Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Mahakama kuu nchini Kenya inasikiliza rufa iliyowasilishwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua anayepinga mchakato wa kutimuliwa kwake Ofisini na Bunge la Seneti wiki iliopita.
Mahakama kuu siku ya Ijumaa iliagiza kusitishwa kwa mchakato wa kumuapisha Naibu mpya wa Rais Kithure Kindiki ambaye sasa ni Waziri wa usalama wa ndani.
Bunge liliimuidhinisha Kithure Kindiki ambaye ndiye chaguo la Rais William Ruto kuchukua nafasi yake Rigathi Gachagua.
Gachagua alitimuliwa na Bunge la Seneti mnamo Alhamisi kwa mashtaka matano kati ya 11 dhidi yake, yakiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu idara ya mahakama.
Rigathi mwenye umri wa miaka 59 alilazwa hospitalini kutokana na maumivu makali kwenye kifua chake kabla ya kikao cha Seneti wiki iliopita ambapo alitakiwa kujitetea, lakini bunge hilo lilikataa rufaa ya mawakili wake kutaka mchakato huo kucheleweshwa.
Kutimuliwa kwake kulisababisha mzozo kati ya Gachagua na Rais William Ruto.
Baada yake kuruhusiwa kuondoka hospitalini siku ya Jumapili ya wiki iliopita, Gachagua alimkashifu bosi wake akimtaja kama mtu “mwovu” na kudai kulikuwa na majaribio ya kumuua siku za nyuma.

Gachagua alisema usalama wake umeondolewa na wafanyikazi wake wote katika Ofisi yake walitumwa kwa likizo ya lazima na serikali.
Jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu jijini Nairobi limeanza kusikiliza rufaa ya Gachagua.
Ruto ambaye alikuwa amemchagua Gachagua kama mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti 2022, bado hajazungumzia kwa umma kuhusu kuondolewa kwake madarakani.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.