Rais wa Colombia aamuru kusitishwa kwa ushirikiano wa kijasusi na Marekani

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na : Cantona Joseph|RFA

.

Rais wa Colombia Gustavo Petro ameamuru kusitishwa kwa ushirikiano wa kijasusi na Marekani kama njia ya kupinga kampeni ya Marekani ya kufanya mashambulizi dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya katika visiwa vya Caribbean na mashariki mwa Pasifiki.

“Mapigano dhidi ya dawa za kulevya lazima yaendane na haki za binadamu za watu wa Caribbean,” Petrol alisema katika chapisho la X, akirejelea historia ya nchi hizo mbili za kushirikiana dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.

Petro, mpiganaji wa zamani wa mrengo wa kushoto wa vita vya guerilla, aliongeza kuwa hatua hiyo itaendelea kutekelezwa hadi pale Marekani itakapositisha mashambulizi dhidi ya meli katika visiwa vya Caribbean.

Marekani imetuma vikosi vyake, katika eneo hilo tangu mwishoni mwa mwezi Agosti kama sehemu ya operesheni ambayo imewauwa watu wasiopungua 76 wanaodaiwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya katika takriban mashambulizi 19 eneo la Caribbean na mashariki mwa Pasifiki.

Pia imetuma meli nyingine nne za kivita, ikiwa ni pamoja na USS Gerald R Ford inayosemekana kuwa kubwa zaidi ya kijeshi ulimwenguni.

Rais wa Venezuela Nicolás Maduro amedai kuwa kutumwa kwa wanajeshi wa Marekani ni kisingizio cha kumuondoa madarakani.

Taliban yaamuru wanawake kuvaa burka ili kuingia kwenye vituo vya afya, shirika la MSF linasema

.

Mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan imewaamuru wagonjwa wa kike, walezi na wafanyakazi kuvaa burka – vazi kamili la Kiislamu – ili kuingia katika vituo vya afya vya umma katika mji wa magharibi wa Herat, shirika la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) linasema.

MSF ilisema vikwazo hivyo vilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 5 Novemba.

“Vikwazo hivi vinatatiza zaidi maisha ya wanawake na kuwazuia kupata huduma za afya,” Sarah Chateau, meneja wa programu wa shirika hilo nchini Afghanistan, aliiambia BBC. Alisema hata wale “wanaohitaji huduma ya haraka ya matibabu” wameathirika.

Msemaji wa serikali ya Taliban amekanusha madai ya MSF. Ripoti zinasema vizuizi vimelegezwa kwa kiasi tangu kuanza kuangaziwa kwa suala hilo.

Jeshi la Venezuela lajiandaa kujibu iwapo Marekani itaishambulia

.

Venezuela inapeleka silaha, ikiwa ni pamoja na vifaa vya miaka mingi vilivyotengenezwa na Urusi, na inajipanga kwa vita vya kuvizia au kusababisha machafuko ikiwa Marekani itaishambulia kwenye anga au ardhini, kulingana na vyanzo vyenye ufahamu wa juhudi zinazoendelea na nyaraka za upangaji zilizoonekana na Reuters.

Mbinu hiyo inatumika kutokana na ukosefu wa wafanyakazi na vifaa katika nchi hiyo ya Amerika Kusini.

Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza uwezekano wa operesheni za ardhini nchini Venezuela, akisema “ndio itakayofuata” kufuatia mashambulizi kadhaa dhidi ya meli zinazodaiwa kusafirisha dawa za kulevya katika visiwa vya Caribbean na kuwasili kwa jeshi kubwa la Marekani katika eneo hilo.

Baadaye alikanusha kwamba alikuwa anafikiria kutekeleza mashambulizi ndani ya Venezuela.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, aliye madarakani tangu 2013, anasema Trump anataka kumuondoa madarakani na kwamba raia wa Venezuela na wanajeshi watapinga jaribio lolote kama hilo.

Wanajeshi wa Marekani wawasili Caribbean

.

Kikosi cha wanamaji cha Marekani kilichojikita katika meli kubwa zaidi ya kivita duniani, USS Gerald R Ford, kimewasili katika visiwa vya Caribbean, Jeshi la Wanamaji la Marekani limethibitisha.

Kuwasili kwa wanajeshi hao ambako ni agizo la Rais Donald Trump mwezi uliopita, kunafanyika huku mashambulizi yikiendelea dhidi ya meli za dawa za kulevya na mvutano wa nchi hiyo na Venezuela ukiendelea kutokota.

Marekani hadi kufikia sasa imetekeleza takriban mashambulizi 19 dhidi ya boti katika visiwa vya Caribbean na mashariki mwa Pasifiki, na kusababisha vifo vya takriban watu 76.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na maafisa wengine wa Venezuela wameishutumu Marekani kwa “kujitengenezea” mgogoro na kutaka kuiangusha serikali ya mrengo wa kushoto ya kisoshalisti.

Hatua za kuwasili kwa meli ya kivita pia kunawadia huku kukiwa na mvutano kati ya utawala wa Trump na serikali ya Colombia ya Rais Gustavo Petro, ambaye Trump amemtaja kama “jambazi na mtu mbaya”.

Petro siku ya Jumanne aliamuru vikosi vya usalama vya umma vya nchi yake kusimamisha ushirikiano wa kijasusi na mashirika ya Marekani hadi mashambulio ya meli katika visiwa vya Caribbean yatakapokoma.

Aliandika kwenye mtandao wa X kwamba mapambano dhidi ya madawa ya kulevya “lazima yawe chini ya haki za binadamu za watu wa Caribbean”.

Mapema mwezi wa Novemba, Trump alipuuza uvumi kwamba alikuwa akipanga kupindua serikali ya Venezuela au kuanzisha vita.

Katika mahojiano na CBS – mshirika wa BBC wa habari wa Marekani – Trump alisema kwamba “kila meli moja unayoona imelipuliwa inaua watu 25,000 kwa madawa ya kulevya na kuharibu familia kote nchini.”

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment