Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na : Cantona Joseph|RFA

Maelezo kuhusu taarifa
Mwanzoni mwa msimu mashabiki wa Liverpool waligundua jambo kuhusu Liverpool. Lilihusu tabia ya kufunga magoli katika dakika za mwisho za mchezo.
Federico Chiesa alishangalia bao lake la dakika 88 dhidi ya Bournemouth siku ya ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu England. Kabla ya Mohamed Salah kufunga bao katika dakika za mwisho na kuweka matokeo 3:2.
Kijana Rio Ngumoha alifunga bao la ushindi katika dakika ya 100 huko St James’ Park huku Newcastle ikishindwa 3-2.
Wiki moja baadaye Dominik Szoboszlai alifunga bao katika dakika ya 83 dhidi ya Arsenal, na wikendi iliyofuata Salah alifunga penalti dakika ya 95 dhidi ya Burnley – ushindi wa 1-0.
Baada ya michezo mitano, Liverpool walikuwa na pointi 15 kwenye ubao. Reds walikuwa kileleni mwa ligi wakipewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao.
Walipata bao la ushindi dakika ya 92 dhidi ya Atletico Madrid katika Ligi ya Mabingwa – mambo yalikuwa mazuri kwa timu ya Arne Slot.
Lakini miezi mitano baadaye, tabia ya Reds ya kufunga mabao ya ushindi mwishoni imegeuka na sasa wao ndio wanaojikuta wakiruhusu bao mwishoni mwa mchezo.
Sasa wanaruhusu mabao

Katika michezo mitatu ya ligi ya Liverpool iliyofuata baada ya kuanza vizuri msimu, walikutana na Crystal Palace, Chelsea na Manchester United na kuruhusu mabao katika dakika ya 84 au zaidi.
Na Erling Haaland alipopiga penalti yake ya dakika za majeruhi huko Anfield Jumapili, ilikuwa mara ya nne kwa Liverpool kukubali kushindwa katika dakika za majeruhi katika ligi msimu huu. Hakuna timu katika msimu mmoja wa Ligi Kuu ambayo imewahi kuruhusu zaidi ya hapo.
Ni timu tatu pekee (Burnley, Leeds na Newcastle) zimeruhusu mabao mengi zaidi katika dakika 10 za mwisho pamoja na muda wa majeruhi wa michezo kuliko Liverpool (10) msimu huu na hakuna timu iliyopoteza pointi zaidi ya Liverpool (nane) kutokana na mabao hayo.
Pointi hizo nane zingewafanya wawe sawa na Aston Villa katika nafasi ya tatu, lakini badala yake Liverpool wanajikuta katika nafasi ya sita na pointi nne nyuma ya Chelsea, ambao wako katika nafasi ya tano.
Msimu uliopita
Mara kwa mara msimu huu, Virgil van Dijk ametumia neno “uzembe” kuelezea mapambano ya Liverpool.
Baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Burnley mwezi Januari, nahodha huyo wa Liverpool alisema: “Baada ya dakika 60, tulianza kuwa wazembe na si mara ya kwanza. Tunapaswa kushughulikia hilo.”
Siku chache baadaye huko Milan, nukuu hiyo ilitolewa na beki wa kushoto Milos Kerkez, ambaye aliambia BBC Sport kwamba anakubaliana na tathmini ya Van Dijk.
“Baada ya dakika 60-70 huwa tunapoteza umakini na kupoteza nidhamu ya kimbinu. Sijui, tunachoka, sina uhakika ni nini, lakini nakubaliana na hilo.”
Mojawapo ya sababu kubwa zilizomfanya Slot kuletwa baada ya Jurgen Klopp ni uwezo wake wa kuvutia wa kuwaweka wachezaji wake katika hali nzuri.
Mholanzi huyo alichagua mtindo wa mazoezi ambayo sio makali sana kuliko yale mazoezi ambayo wachezaji walikuwa wameyazoea.
Msimu ulikuwa mrefu lakini haikuwa na kashkashi, Liverpool ya Slot ilicheza bila kutumia nguvu nyingi kuliko Liverpool ya Klopp.
Mambo haya yote, yaliwafanya wasiwe na majeraha msimu uliopita, na kusababisha Liverpool kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu.
Vipi kuhusu msimu huu?

Liverpool wanatumia mbinu ya kuliandama goli la timu pinzani, mbinu ambayo imewaacha katika hatari ya mashambulizi ya ghafla.
Kutokana na majeraha ya sasa, kuna wasiwasi kwamba mbinu za mazoezi na mbinu za uwanjani zilizoelezwa haziendani na msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita, huku wachezaji wa Liverpool wakishuka kiwango katika dakika za mwisho za michezo.
Kati ya kutaka kuwatuliza mashabiki, kuhakikisha wachezaji wake wanaendelea kuwa fiti, kutaka kufunga mapema na kubaki imara katika safu ya ulinzi, kocha wa Liverpool anapata tabu kuweka mambo sawa.
Na hapo ndipo Liverpool ilipo sasa. Timu inayojua nyufa ziko wapi lakini haiwezi kuzificha, seuzi kuzirekebisha.
Katika historia ya Ligi Kuu, hakuna timu iliyowahi kufunga mabao mengi zaidi ya Liverpool katika dakika za majeruhi. Wana mabao 47, mbele ya Arsenal (36) na Manchester United (34).
Liverpool wamekuwa maarufu kwa matukio ya kufurahisha katika historia yao. Lakini sasa, wanatengeneza historia isiyo sahihi.
Kama Slot alivyosema Jumapili: “Sasa imekuwa kawaida kuruhusu bao katika muda wa ziada.”
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.