Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Muhtasari
- Blinken awasili Israel kushinikiza kusitishwa kwa mapigano Gaza
- China imefanya mazoezi ya silaha karibu na Taiwan
- Rais wa zamani wa Peru ahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela
- Harris anajaribu kushawishi Warepublican
- Kenya: Mahakama kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa kwa Gachagua ofisini
- Rais wa Cameroon hatimaye aonekana hadharani
- Israel bado inazuia misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza – Unrwa
- Umoja wa Mataifa ‘unasikitishwa’ kuwa Kenya iliwarudisha makwao kwa lazima wakimbizi kutoka Uturuki
- Lebanon yasema watu wanne wameuawa katika shambulio la Israel karibu na hospitali iliyo kusini mwa Beirut
Blinken awasili Israel kushinikiza kusitishwa kwa mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewasili nchini Israel kwa mazungumzo na viongozi wa Israel, akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Hiki ni kituo cha kwanza cha ziara pana zaidi katika Mashariki ya Kati – ikiwa ni ya 11 tangu vita vya Gaza kuanza – ambapo atajaribu kushinikiza mazungumzo ya kusitisha mapigano.
Wanamgambo wa kundi la RSF la #Sudan wamesema wameidungua ndege ya mizigo magharibi mwa Darfur. Kufuatia taarifa hiyo, ubalozi wa Urusi umearifu kuwa unachunguza tukio hilo kukiwa na madai kuwa raia wa Urusi walikuwemo ndani ya ndege hiyo. Ndege hiyo inadaiwa kuwa ya Urusi.

Mwanadipiplomasia huyo wa Marekani anatarajiwa kukutana na maafisa wakuu wa Israel ili kujadili namna ya kufufua juhudi za kusitisha mapigano katika ukanda huo baada ya mauaji ya kiongozi mkuu wa Hamas Yahya Sinwar.
Wakati huo huo, Jeshi la Israeli limesema takriban makombora 15 yalirushwa kutoka Lebanon hadi kaskazini mwa Israeli.
Harris anajaribu kushawishi Warepublican, huku Trump akisema ‘mkono wa Mungu unaniongoza’

Tunaendelea kukufahamisha kuhusu taarifa za kampeni za uchaguzi nchini Marekani.
Zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya siku ya kupiga kura tarehe 5 Novemba, kampeni inakaribia kuingia katika kipindi chake cha lala salama:
Yaliyojiri:
Siku ya Jumatatu Kamala Harris alizuru majimbo muhimu na Liz Cheney, mbunge wa zamani wa Republican ambaye amekuwa akimkosoa vikali Donald Trump.
Harris alijaribu kuomba kura kwa wapiga kura wa Republican ambao wamekatishwa tamaa na Trump, akiwaambia “hawako peke yao” katika jaribio la kuwashawishi kubadili chama.
Kwingineko, Trump alihutubia hadhira ya Wakristo wa kiinjili huko North Carolina, jimbo lingine ambalo lina uwezekano wa kuchukuliwa na upande wowote katika uchaguzi huu
Trump alisema “mkono wa kimuujiza” ulimwokoa kutokana na kuuawa mnamo mwezi Julai.
Rais huyo wa zamani anashtakiwa kwa kumchafulia mtu jina katika maoni aliyotoa wakati wa mjadala wa televisheni mwezi uliopita
Steve Bannon, mshirika mkuu wa Trump ambaye alimfanyia kazi katika Ikulu ya White House, ataachiliwa kutoka gerezani wiki ijayo
Kambi ya Kampeni ya Harris ilitumia zaidi ya mara tatu ya kiasi kilichotumiwa naTrump mwezi uliopita, kulingana na takwimu mpya – na kura za maoni bado zinaonyesha kinyang’anyiro hicho kinakaribiana sana
Kenya: Mahakama kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa kwa Gachagua ofisini

Jopo la majaji watatu leo linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa ofisini kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais .
Jopo hilo linaloongozwa na Jaji Eric Ogola pia lina majaji Anthony Mrima na Freda Mugambi na liinatarajiwa kutoa uamuzi leo ikiwa litaondoa au kuongeza muda wa maagizo ya kuzuia kuapishwa kwa Kithure Kindiki kuchukua wadhifa wa Naibu Rais baada ya uteuzi wake na Rais William Ruto na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa siku ya Ijumaa.
Hii ni baada ya majaji Chacha Mwita kutoka Milimani na Richard Mwongo kutoka Kerugoya kutoa maagizo ya kusitisha utekelezwaji wa azimio lililopitishwa na Seneti kumwondoa Gachagua ofisini kupitia kura iliyopitisha mashtaka 5 kati ya 11 dhidi yake yaliyowasilishwa kwa seneti na bunge la Kitaifa na kumzuia Kithure kuchukua usukani katika Ofisi hiyo.
Juhudi za Mwanasheria Mkuu wa serikali Dorcas Oduor kutaka maagizo hayo yaondolewe yalitupiliwa mbali na mahakama ya majaji watatu, ambayo badala yake iliamuru kusikilizwa kwa kesi baina ya pande zote Jumanne.
Wakati huo huo Idara ya DCI nchini Kenya imemtaka Gachagua kufika katika makao yake ili kutoa ufafanuzi kuhusu madai yake kwamba kulikuwa na majaribio mawili ya kumuua kutumia sumu .
Idara hiyo imesema madai hayo yana uzito na hivyo basi Gachagua anafaa kuyatolea ufafanuzi.
Paul Biya: Rais wa Cameroon hatimaye aonekana hadharani

Rais wa Cameroon Paul Biya mwenye umri wa miaka 91 ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza ndani ya wiki sita huku kukiwa na uvumi kuhusu afya yake kudorora.
Kutokuwepo kwake hadharani kulisababisha uvumi usio na msingi wa kifo chake.
Lakini siku ya Jumatatu mchana televisheni ya taifa ilionyesha picha za kuwasili kwa rais katika uwanja wa ndege kwenye mji mkuu, Yaoundé, kwa ndege kutoka Uswizi.
Serikali ilikuwa imepiga marufuku vyombo vya habari kujadili afya ya Biya – ambaye amekuwa madarakani tangu 1982 – ikiainisha kama suala la usalama wa taifa.
Tetesi za kifo chake zimekuwa zikienea kila mara kwa miongo miwili iliyopita.
Picha za Jumatatu zinaonyesha rais akiwa amevalia suti yake nadhifu ya kawaida na mwenye nguvu.
Mara ya mwisho Biya kuonekana ilikuwa tarehe 8 Septemba akihudhuria mkutano wa kilele wa China na Afrika mjini Beijing.
Tangu wakati huo, serikali imekuwa chini ya shinikizo kubwa kuthibitisha kwamba kiongozi huyo wa muda mrefu alikuwa hai.
Maafisa wa serikali hatimaye walikanusha madai kwamba alifariki, wakisema kuwa Biya alikuwa bukheri wa afya na kwamba yuko katika ziara ya faragha huko Geneva.
Anajulikana kwa ziara za mara kwa mara kwenye jiji la Uswizi.
Baada ya kutua, Biya alikaribishwa na viongozi wa serikali na wanachama wa chama tawala.
Ukusanyaji usio wa kawaida wa watu katika baadhi ya mitaa kwenye mji mkuu ulionyesha nia ya wazi ya serikali kukomesha uvumi kuhusu ustawi wake.
China imefanya mazoezi ya kutumia silaha kwenye kisiwa kilicho karibu zaidi na Taiwan

China imefanya mazoezi ya kutumia silaha kutoka eneo lake lililo karibu na Taiwan wiki moja baada ya kuzindua mazoezi makubwa ya kuzunguka kisiwa hicho.
Mazoezi ya kijeshi ya China kwenye pwani ya Taiwan yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni huku madai yake juu ya kisiwa hicho kinachojitawala yakiongezeka.
Beijing ilitangaza Jumatatu kwamba eneo karibu na Niushan – kisiwa kilicho kilomita 105 (maili 66) kutoka Taiwan – litafungwa kwa ajili ya mazoezi kwa saa nne kutoka 09:00 saa za eneo siku ya Jumanne.
Waziri Mkuu wa Taiwan Cho Jung-tai alisema Jumanne kwamba China haipaswi kufanya mazoezi kama hayo kutokana na tishio lao la utulivu wa kikanda.
Rais wa zamani wa Peru ahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela

Mahakama nchini Peru imemhukumu rais wa zamani Alejandro Toledo kifungo cha miaka 20 na miezi sita jela kwa kosa la rushwa na utakatishaji fedha.
Waendesha mashtaka wanasema alichukua $35m (£27m) kama hongo kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya Brazil ambayo ilipewa kandarasi ya kujenga barabara kusini mwa Peru.
Toledo, 78, alikuwa ofisini kati ya 2001 na 2006.
Alikamatwa miaka mitano iliyopita huko California ambako alikuwa ameishi na kufanya kazi kwa miaka mingi, na kurejeshwa Peru mwaka jana.
Kampuni ya Brazil ya Odebrecht ilikiri kulipa mamilioni ya dola kama rushwa kwa maafisa kote Amerika ya Kusini na Marekani ili kupata kandarasi za serikali.
#Viongozi kadhaa wa dunia wanakusanyika nchini Urusi hii leo kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa kilele wa kundi la nchi zinazoinukia kiuchumi, (BRICS). Mkutano huo wa kilele ndio mkutano mkubwa zaidi wa aina hiyo nchini Urusi tangu ilipoamuru wanajeshi kuingia Ukraine na unafanyika wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin akitaka kuonyesha kwamba majaribio ya nchi za Magharibi ya kuitenga Moscow kutokana na mashambulizi ya miaka miwili na nusu yameshindwa.
Kilichomo katika tathmini ya Marekani iliyovuja na kufichua mipango ya Israel kuishambulia Iran

Mabaki ya kombora kusini mwa Israel, mojawapo ya makombora 180 ambayo Iran ilirusha huko tarehe 1 Oktoba.
Wachunguzi wa Marekani wanajaribu kufahamu jinsi nyaraka mbili za kijasusi zenye usiri mkubwa sana zilivyovujishwa mtandaoni.
Nyaraka hizo, ambazo zilionekana kwenye programu ya kutuma ujumbe ya Telegram siku ya Ijumaa, zina madai ya tathmini ya Marekani kuhusu mipango ya Israel kuishambulia Iran.
Tathmini inategemea tafsiri ya taswira za picha za satelaiti na aina nyinginezo za ujasusi.
Siku ya Jumatatu msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House John Kirby alisema Rais Joe Biden “ana wasiwasi mkubwa” kuhusu uvujaji huo.
Maafisa hawajabaini ikiwa hati hizo zilitolewa kwa sababu ya udukuzi au uvujaji, Bw Kirby alisema.
Kwa muda wa wiki tatu sasa, Israel imekuwa ikiapa kuishambulia Iran vikali ili kulipiza kisasi kwa shambulizi kubwa la kombora la balistiki la Iran dhidi ya Israel tarehe 1 Oktoba.
Iran inasema hiyo ilikuwa ni kujibu mauaji ya kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, tarehe 27 Septemba.
Hati hizo ni za kweli?
Wachambuzi wa kijeshi wanasema maneno yaliyotumiwa katika vichwa yanaonekana kuaminika na yanaambatana na hati sawa zilizoainishwa zilizofichuliwa hapo awali.
Vina kichwa “Siri ya Juu”, vinajumuisha kifupi “FGI”, kinachomaanisha “Ujasusi wa Serikali ya Kigeni”.
Nyaraka hizo zinaonekana kusambazwa kwa mashirika ya kijasusi katika muungano wa Five Eyes, mataifa matano ya Magharibi ambayo yyanashirikiana kupashana habari za kijasusi mara kwa mara, yaani Marekani, Uingereza, Kanada, Australia na New Zealand.
Muhtasari wa “TK” katika hati unarejelea “Talent Keyhole”, neno la msimbo linalosheheni Upelelezi wa Ishara za Satelaiti (SIGINT) na Upelelezi wa Picha (IMINT).
Zinatuambia nini?
Nyaraka hizo mbili zikijumlishwa, ni tathmini iliyoainishwa ya Marekani kuhusu maandalizi ya Israel kulenga shabaha nchini Iran, kulingana na taarifa za kijasusi zilizochambuliwa tarehe 15-16 Oktoba na Shirika la Kijasusi la Marekani la Geospatial-Intelligence.
Kinachojulikana zaidi ni kutajwa kwa mifumo miwili ya Air Launched Ballistic Missile (ABLM): Golden Horizon na Rocks.
Rocks ni mfumo wa makombora wa masafa marefu uliotengenezwa na kampuni ya Israel Rafael na iliyoundwa kulenga shabaha mbalimbali juu na chini ya ardhi. Golden Horizon inadhaniwa kuzungumzia mfumo wa kombora wa Blue Sparrow wenye masafa ya takriban kilomita 2,000 (maili 1,240).
Umuhimu wa hili ni kwamba inaashiria kuwa Jeshi la Anga la Israeli linapanga kutekeleza shambulio sawa lakini lililopanuliwa sana la shambulio lake la ABLM kwenye maeneo ya rada ya Irani karibu na Isfahan mnamo Aprili.
Kwa kurusha silaha hizi kutoka masafa marefu na mbali na mipaka ya Iran itaepusha hitaji la ndege za kivita za Israel kuruka juu ya nchi fulani katika eneo kama Jordan.
Nyaraka hizo pia haziripoti dalili zozote za matayarisho yoyote ya Israel ya kuwezesha kuzuia matumizi ya nyuklia.
Kwa ombi la Israel, serikali ya Marekani kamwe haikiri hadharani kwamba mshirika wake wa karibu Israel hata anamiliki silaha za nyuklia, hivyo hii imesababisha aibu fulani huko Washington.
Hazituambii nini ?
Kinachokosekana katika hati hizi ni kutajwa kwa kile ambacho Israeli inakusudia kushambulia nchini Iran, au lini.
Marekani haijaficha pingamizi yake dhidi ya kulengwa kwa vituo vya utafiti wa nyuklia vya Iran au mitambo yake ya mafuta.
Hilo linaacha kambi za kijeshi, kama zaidi zile za Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) na wanamgambo wake wa Basij kwa kuwa taasisi hizi mbili zinaonekana kama uti wa mgongo wa Jamhuri ya Kiislamu, zikionyesha uwezo wake wa kijeshi kufika nje ya nchi na kukandamiza maandamano ya wananchi nyumbani.
Kuhusu wakati, wengi walitarajia Israeli iwe imetekeleza ulipizaji kisasi kilichoahidiwa kufikia sasa. Lakini mwezi wa Aprili, Iran ilisubiri siku 12 kabla ya kuishambulia Israel kwa ndege zisizo na rubani 300 na makombora baada ya shambulio la anga la Israel kugonga majengo yake ya kidiplomasia huko Damascus, na kuua makamanda kadhaa wakuu wa IRGC.
Sehemu ya kucheleweshwa kwa sasa kwa majibu ya Israeli kunawezekana kutokana na wasiwasi wa Marekani kuongezeka ikiwa ni chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa urais wa Marekani.
Je, zilivujishwa kwa makusudi?
Labda ndio, na mtu ambaye alitaka kuharibu mipango ya Israeli.
Iran ina uwezo mkubwa na wa kisasa zaidi wa vita vya mtandao kwa hivyo uwezekano wa udukuzi pia unachunguzwa.
Nyaraka hizi, ikiwa ni za kweli kama inavyofikiriwa, zinaonyesha kuwa licha ya uhusiano wa karibu wa kiulinzi kati ya Marekani na Israel, Washington bado inampeleleza mshirika wake iwapo kujua iwapo haipewi picha kamili ya mambo yalivyo.
Zinaonyesha kwamba mipango ya Jeshi la Wanahewa la Israeli kutekeleza aina fulani ya kulipiza kisasi kwa muda mrefu dhidi ya Iran iko katika hatua za juu sana na kwamba mikakati inawekwa kukailiana na jibu linalotarajiwa la Irani.
Kwa kifupi: ikiwa na wakati Israeli itakapotekeleza mipango hii basi Mashariki ya Kati itajipata tena katika kipindi cha mvutano mkubwa.
Putin anakusanya washirika kuonyesha vikwazo vya Magharibi havifanyi kazi

Fikiria wewe ni Vladimir Putin. Nchi za Magharibi zinakutenga kwa sababu ya kuivamia Ukraine. Vikwazo vinalenga kuumiza uchumi wa nchi yako katika masoko ya kimataifa.
Na kuna hati ya kukamatwa kwako kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Je, utawezaje kuonyesha vikwazo hivyo vyote havifanyi kazi?
Wiki hii katika mji wa Kazan, Rais Putin atakutana na zaidi ya wakuu wa nchi 20 katika mkutano wa kilele wa mataifa yanayoinukia kiuchumi ya Brics. Miongoni mwa viongozi walioalikwa ni pamoja na Xi Jinping wa China, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.
Ikulu ya Kremlin inasema ni moja ya “matukio kubwa juu ya sera za kigeni kuwahi kutokea” nchini Urusi.
“Ujumbe wa wazi ni kwamba majaribio ya kuitenga Urusi yameshindwa,” anasema Chris Weafer, mwanzilishi wa taasisi ya ushauri ya Macro-Advisory.
“Ni ujumbe kutoka Kremlin kwamba Urusi inastahimili vikwazo. Na katika ngazi ya siasa za kijiografia Urusi ina marafiki wote hawa na wote watakuwa washirika wa Urusi.”
Marafiki wa Urusi ni nani?
Brics ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Kundi hilo, ambalo mara nyingi hujulikana kama uzani wa kukabiliana na ulimwengu unaoongozwa na Magharibi, limepanuka na kujumuisha Misri, Ethiopia, Iran na Falme za Kiarabu.
Saudi Arabia, pia, imealikwa kujiunga.
Mataifa ya Brics yanachukua 45% ya idadi ya watu ulimwenguni. Uchumi wa nchi wanachama kwa ujumla una thamani ya zaidi ya dola za kimarekani trilioni 28.5. Karibu 28% ya uchumi wa dunia.
Maafisa wa Urusi wamedokeza kuwa nchi nyingine 30 zinataka kujiunga na Brics. Baadhi ya mataifa haya yatashiriki katika mkutano huo.
Akiwa na nia ya kupunguza ukali wa vikwazo vya Magharibi, kiongozi huyo wa Kremlin atatumia mkutano huu kuwashawishi wanachama wa Brics kuchukua sarafu mbadala dhidi ya dola kwa ajili ya malipo ya kimataifa.
“Matatizo mengi ambayo uchumi Urusi unakabiliwanayo yanahusishwa na biashara na malipo ya mpakani. Na mengi ya hayo yanahusishwa na dola ya Marekani,” anasema Weafer.
“Hazina ya Marekani ina nguvu na ushawishi mkubwa katika biashara ya kimataifa kwa sababu dola ya Marekani ndiyo sarafu kuu ya kutatua hilo. Nia kuu ya Urusi ni kuvunja utawala wa dola ya Marekani. Inataka nchi za Brics kuunda utaratibu mbadala wa biashara – ili vikwazo visiwe na maana.”
BRICS yenyewe

Lakini ndani ya Brics kwenyewe kuna mgawanyiko.
“Kwa namna fulani ni jambo zuri kwa nchi za Magharibi pale China na India zinaposhindwa kukubaliana kuhusu jambo lolote. Kwa sababu kama nchi hizo zingekuwa makini, Brics ingekuwa na ushawishi mkubwa,” anabainisha Jim O’Neill, mtaalamu wa uchumi aliyefanya kazi na taasisi ya Goldman Sachs.
O’Neill anaamini “Bric” ilipaswa kuwa kitovu cha uundaji wa sera za kimataifa.”
Lakini nchi hizo nne zimeendelea na maisha yao wenyewe, baada ya mataifa husika kuunda kundi lao la Bric – na kisha Afrika Kusini ikajiunga na kuwa BRICS. Wangejaribu kupinga utawala wa G7: mataifa saba makubwa zaidi kiuchumi duniani (Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani).
Sio India na China pekee ambao wana tofauti zao. Kuna mvutano kati ya wanachama wawili wapya wa Brics, Misri na Ethiopia. Na Iran na Saudi Arabia kwa muda mrefu wamekuwa wapinzani wa kikanda.
Wakati Urusi, ikichochewa na chuki dhidi ya Magharibi, inataka kuunda “utaratibu mpya wa dunia,” wanachama wengine wa Brics, kama India, wana nia ya kudumisha uhusiano mzuri wa kisiasa na kiuchumi na Magharibi.
Huko Kazan, kazi ya Vladimir Putin itakuwa kuchunguza tofauti na kuchora picha ya umoja, huku akionyesha umma wa Urusi – na jumuiya ya kimataifa – kwamba nchi yake iko mbali na kutengwa.
Yahya Sinwar: Je, tunajua nini kuhusu nyumba iliyoshuhudia wakati wa mwisho wa maisha ya kiongozi wa Hamas?

Mbele ya Hospitali ya Emirati kwenye Mtaa wa Ibn Sina katika kitongoji cha Sultan, magharibi mwa mji wa Rafah, kuna nyumba kijijini ya familia ya Mpalestina.
Hawakuwahi kufikiria kwamba nyumba yao, ambayo walilazimika kuihama ingegeuka kuwa eneo la operesheni ya kijeshi kati ya jeshi la Israeli na kiongozi wa harakati ya Hamas, Yahya Sinwar, na hatimaye kuuawa hapo kwa Sinwar katika makabiliano jeshi.
Ashraf Abu Taha, mmiliki wa nyumba na mkuu wa familia iliyoishi ndani ya nyumba hiyo , alikiambia kipindi cha redio cha Gaza Today : “Nimeishi katika nyumba hii kwa miaka 15 na familia yangu. Hatujawahi kuwa wakimbizi na kulazimika kutoka huko, hata wakati wa vita vya awali. Kitu pekee kilichonilazimisha kuondoka ni mbinu ya utoaji wa amri ya kuhama za jeshi la Israeli na uhamishaji wa majirani zangu wote huko Rafah.”

“Kujenga nyumba hii kulinigharimu shekeli 200,000 (karibu dola 53,800 za Marekani), ambazo nilizihifadhi kwa miaka mingi wakati nikifanya kazi yangu ili niweze kuinunua.
Mwanangu na ndugu zangu pia walinisaidia kulipa, na kisha nikaiweka samani za nyumba kikamilifu. Sikuwahi kufikiria kwamba nyumba hii siku moja ingegeuka kuwa uwanja wa vita kati ya Sinwar na jeshi la Israeli,” anasema Abu Taha.

Kuhusiana na jinsi alivyopokea taarifa za kilichotokea kwenye nyumba yake ambayo imekuwa gumzo duniani kote, anasema: “Sina uhusiano wowote na mitandao ya kisasa ya kijamii, lakini binti yangu aliona picha na klipu za video zilizochapishwa haraka akanionyesha na kuniuliza: Je, hii si nyumba yetu?”
Aliongeza kuwa: “Nilishangaa nilipoiona, sikuamini. Lakini kaka yangu alinipigia simu na kuniambia kuwa ni nyumba yangu, nilikuwa na uhakika wa kile ambacho macho yangu yanaona. Nilipinga mara ya kwanza, ” nilipokea habari kama mshtuko ambao siwezi kuuelezea hadi sasa.”
Abu Taha alithibitisha kuwa nyumba yake ilikuwa shwari wakati alipohamishwa tarehe sita mwezi wa Mei na hakuwahi kushambuliwa kwa bomu, na katika kipindi chote hicho hakuweza kupata taarifa zozote kuhusiana na hilo kwa sababu eneo ilipo nyumba yake lilikuwa limeainishwa kama “eneo hatari la operesheni za kijeshi.”
Picha zilizosambazwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii kufuatia tangazo rasmi la Israel la kuuawa kwa Sinwar ni jambo la kwanza ambalo Mpalestina huyo aliyekimbia makazi yake alilifahamu kuhusu nyumba yake tangu alipoondoka, jambo ambalo lilizidisha hisia zake za mshtuko, kama alivyoeleza.

Kuhusu sofa la kupendeza lililoonekana kwenye kipande cha video kilichochapishwa na Avichai Adraee, msemaji wa jeshi la Israeli kwa Kiarabu, ambapo Sinwar alikuwa ameketi katika dakika zake za mwisho, kulingana na jeshi la Israeli, Abu Taha anasema: “Ni sofa lile lile nililokuwa nimekalia huku nikikusanya baadhi ya vifaa nilivyochukua kwenye safari yangu ya kutoka.” [kwenye makazi yangu].
Aliongeza: “Sofa hii ni kipande cha seti ya viti ambayo mama yangu alinipatia, kwa hiyo ina maana ya kipekee kwangu. Ni sofa hiyo hiyo aliyokalia ambayo wanafamilia wangu wamekuwa wakikusanyika kila wakati kwa kipindi cha miaka 15.”
Siku ya Alhamisi, Oktoba 17, jeshi la Israel lilitangaza kuuawa kwa kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, katika operesheni iliyofanyika kusini mwa Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya jeshi la Israel na shirika la usalama wa ndani (Shin Bet Kwa upande wake). Hamas ilitoa taarifa siku ya Ijumaa ikimuomboleza kiongozi wake, Yahya Sinwar, katika makabiliano hayo ya jijeshi huko Gaza.
Israel bado inazuia misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza – Unrwa

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa) amesema Israel inaendelea kuzuia misheni ya kibinadamu kufika kaskazini mwa Gaza ikiwa na vifaa muhimu kama chakula na dawa.
“Hospitali zimeshambuliwa na kuachwa zimelemazwa huku watu waliojeruhiwa wakiachwa bila huduma,” Philippe Lazzarini aliandika kwenye mtandao wa X.
Pia alisema makazi yaliyosalia ya Unrwa yalikuwa yamejaa kupita kiasi hivi kwamba watu waliokimbia makazi “wanalazimika kuishi kwenye vyoo”, na akataja ripoti kwamba watu wanaojaribu kukimbia walikuwa wakiuawa.
Jeshi la Israel limekuwa likizidisha mashambulizi ya wiki moja katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza dhidi ya kile ilichosema ni wapiganaji wa Hamas waliojikita tena huko.
Siku ya Jumatatu wakaazi na madaktari walisema vikosi vya Israel vilikuwa vinazingira hospitali na makazi ya watu waliokimbia makazi yao.
Jeshi la Israel lilisema linarahisisha uhamishaji wa raia na kuhakikisha hospitali zinaendelea kufanya kazi huku likiendelea “kukabiliana na magaidi na miundombinu ya kigaidi”.
Umoja wa Mataifa ‘unasikitishwa’ kuwa Kenya iliwarudisha makwao kwa lazima wakimbizi kutoka Uturuki

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema “linasikitishwa” na habari kwamba wakimbizi wanne walirejeshwa Uturuki kutoka Kenya.
Wakimbizi hao walirejeshwa makwao kwa ombi la serikali ya Uturuki, wizara ya mambo ya nje ya Kenya inasema.
Kauli hiyo inajiri baada ya ripoti za watu kadhaa kutekwa nyara katika jiji kuu la Nairobi siku ya Ijumaa.
Raia wa Uingereza aliambia BBC kuwa yeye na raia kadhaa wa Uturuki walikuwa wametekwa nyara na watu waliojifunika nyuso zao.
Alisema alikuwa ameachiliwa baada ya saa nane alipowaonyesha watu wanaodaiwa kumteka nakala ya paspoti yake ya Uingereza.
Katika taarifa yake, UNHCR ilisema: “UNHCR inaitaka Serikali ya Kenya kutii wajibu wao wa kisheria wa kimataifa, na hasa, kuheshimu kanuni ya kutorejesha wakimbizi [kwa lazima], ambayo inawalinda wanaotafuta hifadhi na wakimbizi dhidi ya aina yoyote ile ya hatua ambayo inaweza kusababisha kuondolewa kwao hadi mahali ambapo maisha au uhuru wao ungetishiwa.”
Wizara ya mambo ya nje ya Kenya imesema imekubali ombi la Uturuki la kuwarejesha nyumbani watu hao wanne kwa sababu ya “uhusiano thabiti wa kihistoria na kimkakati” wa nchi hiyo na Uturuki, na kwamba imehakikishiwa wakimbizi “watatendewa utu”.
Wanne hao wanaaminika kuwa wafuasi wa vuguvugu la Gulen, jumuiya yenye nguvu ya Kiislamu yenye wafuasi nchini Uturuki na duniani kote, ambayo kiongozi wake amefariki dunia.
Vuguvugu la Gulen linaendesha mtandao wa shule nchini Kenya na duniani kote.
Lebanon yasema watu wanne wameuawa katika shambulio la Israel karibu na hospitali iliyo kusini mwa Beirut

Watu wanne akiwemo mtoto wameuawa katika shambulizi la anga la Israel karibu na hospitali kuu ya serikali kusini mwa Beirut, wizara ya afya ya Lebanon inasema.
Shambulizi hilo lilionekana kulenga maegesho ya magari ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Rafik Hariri, chanzo cha hospitali kililiambia shirika la habari la Reuters.
Wizara ya afya imesema watu 24 wamejeruhiwa.
Ilikuwa ni miongoni mwa mashambulizi 13 ya anga yaliyokumba Beirut kusini Jumatatu jioni.
Jeshi la Israel lilisema lilikuwa linashambulia vituo vinavyohusishwa na Hezbollah.
Msemaji wa Israel hapo awali alikuwa amewaonya watu kuhama kutoka maeneo kadhaa kusini mwa Beirut, hata hivyo hospitali ya Rafik Hariri haikuwa miongoni mwa maeneo yaliyotajwa.
Video kutoka kitongoji cha Dahiyeh kusini mwa Beirut, ambapo maeneo saba yatakayolengwa yalitangazwa mapema, zilionyesha wenyeji wakikimbia kwa magari na kwa miguu huku mashambulizi hayo yakianza.
Eneo moja lililotambuliwa kama shabaha ya jeshi la Israel lilikuwa takriban mita 400 kutoka uwanja wa ndege wa Beirut, ambao ndiyo pekee wa kimataifa unaohudumia Lebanon.
Vyombo vya habari vya ndani vilishirikisha picha za baadhi ya madirisha katika jengo la uwanja wa ndege ambayo yalilipuliwa katika mlipuko huo.
Israel haijatoa maoni yoyote tangu ilipotoa maonyo ya awali ya kuwahamisha.
Awali, Jeshi la Israel lilikuwa limesema mapema Jumatatu kwamba liligundua ngome ya Hezbollah iliyojifichwa chini ya hospitali tofauti kusini mwa Beirut, ambayo tangu wakati huo imehamishwa.
Msemaji wa IDF Admiral Daniel Hagari alisema bila kutoa ushahidi kwamba chumba cha kulala chini ya hospitali ya Sahel huko Haret Hreik kilikuwa na mamia ya mamilioni ya dola taslimu na dhahabu ambazo zilikuwa zikitumika kufadhili mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel.
Hata hivyo, mkurugenzi wa hospitali ya Sahel alikanusha kuwa kulikuwa na chumba cha kulala chini yake na kutoa wito kwa jeshi la Lebanon kukagua eneo hilo.
Israel inaonekana kupanua vita vyake dhidi ya Hezbollah zaidi ya miundombinu ya kijeshi na inasema inalenga mitandao ya kifedha ya kundi hilo.
Urusi kuchunguza kutunguliwa kwa ndege yake nchini Sudan

Machafuko ya nchini Sudan yalianza katikati ya mwezi Aprili, 2023./Picha: AFP
Ubalozi wa Urusi nchini Sudan umeanza uchunguzi wa madai ya kutunguliwa kwa ndege yake kaskazini mwa Sudan, umesema ubalozi huo siku ya Jumatatu.
Kulingana na ubalozi huo, ndege inaweza ikawa imetunguliwa na majeshi ya RSF, yanayogombania mamlaka nchini Sudan.
Kwa sasa, ubalozi huo, kwa kushirikiana na mamlaka za Sudan, unaratibu namna ya kupata taarifa zaidi, na kufahamu hatma ya waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.