Baadhi ya yaliyotokea baada ya bwana Yesu kuzaliwa.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Heri ya sikukuu ya Christmas na nawatakia sikukuu njema.
Namshukuru MUNGU kwa neema yake na ulinzi wake kwangu hadi leo.

Tarehe Kama ya leo tunaadhimisha tukikumbuka kuja kwa ukombozi duniani, huwa nakuletea ujumbe maalumu mtandaoni kwa ajili ya tukio hili Kila mwaka.
Nakumbuka Christmas mwaka Jana 2018 nilikuletea somo linalisema KWANINI BWANA YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

Mwaka 2017 katika ujumbe wa Christmas nikakuletea somo linalosema KILA ALIYE KATIKA SAFARI YA MBINGUNI HUJITAKASA.

Mwaka 2016 nikakuletea somo linalosema KRISMASI NA KUZALIWA KWA BWANA YESU, Namshukuru MUNGU kwa somo hili ambalo liliwekwa pia magazetini kwa miaka miwili mfululizo.

Nakumbuka pia mwaka 2015 nilikuletea ujumbe unaosema BWANA YESU NI HAKI YETU.

Mwaka huu nakuletea ujumbe unaosema BAADHI YA YALIYOTOKEA BAADA YA BWANA YESU KUZALIWA.

Sina mambo mengi sana leo ila naamini katika somo hili utajifunza kitu.

Baadhi ya yaliyotokea baada ya Bwana YESU Kuzaliwa.

  1. Malaika alijulisha kwamba Mwokozi amezaliwa, ndiye KRISTO Bwana.

Luka 2:9-11 “Malaika wa BWANA akawatokea ghafula, utukufu wa BWANA ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye KRISTO Bwana.”

Tukio la Kuzaliwa kwa YESU KRISTO lilikuwa tukio kubwa Sana hivyo ndio maana tunaona hadi Malaika wa MUNGU akiwajulisha wanadamu maana hiyo Ni habari njema itakayoleta furaha kuu Sana kwa wanadamu.

  1. Maelfu ya Malaika wa MUNGU walimsifu MUNGU.

Luka 2:13-14 ” Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu MUNGU, na kusema, Atukuzwe MUNGU juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

  1. Wachungaji walimtukuza MUNGU.

Luka 2:20 “Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza MUNGU na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.”

Nini nataka kusema?
Ni kwamba unapokumbuka Kuzaliwa kwa Bwana YESU KRISTO Naomba uwe na maana ya kuadhimisha kuja kwa ukombozi duniani na hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako binafsi.

Tunasherekea sikukuu hii tukikumbuka kuja kwa ukombozi wetu duniani.

Kuzaliwa kwa YESU KRISTO ni sherehe kubwa mno maana hata siku alipozaliwa tunaona Malaika wakisherekea kwa kumsifu MUNGU na kumtukuza.

Hata wewe itumie siku hii kumsifu MUNGU Kama Malaika walivyofanya.

Hata wewe itumie siku hii kumtukuza MUNGU Kama Wachungaji walivyofanya siku YESU KRISTO anazaliwa.

Hata wewe ndugu itumie siku hii kumsifu MUNGU.

Katika siku hii hatusherekei birthday ya YESU Bali tunaadhimisha kuja kwa ukombozi wetu duniani.
Sio kwamba YESU alizaliwa tarehe 25 December bali mwanzoni mwanzoni mwa Kanisa ufalme mkubwa uliokuwa unatawala duniani Ni ufalme wa Rumi chini ya Kaisari aitwaye Constantine, hii Ni Kama miaka 300 baada ya Bwana YESU KRISTO Kuzaliwa duniani.
Sasa watu wote wakati huo walikuwa wanalazimishwa kutumia siku ya tarehe 25 mwezi wa mwisho wa Mwaka kusherekea miungu ya mvua, lakini viongozi wa Kanisa wakaona ili Wakristo wasinaswe na mambo ya miungu wakaamua tarehe hiyo hiyo ambayo wapagani wanaabudu miungu basi Kanisa lisherekee kuja kwa Bwana YESU KRISTO Mwokozi, ni utaratibu mzuri sana, maana badala Kanisa kulazimishwa kuabudu miungu siku hiyo basi wanamwabudu MUNGU wakimtukuza pia kwa kumleta Mwanaye wa pekee duniani ili kuja kutuokoa.
Hivyo YESU KRISTO hakuzaliwa tarehe 25 December lakini hiyo haifuti tukio la kwamba Bwana YESU KRISTO alikuja duniani na akaishi Kama mwanadamu ili atuokoe.

Najua pia Kuna baadhi ya Wakristo hawaadhimishi siku hii, lakini pia baadhi ya Wakristo huadhimisha mwezi wa pili yaani February, yote Ni sawa Kama wanaitumia siku hii kwa ajili ya KRISTO na kwa utukufu wa MUNGU.

Warumi 14:5-6 ” Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana(YESU); naye alaye, hula kwa Bwana(YESU), kwa maana amshukuru MUNGU; tena asiyekula, hali kwa Bwana(YESU), naye pia amshukuru MUNGU.”

Kumbe hakuna tatizo katika kusherekea na hakuna tatizo pia katika kutokusherekea.

Muhimu tu ni kwamba, Kama unaadhimisha siku hii basi iadhimishe katika Bwana YESU KRISTO na kwa utakatifu wote.
Biblia inasema kwamba katika mienendo yetu siku zote tuishi kwa utakatifu Kama YESU aliyetuokoa alivyo mtakatifu.

1 Petro 1:15 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;”

Kumbuka pia kuadhimisha siku hii huku hauna YESU haikusaidii chochote wala haikuletei faida yeyote, hivyo hakikisha unasherekea siku hii huku YESU KRISTO akiwa Ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako.



CantonaJoseph’s contacts
Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/
Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.
Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph
LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo
Management Fortune Baraka Entertainments
Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com
Email fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com cantona.online254@gmail.com
Contacts +254748836127
Wewe ni wa maana sana!

Copyrights Reserved @2019 FortuneBaraka Entertainments.




Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment