AFRIKA LEO JIONI -HABARI KAMILI

1.Tangu ulipozuka wiki za karibuni nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ugonjwa wa homa ya nyani (mpox) unaendelea kusambaa kwa kasi. Mkoa wa Kivu Kusini ni miongoni mwa ile inayoshuhudia visa vingi vya maambukizo. Ruth Alonga alikitembelea moja ya vituo vinavyowahudumia waathirika na kuona juhudi za kujaribu kupambana na kudhibiti mpox.

2.Namibia inapanga kuwaua wanyama pori 723, wakiwemo tembo 83, na kusambaza nyama hiyo kwa watu wasio na chakula kutokana na ukame mkubwa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. Nchi hiyo pia inapanga kuwaua viboko 30, nyati 60, swala 50, nyumbu wa buluu 100, na pundamilia 300. Kanda ya Kusini mwa Afrika inakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa. Kulingana na Umoja wa Mataifa #Namibia ilimaliza asilimia 84 ya akiba yake ya chakula mwezi uliopita. Karibu nusu ya wakazi wa Namibia wamo kwenye hatari ya kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula katika miezi ijayo.

3Nchini Kenya Manaibu Gavana wakiongozwa na Naibu Gavana wa Laikipia Reuben Kamuri wamefika mbele ya kamati ya bunge la Seneti wakitaka kurekebisha sheria ya serikali za kaunti ili kubainisha majukumu yao. Wanasema Magavana wengi wanawakabidhi wasaidizi wao wakuu majukumu yao na kuwaacha wao bila kazi.

4.Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan amekutana leo na Rais wa China Xi Jinping mjini Beijing, na kukamilisha siku tatu za mazungumzo yaliolenga kupunguza msuguano kati ya mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa duniani kabla ya uchaguzi wa Marekani wa mwezi Novemba.

  1. Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kusitishwa mapigano katika vita vya Hamas na Israel ili kutoa nafasi ya kufikishwa chanjo ya dhidi ya polio. Gaza ilikuwa imeondokana na ugonjwa wa polio kwa zaidi ya miaka 25.

Wakati huo huo, kiongozi wa upinzani wa Israel, Yair Lapid amekataa madai yaliyotolewa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwamba kiongozi wa Israel hakupokea onyo kuhusu shambulizi la Hamas.

6.Kituo cha sheria na haki za binadamu Tanzania kimezindua ripoti ya haki za binadamu na biashara ya mwaka 2023/2024, ikiwa ni ripoti ya 10 ya shirika hilo kuhusu biashara na haki za binadamu Tanzania bara. Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imeonesha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za kazi, asilimia 51 ya watu wakiripoti kunyimwa fursa ya kufanya kazi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watu wenye ulemavu.

  1. Polisi nchini Tanzania inamshikilia mganga wa kienyeji mkoani Singida kwa jina la Nkamba Kasubi baada ya miili mitatu ya watu kukutwa imezikwa katika eneo lake la shughuli za uganga. Mganga huyo amelitaja eneo jingine lililopo mjini Dodoma, ambako ameizika miili ya watu wengine na jeshi la polisi lilikwenda na kuifukua miili 6 iliyokuwa imezikwa kwa kukalishwa, na kufanya jumla ya idadi ya maiti kufikia 10. Msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania David Misime anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi ili kuendelea kufichua vitendo hivyo.
  2. Serikali ya Tanzania imewatoa hofu wananchi kwamba hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa kupata maambukizi ya Mpox. Kulingana na gazeti la Mwananchi la nchini humo, taarifa iliyotolewa na naibu waziri wa afya Dk. Godwin Mollel imewataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi Afrika.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment