Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu popote ulipo.
Namshukuru sana MUNGU Baba wa mbinguni kwa neema yake ya ajabu katika KRISTO YESU juu yangu, naamini na kwako pia ni neema ya MUNGU pia ndio imefanya kazi.
Tunaelekea mwisho wa mwaka hivyo nakuletea ujumbe huu kwa kusudi la MUNGU.
Kwangu Mimi mwezi wa kumi na mbili ni mwezi wa kumshukuru MUNGU wangu.
Ni hakika kabisa kwamba majira yataendelea kuwepo, usiku na vitaendelea kutokea, mwaka hadi mwaka mwingine vitaendelea kuwepo maana ni ratiba ya MUNGU ya kudumu hadi siku ya mwisho.
Mwanzo 8:22 “Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.”
Kwa maana hivyo kila mwanadamu ana mwisho wake duniani lakini miaka mipya, miezi mipya na siku mpya zitaendelea kuja.
Kuna watu waliishi katika nyakati za zamani kisha wakaondoka, Kuna watu waliishi nyakati zilizopita kisha wakaondoka, Kuna watu tunaishi nyakati hizi na sisi nyakati zetu zikiisha tutaondoka duniani na Kuna watu wataishi nyakati zijazo nao nyakati zao zikiisha wataondoka.
Nini nataka kusema?
Tunaishi kwa kusudi la MUNGU.
Sasa unapopata neema ya kumaliza mwaka na ukapata neema ya kuingia mwaka mwingine basi ni kwa sababu ya MUNGU tu.
Sasa nimekueleza hayo ili utafakari na umtukuze MUNGU katika KRISTO YESU kwa neema aliyokupa.
Sasa kwa ufunuo nimejulishwa mambo haya Saba(7) muhimu ya kufanya unapojiandaa kuingia mwaka mwingine.
- Mshukuru MUNGU.
Unapomaliza mwaka na unapojiandaa kuingia mwaka mwingine ni vizuri Sana kuwa na muda wa kumshukuru MUNGU.
Mshukuru MUNGU kwa maombi na kwa sadaka ya shukrani.
Zaburi 50:22-23 ” Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau MUNGU, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya. Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa MUNGU.”
Kumbe hatutakiwi kumsahau MUNGU, tena mtu anayetoa sadaka za shukrani ndiye anayemtukuza MUNGU.
Ndugu unapojiandaa kuingia mwaka mwingine usimsahau MUNGU kamwe bali mshukuru MUNGU kwa maombi na sadaka ya shukrani.
Hata kama Kanisani kwenu hamna utaratibu wa kumshukuru MUNGU kwa sadaka ya shukrani kipindi hiki Cha mwisho wa mwaka, wewe peleka sadaka yako ya shukrani kule ambako ROHO wa MUNGU atakuelekeza au atakupa amani kupeleka, hata kama uko katika mazingira ambayo uko mbali na Kanisani Safi la KRISTO wewe itume sadaka yako ya shukrani kwa watumishi sahihi waaminifu wa Bwana YESU.
Ni Jambo la maana Sana kumtolea MUNGU sadaka ya shukrani kwa neema yake kwako mwaka huu.
Tuwe watu wa shukrani mbele za MUNGU maana Kuna faida kubwa.
Ukisoma Walawi 22:29 Biblia inasema kwamba sadaka ya shukrani huleta kukubaliwa zaidi.
Kuna watu kumi walitendewa muujiza na MUNGU ila aliyekuja kumshukuru MUNGU ni mtu mmoja tu Kati ya hao 10, ona sasa ambacho Bwana YESU KRISTO alikisema
Luka 17:17-19 “YESU akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa MUNGU utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.”
Usisababishe MUNGU akakushangaa kwa sababu hauna shukrani.
Hivyo kuwa watu wa shukrani ni Jambo la maana Sana mbele za MUNGU.
Shukrani kwa MUNGU ni Jambo la kiroho na lenye maana muhimu Sana.
- Omba juu ya mwaka mpya unaouendea ili majira hayo ya mwaka huo mpya, hayo majira kulingana na mbinguni yatimie kwako.
Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.”
Kwa kila Jambo Kuna majira yake, hivyo hata mwaka mpya unaouendea, huo mwaka umebeba vitu vyake kulingana na mbingu kwa ajili yako.
Na kumbuka Kuna majira ya MUNGU kwako, Kuna majira ya kibinadamu kwako na Kuna majira yako lakini shetani anaweza kupitisha vitu vyake na ukaharibikiwa wewe katika majira ambayo hukutakiwa kuharibikiwa lolote.
Muhimu kwako omba mbele za MUNGU katika KRISTO YESU ili vitu vya ki MUNGU vilivyoambatanishwa na MUNGU katika mwaka huo vitimie, vikitimia vya MUNGU ujue vya shetani havitapata nafasi.
Inawezekana mwaka unaouingia ni mwaka wako wa kufunga ndoa, kupata kazi, kupata mtoto, kupata cheo, kuinuliwa kihuduma n.k lakini nguvu za giza usipokuwa mtu wa kuisikiliza sauti ya MUNGU watakuzuia kupata haki yako katika majira yako sahihi kabisa, ndugu omba kwa MUNGU ili baraka za ki MUNGU ziliambatanishwa na mwaka huo, hizo baraka zitimie kwako.
- Omba MUNGU aseme na wewe juu ya mwaka mpya unaouendea.
Ngoja nikupe maandiko matatu hapa ya kukusaidia.
Ukisoma Isaya 42:9 MUNGU anasema “Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.”
Kumbe mambo mapya kabla hayajatokea MUNGU hutujulisha, hivyo omba katika jina la YESU KRISTO ili ujulishwe juu ya mambo ya mwaka mpya unaouendea.
Ngoja nikupe ushuhuda kidogo.
Mimi Cantona Joseph Kuna mwaka mmoja katika mkesha wa kuingia mwaka mpya, nikiwa nimefumba macho nikiomba niliona maono ya baadhi ya mambo yatakayotokea mwaka mpya ninaouendea na ikaja ikawa vile vile.
Hivyo ni vyema Sana kuwa na maombi ya kumuuliza ROHO MTAKATIFU juu ya mwaka mwingine tunaouendea, hivyo kwa neema ya MUNGU unaweza ukajulishwa baadhi ya vitu muhimu ambavyo MUNGU atapenda kukujulisha.
Inawezekana una mashaka mengi Sana juu ya afya yako ukidhani miezi ijao utakuwa haupo duniani, MUNGU anaweza kukujulisha kwa ndoto au maono ukajiona ukifanya jukumu fulani ambalo linahitaji muda mrefu ujao, hapo tu unakuwa umejulishwa juu ya wakati ujao kwamba utakuwepo.
Inawezekana unatamani Sana kufunga ndoa, unaweza ukashangaa kwenye ulimwengu wa roho ukajulishwa kwamba ipo siku utafunga ndoa, hiyo tu ni taarifa juu ya wakati ujao kwamba utakuwepo.
Kumbuka kazi mojawapo ya ROHO MTAKATIFU ni kutujulisha juu ya mambo yajayo.
Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”
Hivyo omba MUNGU ili ujulishwe juu ya mambo ya mwaka mpya unaouendea.
Na sio lazima MUNGU akujulishe wewe, anaweza hata kuwajulisha wengine na hao wakakuambia, hapo MUNGU anakuwa amekujulisha pia.
Kuna njia nyingi MUNGU anaweza kusema na wewe baadhi ya njia ambazo MUNGU hutumia kusema na wateule wake ni hizi; ndoto, maono, Malaika, Neno la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU, Sauti ya MUNGU ya moja kwa moja, kupitia kusoma Biblia, kupitia watumishi wake, kupitia mazingira na kupitia mafundisho ya Neno lake.
Kumbuka Biblia inasema kwamba MUNGU hatafanya Jambo lolote bila kuwaambia watumishi wake.
Amosi 3:7 “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”
Watumishi wa MUNGU ni watu wote waliompokea YESU KRISTO Kama Bwana na Mwokozi wao.
Hivyo omba MUNGU aseme na wewe juu ya mambo ya mwaka mpya unaouendea.
- Omba MUNGU kwamba baraka zilizo ndani ya utoaji ziambatane na wewe.
Tangu mwaka huu uanze Kuna sadaka mbalimbali ulimtolea MUNGU.
Sasa ni kawaida ya MUNGU kuzikumbuka sadaka za wateule wake wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu ili tu awatimizie mahitaji yao.
Zaburi 20:3-4 “Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.”
Naamini unazo sadaka za kukumbukwa mbele za MUNGU ulizotoa mwaka huu, basi tambua neno hili kwamba watumishi wanaweza wakasahau, wanadamu wanaweza wakasahau, hata wewe unaweza ukasahau lakini MUNGU hasahau kamwe, hivyo omba MUNGU ili baraka zilizo ndani ya utoaji wako ziambatane na wewe na itakuwa katika jina la YESU KRISTO.
Kumbuka tu pia kwamba sadaka za kukumbukwa mbele za MUNGU hata akutendee mahitaji yako ni sadaka tu zile ambazo ulizitoa kwake kwa hiari na kwa moyo wa upendo, hukutoa ili watu wakutambue wewe na ulitoa kwa Imani huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU.
Naamini unayo sadaka ya kukumbukwa mbele za MUNGU, omba baraka zilizo ndani ya utoaji ziambatane na wewe katika majira ya mwaka mpya unaouendea.
MUNGU sio kwamba amesahau bali ameagiza tuombe, pasipo maombi unaweza usirithi baraka hata kama ni haki yako, hivyo omba ndugu.
Isaya 43:26 “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.”
- Omba MUNGU akupe kuishi maisha marefu.
Ni wazi kwamba Kuna watu walianza mwaka huu kwa furaha lakini pia ni mwaka huu huu ndio ulikuwa mwaka wa mwisho wao kuishi duniani maana waliondoka duniani.
Na hata mwaka mpya tunaouendea Kuna watu ni mwaka wao wa kuondoka duniani.
Kwanini nasema hivyo?
Ni kwa sababu kuna watu huondoka duniani kwa kusudi la MUNGU Kuna watu pia huondoka duniani kwa hila za shetani na Kuna watu pia huondoka duniani kwa hila za wanadamu.
Hivyo kifo sahihi ni kile tu Cha kusudi la MUNGU.
Lakini pia ni muhimu kujua kwamba ukikaa vizuri na YESU KRISTO hakika MUNGU ataitimiza hesabu ya siku zako.
Ni ahadi ya MUNGU wewe mteule wa KRISTO uishi miaka mingi duniani.
Kutoka 23:26 “Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.”
Unaweza ukaingia mwaka mpya kwa furaha na kumbe kuna kalenda za kichawi kukuondoa duniani kupitia magonjwa ya ajabu ajabu tu n.k
Ndugu omba kwa MUNGU ili hesabu ya siku zako itimizwe na MUNGU hivyo rariba za kipepo na kalenda za kichawi hazotafanya kazi kwako.
- Ifunge kila mipango ya kishetani dhidi yako katika mwaka mpya unaouendea. Mathayo 16:19 “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
Umepewa mamlaka katika KRISTO YESU ya kufunga kazi za giza huku ukifungulia ushindi wako, huo ufunguo unao wewe hivyo utumie leo kwa maombi ya kuzifunga kila mipango za kishetani katika ndoa yako, familia yako, uchumi wako, kazi yako, uzao wako, kibali chako na katika kila kitu chako.
Mathayo 18:18 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”
7.Omba MUNGU akukutanishe na watu waliobeba kusudi lake.
Kuna watu ni baraka kwako, Kuna watu ni darasa kwako na Kuna watu wamebeba vifungo vya giza kwa ajili yako.
Hivyo katika mwaka mpya unaouendea omba MUNGU akukutanishe na watu walio baraka kwako.
Inawezekana unatamani kuingia katika ndoa, unaweza ukaomba na MUNGU mwakani akakutanisha na mwenzi wako sahihi hata mkafunga ndoa, mtu huyo ni baraka.
Mtu akikuelekeza kwenda kwa mganga wa kienyeji ujue mtu huyo ni laana kwako.
Mtu akikushawishi kutenda dhambi ujue mtu huyo amebeba vifungo vya giza kwa ajili yako.
Hivyo omba kwa MUNGU katika jina la YESU KRISTO ili katika mwaka mpya unaouendea ukutane na watu waliobeba kusudi lake la MUNGU kwa ajili yako.
Inawezekana unahitaji kazi, Kuna mtu mwakani anaweza kukuajiri au kukuelekeza kazi ilipo na ukapata kazi, mtu huyo ni baraka kwako.
Kuna mtu akikaa kwenye nafasi yake wewe unapata VISA na kusafiri, unapata kazi, unapata ongezeko n.k
Mtumishi yeyote anayekuombea kwa MUNGU, mtu huyo ni baraka kwako.
Omba MUNGU akukutanishe na watu walio baraka kwako.
Inawezekana hujanielewa vyema ngoja nikupe maandiko haya mawili.
Miaka yote Labani alikuwa na uchumi wa kawaida Sana hadi Yakobo alipotokea kwenye maisha yake, ni mwaka mmoja hatimaye ulifika wa Yakobo kwenda kwa Labani na ndio uchumi mkubwa ukafika kwa Labani.
Mwanzo 30:27 “Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako.”
Potifa alikuwa na maisha yake ya kawaida lakini kutokea kwa Yusufu katika maisha ya Potifa kulibadilisha uchumi wa Potifa.
Mwanzo 39:3-5 ” Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.”
Ndugu, omba MUNGU akukutanishe na watu walio baraka kwako kulingana na mahitaji yako.
Ndugu, zingatia vipengele vyote 7 katika maombi na vitendo huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO na hakika utamuona MUNGU wa miujiza.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
CantonaJoseph’s contacts
Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/
Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.
Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph
LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo…
Management Fortune Baraka Entertainments
Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com
Email fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com cantona.online254@gmail.com
Contacts +254748836127
Wewe ni wa maana sana!
Copyrights Reserved @2019 FortuneBaraka Entertainments.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.