ECOWAS na EU wakemea tishio la Trump kuhusu madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya wakristo nchini Nigeria

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na: Cantona Joseph|RFA

gg

ECOWAS NA EU WAKIKITANA NA TRUMP, KUHUSU TUHUMA ZA MAUAJI YA KIMBARI YA KIKRISTO NCHINI NIGERIA.

Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imekanusha kama ya uongo na yenye hatari madai kwamba makundi yenye misimamo mikali katika eneo hilo yanawalenga watu wa dini fulani au yanafanya mauaji ya kimbari dhidi ya waumini wa wakristo.

Taarifa hii inatolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia kuchukua hatua za kijeshi nchini Nigeria kutokana na kile alichokiita “mauaji ya halaiki ya Wakristo.”

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, ECOWAS ilisema madai kama hayo yanaweza kuongeza hali ya kutokuwa na usalama na kudhoofisha mshikamano wa kijamii katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na vurugu za kigaidi.

“Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) inapenda kuwakumbusha washirika na jumuiya ya kimataifa kuhusu ongezeko la kiwango cha vurugu ambazo makundi ya kigaidi ya aina mbalimbali yamekuwa yakifanya katika baadhi ya nchi za eneo hili, zikiwemo Nigeria,” taarifa hiyo ilisema.

ECOWAS ilisisitiza kwamba mashambulizi ya kigaidi katika Afrika Magharibi yanalenga raia wasio na hatia bila kujali dini, kabila, au jinsia.

Iliitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono nchi wanachama katika mapambano dhidi ya ugaidi “unaolenga jamii zote.”

Umoja wa Ulaya (EU) pia ulitoa maoni kuhusu sakata hilo, ukisema umezingatia kauli zilizotolewa na serikali ya Marekani.

Msemaji wa mambo ya nje wa EU, Anouar El Anouni, alionesha mshikamano na waathirika wote wa vurugu nchini Nigeria, wakiwemo walioathirika na mashambulizi ya hivi karibuni katika maeneo ya kusini na kaskazini mashariki.

“Tunatambua kuna sababu nyingi zinazopelekea vurugu nchini Nigeria. Dini ni moja tu kati ya hizo na hata hivyo, ni katika baadhi ya matukio pekee,” alisema Bwana El Anouni.

Alisisitiza dhamira ya EU ya kuhakikisha umoja na kuishi kwa amani miongoni mwa wananchi wa Nigeria, “bila kujali tofauti za kijiografia, kikabila, kisiasa au kidini.”

Onyo la Rais Trump lililochapishwa katika jukwaa lake la kijamii Truth Social limezua mjadala mpana na hisia kali.

Wachambuzi wanasema kauli zake zinagusa nyufa nyeti za kidini na kisiasa nchini Nigeria.

Nigeria imegawanyika karibu sawa kati ya kaskazini yenye Waislamu wengi na kusini yenye Wakristo wengi.

Wakati makundi yenye misimamo mikali kama Boko Haram na ISWAP (Islamic State West Africa Province) yameshambulia makanisa na jamii za Kikristo, pia yamewaua mamia ya Waislamu wanaopinga itikadi zao.

Wachambuzi wanaonya kwamba kuelezea vurugu hizi kama “mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo” kunarahisisha kupita kiasi mchanganyiko wa sababu mbalimbali ikiwemo umasikini, migogoro ya ardhi, na mvutano wa kikabila vinavyochangia ukosefu wa usalama nchini Nigeria na eneo zima la Sahel.

Wito wa ECOWAS na EU huenda unalenga kuhimiza utulivu na kushirikiana kimataifa katika kushughulikia mizizi ya vurugu, hasa katika Afrika Magharibi na eneo la Sahel.

ICC yaonya ukatili unaoshuhudiwa El Fasher unaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu

Ni mahakama ya kudumu ya kimataifa ambayo ina uwezo wa kuwashtaki watu binafsi na viongozi kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Maelezo ya picha,Ni mahakama ya kudumu ya kimataifa ambayo ina uwezo wa kuwashtaki watu binafsi na viongozi kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeonya kwamba ukatili unaoripotiwa mjini El-Fasher unaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo imesema ina wasiwasi mkubwa kutokana na taarifa za mauaji ya halaiki, ubakaji, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu nchini Sudan.

Wakati huo huo, serikali ya kijeshi ya Sudan inaendelea na mazungumzo kuhusu masuala ya usalama, kufuatia kutekwa kwa mji wa El-Fasher — ngome ya mwisho ya jeshi katika eneo la Darfur — na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).

Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, kiongozi wa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, alikiri kwamba baadhi ya wanajeshi wake walihusika katika makosa na ameahidi kufanyia uchunguzi suala hilo.

Hemeti, ambaye alijipatia utajiri wake kupitia biashara ya ngamia na dhahabu, sasa ameibuka kama mtu mwenye ushawishi mkubwa katika ulingo wa siasa za Sudan, huku wanamgambo wake wakidhibiti takriban nusu ya nchi.

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva ameonya kwamba ukatili unaofanyika Al-Fasher unafikia kiwango cha mauaji ya kimbari, na amesema hali inayofanana na njaa kali inaendelea kutokana na hatua ya RSF kuzuilia misaada ya kibinadamu madai ambayo RSF wamekanusha.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kwamba “mji wa Fasher na maeneo yanayouzunguka huko Kaskazini mwa Darfur ndio kitovu cha mateso, njaa, ghasia, na uhamishaji wa watu.”

Amesisitiza pia kuwa kuna “taarifa endelevu za ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.”

Chanzo cha serikali ya Sudan kimeiambia shirika la habari la AFP kwamba mamlaka zinazingatia pendekezo la Marekani kuhusu kusitisha mapigano.

Washington, kupitia kundi la Quad, imekuwa ikisukuma juhudi za kusitisha vita na kuweka ramani ya amani ya kumaliza mzozo huo.

Kikundi cha Majadiliano ya Usalama cha Quadrilateral (Quad) ni jukwaa la kimkakati kati ya Marekani, India, Japani, na Australia, lililoanzishwa mwaka 2007.

Watu wasiopungua 40 nchini Sudan wameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga mazishi yaliyokuwa yakifanyika nje ya mji wa el-Obeid, ambao unashikiliwa na jeshi, katika jimbo la Kordofan Kaskazini, maafisa na wanaharakati wamesema.

Wamelilaumu jeshi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kwa shambulio hilo lililotokea Jumatatu katika kijiji cha al-Luweib, wakati waombolezaji walipokuwa wamekusanyika ndani ya hema. RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo.

Mwisho wa mwezi Oktoba, kikosi cha RSF, ambacho kimekuwa katika vita na jeshi la Sudan kwa zaidi ya miaka miwili, kiliteka mji wa kimkakati wa Fasher baada ya mzingiro wa miezi 18.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) yatangaza wajumbe wa viti maalum vya wanawake

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)
Maelezo ya picha,Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza majina ya wajumbe wa viti maalum vya wanawake watakaokuwemo katika Baraza la Wawakilishi, kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Thabit Aidarous, uteuzi huo umefanyika katika kikao maalum cha tume hiyo kilichofanyika tarehe 4 Novemba.

Jumla ya wajumbe 20 wa viti maalum wameteuliwa, wakiwemo wajumbe 16 kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na wajumbe 4 kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, kwa uwiano unaoakisi uwakilishi wa vyama hivyo katika Baraza la Wawakilishi.

Tume imesema uteuzi huo umefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 67(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na kifungu cha 55(3) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018.

Haya yanajiri, baada ya Chama cha upinzani, ACT-Wazalendo, kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais visiwani Zanzibar.

Mgombea wa urais wa chama hicho Outhman Masoud alieleza kutoridhishwa kwake.

“Wananchi wa wameibiwa sauti yao… suluhu pekee ya kupata haki ni uchaguzi mpya,”

Maandamano Tanzania: Chadema ‘yatangaza siku saba ya maombolezo’

gg

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza ”siku saba za maombolezo ya kitaifa,” kuanzia leo tarehe 5 Novemba kuwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha katika ghasia zilizokumba uchaguzi mkuu.

”Tumechukua hatua hii kutokana na matukio ya kusikitisha yaliyosababisha vifo, majeruhi na baadhi ya wananchi kupotea,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho Brenda Rupia.

Akitangaza uamuzi huo, katika mtandao wa kijamii wa Instagram , Bi. Brenda Rupia, amesema hatua hiyo ni njia ya kuonyesha heshima kwa wale waliopoteza maisha katika maandamano yaliyofanyika Tanzania tangu siku ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba.

Aidha, chama hicho kimeeleza kuwa bendera zote za CHADEMA zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni, kwa siku zote saba za maombolezo.

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan bado haijatoa idadi kamili ya watu waliofariki dunia katika maandamano hayo yaliyokumbwa na ghasia.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia, idadi ya waliouawa inakadiriwa kufikia watu 500, ingawa CHADEMA imedai kuwa idadi hiyo huenda ni ya juu zaidi.

Kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, bado anazuiliwa tangu mwezi Aprili kwa tuhuma za uhaini.

Kabla ya kukamatwa kwake, aliwataka wafuasi wa chama hicho wasishiriki uchaguzi wa Oktoba 29 hadi pale mageuzi ya sheria ya uchaguzi yatakapofanyika.

Baada ya kuapishwa kwake, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaonya wale aliowaita “wanaoendeleza maandamano haramu”, akidai kuwa baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakizua ghasia katika maeneo kadhaa ya Tanzania ni raia wa nchi jirani, ingawa hakubainisha ni wa taifa gani.

Vile vile, Rais Samia alikemea vikali matendo hayo akisema “kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania.

“Sasa tuchague lenye manufaa kwetu kwani usalama wa taifa lolote hulindwa kwa wote, kwa nguvu zote na kwa gharama zozote.”alisema Rais Samia.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment