Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na : Cantona Joseph|RFA

Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wameweka hadharani barua pepe mpya za Jeffrey Epstein ambazo zinamtaja Rais wa Marekani Donald Trump.
Barua pepe moja ni kati ya Jeffrey Epstein na mshirika wake Ghislaine Maxwell.
Katika taarifa yao, chama cha Democrat kinaeleza katika barua pepe walizotoa leo kwamba moja inaonyesha mawasiliano binafsi kati ya Ghislaine Maxwell, na Jeffrey Epstein mwaka 2011, ambapo Epstein anasema Trump “alikaa saa nyingi nyumbani kwangu” na mwathirika wa biashara ya ngono, na kisha kumtaja Trump kama “mbwa ambaye hajabweka.”
Katika barua pepe nyingine kati ya Epstein na mwandishi Michael Wolff mwaka 2019, chama hicho kinasema Epstein anasema Trump “alijua kuhusu wasichana hao kwani alimtaka Ghislaine kuachana na mambo hayo.”
Hayati Jeffrey Epstein alikuwa tajiri wa Marekani aliyepatikana na hatia ya uhalifu wa ngono dhidi ya watoto. Alikutwa amekufa kwenye chumba cha gereza 2019 akisubiri kesi nyingine kuhusu biashara ya ngono.
Alikuwa na ukaribu na watu mashuhuri, wakiwemo wanasiasa, wasomi, na wafanyabiashara, na alitumia utajiri na ushawishi wake kuwanyanyasa kingono na kuwasafirisha wasichana wengi wa umri mdogo kwa msaada wa mshirika wake wa muda mrefu, Ghislaine Maxwell.
Democratic wanasema kuwa bado wanakagua hati 23,000 katika mafaili ya kesi ya Epstein.
Trump alikuwa rafiki wa Epstein katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, na hajawahi kushtakiwa kwa makosa kuhusiana na ukaribu wake na Epstein.
Trump amekuwa akikana makosa yoyote kuhusiana na Epstein, akisema tuhuma dhidi yake ni “uongo” ulioratibiwa na chama cha Democratic.
Sita wafariki katika mkanyagano wakati wa usaili wa ajira za jeshi

Takriban watu sita wamefariki dunia kufuatia mkanyagano wakati wa zoezi la kuwasaili vijana kwa ajili ya ajira za jeshi katika uwanja wa El-Wak katika mji mkuu wa Ghana, Accra. Wengine kadhaa wamejeruhiwa na kwa sasa wanapokea matibabu katika Hospitali ya Jeshi.
Kulingana na Jeshi la Ghana, mkanyagano huo ulitokea kabla ya kuanza kwa zoezi la kusajili watu Jumatano asubuhi.
Msemaji wa jeshi Kapteni Veronica Adzo Arhin katika taarifa yake Jumatano alisema mkanyagano huo ulichochewa na idadi kubwa ambayo haikutarajiwa ya waombaji ambao walikiuka itifaki za usalama na kukimbilia katika milango kabla ya uchunguzi wa kuwaruhusu kupita.
Maelfu ya watu wanaotarajiwa kuajiriwa walikusanyika katika uwanja wa El-Wak ili kuandikishwa katika Jeshi la Ghana. Ghana ina kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana cha takriban 13%, na mazoezi kama haya ya kuajiri yana sifa ya kuwa na umati mkubwa wa watu na mara nyingi husababisha matukio ya fujo.
Jeshi la Ghana lililazimika kuongeza muda wa kuajiri kwa wiki moja ili kushughulikia waombaji zaidi, kwani wengine walikuwa na shida katika mchakato wa kutuma maombi.
Utulivu umerejeshwa, na zoezi la kuwasajili waajiriwa wa jeshi linaendelea.
Bunge la Marekani lapanga kupiga kura kumaliza kufungwa kwa shughuli za serikali

Bajeti ambayo itamaliza kufungwa kwa muda mrefu zaidi kwa shughuli za serikali nchini Marekani inaelekea kupigwa kwenye Baraza la Wawakilishi siku ya Jumatano.
Siku ya 42 ya mzozo huo, wawakilishi wanarudi Washington kuamua kama wataidhinisha mpango wa Seneti wa fedha ambazo zitafadhili mashirika ya shirikisho kwa miezi miwili.
Uongozi wa Republican ulionyesha imani kuwa mpango huo wa matumizi utapita katika baraza la chini la Congress, licha ya wingi wao finyu. Lakini viongozi wakuu wa chama cha Democratic wameapa kupinga mpango huo.
Rais Donald Trump amedokeza kuwa atatia saini mpango huo kuwa sheria, Jumanne katika hafla ya Siku ya Veterani huko Arlington, Virginia.
Ufungaji wa shughuli za serikali ulioanza tarehe 1 Oktoba, umewaacha wafanyakazi wa shirikisho milioni bila malipo, kukosa ufadhili wa chakula kwa Wamarekani wa kipato cha chini, na kuchelewesha safari za ndege.
Walowezi wa Israel wachoma moto ghala la bidhaa huko Palestina

Makumi ya walowezi wa Israel wamefanya mashambulizi ya kuteketeza ghala la bidhaa huko Palestina, katika Kijiji cha cha Bedouin, na mashamba kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu siku ya Jumanne.
Wapalestina kadhaa walijeruhiwa. Matukio hayo yalikuwa ya hivi punde zaidi katika msururu wa ghasia za walowezi.
Haya yanajiri baada ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu kusema idadi ya mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na walowezi mwezi uliopita ni ya juu zaidi tangu ilipoanza kukusanya takwimu takriban miaka 20 iliyopita.
Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi wapatao 700,000 tangu ilipoukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya 1967. – ni ardhi ambayo Wapalestina wanataka, pamoja na Gaza, kuwa taifa lao la baadaye. Takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi kando yao.
Makazi hayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa.
Video za Jumanne zinaonyesha makumi ya wanaume waliofunika nyuso zao kwenye mlima mashariki mwa Tulkarm, na kisha ghala la Wapalestina huko Beit Lid lilishambuliwa, na lori kuchomwa moto.
Mahema yanaweza kuonekana yakiwaka moto katika kijiji cha Bedouin cha Deir Sharaf, na sauti ya wanawake wakipiga kelele.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema kuwa wanajeshi walikwenda kwenye eneo la tukio “kutawanya ghasia na kuwakamata raia kadhaa wa Israel.” Iliongeza kuwa askari walishambuliwa na walowezi waliokuwa wamekusanyika karibu na gari lao kuharibiwa.
Polisi wa Israel walisema kuwa washukiwa wanne walikamatwa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inasema kuwa Oktoba ilishuhudia zaidi ya mashambulizi 260 ya walowezi wa Israel na kusababisha hasara, uharibifu wa mali au vyote viwili – wastani wa matukio manane kwa siku.
Ukungu wavisaidia vikosi vya Urusi kusonga mbele katika mji wa Ukraine wa Pokrovsk

Ukungu mnene umewawezesha wanajeshi wa Urusi kusonga mbele zaidi katika mji muhimu wa kimkakati wa Pokrovsk mashariki mwa Ukraine.
Kikosi cha Ukraine kinasema hali ya hewa, haswa ukungu mnene, imeifanya Moscow kuzidisha azma yake ya kuongeza idadi ya wanajeshi katika jiji hilo lililoharibiwa na kuvizingira vikosi vya Ukraine.
Vikosi vya Urusi vimetumia zaidi ya mwaka mmoja kujaribu kuuteka mji huo. Jeshi la Ukraine linasema huenda sasa kuna wanajeshi 300-500 wa Urusi huko na Rais Voloydymyr Zelensky anasema hali bado ni ngumu.
Wakati huo huo, mkuu wa jeshi Oleksandr Syrskyi anasema hali katika mstari wa mbele wa mapigano katika eneo la kusini mashariki mwa Zaporizhzhia “imezidi kuwa mbaya.”
Video imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha wanajeshi wa Urusi kwenye barabara wakiwa kwenye magari na pikipiki za kiraia.
BBC imethibitisha mahali ambapo video hiyo ilirekodiwa ni kusini mwa mji huo kwenye barabara kuu ya Selidove-Pokrovsk.
Kwa siku kadhaa ukungu umezuia ndege kuona, anasema rubani wa droni.
Wiki moja iliyopita, Zelensky alikadiria kuwa kuna wanajeshi 300 wa Urusi wakipigana huko Pokrovsk. Video hiyo inaonyesha kwamba idadi hiyo huenda imeongezeka.
Ndugu wawili washtakiwa kwa mauaji ya mwanamuziki wa Afrika Kusini AKA

Ndugu wawili wameshtakiwa kwa mauaji ya rapa wa Afrika Kusini, Kiernan Forbes, maarufu “AKA,” baada ya kurejeshwa kutoka nchi jirani ya Eswatini.
Siyabonga na Malusi Ndimande walirudishwa baada ya kushindikana kwa jaribio la muda mrefu la kisheria la kuzuia kurejeshwa Afrika Kusini.
Forbes, msanii wa muziki wa kufoka foka, aliuawa nje ya mkahawa katika jiji la pwani la Durban mwaka 2023 pamoja na rafiki yake wa karibu, mpishi maarufu Tebello “Tibz” Motsoane.
Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu vya mauaji duniani.
Ndugu hao pia wameshtakiwa kwa mauaji ya Motsoane na watafikishwa mahakamani pamoja na washtakiwa wengine watano ambao tayari wako rumande kesi itakapoanza. Pia wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua na kumiliki bunduki kinyume cha sheria.
Waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Durban siku ya Jumanne chini ya ulinzi mkali wa polisi, huku mikono na miguu yao vikiwa vimefungwa pingu.
Wakati wa mauaji yake, Forbes alikuwa Durban kutumbuiza wakati wa sherehe ya siku yake ya kuzaliwa.
Polisi walitaja shambulio hilo dhidi ya watu hao wawili kuwa ni shambulio lililoratibiwa. Ingawa inaaminika Forbes ndiye aliyekusudiwa, huku bado haijafahamika ya kufanya mauaji hayo.
Ndimande watarejea tena mahakamani Novemba 25 kwa ajili ya kusikilizwa kwa dhamana.
Israel imeharibu zaidi ya majengo 1,500 Gaza tangu kusitishwa mapigano

Israel imeharibu zaidi ya majengo 1,500 katika maeneo ya Gaza ambayo yako chini ya udhibiti wa jeshi lake tangu kusitishwa kwa mapigano na Hamas kuanza tarehe 10 Oktoba, picha za satelaiti zilizokaguliwa na BBC zinathibitisha.
Picha mpya – za hivi punde zaidi zilipigwa tarehe 8 Novemba – zinaonyesha majengo yote katika vitongoji vinavyodhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) yamedondoshwa ndani ya mwezi mmoja, kwa njia ya ubomoaji.
Idadi halisi ya majengo yaliyoharibiwa inaweza kuwa kubwa zaidi, kwani BBC imeshindwa kupata baadhi ya picha za setilaiti katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya tathimini.
Baadhi ya wataalam wanasema ubomoaji huo unaweza kukiuka masharti ya usitishaji mapigano yanayosimamiwa na Marekani, Misri, Qatar na Uturuki. Lakini msemaji wa IDF aliiambia BBC, ilikuwa ikitenda “ndani ya makubaliano ya kusitisha mapigano.”
Mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa Gaza – unasema “operesheni zote za kijeshi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya angani na mizinga, zitasitishwa.”
Uchunguzi wa picha za satelaiti wa BBC umegundua kuwa uharibifu wa majengo huko Gaza unaofanywa na jeshi la Israel umekuwa ukiendelea kwa kiwango kikubwa.
BBC ilitumia picha zilizopigwa kabla na baada ya kusitishwa kwa mapigano ili kuangazia mabadiliko, ambayo yanaweza kuonyesha uharibifu, kisha tukahesabu majengo yaliyoharibiwa.
Trump asema ana haki ya kuishtaki BBC

Rais wa Marekani Donald Trump amesema ana “haki ya” kuishtaki BBC kuhusu jinsi hotuba yake ilivyohaririwa katika makala ya Panorama.
Akizungumza na Fox News, amesema hotuba yake ya Januari 6, 2021 “ilikatwa” na jinsi ilivyowasilishwa “iliwapotosha” watazamaji.
Ni mara ya kwanza kwa Trump kuzungumza hadharani kuhusu suala hilo tangu mawakili wake waiandikie BBC na kusema kwamba ataishitaki BBC kwa fidia ya dola bilioni 1 (£759m), ama shirika hilo liondoe makala hiyo, liombe msamaha na kumfidia.
Msemaji wa BBC amesema: “Tunapitia barua hiyo na tutajibu moja kwa moja kwa wakati unaofaa.”
Mwenyekiti wa BBC Samir Shah hapo awali aliomba msamaha kwa “kosa katika uhariri.”
Trump amesema: “Kwa kweli walibadilisha hotuba yangu ya Januari 6, ambayo ilikuwa hotuba nzuri, ilikuwa hotuba iliyopoa, na waliifanya isikike kama hotuba kali.
Waandamanaji waingia katika ukumbi wa COP30 nchini Brazil

Waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yanayosema “misitu yetu haiuzwi” walivuka vizuizi vya usalama wakati mazungumzo ya hali ya hewa ya COP30 yakiendelea Jumanne usiku huko Belém, Brazili.
Waandishi wa habari wa BBC waliwaona wafanyakazi wa usalama wa Umoja wa Mataifa wakikimbia nyuma ya safu ya wanajeshi wa Brazil wakipaza sauti kwa wajumbe kuwataka kuondoka mara moja kwenye ukumbi huo.
Umoja wa Mataifa uliambia BBC kwamba tukio hilo lilisababisha majeraha madogo kwa wafanyakazi wawili wa usalama, pamoja na uharibifu mdogo katika ukumbi huo.
Video katika mitandao ya kijamii zilionyesha waandamanaji ambao walionekana kutoka katika makundi ya kiasili na wengine wakipeperusha bendera zenye nembo ya vuguvugu la vijana wa mrengo wa kushoto wa Brazil liitwalo Juntos.
Programu mbili maarufu za wapenzi wa jinsia moja zaondolewa kwenye Apple China

Apple imethibitisha kuwa imeondoa programu mbili maarufu za uchumba za wapenzi wa jinsia moja nchini China – Blued na Finka – kutoka eneo la kupakua programu nchini humo kufuatia agizo kutoka kwa mamlaka.
“Tunafuata sheria za nchi ambazo tunafanya kazi. Kulingana na agizo kutoka kwa Utawala wa Mtandao wa China, tumeondoa programu hizi mbili kutoka eneo la kununua huduma za mtandao la China pekee,” msemaji wa Apple alisema.
Hatua hiyo imeibua wasiwasi miongoni mwa jumuiya ya LGBT nchini humo.
BBC imewasiliana na ubalozi wa China mjini Washington na makampuni yaliyo nyuma ya programu zote mbili kwa maoni.
Blued ni mojawapo ya programu zinazotumiwa sana na wapenzi wa jinsia moja nchini China, ikiwa na makumi ya mamilioni ya wanaopakua programu hiyo.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.