nyingi za Ulaya itakuwa kukunga mkono kwa kile wanachokiita haki ya Israeli ya kujitetea.
Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kubainisha kwamba mapambano yanayoibuka kati ya Marekani na washirika wake juu ya Israeli ni sehemu ya mjadala mpana zaidi juu ya mustakabali wa mfumo wa kimataifa. Kama taifa lenye nguvu zaidi ulimwenguni, Marekani inaweza kuhisi kuwa changamoto ya sheria za kimataifa na taasisi za kimataifa ni kitu ambacho wanakihitaji ni watu dhaifu wa Ulaya wanaokihitaji.
KIPENGA CHA NICHEZO
UEFA: Arsenal waah, Man City wooi!

Wachezaji wa Arsenal Bukayo Saka na Kai Havertz wakipongezana wakati wa mechi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya kati yao na Sporting Lisbon. Picha|Hisani
MANCHESTER, UINGEREZA
SHARTI klabu zinazoshiriki kabumbu ya Klabu Bingwa Ulaya pamoja na Liverpool inayopaa katika Ligi Kuu ya Uingereza zianze kuingiwa na kiwewe kutokana na makali ya Arsenal, wachambuzi wa kandanda barani Ulaya sasa wanasema.
Jarida la standard.co.uk linasema kipigo kikali ambacho Arsenal waliwapokeza wenyeji wake Sporting CP ya Ureno mnamo Jumanne usiku, ni onyo tosha kwa klabu zinazoshiriki mashindano hayo mawili maarufu.
Sporting iliyokuwa chini ya kocha Ruben Amorim aliyehamia Manchester United majuzi, ilikuwa imeitia fedheha Manchester City katika uwanja huo huo wa Estadio Jose Alvade kwa mabao 4-1 mapema mwezi huu.
Huku ikijivunia straika mahiri Victor Gyokeres, matarajio ya wengi yalikuwa kikosi hicho kingetatiza Arsenal nyumbani kwao.
Lakini mambo yalitokea vinginevyo. Vijana wa Mikel Arteta hawakushangaza wengi tu kwa ushindi wa mabao 5-1, bali waliwanyima kabisa wenyeji wao fursa yoyote ya kung’ara. Waingereza waling’aa katika kila idara.
“Pamekuwepo mjadala mkali katika majuma kadhaa yaliyopita kuhusu uwezo wa Arsenal katika kinyang’anyiro cha kushinda taji, lakini sasa ushindi wao mnono dhidi ya Sporting ulidhihirisha uwezo wao mwingi wa kushinda mataji ya Champions League na ligi kuu ya EPL,” likasema jarida hilo.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Gabriel Martinelli kunako dakika ya saba, Kai Havertz (22), Gabriel Magalhaes (45+1), Bukayo Saka (penalti, 65) na Leandro Trossard (82).
Kwa matokeo hayo, Arsenal ilisonga hadi nafasi ya saba katika jedwali la Champions League kwa alama 10 bila kuzingatia matokeo ya mechi za jana usiku. Sporting inafuatia kwa alama hizo hizo 10.
Kwingineko, shida za ulinzi katika kikosi cha Manchester City ziliendelea baada ya kukosa kutulia walipokuwa mbele kwa mabao 3-0 dhidi ya Feyenoord kabla ya kutupa mechi hiyo iliyomalizika kwa 3-3 ugani Etihad.
Kutokana na matokeo hayo, City wanashikilia nafasi ya 15 jedwalini, na huenda wakashuka zaidi baada ya mechi nyingine zilizochezwa jana.
Feyenoord inashika nafasi ya 20 kwa alama saba.
Kiungo Ilkay Gundogan, 34, alisema walipoteza mechi hiyo mtindo wa kushangaza. “Sijaamini, kwa sababu tulikuwa tukiongoza zikibakia dakika 15 mechi kumalizika,” alisema Mjerumani huyo.
“Tutajilaumu wenyewe kwa yaliyotokea. Nimekosa majibu kwa maswali mnaoniuliza,” aliongeza.
Kocha Pep Guadiola kwa upande wake alisema wachezaji wake walionekana wadhaifu hasa mechi ikielekea kumalizika.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu watakuwa ugenini Jumapili kucheza na Liverpool katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mechi ambayo Liverpool wanawekewa nafasi kubwa ya kushinda na kuongoza msimamo kwa pengo la pointi 11.
“Sijui kama ni jambo la wachezaji kuchanganyikiwa kiakili, alisema Guardiola huku akionyesha kukatishwa tamaa na utendaji wa upande wake.”
“Tulicheza vizuri wakati tulipokuwa juu kwa 3-0, lakini tukawapa nafasi ya kufunga mabao mengi kwa sababu hatukuwa imara,” aliongeza kocha huyo.
Wakati huo huo, Robert Lewandowski aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu kufunga mabao 100 katika kabumbu hii alipoongoza Barcelona kuibamiza Brest 3-0 ugani Camp Nou.
Cristiano Ronaldo ndiye anayeongoza kwa ufungaji mabao katika mashindano haya ya Ulaya baada ya kucheka na nyavu mara 141 akifuantwa na Lionel Messi.
Jijini Barcelona bao la Lewandowski lilipatikana kupitia kwa mkwaju wa peanlti. Ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Brest umwawezesha kusonga hadi nafasi ya pili jedalini baada ya kushinda nne kati ya mechi tano, wakati Brest walishuka hadi nafasi ya nane kwenye msimamo huo unaojumuisha timu 36.
Kwingineko, Inter Milan waliandikisha ushindi wanne mfulilizo kwenye michuano hiyo baada ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya RB Leipzig ugani San Siro.
Kabla ya mechi za jana, vijana hao wa kocha Simone Inzaghi walikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo. Bao la ushindi lilifungwa na Castello Lukeba aliyefunga langoni mwake akijaribu kuokoa fri-kiki ya Federico Dimarco dakika ya 27.
Kwenye mechi nyingine iliyochezewa Wankdorf, Atalanta waliendeleza rekodi yao ya kutofungwa walipowakung’uta Young Boys 6-0. Charles de Ketelaere alifunga mabao mawili huku mengine yakipatikana kupitia kwa Mateo Retegui, Sead Kolasinac na Lazar Samardzic, wakati Bayern Leverkusen wakiandikisha ushindi mkubwa wa 5-0 dhidi ya Red Bull Salzburg.
Matokeo ya mechi za Jumanne yalikuwa:
Sporting Lisbon 1 Arsenal 5, Young Boys 1 Atalanta 6, Barcelona 3 Brest 0, Leverkusen 5 RB Salzburg 0, Inter Milan 1 RB Leipzig 0, Bayern Munich 1 PSG 0.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.