DRC: Wanne wafariki na zaidi ya arobaini hawajulikani walipo baada ya boti kuzama

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Takriban watu wanne wamefariki na wengine zaidi ya 40 hawajulikani waliko baada ya boti iliyotengenezwa kwa mbao kuzama katika Mto Kwango kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Vyanzo vya ndani vinasema kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba mizigo kupita kiasi na kubainisha kwamba ajali hiyo imetokea siku ya Jumatatu.

Wafanyakazi wa kujitolea kutoka mashirika ya Msalaba Mwekundu ya DRC na Rwanda wakipakia miili iliyoopolewa kutoka Ziwa Kivu, kwenye ufuo wa Gisenyi, Aprili 20, 2019.
Wafanyakazi wa kujitolea kutoka mashirika ya Msalaba Mwekundu ya DRC na Rwanda wakipakia miili iliyoopolewa kutoka Ziwa Kivu, kwenye ufuo wa Gisenyi, Aprili 20, 2019. ALEXIS HUGUET / AFP

“Miili minne imeopolewa kufikia sasa, watu 79 wamenusurika na zaidi ya arobaini hawajulikani walipo,” Naibu gavana wa mkoa wa Kwango Rémy Saki ameliambia shirika la habari la AFP. Utafutaji umekuwa ukiendelea siku ya Jumatatu jioni, katika mazingira magumu: “Tutalazimika kungoja siku moja au mbili ili kufanikiwa kupata boti hiyo, kujaribu kuondoa jahazi na kuona ikiwa kuna miili iliyokwama,” ameongeza Bw. Saki.

Tukio la kuuzama kwa boti iliyokuwa na abiria 150, kulingana na shuhuda zilizokusanywa na mamlaka, lilitokea asubuhi kwenye Mto Kwango, Mto mdogo unaokutana na Mto Kongo. “Boti hiyo iligonga daraja” katika mazingira ambayo bado hayajabainishwa, ameeleza meya wa kijiji cha Pont Kwango, Jean-Baptiste Nkololo. “Kulingana na abiria, kulikuwa na karibu watu 150 ndani ya boti. Kwa sasa manusura chini ya mia moja ndio wamepatikana, wengine wako chini ya maji,” amesema.

Nchi kubwa katika Afrika ya Kati, DRC ina barabara chache sana zinazopitika na mara nyingi safari hufanywa kwenye maziwa na vile vile kwenye Mto Kongo na vijito vyake, ambapo ajali za meli hutokea mara kwa mara. Takriban watu 25 walikufa maji mwishoni mwa mwezi wa Julai baada ya boti kuzama kwenye Mto Kongo, katika mkoa wa Maniema (katikati-mashariki). Mnamo mwaka 2019, zaidi ya watu mia moja wwaliuawa baada ya boti yao kuzama. Kutokuwepo kwa orodha ya abiria kwa muda mrefu kunatatiza shughuli za utafutaji.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment