Somo la leo mpendwa limelenga kuwasaidia watu ambao wapo katika mahusiano ambayo sio sahihi lakini wanajiona kama wanashindwa kunasuka nayo. Hili somo linataka litusaidie kunasua nafsi zetu toka kwenye mtego ambao umesababishwa na mahusiano yasiyo sahihi ambayo ama tayari yanatuletea madhara au kuna dalili zote za hayo mahusiano kuja kutuletea madhara huko mbeleni. Hili somo linalenga kuwasaidia wanawake na wanaume, wakaka na wadada, wamama na wababa ambao wameshanasa kwenye mahusiano ambayo sio sahihi na wanajiona kama hawana namna ya kutoka. Roho Mtakatifu atufungue macho yetu ili tuione kweli ambayo itaenda kutuweka huru.
Msisitizo mkubwa wa hili somo utakua kuhusu kuambatana kwa nafsi (soul tie). Na tutakaza zaidi kwenye kuambatana kwa nafsi kusiko sahihi.
Kabla hatujaingia kuangalia maswala ya kuambatana huko kwa nafsi ni vema kwanza kutambua kuwa mwanadamu ni roho anayo nafsi anakaa ndani ya mwili.
Kwa sababu mkazo wetu utakuwa kwenye maswala ya nafsi ni vizuri kila mmoja wetu ajue huko kwenye nafsi kuna nini?
Kwenye nafsi kuna vitu vitatu:
1). Hisia: ambayo kwayo tunahisi. Tunapenda au kuchukia, tunafurahi au kusikitika nk.
2). Nia: ambayo kwayo tunafikiri.
3). Utashi: ambayo kwayo tunaamua.
Mwanadamu mmoja anahusiana na mwanadamu mwingine kwa nafsi yake. Unapokuwa katika mahusiano na mtu hisia zako, nia yako na utashi wako kwa kiwango fulani inaungamanishwa na huyo mtu na huwezi ukawa unafikiri sawa na ulivyokuwa unafikiri kabla ya kuingia kwenye huo uhusiano, huwezi ukawa una hisia sawa na zile ambazo ulikuwa nazo kabla hujaingia katika huo uhusiano na huwezi kuwa na maamuzi sawa na yale ulikuwa nayo kabla hujaingia kwenye huo uhusiano.
Mahusiano yanapokuwa sio sahihi mtu unahisi wazi kufungwa kwenye nafsi yako na japo unatamani hisia zako ziwe sahihi lakini zinakuwa zimevurugwa na iko kama hujui ufanyaje.
Mahusiano yanapokuwa si sahihi kufikiri kwako kunavurugwa na unatamani usiwe unafikiri hivyo lakini iko kama hujui ufanyaje ili unasuke.
Mahusiano yanapokuwa sio sahihi mpaka maamuzi yako yanavurugwa na japo unajua kabisa kwamba huu uamuzi sio sahihi ni kama umefungwa na unalazimishwa kufanya uhusiano usiyo sahihi na ni kama huna uwezalo kufanya kuzuia.
Ukishaona hivyo ujue nafsi yako ishakamatwa, imefungwa kwenye mwabatano nafsi usio sahihi na mtu mwingine. Kila kuhusiana kusiko sahihi hupelekea mwambatano wa nafsi usio sahihi. Kila mwabatano wa nafsi usio sahihi kupelekea mtu kufungwa kwenye nafsi yake na kuhisi wazi kuwa yanayotokana na nafsi yake sio yake kwa hiari ila ni kama kuna nguvu ya ziada imemkamata na inamfanya atii kwa shuruti kile ambacho kwa kweli kama angekua na hiari asingetii.
Watu wa Mungu wanauelewa sana ulimwengu wa mwili, na kwa kiasi kikubwa pia wanauelewa ulimwengu wa roho ila ufahamu wetu wa ulimwengu wa nafsi ni mdogo sana.
Mara nyingi mtu akishajikuta amebanwa eneo hilo au ataomba au atatafuta kuombewa na mara nyingi huku kuomba au kuombewa hakumzalii sana matunda maana kuomba kwenye eneo ambalo una ufahamu mdogo sana nalo ni kama tu kupiga ngumi hewani. Unapigana na adui usiyemwona. Unatumia nguvu nyingi kurusha makonde ambayo huna uhakika kama yanampata mwisho wa siku hujapiga kitu, unakata tamaa alafu unasema hapa siwezi kunasuka kwa hiyo unaendelea tu japo unajua sio sahihi.
Wengi wanakemea mapepo wakati kwa kweli hakuna kitu km hicho ni nafsi ndo imevurugwa.
Mungu atufungue macho tuelewe haya mambo yanaendaje ili tuweze kuyashughulikia ipasavyo maana ugonjwa usiyoujua unautibuje? Na hata kama unaujua usipotumia dawa sahihi unaponaje. Huwezi ukaponya malaria kwa kutumia antibiotics.
Huwezi ukawa unaumwa kichwa alafu ukawa unatumia sindani za christapen. Kila ugonjwa una dawa sahihi ya kuitibu. Na vile vile kila tatizo la mwanadamu lina ufunguo sahihi wa Ufalme wa Mungu wa kulitatua.
Wakaka na wadada ambao hawapo kwenye ndoa na wapo katika mahusiano hatarishi, wanayojua sio sahihi ila wameshindwa kujinasua kwa hiyo wanayatetea japo wanajua kabisa sio sahihi na mwisho wake hautakua mzuri. Wababa na wamama waliyopo kwenye ndoa wanatoka nje ya ndoa zao na wamenasa kwenye hayo mahusiano yasiyo sahihi na wamefanya kila namna ya kutoka ila wameshindwa.
Katika jamii leo tabia zisizompendeza Mungu kama uasherati na zinaa zimekubalika sio kwa sababu jamii wanapenda kumkosea Mungu ila jamii imenaswa wanashindwa kutoka kwa hiyo badala ya kukubali wameshindwa wamtake Mungu msaada jamii inatetea hiyo tabia japo hiyo tabia imeacha majanga makubwa ya madhara ndani ya jamii kama watoto wa mtaani, yatima, ndoa zilizovunjika, mioyo iliyoumizwa, magonjwa ya zinaa mengine yakiwa yanaua watu kwa maelfu.
Nini shida, wanadamu wamekamatwa pabaya, kwenye nafsi zao mahali ambapo sio tu ndipo wanapohusiana na wengine kupitia hapo lakini pia maamuzi yao, kufikiri kwa na hisia zao hutokea huko. Fikiria kukishavurugwa kutakuwaje. Na watu wamevurugwa hatari.
ILA DAWA IPO.
SASA KUAMBATANA KWA NAFSI NDO NINI?
Kuambatana kwa nafsi ni kuunganishwa kwa nafsi kati ya watu wawili ambako kunapelekea watu hawa wawili katika ulimwengu wa nafsi kuwa kama kitu kimoja kiasi kwamba hisia ya mmoja inaathiri ya mwingine, kufikiri kwa mmoja kunaathiri kufikiri kwa mwingine na kuamua kwa mmoja kuna athari ya moja kwa moja juu ya maamuzi ya mwingine.
Nafsi mbili zinapounganishwa ni kama kwenye huo ulimwengu wa nafsi hizo nafsi mbili zinafanywa vitu kwa pamoja au kwa kushabiana. Nafsi mbili hizo zikuunganishwa, hawa watu wawili kuna namna wanakuwa wameunganishwa ambako kunapelekea mambo yote yanayofanyika kwenye huo ulimwengu au upeo wa nafsi iwe ni kama ni mtu mmoja kumbe ni wawili tofauti.
Watu wawili wanaunganishwa kwenye upeo wa nafsi wakati mmoja wao au wote wawili wanapofungua mioyo (isomeke nafsi) yao mmoja kwa mwingine. Unapofungua nafsi yako kwa mtu mwingine unamruhusu huyo mtu aingie huko ndani na aathiri hisia zako, kufikiri kwako na maamuzi yako.
Kwa sababu kuambatana kwa nafsi ni kitu kikubwa sana, lazima tuwe makini sana ni nani tunamfungulia moyo aingie maana sio kila mtu ana nia njema na wewe na wengi wamekuja tu kuyavuruga maisha yako na kuharibu hatima yako.
Daudi alipokuwa anazungumza na Sauli baba yake Yonathani, Yonathani alikuwa hapo pembeni anamsikiliza. Cha ajabu kabla hata Daudi hajatenda neno lolote zuri au baya kwa Yonathani, kupitia tu yale maneno ya Daudi, Yonathani akampenda Daudi na kuufungua moyo wake kwa Daudi. Fikiria nguvu ya maneno ya Daudi kumpa kibali kwa Yonathani. Fikiria Yonathani hata hamjui Daudi, hajui tabia yake, hajui ni mtu wa namna gani lakini kwa kusikiliza tu maneno yake anaufungua moyo wake kumkubali na kumkaribisha nafsini mwake.
Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. (1 SAM. 18:1, 3, 4 SUV).
Katika mistari hiyo hapo juu neno roho lisomeke nafsi kama inavyoonekana kwenye tafsiri zingine za kiingereza.
Katika lugha ya asili ambayo andiko hili liliandikwa yaani kiebrania, neno roho hapo ni neno nephesh linalomaanisha nafsi. Kwa hiyo kwenye hayo maandiko hapo juu kila inapoonekana neno roho isomeke nafsi.
Tukisoma hayo maandiko niliyonukuu hapo juu tunaona Yonathani aliposikia jinsi Daudi alivyokuwa akizungumza na baba yake nafsi ya Yonathani ikaambatana na nafsi ya Daudi.
Hilo neno kuambatana ni neno linaloashria mioyo hiyo miwili au nafsi hizo mbili kuungamanishwa kuwa moja kama vile ambavyo vitambaa viwili vinaweza kuunganishwa kwa kushona na uzi. Mioyo yao au nafsi zao zilipoambatana bibilia inasema Yonathani akampenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe.
Hii inaashiria kuwa Yonathani alifungua nafasi kwenye moyo wake kwa ajili ya Daudi na ukiendelea kufuatilia habari za hawa watu wawili kuna mara nyingi kwa sababu ya muunganiko huu Yonathani alifanya maamuzi ya kumpendelea Daudi hata kinyume na matakwa ya baba yake maana Yonathani alihisi ameungamanishwa na Daudi kuliko alivyoungamanishwa na baba yake. Ndo maana lazima tuwe makini sana nani tunamfungulia mlango wa mioyo yetu.
Tunaweza tukamwona wa muhimu na wa maana kuliko wazazi wetu kama tu vijana, mume au mke wako kama upo kwenye ndoa, nk. Kuwa makini nani unamfungulia mlango wa moyo wako.
Unaweza kumfungulia mtu mlango wa moyo wako ghafla akawa wa muhimu na maana kwako hata kuliko Baba yako wa mbinguni na hutaona shida kumpendeza uliyemfungulia moyo hata kama unajua unamkosea Baba yako wa mbinguni. Hutaona shida kumpendeza huyo mtu ambaye umemfungulia moyo hata kama kwa njia hiyo unawakosea wazazi wako au unasaliti mahusiano yako na mwingine au hata unasaliti ndoa yako. Haya mambo yanatokea moyoni, ni mambo ya ulimwengu wa nafsi.
Ukiendelea kusoma andiko nililonuku hapo juu utaona Yonathani na Daudi wakaahidiana au wakasemeshana maneno ya ahadi ambayo yalimfunga mmoja kwa mwingine. Ukishamfungulia mtu moyo itapelekea tu kuingia katika viapo naye, itakupelekea tu kujifunga kwake kwa maneno. Utajikuta tu unasema hata watu wasipoelewa shauri yao, hata baba asiponielewa shauri yake.
Hata Mungu kama hanielewi atajiju? Hata kama mume wangu au mke wangu hanielewi shauri yake. Tena unaweza kukuta haya maneno yanakamuliwa kwako kijanja alafu unajikuta umeshasema.
Ukishayasema yale maneno yanaifunga nafsi yako sawa na hicho kiapo. Unasema hata baba aniambiaje sikuachi maana tayari unajua ni shida na haitapata kibali kwa baba kwa hiyo bila kujua unajifunga katika maamuzi yasiyo sahihi kwa maneno yako.
Katika andiko lifuatalo japo linazungumzia kumwekea Bwana nadhiri lakini linatusaidia kuiona hii dhana kimaandiko.
Mtu atakapomwekea BWANA nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake. Tena mtu mke atakapomwekea BWANA nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake; (HES. 30:2, 3 SUV).
Mtu anapoweka kiapo chochote iwe kwa Bwana au kwa yeyote mwingine yule anaifunga nafsi yake kwa yule aliyemwekea kiapo iwe ni Bwana au mtu mwingine. Analazimika katika ulimwengu wa nafsi kutimiza uapo ule iwe kwa Mungu au uwe kwa mtu. Na kama uapo ule umetolewa katika hali ya kuvurugwa basi utatimizwa na kuleta matokeo ya kuvurugwa katika maisha ya mhusika.
Nini kinampelekea mtu kufanya hivyo? Nafsi imekamatwa. Nafsi imeambatana na mtu mwingine.
Wakati mwingine unajikuta umesema maneno alafu unasema sikumaanisha nilichosema. Lakini kama umesema ndo tayari umeachilia kitu kwenye ulimwengu wa roho. Ulimwengu wa roho unapandwa mbegu ya maneno yetu na yale maneno yanazaaga matunda yake ambayo baadaye yanaonekana kwenye ulimwengu wa mwili. Usiseme kitu alafu ukasema ulikuwa unatania, hukuwa unamaanisha.
Kama mtu mwenye wazimu atupaye mienge, Na mishale, na mauti; Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, Je! Sikufanya mzaha tu? (MIT. 26:18, 19 SUV).
Usiseme maneno alafu ukaja kusema ulikuwa unafanya mzaha.
Usiseme umepitiwa au kughafilika. Chunga maneno yako. Hilo linakuwa gumu sana wakati nafsi yako inapokuwa imekamatwa.
Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache. Usikiache kinywa chako kuukosesha mwili wako; wala usiseme mbele ya huyo malaika ya kwamba umepitiliwa; kwani Mungu akukasirikie sauti yako, na kuiharibu kazi ya mikono yako? (MHU. 5:2, 6 SUV).
Maneno yanatumika sana kuwafunga watu. Watu wakishafunguliana mioyo yao na nafsi zao zikaambatana wanasemeana maneno ambayo yanawafunga na kuwafanya washindwe kuchomoka. Wakati mwingine kweli unakuwa umesema ili tu kumridhisha mwenzio japo hukumaanisha lakini kwa kuwa umeshasema, iwe umemaanisha au vinginevyo unakamatika.
Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, Ikiwa wewe na mgeni mmepana mikono, Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, (MIT. 6:1, 2 SUV).
Unayaona maneno ya huo mstari hapo juu hasa sehemu ya pili ya mstari wa kwanza, “.. Ikiwa wewe na mgeni mmepeana mikono…” Katika utamaduni wa watu wa eneo ambalo maandiko haya yaliandikwa kupeana mikono ni ishara ya kukubaliana na huyo unayepeana mikono naye. Kupeana mkono maana yake umekubaliana naye. Sasa shida kutokana na huu mstari umepeana mikono na mgeni, mtu humjui, humfahamu, hujui tabia zake wala hufahamu ni mtu wa namna gani na sio tu umepeana naye mikono ila kuna viapo umeweka. Sasa anasema umetegwa na kukamatwa na maneno ya kinywa chako.
Mpenzi ahadi ni deni. Ukishaweka ahadi utajisikia kabisa kudaiwa na yule uliyempa ahadi na lazima ujue akopaye au anayedaiwa ni mtumwa wa yule anayedai. Kwenye ulimwengu wa nafsi yale maneno ambayo umejifunga nayo kwa huyu mtu uliyeahidiana naye yatakufuatilia na yatakufanya kuwa mtumwa sio wa yale maneno bali wa yule uliyemwahidi. Ifungue nafsi yako na mtego huo ifuatavyo:
Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe, Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako. Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia. Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego. (MIT. 6:3-5 SUV).
Tunapewa maelekezo tufanye nini ili kujiokoa kwa sababu kwa maneno yetu tumejitia wenyewe katika mikono ya jirani yetu au huyo mtu ambaye tupo naye kwenye mahusiano yasiyo sahihi. Nenda kwa huyo mtu kanyenyekee alafu mwambie kuwa ulikosea sana ulivyomwambia yale maneno na unaomba akusamehe na unayabatilisha hayo maneno. Ukifanya hivyo utakuwa umejiponya kama paa na mkono wa mwindaji na kama ndege na mkono wa mtega mitego.
Sasa yule ndugu asipokuwa tayari kukuachia hiyo haizuii. Alimradi wewe umefanya hiki ambacho neno linaagiza utakuwa umejiponya.
Daudi alilisema hili hivi:
Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. (ZAB. 124:7 SUV).
Huo uhusiano uliyopo ndani yake ni kama mtego na unajua. Jiokoe. Wengine wanashindwa kutoka kwa kuwa wanatishiwa kuwa watasemwa vibaya na majina yao kuchafuliwa. Toka humo hata kama jina litachafuliwa. Afadhali jina lichafuliwe na upo huru kuliko uendelee kufunikwa funikwa alafu umefungwa. Nakuambia kaka toka, dada toka. Jiokoe.
Kwa hiyo tumeona jinsi ambavyo maneno yanatuingiza katika mtego wa nafsi zetu kufungamanishwa na nafsi ya mtu mwingine. Kama Yonathani asingesikia yale maneno ya Daudi asingeambatana nafsi yake na Daudi.
Ukiwa makini kutoruhusu maneno ya kijinga yakufikie nafsi yako haitafungwa. Unamsikiliza nini mtu ambaye unajua kabisa nia yake sio nzuri na anataka kukushawishi kuingia mahali pagumu. Unatoaje namba yako ya simu alafu kutwa kucha ni maneno tu yanatembea kati yenu. Ndo mnafungana na hayo maneno.
Mwanzoni utasema I miss you ili kumpendeza huyo mtu ghafla utaanza kujisikia kummiss. Utaanza kusema kimzaha I need you, ghafla utaona kweli u need him/her. Acha kucheza na maneno. Maneno yanafunga nafsi ya mtu kwa mwingine na baadaye atakupelekea kufikiri, kuhisi na kuamua visivyo, kwa faida yake yeye na hasara yako wewe.
Hakuna takwimu za kutosha za kutonyesha ni watu wangapi leo wana gonjwa hatari la ukimwi ila nyavu iliyotumika kuwanasa ilikuwa ni simu na maneno ya mesg. Mimba za nje ya ndoa, na nyavu ilikuwa maneno ya kupitia simu.
Ndoa zilizovurugwa na mtuhumiwa ni simu na maneno kwa njia ya mesg. Watu wamefunga nafsi zao na watu wengine kupitia maneno na hayo maneno yamekuwa sababu ya maumivu, vilio, misiba, maombolezo na majuto mengi.
Namna nyingine ambayo imekuwa ikiambatanisha nafsi za watu pamoja ni ngono zembe au kwa maneno mengine ngono nje ya utaratibu wa Kimungu na hili limewagharimu sana watu wengi. Kitu ambacho watu wengi hawajui ni kwamba ngono ni zaidi ya kitendo cha kimwili.
Hiki ni kitendo ambacho kinaunganisha miili, nafsi na roho mbili. Iwe ni uasherati, iwe ni zinaa, iwe ni ulawiti, iwe ni ufiraji, iwe ni usagaji, vitendo hivi vinaunganisha nafsi mbili na hizi nafsi mbili zikishaunganishwa au kuambatanishwa matatizo ya kujinasua yanakuwa makubwa sana maana hata ukitaka kutoka huwezi maana hata uende wapi nafsi ya yule mtu upo nayo maana umeunganishwa nayo.
Ngono inaunganisha miili miwili, nafsi mbili na roho mbili ndo maana Mungu ameweka utaratibu kuwa hili tendo lifanyike kati ya mwanaume na mwanamke waliyooana na sio vinginevyo. Athari za kwenye nafsi za watu za tendo hili la ngono ni mbaya sana hasa inapokuwa nje ya utaratibu wa Kimungu.
Ukiangalia kwenye maandiko utaona kitu cha ajabu sana:
Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. (MWA. 34:1-3 SUV).
Unaweza kuona hapa Shekemu alimtwaa Dinah, akalala naye akambikiri. Alipombikiri moyo wake ukaambatana na moyo wa Dinah. Kila tujihusishapo na ngono tunaambatanisha nafsi zetu na yule tunayeshiriki naye. Ikiwa ndani ya utaratibu wa Kimungu kuambatana huko kunakuwa kuzuri. Ikiwa nje ya utaratibu wa Kimungu kuambatana huko kunakuwa kubaya ambako kuna athari mbaya. Hiyo habari hapo juu ukiendelea kuisoma tunaiona mpaka Dinah alihama kwao akahamia kwa kina Shekemu. Ghafla mapenzi ya binti kwa ndugu zake yakakatika akawa hana mwingine anamwaza ila Shekemu. Alianza kummiss mtu ambaye hata hamjui. Alitamani amwone saa zote akajikuta katoroka nyumbani kwa baba yake kwenda huko kwa Shekemu. Ilanza kwa yeye kwenda kuwaona tu wenyeji wa nchi akarubuniwa akalala naye akabikiriwa, moyo ukakamatwa. Na sio tu wadada mioyo yao inakamatwa kwa njia hiyo mpaka wakaka pia. Kupitia ngono nje ya utaratibu mioyo ya wengi imekamatwa. Watu wamehama makwao, wamehama ndoa zao, wamehama kwa Baba yao wa mbinguni. Kwanini? Nafsi imekamatwa kupitia kulala na usiyepaswa kulala naye. Kama sio Simeoni na Lawi kutumia nguvu za ziada kwenda kumtoa dada yao huko, ilikuwa ishakuwa majanga kwa Dinah. Na Dinah alilewa maneno matamu ya Shekemu ambayo sidhani yalikuwa matamu kiasi hicho lakini kwa sababu ameshavurugwa alikuwa haoni mtego uliyo nyuma ya maneno kama dear, sweetie, darling, honey na kadhalika. Wewe mke wa mtu, mtu sio mumeo hayo maneno matamu yametoka wapi? Umevurugwa au? Alafu ukishajikuta kitandani kwake utajuta au? Hukuiona hiyo hatari mapema? Wewe mume wa mtu hayo maneno matamu kwa asiye mkeo au kutoka kwa asiye mkeo hujayashtukia tu? Haya endelea tu ila matunda itakayo kuzalia!!!!!!
Unapofanya ngono nje ya utaratibu kunakuwa na madhara makubwa sana kwenye nafsi yako. Madhara kwenye hisia, madhara kwenye kufikiri na madhara kwenye maamuzi yako.
Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. (MIT. 6:32, 33 SUV).
Zinaa (soma pia uasherati, ulawiti, ufiraji, usagaji na dhambi zinazofanana na hizo) huleta maangamizo kwenye nafsi ya mtu. Uwezo wake kuhusiana na watu utavurugwa kabisa na maamuzi, kufikiri na hisia nazo zitavurugwa mbaya. Itakusababishia jeraha nafsini, itakusababishia kuvunjiwa heshima, itakusababishia fadheha isiyofutika. Haya mambo yana madhara makubwa iwe umejulikana au hujajulikana. Itadhuru nafsi yako. Itakamatisha nafsi yako na mtu ambaye hukuwa na sababu nafsi yako ikamatane nayo. Itakusababishia maumivu yasiyo ya lazima.
Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani (MIT. 6:26 SUV).
Kwenye andiko hilo hapo juu kahaba, ambaye kwa mujibu wa maandiko sehemu zingine ni mtu yeyote anayefanya mapenzi nje ya utaratibu ambao Mungu ameuweka. Kama haupo kwenye ndoa halali na huyo unayeshiriki naye sio mwenzi wako wa ndoa kwa Mungu unasomeka kahaba. Kwa hiyo basi yeyote yule awe mwanaume au mwanamke anayekushawishi kushiriki hili tendo nje ya utaratibu wa Kimungu anatafuta tu kuinasa nafsi yako yenye thamani na ikishanaswa matatizo ya kihisia, kiuamuzi na kifikra yatafuata. Utakuwa umevurugwa kuliko maelezo. Utajikuta kwenye muunganiko wa nafsi usiyo sahihi ambao hauwezi kukuzalia matunda sahihi maishani mwako.
Moja ya maeneo ambayo yanavurugwa mbaya na hili jambo ni eneo la maamuzi ya kiuchumi.
Ghafla unajikuta unaingizwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate.
Unaanza kufanya maamuzi ambayo sio sahihi ya kiuchumi:
Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali. (MIT. 29:3 SUV).
Ukishikamana na makahaba utatapanya mali.
Kutapanya mali ni kuzitumia kwa kusudi lisilokusudiwa. Ndicho alichofanya mwana mpotevu.
Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. (LK. 15:13, 14 SUV).
Wanandoa ukishaanza kuona huelewi elewi uchumi wa mwenzio, huna maelezo ya kutosha hela zinaenda wapi ujue tayari kuna wa tatu kaingia. Hampo wawili tena kuna na mwingine. Ghafla unapojiingiza kwenye tabia hizi majukumu ya kifedha yanaongezeka na fedha zinaanza kupotea bila maelezo.
Nafsi imekamatwa na maamuzi yanavurugwa.
Kunasuka hapa ni kutubia tu hiyo tabia ili msamaha wa Mungu upite na uponyaji uachiliwe ndani ya nafsi yako ambayo imejeruhiwa. Alafu kwa makusudi achamanisha nafsi yako na ya huyo mtu.
Simeoni na Lawi walienda kumwokoa dada yao kwa upanga. Upanga ni maneno. Tumia maneno yako mwenyewe kuachamanisha nafsi yako na ya huyo mtu. Kwa mfano ukishatubia uzinzi na uasherati wako unaweza kusema maneno kama haya, “Mimi Alfred naiachamanisha nafsi yangu na nafsi ya Rose kwa Jina la Yesu.” Futa maneno ya agano ambayo umeingia kwa damu ya Yesu, jiweke huru na huo mtego kwa Jina la Yesu.
Eneo lingine ambalo linatumika kukamata nafsi za watu au kuambatanisha nafsi ya mmoja na mwingine ni zawadi. Kuwa makini sana na zawadi unazopokea. Mtu humjui anakupa zawadi au usiipokee au ukiipokea ipokee na mikono wazi sio moyo uliyo wazi. Usimpe mtu nafasi ya mume au mke kwa sababu ya zawadi aliyokupa au msaada aliyoutoa. Mshukuru kwa msaada wake yatosha sio uwe mkewe au mumewe kwa sababu ya hiyo zawadi.
Anagalia janga la Gomeri kahaba kupitia zawadi alizokuwa anapewa na wanaume:
Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu. (HOS. 2:5 SUV).
Hawa watu walipewa penzi kwa sababu tu wamempa chakula, maji, nguo, mafuta, marashi. Kusaidiwa na hawa watu kukamwacha afungue moyo wake kwao kumbe nyuma ya ile zawadi kulikuwa na mtego wa kumwingiza katika kumkosea Mungu na mumewe. Kuwa makini na zawadi.
Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humaliza ghadhabu kali. (MIT. 21:14 SUV).
Zawadi ina nguvu ya kutuliza hasira na ukali wako na hata msimamo wako. Kuwa makini na zawadi unazopokea. Ukishaona unasita achana nayo kabisaaaaaa. Nafsi yako inaweza kukamatwa kupitia zawadi ukaona umepata kumbe umepatwa.
Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. (KUT. 23:8 SUV).
Rushwa ni zawadi yoyote inayotolewa ili kubadilisha msimamo wa mtu. Sio tu inabadilisha msimamo ila pia inapofusha macho yako ya ndani na kuathiri kabisa uamuzi wako. Utafanya maamuzi hatari huku huoni hatari iliyopo. Maana ndo ushapigwa changa la macho.
Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki. (KUM. 16:19 SUV).
Ukipokea zawadi itapotoa maamuzi yako, itakufanya upendelee uso wa mtu asiyestahili upendeleo wako, itapofusha macho yako kuuona mtego wa adui ndani ya huo uhusiano na utaufungua moyo wako na kuambatanisha nafsi yako na mtu asiyestahili kuambatana huko.
Mwisho kabisa kuwa makini na ofa za mlo. Sijui lunch, sijui dinner, sijui bites. Hizi ofa za hivi zinakamatisha nafsi ya mtoa ofa na mpokea ofa. Kuwa makini sana nafsi yako isije ikafungiwa usikotaka ifungiwe.
CantonaJoseph’s contacts
Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/
Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.
Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph
LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo…
Management Fortune Baraka Entertainments
Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com
Email fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com
cantona.online254@gmail.com
Contacts +254748836127
Wewe ni wa maana sana!
Copyrights Reserved @2019 FortuneBaraka Entertainments.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.