Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo facebook,Whatsapp, vimekatwa siku ya Alhamisi nchini Msumbiji, huku upinzani ukiitisha maandamano mapya wakati wa mchana, idara ya ufuatiliaji wa mtandao wa Netblocks ilmelithibitishia shirika la habari la AFP.
“Tunaweza kuthibitisha kwamba vikwazo katika mitandao ya kijamii vimewekwa nchini Msumbiji,” idara hiyo yenye makao yake makuu jijini London, Uingereza imesema. Waandishi wa shirika la habari la AFP walibaini habari hizi mapema asubuhi.
Siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, nchi hii ilikumbwa na hitilafu ya jumla ya mtandao miongoni mwa makampuni mbalimbali ya simu, ambayo ilidumu kwa saa kadhaa, siku moja baada ya kutangazwa kwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa Oktoba 9.
Matokeo haya mara moja yalizua maandamano ya vurugu katika miji kadhaa, huku upinzani ukilaani uchaguzi “uliyofaniwa udanganyifu”. Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, 50, akiungwa mkono na chama kidogo cha Podemos, aliitisha mgomo wa kitaifa kuanzia siku ya Alhamisi hadi Novemba 7. Haikuwa wazi kama mwito wake wa “kuzorotesha” shughuli za nchi ungefuatwa, lakini mji mkuu Maputo ulifanana na mji usiokuwepo siku ya Alhamisi asubuhi. Polisi walituma ujumbe zaidi wa maandishi siku ya Jumatano jioni na Alhamisi asubuhi, ikiwa ni pamoja na mwandishi wa shirika la habari la AFP, kuwataka wakazi wasishiriki katika vitendo vya “hujuma”. Mwanasheria mkuu pia alitoa taarifa akionya kwamba ingawa haki ya kuandamana ni “haki ya kimsingi,” “mtu yeyote ambaye … atasababisha uharibifu wa vifaa mbalimbali au kibinafsi ataadhibiwa.”

Tume ya uchaguzi wiki iliyopita ilimtangaza Daniel Chapo, 47, wa chama cha FRELIMO madarakani kwa miaka 49, mshindi wa uchaguzi huo kwa karibu 71% ya kura. Venancio Mondlane, mtangazaji wa zamani wa redio ambaye aliondoka RENAMO, chama cha kihistoria cha upinzani, miezi michache tu iliyopita, alishika nafasi ya pili kwa asilimia 20 ya kura, kulingana na matokeo rasmi. Upinzani uliwasilisha rufaa siku ya Jumapili mbele ya Baraza la Katiba, mahakama ya juu zaidi nchini, kutaka kuhesabiwa upya kwa kura. Siku ya Jumatano, mahakama hii iliitaka tume ya uchaguzi kuwasilisha kwake matokeo yote ya vituo vya kupigia kura vya majimbo sita kati ya kumi na moja, pamoja na yale ya mji mkuu Maputo.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.