Uchaguzi Tanzania 2025 ulikiuka maadili ya kidemokrasia – AU

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na : Cantona Joseph|RFA

Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika umeelezea kusikitishwa na vurugu zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali zilizokumba Uchaguzi Mkuu wa Tanzania.

Serikali ya Israel yatambua mwili wa mwanafunzi wa Tanzania aliyekuwa mateka Gaza

Joshua Mollel aliwasili Israel mwezi mmoja tu kabla ya shambulio la Hamas
Maelezo ya picha,Joshua Mollel aliwasili Israel mwezi mmoja tu kabla ya shambulio la Hamas

Serikali ya Israel imethibitisha kuwa mwili wa marehemu Joshua Luito Mollel, mwanafunzi kutoka Tanzania aliyechukuliwa mateka katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, umetambuliwa rasmi.

Utambulisho huo umefanywa na Kituo cha Kitaifa cha Tiba ya Uchunguzi wa Vifo kwa ushirikiano na Polisi ya Israel na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF).

Familia ya marehemu imejulishwa rasmi, na mwili wake umerejeshwa nchini Israel.

Serikali ya Israel imetoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mulal na kwa familia zote za mateka waliopoteza maisha.

Serikali na Jeshi la Ulinzi la Israel wamesisitiza kuwa wanaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa miili ya mateka wote inarejeshwa kwa maziko yenye heshima.

Vilevile, serikali imeitaka Hamas kutekeleza makubaliano na kurejesha miili ya mateka waliobaki.

Wamesema hawatapumzika hadi kila mmoja arejeshwe nyumbani.

Maandalizi ya kongamano la COP 30 yaendelea mjini Belem, Brazil

Viongozi wa dunia waanza kuwasili Brazil
Maelezo ya picha,Viongozi wa dunia waanza kuwasili Brazil

Viongozi wa dunia wameanza kuwasili mjini Belém, Brazili, kwa mkutano wao wa kila mwaka wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Baadhi ya viongozi wametemmbela msitu wa Amazon wakisubiri kikao cha awali kabla ya kongamano kuu kuanza Jumatatu ijayo.

COP30 inafanyika miaka 10 baada ya makubaliano ya hali ya hewa ya Paris, ambapo nchi ziliahidi kujaribu kuzuia kupanda kwa joto duniani hadi 1.5C.

Hata hivyo, mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) anasema “kupindua” lengo la 1.5C sasa ni jambo lisiloepukika na Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi wasiotarajiwa kuhudhuria.

COP30 ni nini na inawakilisha nini?

COP30 ni mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa.

COP inasimama kwa “Mkutano wa Vyama”. “Vyama” inarejelea karibu nchi 200 ambazo zilitia saini makubaliano ya asili ya hali ya hewa ya Umoja wa mataifa UN mnamo 1992.

Kongamano la COP30 linaanza lini?

COP30 inaanza rasmi Jumatatu Novemba 10 hadi Ijumaa Novemba 21.

Mara nyingi muda wa kikao huongezeka kwa sababu ya mazungumzo ya dakika za mwisho ili kupata makubaliano.

g

Kwa nini COP30 inafanyika nchini Brazil?

Taifa mwenyeji huchaguliwa na nchi zinazoshiriki baada ya uteuzi kutoka eneo la mwenyeji. Ni mara ya kwanza mkutano huo unafanyika nchini Brazil.

Uchaguzi wa Belém, katika msitu wa Amazon, umesababisha changamoto kubwa.

Baadhi ya wajumbe wametatizika kupata malazi ya bei nafuu, na kusababisha wasiwasi kwamba mataifa maskini yanaweza kutomudu gharama.

Uamuzi wa kusafisha sehemu ya msitu wa Amazon ili kujenga barabara kwa ajili ya mkutano huo pia umeonekana kuwa na utata.

Brazili pia imeendelea kutoa leseni mpya kwa mafuta na gesi ambayo, pamoja na makaa ya mawe, ni nishati ya mafuta, sababu kuu ya ongezeko la joto duniani.

Nini kitajadiliwa katika COP30?

1.Nishati ya Kisukuku

Katika COP28 (2023), nchi zilikubaliana kuachana na nishati za kisukuku, lakini makubaliano hayo hayakuimarishwa katika COP29 (2024) kama ilivyotarajiwa.

2. Fedha

COP29 ilishuhudia nchi tajiri zikiahidi kutoa dola bilioni 300 kila mwaka hadi 2035 kusaidia mataifa maskini kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni kiwango kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.

Pia walipendekeza kuongeza hadi dola trilioni 1.3, lakini mpango huo hauna maelezo ya utekelezaji.

3. Nishati Mbadala

COP28 ilikubaliana kuongeza mara tatu uzalishaji wa nishati mbadala kama upepo na jua ifikapo 2030, lakini Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) linasema dunia bado haiko kwenye mwendo wa kufikia lengo hilo.

4. Mazao ya Asili

Inawezekana COP30 ikazindua mfuko mpya wa “Tropical Forests Forever Facility” kusaidia kuhifadhi misitu ya kitropiki.

Rais wa Marekani Donald Trump mapema mwaka huu aliuita mabadiliko ya tabia nchi ”udanganyifu mkubwa kufanya duniani”na kuahidi kuongeza uzalishaji wa mafuta na gesi.

Juhudi nyingine za kimataifa kama makubaliano ya plastiki na kupunguza hewa chafu kutoka usafirishaji zimeshindwa kufikia muafaka.

Afrika Kusini kuchunguza jinsi raia wake 17 walivyoishia kupigania Ukraine

hh

Serikali ya Afrika Kusini imesema Alhamisi ya Novemba 6, 2025 kwamba imepokea simu za dharura kutoka kwa raia wake 17 waliokuwa wamejiunga na vikosi vya wapiganaji wa kulipwa katika mzozo wa Urusi-Ukraine na kwamba inafanya kazi kuwatafutia njia ya kurudishwa nyumbani.Haya ni kwa mujibu wa shirika la Reuters.

Tume ya taifa ilisema kuwa wanaume hao walishawishiwa kushiriki mapigano kwa kudanganywa na mikataba ya ajira yenye faida kubwa.

Wote wako kati ya umri wa miaka 20 na 39 na wamesalia katika eneo la Donbas lililoharibiwa na vita nchini Ukraine.

“Rais Cyril Ramaphosa ametoa agizo la kufanya uchunguzi kuhusu hali zilizosababisha kuajiriwa kwa vijana hawa katika shughuli hizi za wapiganaji wa kulipwa,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo haikufafanua upande gani wa mzozo wananchi hao wa Afrika Kusini walikuwa wanapigania.

Kulingana na sheria za Afrika Kusini, ni kinyume cha sheria kwa raia kutoa msaada wa kijeshi kwa serikali za kigeni au kushiriki katika majeshi ya serikali za kigeni isipokuwa iwapo wameidhinishwa na serikali ya Afrika Kusini, iliongeza taarifa hiyo.

Mnamo Agosti, serikali ya Afrika Kusini iliwatahadharisha vijana kuhusu ofa za kazi za uongo nchini Urusi, ambazo zilienea kwenye mitandao ya kijamii, baada ya ripoti kuwa baadhi ya wanawake wa Afrika Kusini walidanganywa kushiriki katika utengenezaji wa ndege zisizo na rubani.

Ukraine yaishambulia Volgograd ya Urusi kwa kutumia ndege zisizo na rubani, mtu mmoja auawa

Volodymyr Zelensky wa Ukraine alitembelea wanajeshi karibu na Pokrovsk wiki hii
Maelezo ya picha,Volodymyr Zelensky wa Ukraine alitembelea wanajeshi karibu na Pokrovsk wiki hii

Ukraine imeshambulia Urusi kwa angalau ndege zisizo na rubani 75 Alhamisi ya Novemba 6,2025 ikisababisha moto katika eneo la viwandani mjini Volgograd kusini mwa nchi hiyo, na kuua angalau mtu mmoja na kusitisha ndege kadhaa kote nchini, wanasema maafisa wa Urusi.

Kwa miezi kadhaa, Ukraine imekuwa ikishambulia viwanda vya mafuta, maghala na mabomba ya mafuta ya Urusi katika juhudi za kudhoofisha uchumi wa Urusi huku nguvu za Urusi zikiendelea kusonga mashariki mwa Ukraine.

Gavana wa Volgograd, Andrei Bocharov, alisema kuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 48 aliuwawa na mabaki ya mlipuko na kwamba moto ulizuka katika eneo la viwandani katika wilaya ya Krasnoarmeysk ya jiji hilo, ambalo hapo awali lilijulikana kama Stalingrad.

Wilaya hiyo ina kiwanda kikuu cha mafuta cha Lukoil, ambacho kimekuwa kikilengwa mara kwa mara na Ukraine.

Mnamo 2024, kiwanda cha Volgograd kilichakata tani milioni 13.7 za mafuta, sawa na 5.1% ya jumla ya mafuta yaliyokatwa katika viwanda vya Urusi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema ndege zisizo na rubani 75 za Ukraine ziliangushwa usiku kucha, ikiwa ni pamoja na 49 katika mkoa wa Volgograd.

Vyombo vya habari vya Urusi viliripoti kuwa viwanja 13 vya ndege kote Urusi vilisimamisha safari za ndege kutokana na shambulio hilo la ndege zisizo na rubani.Hya ni kwa mujibu wa shirika la Reuters.

Urusi ilisema Jumatano kuwa majeshi yake yanapanuka kaskazini ndani ya Pokrovsk katika jitihada za kudhibiti jiji lote la Ukraine.

Jeshi la Urusi linasema sasa lina udhibiti wa zaidi ya asilimia 19% ya Ukraine, sawa na kilomita za mraba 116,000 (maili za mraba 44,800).

Kulingana na ramani zinazounga mkono Ukraine zilizotolewa na Reuters, Urusi imechukua zaidi ya kilomita za mraba 3,400 za ardhi ya Ukraine hadi sasa mwaka huu ramani hizo hizo zinaonyesha kwamba mwishoni mwa 2023, Urusi ilidhibiti asilimia 18% ya Ukraine.

Wakenya wahakikishwa usalama wao Tanzania

Hali ilivyokuwa siku ya maandamano ya vurugu Tanzania
Maelezo ya picha,Hali ilivyokuwa siku ya maandamano ya vurugu Tanzania

Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania umewaomba Wakenya waliopo nchini humo kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa mujibu wa sheria bila hofu, ukibainisha kuwa hakuna tukio lolotea dhidi ya raia wa Kenya liliripotiwa hadi sasa, ilisema katika taarifa.

“Tunawahimiza Wakenya wote kuwa watulivu na kuzingatia sheria za ndani, na kuripoti mara moja matukio yoyote yatakayohatarisha usalama wao kwa ubalozi wetu jijini Dar es Salaam,” iliongeza taarifa hiyo.

Wakenya pia wameshauriwa kuwasiliana na Ubalozi huo kupitia nambari ya simu +255 22 2668285/6.

Ubalozi huo pia umeahidi kutoa taarifa za mara kwa mara kupitia njia rasmi za mawasiliano na mitandao ya jamii, ili kuhakikisha Wakenya wanapata taarifa sahihi kuhusu usalama na ustawi wao nchini Tanzania.

Haya yanajiri baada ya ripoti zinazoashiria kuwa Wakenya wanaoishi Tanzania wanahofia usalama wao kusambaa mitandaoni.

Mamlaka nchini Tanzania zilisema raia kuwa raia wa mataifa jirani (bila kutaja ni wa taifa gani) walichagia vurugu zilizokumba nchini hiyo wakati wa uchaguzi.

Kundi la kutetea haki za binadamu, likiongozwa na Vocal Africa, pia liliitaka serikali ya Kenya kufuatilia hali ya Wakenya nchini Tanzania baada ya ghasia za uchaguzi.

Hii ni baada ya Mkenya John Okoth Ogutu, mwalimu wa Sky Schools Dar es Salaam, kupigwa risasi na kuawa Oktoba 29, 2025.

Familia ilisema mwili wake ulipelekwa katika makafani ya Hospitali ya Mwananyamala lakini haujapatikana.

Mbunge wa Embakasi Mashariki nchini Kenya, Babu Owino, ameandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, kuelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za mauaji ya Ogutu.

Babu Owino anaitaka Wizara hiyo kuwasilisha taarifa bungeni ikieleza hatua zinazochukuliwa kuwalinda raia wa Kenya wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi, hasa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Marekani yapanga kupunguza safari za ndege ikiwa kufungwa kwa serikali kutaendelea

Waziri wa Uchukuzi wa Marekani
Maelezo ya picha,Waziri wa Uchukuzi wa Marekani

Waziri wa uchukuzi wa Marekani, Sean Duffy, amewaonya kuwa, kuanzia asubuhi ya Ijumaa, kutakuwa na upungufu wa asilimia 10% katika uwezo wa usafirishaji wa anga katika viwanja 40 vikuu vya ndege endapo kufungwa kwa serikali kutaendelea.

Kupunguzwa kwa safari za ndege kutakuwa kwa awamu,kuanzia 4% ya safari za ndani siku ya Ijumaa, kisha kupanda hadi 5% Jumamosi na 6% Jumapili, kabla ya kufikia 10% kamili wiki ijayo, Reuters iliripoti baada ya tangazo hilo, ikinukuu vyanzo vinne ambavyo havikutajwa.

Kufutwa kwa safari za ndege kutaathiri kati ya safari za ndege 3,500 na 4,000 kwa siku.

Uamuzi huu umetokana na ripoti zinazotolewa na wadhibiti wa trafiki ya anga, alisema Bryan Bedford, mkuu wa Utawala wa Serikali wa Anga (FAA), wakati wa mkutano na Duffy Jumatano.

“Hili ni jambo lisilo la kawaida, kama vile kufungwa kwa serikali ni jambo lisilo la kawaida, na kama vile ukweli kwamba wadhibiti wetu hawajalipwa kwa mwezi mzima ni jambo lisilo la kawaida pia,” alisema Bedford.

Wakati huu wa kufungwa kwa serikali, ambao ni mrefu zaidi katika historia ya Marekani, wadhibiti wameendelea kufanya kazi bila malipo, jambo lililosababisha baadhi yao kudai likizo za ugonjwa au kuchukua kazi za ziada.

Mara tu baada ya serikali kufungwa, viwanja vya ndege vilianza kuathirika.

Baadhi vililazimika kusimamisha ndege kwa saa kadhaa baada ya wadhibiti kudai likizo ya ugonjwa, huku wengine wakitegemea wadhibiti kutoka viwanja vingine.

Nick Daniels, rais wa chama cha wafanyakazi kinachowakilisha zaidi ya wafanyakazi 20,000 wa anga, alielezea hali hiyo kwa maneno makali: “Wadhibiti wa trafiki ya anga wanatuma ujumbe wa maandishi wakisema, ‘Sina hata pesa za kununua mafuta ya gari ili kuja kazini.’”

Duffy alionya mwanzoni mwa wiki kuwa kusitishwa kwa safari za ndege kunaweza kuanza, kwani nusu ya viwanja vikuu 30 vya ndege nchini vina uhaba wa wafanyakazi.

Aidha, aliashiria kuwa kuchukua kazi za ziada na wadhibiti wa trafiki ya anga wakati wa kufungwa kwa serikali kunaleta hatari, na aliwatishia kuwafukuza waliokosa kufika kazini.

“Wadhibiti wanapaswa kufanya uamuzi: je, ninaenda kazini bila mshahara na bila kuweka chakula mezani, au naendesha Uber, DoorDash, au kusubiri wageni mezani?” alisema Duffy katika kipindi cha ABC Jumapili.

Uchaguzi Tanzania 2025 ulikiuka maadili ya kidemokrasia – waangalizi wa AU

GG

Uchaguzi wa Tanzania haukikidhi kanuni na viwango vya demokrasia, waangalizi wa Umoja wa Afrika walisema katika taarifa siku ya Jumatano.

Waangalizi wa AU walishuhudia kanuni za uchaguzi zikikiukwa katika vituo kadhaa vya kupigia kura, ambapo baadhi ya wapiga kura walipatikana na zaidi ya karatasi moja ya kupigia kura.

Mawakala wa vyama vya kisiasa hawakuwepo katika baadhi ya vituo vilivyokumbwa na dosari hizo.

Wakati wa kuhesabu kura, waangalizi wengine waliamriwa kuondoka vituoni, taarifa hiyo iliongeza. Haya yanajiri siku kadhaa baada ya Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pia kutoa taarifa sawia na hiyo kuhusu uchaguzi Mkuu wa Tanzania.

Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Ujumbe wa Waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) uliongeza kuwa: “Tanzania inapaswa kutoa kipaumbele kwa mageuzi yanayopendekezwa na upinzani ili kushughulikia changamoto za zilizoibuka kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita.”Marekebisho haya ni pamoja na:

  • Uwajibikaji na uwazi wa taasisi za serikali;
  • Ujumuishwaji na kuheshimu maoni tofauti ya wadau wa kisiasa na wananchi;
  • Ushiriki wa wananchi katika michakato ya kisiasa na ya uchaguzi; na
  • Ulinzi na heshima kwa haki za binadamu katika ngazi zote za utawala.

Ujumbe huo wa AU pia imeeleza kutamaushwa na vifo vilivyotokana na maandamano ya baada ya uchaguzi, na kutoa rambirambi kwa familia zote zilizoondokewa na wapendwa wao.

Umetoa wito kwa mamlaka husika kuchunguza matukio hayo kwa uwazi, na kuhakikisha haki inatendeka kwa wote walioathirika.

Hapo jana Jumanne Novemba tarehe 4, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Nchini Tanzania (THBUB) imesema itaanzisha uchunguzi wa kina kufuatia maandamano yalioshuhudiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, na kusababisha uharibifu wa mali na vifo vya raia.

Rais Samia Suluhu alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa Tarehe 29 Oktoba 2025, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA ambaye kiongozi wake Tundu Lussi anazuiliwa jela kwa tuhuma za uhaini, kilipinga matokeo hayo na kudai kuwa uchaguzi huo kama kejeli kwa demokrasia.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment