Afrika Leo Jioni-16th Oktoba 2024

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Muhtasari

  • Mwanamume akamatwa baada ya mbwa kutelekezwa wakati wa kimbunga Milton
  • Spika Kingi amruhusu Gavana Orengo kuwa wakili wa Bunge la Kitaifa
  • Naibu Rais Rigathi Gachagua akanusha mashtaka yote 11 yanayomkabili
  • Watu 94 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka
  • Korea Kaskazini yalipua barabara kuu na leri inayoiunganisha na Korea Kusini ili “kutenganisha kabisa” nchi zote mbili
  • Israel yaushambulia mji mkuu wa Lebanon kwa mara ya kwanza baada ya siku tano
  • Tuchel akubali kuwa meneja ajaye wa England
  • Mahakama yakataa kuzuia kushtakiwa kwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua
  • Tazama: Shambulio la Israel lilivyopiga kambi ya mahema ya wakimbizi katika hospitali ya Gaza
  • Walioshuhudia shambulio la Israel kwenye hospitali ya Gaza waliona ‘watu wengi wakiungua’
  • Bunge la Seneti Kenya kuanza kusikiliza hoja ya kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua
  • Marekani yaipa Israel siku 30 kuongeza msaada wa Gaza la sivyo itakuwa katika hatari ya kukatwa kwa msaada wa kijeshi

Spika Kingi amruhusu Gavana Orengo kuwa wakili wa Bunge la Kitaifa

.

Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi amemruhusu Gavana wa Siaya James Orengo kuwakilisha Bunge la Kitaifa kama wakili wake, hatua ambayo ilikuwa imepingwa na mawakili wa upande wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, wakitaja wadhifa wake kama afisa wa serikali.

Katika uamuzi wake, Kingi alitupilia mbali pingamizi zilizowasilishwa na wakili wa Gachagua, akieleza kuwa wameshindwa kuonyesha upendeleo wowote uliyotokana na kushiriki kwa Orengo katika kesi hiyo ya siku mbili yenye kujikita katika suala la kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua

Wakili Ndegwa Njiru alidai kuwa Orengo alikuwa afisa wa serikali anayehudumu kama gavana wa awamu ya kwanza na maamuzi ya hapo awali yaliyofanywa na bunge hilo yalizuia maafisa wa umma kuwawakilisha wateja kutokana na mgongano wa kimaslahi.

“Gavana James Orengo ni afisa wa serikali anayehudumu kwa muda wote kulingana na Kifungu cha 260 cha katiba, ambacho kinamzuia afisa wa serikali wa muda wote kujihusisha na kazi nyingine. Itakuwa visivyo kwa bunge hili kumruhusu Orengo kuwakilisha Bunge la Kitaifa katika kesi hii,” Njiru alisema.

“Wakili hakutoa ushahidi kwamba Gavana Orengo alikuwa akijishughulisha na kazi nyingine. Ukweli ni kwamba, wakili alihamishia Bunge mzigo wa ushahidi. Hoja hiyo haina mashiko,” Spika wa Seneti alisema.

Naibu Rais Rigathi Gachagua akanusha mashtaka yote 11 yanayomkabili

.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekanusha mashtaka yote 11 yanayomkabili akiwa mbele ya Bunge la Seneti ambaye pia aliandamana na mawakili wake.

Mashtaka hayo yalisomwa na karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye leo siku ya Jumatano.

Sasa, kesi hiyo imefikia hatua ya kusikilizwa kikamilifu na kikao cha Bunge la Seneti.

Haya yanajiri baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kushtakiwa na Bunge la Kitaifa kwa msururu wa tuhuma zikiwemo ufisadi, kumhujumu rais na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila.

Bunge la Kitaifa lilipiga kura ya kumuondoa Gachagua madarakani ambapo wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo, huku 44 wakipiga kura kupinga na mmoja akikataa kupiga kura na hivyobasi kuafikia thuluthi mbili ya kura zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa afisini.

Bunge la Seneti limepanga siku mbili mfululizo za kusikiliza na kubaini hatima ya Gachagua.

Rigathi Gachagua anahitaji angalau maseneta 23 ili kunusurika kuondolewa kwake.

Watu 94 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka

.

Takriban watu 94 wameteketea hadi kufa na wengine 50 wakiwa katika hali mbaya kufuatia moto mkubwa uliosababishwa na mlipuko wa lori la mafuta usiku wa kuamkia jana katika jimbo la Jigawa kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Polisi wa Jigawa waliambia BBC kuwa tukio hilo katika barabara kuu ya Kano-Hadejia lilitokea mwendo wa saa tano na nusu usiku kwa saa za eneo katika kijiji cha Majiya, eneo la serikali ya mtaa wa Taura, ambapo lori lililokuwa limebeba petroli, liliharibika.

Kulingana na msemaji wa polisi, DSP Lawan Shiisu Adam, waathiriwa walikuwa wamekimbilia kuchota mafuta ya petroli iliyokuwa ikivuja kutoka kwa lori lililoharibika wakati cheche iliposababisha mlipuko.

“Wakati mafuta yalipokuwa yakivuja kutoka kwa lori, watu walionywa mara kwa mara kutokaribia mahali hapo.

Polisi walizingira eneo hilo kuzuia watu kwenda eneo la tukio lakini kulikuwa na umati wa watu na waliwazidi nguvu polisi, na kuanza kuchota mafuta yaliyovuja.

Ghafla ukatokea mlipuko,” Bwana Adam alisema.

Wengi wa waathiriwa waliteketezwa kiasi cha kutoweza kutambuliwa.

Wengine ambao walinusurika, walipata majeraha ya viwango tofauti – mengi yakitishia maisha na kukimbizwa hospitalini.

Nigeria inaendelea kushuhudia vifo vya watu wengi vinavyosababishwa na kulipuka kwa malori ya mafuta mara kwa mara.

Mwezi uliopita, takriban watu 48 waliuawa wakati lori la mafuta lilipogongana na gari lingine katika Jimbo la Kati la Niger.

Mamlaka ilisema kuwa lori hilo la mafuta liligongana na lori lililokuwa limebeba wasafiri na ng’ombe, 50 kati yao waliteketezwa wakiwa hai.

Mnamo mwezi Julai 2023, lori la mafuta lililipuka katika jimbo la Ondo Kusini Magharibi mwa Nigeria na kuua watu wasiopungua wanane.

Inasemekana kuwa waathiriwa walikuwa wameenda kuchota mafuta kutoka kwa lori la kubeba petroli ambalo lilihusika katika ajali.

Korea Kaskazini yalipua barabara kuu na reli inayoiunganisha na Korea Kusini ili “kutenganisha kabisa” nchi zote mbili

g

Korea Kaskazini imelipua sehemu kadhaa za barabara na njia za reli zilizoiunganisha na Korea Kusini na vilipuzi siku ya Jumanne.

Miundombinu hii iliyopo katika sehemu ya kaskazini ya mpaka wa kijeshi, zilikuwa zimeundwa hapo awali kwa nia ya kuunganishwa nchi hizo tena siku zijazo na hazikufunguliwa kamwe kwa ajili ya safari.

g
Maelezo ya picha,Milipuko hiyo mikubwa iliharibu barabara na reli kadhaa kwenye mpaka baina ya nchi mbili

Tukio hilo lilitokea wakati wa mvutano uliosababishwa na malalamiko ya pande zote mbili.

Korea Kaskazini, ambayo tayari ilikuwa imeendeleza mpango wake siku zilizopita wa kuharibu barabara ili “kuzitenganisha kabisa” nchi zote mbili, iliishutumu Kusinikupelekandege zisizo na rubani katika eneo lake kueneza propaganda.

Kim Yo Jong, dada yake kiongozi Kim Jong-un, alitoa onyo la kulipiza kisasi dhidi ya nchi hiyo jirani, akionya kwamba “italipa gharama kubwa” kwa madai ya mashambulizi ya anga.

Israel yaushambulia mji mkuu wa Lebanon kwa mara ya kwanza baada ya siku tano

c

Usiku kucha kuamkia leo, Israel imefanya ashambulizi ya anga kwenye viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Hii ni mara ya kwanza kwa mji mkuu kulengwa kwa kipindi cha karibu wiki.

Israel imesema imepiga ghala la chini la ardhi linalotumiwa na Hezbollah kuhifadhi silaha. Wakati huo huo, inasema roketi 50 zilirushwa kuelekea mji wa Safed kaskazini mwa Israel usiku kucha.

Mashambulizi ya mjini Beirut yamekuja baada ya mamlaka ya Lebanon kuripoti kwamba mashambulizi ya anga ya Israel yaliwaua watu kote mashariki na kusini mwa nchi.

Haya yanajiri baada ya Israel kutoa agizo lake la kwanza la kuuhama mji wa Dahieh katika muda wa wiki moja, na kuwaamuru wakaazi kuondoka eneo moja huko Harek Hreik.

Baada ya kulishambulia jiji hilo kwa mashambulizi ya kila siku na kutoa amri kadhaa za kuhama, Israel ilisitisha mashambulizi mjini Beirut wiki iliyopita, ingawa operesheni yake ya ardhini kusini mwa Lebanon, na mashambulizi ya anga katika maeneo mengine ya nchi, yaliendelea.

Tuchel akubali kuwa meneja ajaye wa England

c
Maelezo ya picha,Thomas Tuchel aliondoka Baynern Munich mwezi Mei baada ya klabu hiyo ya Ujerumani kushindwa kushinda taji la Bundesliga

Kocha wa zamani wa Chelsea Thomas Tuchel amekubali kuwa meneja ajaye wa Uingereza.

BBC imeambiwa na vyanzo viwili tofauti kwamba Mjerumani Tuchel atakuwa meneja wa tatu wa kudumu asiye Mwingereza wa timu ya wanaume ya Uingereza baada ya Sven-Goran Eriksson na Fabio Capello.

Uingereza imekuwa bila meneja wa kudumu tangu Gareth Southgate ajiuzulu kufuatia kushindwa kwa Three Lions kwenye fainali ya Euro 2024 dhidi ya Uhispania.

Lee Carsley, ambaye Chama cha Soka kilimteua kwa muda, atasalia katika nafasi yake kwa mechi mbili za mwisho za Ligi ya Mataifa ya Uingereza dhidi ya Ugiriki na Jamhuri ya Ireland mnamo Novemba, huku Tuchel akitarajiwa kuchukua rasmi baada ya hapo.

Utambulisho rasmi wa Tuchel unatarajiwa kufanyika Jumatano huko Wembley.

Lengo lake kuu litakuwa kuiongoza England kupitia kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 ambalo litafanyika Marekani , Canada na Mexico.

Tuchel si mgeni katika la Uingereza akiwa ameiongoza Chelsea kati ya Januari 2021 na Septemba 2022.

Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 51 alinyanyua mataji kama vile Champions League, Kombe la dunia la Fifa na Uefa Super Cup akiwa na The Blues kabla ya kutimuliwa.

Tazama: Shambulio la Israel lilivyopiga kambi ya mahema ya wakimbizi katika hospitali ya Gaza

Maelezo ya video,Tazama: Shambulio la Israel lilivyopiga kambi ya mahema ya wakimbizi katika hospitali ya Gaza

Madaktari wa Palestina wanasema shambulizi la anga la Israel limepiga kambi moja ndani ya hospitali ya Al-Aqsa iliyopo Gaza.

Picha kutok shirika la habari la Reuters zinaonyesha watu wakizima moto katika kambi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao.

Takriban watu wanne waliuawa katika hospitali ya mji wa Deir Al-Balah, madaktari wanasema.

Jeshi la Israel limesema liliwashambulia wanamgambo waliokuwa wakiendesha shughuli zao kutoka katika kituo cha amri ndani ya eneo hilo la hospitali.

SENETI Jumanne ilizamika kuahirisha kikao chake kutokana na ukosefu wa idadi hitajika ya maseneta 15 jinsi inavyoamrishwa kwenye katiba.

Seneti ina maseneta 67 na idadi inayohitajika kuendesha shughuli zake ni maseneta 15 na zaidi. Kwa mujibu wa katiba, Bunge la Kitaifa nalo lazima liwe na wabunge 50 au zaidi ili kuendelea na vikao vyake.

Hii ni kinyume na mnamo Jumatatu ambapo maseneta walifika wote wakati wa kujadili hoja ya kumtimua Gavana wa Kericho Erick Mutai.

Kukosekana kwa idadi inayofaa ya maseneta kulitokea wiki moja baada ya Bunge la Kitaifa nalo kulazimika kutoendelea na vikao vyake kwa kuwa wabunge hawakuwepo.

Kinaya ni kuwa wakati wa kujadili na kuipigia kura hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua, wabunge 326 walikuwepo.

Siku hiyo hata kengele ambayo Naibu Spika Gladys Shollei aliamrisha ipigwe haikusaidia kitu kwa sababu wabunge hawakuwepo.

Jana, seneti ilifuata mkondo, kwa kuwa kulikuwa na chini ya maseneta 10 wakati wa kikao cha asubuhi. Licha ya Naibu Spika Kathuri Murungi kuamrisha kengele ipigwe kuwaamrisha maseneta waje kikaoni, bado idadi hitajika haikufika.

“Waheshimiwa maseneta, kutokana na kutotimia kwa idadi hitajika ya maseneta, naahirisha kikao hadi saa 2.30 leo (jana),” Bw Murungi akasema akiahirisha kikao cha jana.

Seneti ilikuwa imeorodhesha kusomwa kwa hoja 14 na miswada mitatu. Pia kulikuwa na miswada mitatu ambayo ilikuwa iangaziwe kwa sababu ilipendekezewa ifanyiwe marekebisho.

Miswada hiyo ilikuwa ni Mswada wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa 2023 na Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi, ambayo inadhaminiwa na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.

Pia kulikuwa na Mswada wa Kuzuia na Kudhibiti Saratani 2023 ambao unadhaminiwa na Seneta wa Nandi Samson Cherarkey.

Miswada mingine ambayo ilikuwa iangaziwe ni Usimamizi wa Fedha za Umma (Seneta Hamida Kibwana), Huduma za Dharura za Uokoaji wakati wa Moto 2023 (Mohamed Abass) na Uchukuzi wa Umma 2023 (Bonny Khalwale).

Miswada mitatu kuhusu Ripoti ya Maridhiano Nchini (NADCO), Mswada wa Vyama vya Kisiasa na Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi 2024 pia ilikuwa iangaziwe.

Kulikuwa na ripoti kadhaa za uchunguzi kutoka kwa kamati ambazo zilikuwa ziwasilishwe.

Kati ya ripoti hizo ni uajiri katika idara mbalimbali za serikali, kurefushwa kwa mikataba ya ununuzi na kusambazwa kwa kawi nchini, ripoti kuhusu mlipuko wa gesi Embakasi na pia kudadavuliwa kwa ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya fedha kwenye kaunti.

Hatua ya wabunge na maseneta kukosa kufika bungeni inaonyesha kuwa hawachukulii kwa uzito kazi zao.

Mwaka jana Bw Cheruiyot aliwachemkia maseneta, akisema anashangaa kwa nini wanapigania wachaguliwe kisha mwishowe wanatelekeza majukumu yao waliyopewa na Wakenya.

Uhusika wa Orengo katika kikosi cha mawakili wa Bunge wapingwa na Gachagua

MAWAKILI wawili wandani wa Raila ambao ni viongozi waliochaguliwa, wamejiunga na kesi ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua wakiwakilisha Bunge la Kitaifa katika kikao cha Seneti.

Wakili James Orengo ambaye ni Seneta wa Siaya na mbunge wa Rarieda Otiende Omollo wameungana na, Paul Nyamodi, Erick Gumbo, Muthomi Thiankolu, Moses Kipkogei, Peter Wanyama, Ken Melly, Mwangi Kang’u, George Murugara, Samwel Chepkonga, John Makali na  Zamzam Mohamed kuwakilisha Bunge la Taifa.

Bw Murugara, Bw Chepkonga, Bw Makali na Bi Mohammed pia ni wabunge.

Upande wa Bw Gachagua unaongozwa na Wakili Paul Muite, Elisha Ongoya, Tom Macharia, Swanya Victor, Ndegwa Njiru, Faith Waigwa, Amos Kisilu, John Njomo, George Wandati Andrew Muge, Julia Omwamba, Eric Naibei na Willis Echesa.

Tayari, mawakili wa Bw Gachagua wamepinga uwepo wa Bw Orengo kuwakilisha Bunge la Taifa.

Bw Njiru alisema suala kama hili liliibuliwa wakati wa hoja ya kumtimua aliyekuwa naibu gavana wa Kisii Robert Monda na kwamba mahakama kuu iliamua kuwa mtu aliye katika kazi ya kuajiriwa hawezi kuwakilisha upande wowote mbele ya bunge.

Spika Kingi atafanya uamuzi baada ya Gachagua kusomewa mashtaka.

Nderitu Gachagua alinusurika Seneti 2016, hivyo Rigathi pia aombea nyota ishuke kumuokoa

FAMILIA ya Naibu Rais Geoffrey Rigathi Gachagua si geni kwa hoja ya kutimuliwa mamlakani katika Seneti kwa kuwa marehemu kakake James Nderitu alikabiliana nayo miaka minane iliyopita alipokuwa Gavana wa Nyeri.

Marehemu Gavana Nderitu, ambaye aliaga dunia kutokana na saratani ya kongosho mnamo Februari 24, 2017, alikuwa ameondolewa na madiwani 35 kati ya 47 wa Bunge la Kaunti ya Nyeri mnamo Septemba 2, 2016—na hivyo kufika Seneti kujitetea mnamo Septemba 15.

Miaka minane baadaye, kakake mdogo, Rigathi, anajitetea dhidi ya kuondolewa mamlakani kama Naibu Rais wa Kenya.

Bw Nderitu alipokuwa akijitetea Seneti, alikuwa na umri wa miaka 62, Rigathi amefika katika Bunge hilo kujitetea akiwa na umri wa miaka 59.

Japo Bw Nderitu alitakaswa makosa yoyote na Seneti, hatima ya Bw Rigathi haijulikani, huku wafuasi wake wakisubiri matokeo baada ya maseneta kupiga kura Alhamisi.

Ndugu hao wawili walizaliwa katika kijiji cha Hiriga Kaunti ya Nyeri wakiwa watoto wa Bw Gachagua Reriani na Martha Kirigo—wapiganiaji wa uhuru wa Mau Mau katika msitu wa Mlima Kenya.

Baba yao alipokuwa akiwahudumia askari wa Mau Mau, mama yao alisaidia kuwalisha kwa siri, pamoja na kuwapelekea silaha.

Kulingana na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, “hii ni familia ambayo ilibarikiwa kuwa na talanta za uongozi lakini inavyotarajiwa, maadui wa baraka hiyo wamekuwa wakijaribu kuiangamiza”.

Bw Kahiga mnamo Oktoba 16, 2024 aliambia Radio Fortune Africa kuwa “kama baba wa sasa wa Kaunti ya Nyeri, naweza kuapa kwamba hakuna ubaya katika familia ya Gachagua, ni kwamba nyota yake ya uongozi inatatizwa na wale wanaofurahia kuangusha talanta.”

Nderitu alitimuliwa na bunge la kaunti yake, kufuatia hoja iliyowasilishwa na diwani wa Mathari Baragu Mutahi.

Kuhusu kuondolewa kwa mashtaka ya Rigathi, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse aliwasilisha Oktoba 1, 2024 akiibua mashtaka 11, na wabunge 291, wakiwemo takriban wabunge wote kutoka eneo la Mlima Kenya, waliungana dhidi yake.

Kabla ya kuondolewa mamlakani, Bw Nderitu aliomba msamaha wakazi wa Nyeri kwa kuruhusu suala hilo kuzidi hadi kuwa mjadala wa kitaifa.

Kadhalika, Bw Rigathi, ameomba msamaha kwa Rais William Ruto, Bunge na wananchi wa Kenya kwa mchakato wa kumuondoa mamlakani.

Hata hivyo, maombi yote mawili ya msamaha, hayakufanya kazi na michakato ya kuwashtaki ilifikia Seneti.

Mnamo Septemba 15, 2016, Bw Nderitu alikabiliana na Seneti ambapo iliamuliwa kuwa mashtaka dhidi yake hayajatimiza kiwango cha kuondolewa mamlakani.

Alikuwa ameshutumiwa kwa kumteua Alice Wachira kama kaimu Katibu wa Kaunti licha ya, kulingana na  madiwani, hakutimiza mahitaji ya majukumu ya kazi hiyo.

Bunge lilikuwa limependekeza kutimuliwa kwake ofisini mnamo Julai 2016 kwa misingi kwamba hakuwa ametimiza sifa zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na kukosa uzoefu wa miaka 10 katika nafasi ya usimamizi.

Vile vile, madiwani walikuwa wamedai kwamba Bw Nderitu alikuwa amefuja Sh1.7 bilioni.

Wawakilishi hao wa wadi pia walikuwa wamemlaumu gavana huyo kwa kukiuka Katiba kwa kuendesha kaunti bila Baraza la Mawaziri, huku wakidai kuwa serikali yake ilitenga Sh740 milioni kutoka kwa maendeleo hadi shughuli za kawaida bila kufuata utaratibu uliowekwa.

Seneti ilipata madai hayo kuwa hayakuthibitishwa.

Huku Rigathi akikabiliana na Seneti, na kusubiri uamuzi wake Alhamisi, atakuwa na matumaini ya kuwa na bahati ya marehemu kaka yake itamuokoa.

Miongoni mwa madai ya Mutuse ni kwamba Bw Rigathi alihujumu wosia wa Nderitu wa kuwanyima warithi halali wa mali ya marehemu, jambo ambalo limeshuhudia wosia wa kibinafsi ‘kufichuliwa’ na kuwa hati ya umma.

“Kimsingi, Wosia wa marehemu ni miongoni mwa sababu zilizowasilishwa kushinikiza kuondolewa kwa naibu rais…hivyo aombe kwa bidii ili roho ya kaka yake ishuke na kusimama naye kwenye dhoruba inayomkumba,” anasema Wakili wa Mahakama Kuu Timothy Kariuki.

HABARI NCHINI TANZANIA

MIKATABA YA UJENZI WA MASOKO, BARABARA MWANZA YASAINIWA

Serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 22.7, kutekeleza mradi wa soko la Kirumba na barabara ya Kirumba katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na soko la samaki mkuyuni jijini Mwanza.

Mpango huo unatekelezwa kupitia miradi ya uboreshaji miji Tanzania (TACTIC).

Akishuhudia utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ameziagiza halmashauri husika kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilimela na jiji, ndizo zilizoingia mikataba hiyo na wakandarasi Kampuni ya M/s Comfix and Engineering L.T.D na M/s China Railway 15 Bureau Group Corporation.

Ujenzi wa soko la kirumba na barabara ya kuzunguka soko yenye urefu wa kilomita 2.9, unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 14.7, huku soko la samaki Mkuyuni likigharimu zaidi ya shilingi bilioni 7.3.

KANISA LA FPCT LAJITOSA KUTOKOMEZA UKATILI NA ULEVI ROMBO

Viongozi wa dini wilaya rombo mkoani Kilimanjaro kutoka kanisa la free pentecostal church of tanzania FPCT wameanza mpango wa kutoa elimu mashuleni na vyuoni juu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyotajwa kuongezeka wilayani humo Ili kuondoa kabisa vitendo hivyo.

Viongozi hao wametoa kauli hiyo katika tukio maalum la kuzindua kanisa hilo kwa wilaya ya rombo mkoani humo tukio lililoshirikisha viongozi mbalimbali mkoani humo.

Viongozi hao wamesema ulevi na ukatili wa kijinsia umekua ukiongezeka siku hadi siku jambo linalotia mashaka endapo dini hazitaingilia na kuwafundisha vijana kuwa na hofu ya Mungu kuacha ulevi uliokithiri.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Makazi Duniani ( UN HABITAT) Anaclaudia Rossbach.

Viongozi hao walikutana hivi karibuni mjini Zanzibar katika kikao kilichohudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Bw. Deogratius Kalimenze, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya urasimishaji makazi Bw. Nicolaus Mwakasege pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Mbaraka Abdulrahman.

Katika mazungumzo yao. Mhe. Pinda alimueleza Mkurugenzi huyo wa UN-HABITAT kuwa, Tanzania inaunga mkono juhudi zinazofanywa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa katika kusaidia miradi mbalimbali nchini aliyoieleza kuwa imefikia takriban dola milioni 29.3.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa, ni uwepo wa miji salama na kuzuia uhalifu, maji na usafi wa mazingira, mfuko wa kuwezesha wanawake kumiliki ardhi pamoja na mradi wa usambazaji maji ziwa victoria ambapo ameielezea miradi hiyo yote kuwa imesaidia kuboresha maisha ya watanzania.

Aidha, amemueleza mkurugenzi huyo wa UN -HABITAT nia ya Serikali kulipatia shirika hilo ofisi hapa Tanzania ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ambapo Mkurugenzi huyo amekubali ombi la shirika lake kuwa na ofisi nchini Tanzania.

” tutaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika miradi tofauti itakayoboresha makazi katika miji mbalimbali pamoja na mchakato mzima wa uanzishwaji ofisi ya UN-HABITAT Tanzania” alisema Anaclaudia.

BITEKO AAHIDI MAKUBWA SEKTA YA NISHATI

Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati Tanzania, imeandaa Jukwaa la majadiliano kwenye bara la Afrika litakalofanyika Tanzania, lenye lengo la kujadili juu ya namna ya kuhakikisha inasukuma ajenda ya kuwafikia waafrika Milioni 300 wanaotumia Nishati ya Umeme ifikapo 2030.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo wa siku mbili, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Tanzania Doto Biteko amesema kuwa heshima ya kufanyika Kwa mkutano huo ni kutokana na Mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambapo utasaidia Tanzania kupekeka ujumbe kwa wengine ya kwamba Kila kitu kinawezekana kama Serikali itasimamiwa vizuri.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki amesema kuwa AfDB imeweka nguvu kubwa katika kuipigia debe Tanzania katika fursa za hizo yakiwemo makongamano ya Nishati kutokana na kuonyesha nia na juhudi zinazofanyika za kuibadilisha Tanzania katika matumizi ya Nishati safi.

MRADI WA URAIA WETU UMELETA UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR

Imeelezwa kuwa mradi wa Uraia wetu unatokelezwa na Centre for youth Dialogue umesaidia kwa kiasi kikubwa utatuzi wa changamoto za kisera na kisheria hasa kwa makundi ya watu wenye ulemavu

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi na Mratibu wa Mradi wa Urai wetu Joelbert Shamte amesema mradi huo ambao umeanza Mwaka 2023 na kutegemewa kukamilika Disemba 2024 umekuwa ni wa mafanikio makubwa katika kuziunganisha asasi za kiraia na serikali pamoja na kufanya mapitio ya sera na sheria katika kulinda haki wa wananchi wakiwemo makundi ya watu wenye ulemavu, Vijana na wanawake nchini

Akitoa ushuhuda wa utekelezaji wa mradi huo Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wakalimani wa Lugha ya Alama Zanzibar Kheri Mohamed amesema kupitia mradi huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kufanya marekebisho ya sheria za uajiri katika taasisi Mbalimbali za serikali hasa zinazoa huduma kwa jamii ikiwemo ofisi ya mufti Mkuu na kufanikisha kutolewa kibali cha ajira kwa wakalimani wa lugha ya alama ili kutatuliwa changamoto za watu wenye ulemavu wa uziwi wanapoenda kufata huduma katika ofisi hizo

DC MAPUNDA AHIMIZA WANA TEMEKE | KUSHIRIKI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda ametoa rai kwa Wananchi wa Mbagala kujiandikisha katika Daftari la Mkazi ili kujipa uhalali wa Kushiriki kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao umepangwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu na kuchagua kiongozi wa Mtaa atakayeweza kusikiliza na Kutatua kero kwenye maeneo yao.

DC Mapunda ametoa kauli hiyo leo Oktoba 16, 2024 wakati akiwahamasisha Wananchi wa Mbagala Rangi tatu kuendelea kujitokeza kwenye Zoezi hilo la Uandikishaji linaloendelea nchini.

“Kulingana na kalenda ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zoezi hili limepangwa kufika Mwisho Oktoba 20, kwa hiyo niwapongeze ambao tayari wamejiandikisha, lakini hata hivyo wale ambao bado, niwaombe tujitokeze ili tuweze kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi huu muhimu kwa Maendeleo yetu wana Temeke” amesema DC Mapunda.

Watafiti 111 kutoka mataifa kumi mbalimbali wamekutana mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani, ili kuwasilisha na kujadili tafiti zao zinazohusiana na elimu ya msingi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia katika sekta hii kwa maendeleo endelevu nchini Tanzania.

Mataifa hayo ni Uganda, Zambia, Jamaica, Uswisi, Uholanzi, Jamhuri ya Kongo, Nigeria, Kenya, na wenyeji Tanzania Bara na Zanzibar. Wajumbe wa mataifa haya watawasilisha mada za utafiti zinazohusiana na elimu ya msingi, huku mada nyingine zikijumuisha ushiriki wa wananchi katika elimu na masuala ya chakula.

Tafiti hizo zitawasilishwa Oktoba 16 /2024 kwenye kongamano la kimataifa la siku tatu kuhusu elimu, lililoandaliwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Kitivo cha Elimu.

Dokta Wilson Mahera, Naibu Katibu Mkuu wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, akimuwakilisha Waziri Profesa Adolf Mkenda, amesema mada zilizowakutanisha watafiti ni muhimu sana kwani zinaendana na malengo ya sasa ya Tanzania.

Alisisitiza kuwa kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sera na mfumo wa elimu nchini, ambapo elimu ya msingi inachukuliwa kama nguzo muhimu ya kuandaa watoto kuwa na uwezo wa kufikiri kwa kina, kuwa wabunifu, na kujiendeleza kimaadili.

Katibu wa kongamano hilo, Dr. Janeth Kigobe, ambaye pia ni mhadhiri wa chuo hicho, alisema kuwa hili ni kongamano la pili linaloandaliwa na Kitivo cha Elimu, likilenga kuboresha elimu ya msingi.

Amefafanua kuwa mwaka huu kongamano limejikita kwenye mabadiliko mapya ya mfumo wa elimu yanayoanza kutumika, na kwamba ni njia ya kusaidia serikali katika kutekeleza mipango yake ya kuboresha elimu.

Profesa Elifas Bisanda, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, alisisitiza umuhimu wa chuo hicho katika kuendeleza elimu ya msingi nchini. Alieleza kuwa tangu mwaka 2008, chuo kimeanzisha stashahada ya elimu ya msingi ili kukabiliana na upungufu wa walimu waliohitimu katika ngazi hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameielekeza menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kubuni mikakati ya kuongeza mapato yatokanayo na Utalii ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 16,2024 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika Ofisi zao zilizopo jijini Arusha.

” Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya lakini Mheshimiwa Rais anataka tuongeze mapato na tubuni mazao mapya ya utalii ” amesisitiza.

Aidha, ameielekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ihakikishe inatoa ufumbuzi wa changamoto ya magugu vamizi yanayoharibu uoto wa asili ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

“Natoa siku saba kwa TAFORI waende katika bonde la Kreta na kutoa ufumbuzi wa namna ya kudhibiti mimea vamizi ” amesisitiza Mhe. Chana.

Naye, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula ameitaka mamlaka hiyo kuwa wabunifu, kuangalia namna ya kujitangaza na kubuni mazao mengine ya utalii ili kuiongezea Serikali mapato.

Kikao hicho ni muendelezo wa Vikao kazi vya Waziri wa Maliasili na Utalii kusikiliza changamoto za Watumishi na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi.

Wanannchi wa Kata ya Bugarama Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera wamejitokeza kwa wingi kumlaki mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndg. Mohamed Kawaida.

@comrade_kawaida ameanza ziara ya Kikazi Mkoani Kagera yenye lengo la kuhamasisha wananchi kuendelea Kujiandikisha kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

@sirallawi

MRADI WA MAJI CHANZO CHA ZIWA VICTORIA BUTIMBA MWANZA KAZI IMEKAMILIKA

Ikumbukwe kwamba Tarehe 14 mwezi October 2024 katika Maadhimisho ya Kilele cha Mwenge wa Uhuru Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumzia hali ya huduma ya Maji Mwanza aliweka bayana kuwa mwezi huu wa Octoba mradi mkubwa wa Maji wa chanzo cha Ziwa Victoria utakamilika.

Mashuhuda wamefika na wamejihakikisha hakika kweli kazi imekamilika kama Mhe Rais alivyowajulisha wana Mwanza na wanatuma salam za shukrani kwa Mhe Rais na kumpa ripoti ya kazi.

Jambo kubwa na shauku ni kumsubiri Mhe Rais kuja kuzindua rasmi Mradi huu muhimu sana kwa wana Mwanza na viunga vyake.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini (CGP), Jeremiah Katungu leo Oktoba 16, 2024, ametembelea mradi wa nishati safi ya kupikia katika Gereza Kuu Butimba na kupongeza uongozi wa Magereza Mkoa wa Mwanza kwa kuhakikisha maono ya Rais Samia Suluhu Hassan yanatimia kwa kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

CGP Katungu ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mwanza kwenye kikao alichokiitisha baada ya kukagua miradi inayotekelezwa katika mkoa huo. Katika kikao hicho, amesisitiza umuhimu wa kusimamia vizuri miradi ili kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye vituo husika.

Aidha, amebainisha kuwa katika ukusanyaji maduhuli kwa mwaka huu lengo ni kukusanya shilingi milioni 800, huku akiwapongeza watendaji kwa kufanikisha malengo kwa kukusanya shilingi milioni 260 katika kota ya kwanza badala ya milioni 200 zilizokuwa zimepangwa.

Ametoa wito kwa wakuu wa magereza wa mikoa kushirikiana na maafisa kuhakikisha miradi inatangazwa na mapato na matumizi yanawekwa wazi.

Pia, amejibu hoja mbalimbali kutoka kwa maafisa na askari, akiahidi kwamba jeshi linafuatilia changamoto zinazowakabili na kuahidi ufumbuzi huku akiwataka kuongeza ushirikiano.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment