Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Israel imefanya mashambulizi ya anga huko Gaza, kujibu kile maafisa wa Israel wanachosema ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yanayosimamiwa na Marekani.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz ameishutumu Hamas kwa kuwashambulia wanajeshi wa Israel huko Gaza siku ya Jumanne, na kukiuka masharti ya kurejesha miili ya mateka waliofariki dunia.
Lakini kundi hilo la wapiganaji wa Palestina linasema, halikuhusika na shambulio hilo na kusisitiza kuwa limejitolea kuendelea na makubaliano ya kusitisha mapigano.
Takriban Wapalestina 33 waliuawa katika mfululizo wa mashambulizi ya Israel, kulingana na Shirika la Ulinzi wa Raia wa Gaza linaoendeshwa na Hamas na maafisa wa hospitali.
Mashambulizi hayo yalipiga nyumba na shule katika Jiji la Gaza, Beit Lahia, al-Bureij, Nuseirat na Khan Younis.
Licha ya mashambulizi hayo, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema anaamini usitishaji mapigano unaendelea.
Taarifa fupi iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumanne jioni ilisema aliamuru “mashambulizi ya makali” lakini hakutaja sababu.
Katz alisema Hamas imevuka “mstari mwekundu” kwa kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Israel huko Gaza siku ya Jumanne.
“Hamas italipa kwa kuwashambulia wanajeshi na kwa kukiuka makubaliano ya kuwarudisha mateka,” alionya.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba wanajeshi katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah walishambuliwa kwa makombora na walenga shabaha siku ya Jumanne mchana, huku vyombo vya habari vya Palestina vikiripoti mashambulizi ya makombora ya Israel katika eneo hilo.
Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu leo

Ni uchaguzi wa saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na unafanyika wakati vyama vikuu vya upinzani vikiwa na misimamo tofauti kuhusu ushiriki wao katika mchakato huu.
Watu milioni 37.6 wanatarajiwa kupiga kura leo

Watu milioni 37.6 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema jumla ya Watanzania milioni 37.6 wameandikishwa kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu.
Kati yao, milioni 36.65 wapo Tanzania Bara na takribani 996,000 wapo Zanzibar.

Wanawake ni asilimia 50.34 ya wapiga kura wote, sawa na watu milioni 18.95, huku wanaume wakiwa 49.66%. Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacob Mwambegele, amesema kati ya wapiga kura hao, milioni 7.6 ni wapya, ikionesha ongezeko la zaidi ya asilimia 26 kutoka uchaguzi wa mwaka 2020.
Tume imesema idadi hiyo kubwa ya wapiga kura ni kielelezo cha mwamko wa kisiasa unaoongezeka nchini, hasa miongoni mwa vijana.
- Spika wa Bunge la Tanzania apiga kura Mbeya
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Ubunge Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Tulia Ackson, leo tarehe 29 Oktoba, 2025 amejitokeza kupiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Tambukareli mkoni Mbeya.
Mshirikishe mwenzako, Spika wa Bunge la Tanzania apiga kura Mbeya - Rais Mwinyi apiga kura Zanzibar
Rais Dkt. Hussein Mwinyi amepiga kura yake katika kituo cha Kariakoo jimbo la Kwahani.
Zaidi ya wapiga kura 700,000 waliojiandikisha wanatarajiwa kupiga kura zao katika uchaguzi mkuu ambao hadi sasa umebaki shwari kwa kiasi kikubwa katika visiwa hivyo, ambavyo vina historia ya mashindano ya kisiasa yenye mvutano.
Kiongozi wa upinzani Cameroon atashtakiwa kufuatia machafuko ya uchaguzi – serikali

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cameroon Paul Atanga Nji amesema kiongozi wa upinzani Issa Tchiroma Bakary atachukuliwa hatua za kisheria kwa madai ya kuchochea “maandamano yenye vurugu baada ya uchaguzi.”
Takriban waandamanaji wanne wameuawa wakati wa mapigano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani tangu uchaguzi wa Cameroon tarehe 12 Oktoba, huku Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 92 akishinda kwa muhula wa nane mfululizo.
Tchiroma Bakary anasisitiza kuwa alishinda uchaguzi huo, madai ambayo yametupiliwa mbali na chama tawala cha Biya, Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM).
Ukandamizaji mkali unaofanywa na maafisa wa usalama dhidi ya waandamanaji umeitia wasiwasi jumuiya ya kimataifa, huku Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya zikitoa wito wa kujizuia vurugu.
Siku ya Jumanne, Nji alimshutumu Tchiroma Bakary kwa kuandaa maandamano aliyosema ni “haramu” na kusababisha watu kupoteza maisha, na pia alimkosoa kwa kujitangazia ushindi katika uchaguzi huo.
Aliongeza kuwa “washirika wa Tchiroma Bakary wanaohusika na mpango wa uasi” pia watachukuliwa hatua za kisheria.
Paul Biya, aliyeingia madarakani mwaka 1982, sasa ndiye mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani, alishinda uchaguzi wa Oktoba 12 kwa 53.7% ya kura, ikilinganishwa na 35.2% ya Tchiroma Bakary, kulingana na Baraza la Katiba la Cameroon.
Tchiroma Bakary bado hajajibu uamuzi wa serikali wa kumshitaki, lakini hapo awali aliambia BBC, hatakubali kuibiwa kura na haogopi kukamatwa.
Katika siku ya matokeo ya uchaguzi, alisema watu wenye silaha waliwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wamekusanyika karibu na makazi yake huko Garoua, na kuwajeruhi vibaya takriban raia wawili.
Siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya ndani alifichua kuwa uchunguzi utaanzishwa kuhusu visa vya ghasia kabla na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Ingawa Nji alisisitiza kuwa hali sasa imedhibitiwa nchini kote, waandamanaji wanaendelea kufanya maandamano katika baadhi ya maeneo ya nchi, hasa huko Douala na Garoua, ambako waandamanaji waliweka vizuizi vya barabarani siku ya Jumanne, na kuchoma matairi barabarani.
Wachambuzi wanaonya kwamba ghasia za baada ya uchaguzi zinaweza kuitumbukiza nchi katika mzozo wa kisiasa.
Kimbunga Melissa kinaelekea Cuba baada ya kupiga Jamaica

Kimbunga Melissa kinaelekea Cuba baada ya kupiga Jamaica kikiwa ni kimbunga kikali zaidi kuwahi kulikumba taifa la Caribbean katika miaka ya hivi karibuni.
Kimbunga hicho kimejiimarisha zaidi hadi kufikia kiwango cha kimbunga cha aina ya nne (kinatembea kwa maili 130 -156 kwa saa), na kusababisha watu kuhama nchini Cuba.
Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel Bermúdez amechapisha taarifa kwenye X na kusema zaidi ya watu 735,000 kote nchini wamehamishwa kutokana na Melissa.
Vifo vitatu viliripotiwa Jamaica kwa sababu ya dhoruba hiyo na waziri wa serikali anasema ni mapema sana kujua kama kuna idadi zaidi ya waliofariki.
Akizungumza na BBC, Brian Bogart, ambaye anaongoza Ofisi ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani huko Barbados, amesema, kimbunga hicho kitaleta “janga kubwa” katika historia ya eneo hilo.
Mvua ya hadi inchi 30 (76cm) inatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Jamaica, huku maeneo yakikumbwa na mafuriko.
Mwanaume mmoja kutoka Jamaica ameiambia BBC “upepo ni mkali sana huwezi kusimama,” huku mwanamke akisema “maji yanapita kwenye paa langu – hali si nzuri.”
Shirika la ufuatiliaji wa intaneti la Netblocks limeripoti kushuka kwa ya intaneti kote Jamaica na kusema maelfu ya watu hawana umeme na mawasiliano ya simu kutokana na upepo mkali na miundombinu ya umeme kukatika.
Unyanyasaji wa kijinsia waathiri maisha na afya ya mke wa rais wa Ufaransa – bintiye

Binti wa Brigitte Macron, ambaye ni mke wa rais wa Ufaransa ameiambia mahakama jijini Paris, unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni umeathiri vibaya afya na hali ya maisha ya mamake.
Tiphaine Auzière, 41, ni binti wa kambo wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Aliyasema hayo katika siku ya pili na ya mwisho ya kesi dhidi ya watu 10 wanaotuhumiwa kueneza madai ambayo hayajathibitishwa kuhusu jinsia ya Brigitte Macron.
Bi Macron, 72, amekuwa akilengwa kwa muda mrefu na tuhuma zinazodai kuwa yeye ni mwanaume aliyebadili jinsia kuwa mwanamke.
Auzière amesema, aliona mabadiliko na “kuzorota” kwa afya ya mama yake tangu madai kuhusu jinsia kuanza kuzunguka.
“Imebidi awe mwangalifu kuhusu uchaguzi wake wa mavazi na mikao… Anajua vyema kwamba picha zake zitatumika kuunga mkono nadharia hizi,” amesema Bi Auzière.
Wakati mama yake “amejifunza kuishi na tuhuma hizo”, Bi Auzière anasema, kulikuwa na athari kwa wajukuu zake ambao walidhihakiwa shuleni.
“Hajachaguliwa kwenye nafasi ya uongozi, hajaomba chochote kwa mtu yeyote, na anashambuliwa.”
Waendesha mashitaka huenda wakatoa kifungo cha jela cha miezi mitatu hadi 12 kwa washtakiwa, na faini ya hadi dola za kimarekani 9,300.
Miongoni mwa washtakiwa – wote wenye umri wa miaka 41 hadi 65 – ni afisa wa serikali, mmiliki wa nyumba ya sanaa na mwalimu.
Mmoja – mwanaume anayeitwa Aurélien Poirson-Atlan – anatuhumiwa kuwaambia wafuasi wake 200,000 mtandaoni kwamba Bi Macron ni mwanaume aliyebadili jinsia na kwamba pengo la umri wa miaka 24 kati yake na Emmanuel Macron ni sawa na “fatari anayefadhiliwa na serikali.”
Washtakiwa wengine wawili – aliyejiita mwanahabari wa kujitegemea Natacha Rey na mtabiri wa mtandaoni Amandine Roy – tayari walipatikana na hatia ya kashfa mwaka jana. Baadaye waliachiliwa na mahakama ya rufaa.
Washtakiwa wengine pia walisema walikuwa wanatumia “uhuru wao wa kujieleza.” Mmoja aliomba Macrons kuchapisha picha za Brigitte Macron mjamzito ili kuthibitisha yeye ni mwanamke kibaolojia.
Wana ndoa hao wamesema watawasilisha ushahidi huo katika kesi mahakamani dhidi ya mtu mwenye ushawishi kutoka mrengo wa kulia nchini Marekani Candace Owens.
Owens amesisitiza mara kwa mara maoni yake kwamba Brigitte Macron ni mwanaume na Machi 2024.
Mapema mwaka huu wakili wa Macrons katika kesi hiyo, Tom Clare, aliambia BBC wanandoa hao watawasilisha ushahidi wa picha na kisayansi katika mahakama ya Marekani kuthibitisha Bi Macron ni mwanamke.
Bi Macron alikutana na mume wake wa sasa alipokuwa mwalimu katika shule ya upili.
Wenzi hao walioana mwaka 2007, wakati Bw Macron alipokuwa na umri wa miaka 29 na Bi Macron akiwa na miaka 54.
Watu 64 wameuawa katika operesheni dhidi ya genge la madawa ya kulevya Brazil

Takriban watu 64 wameuawa katika operesheni ya polisi dhidi ya genge la Red Command katika vitongoji vya kaskazini mwa Rio de Janeiro – ni uvamizi mkubwa na mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya jimbo hilo la Brazil.
Maafisa wanne wa polisi ni miongoni mwa waliouawa wakati wa Operesheni ya Containment katika wilaya za Alemão na Penha, amesema Gavana wa jimbo hilo Cláudio Castro. Zaidi ya watu 80 walikamatwa.
Mapigano makali yalizuka wakati maafisa wa usalama wapatao 2,500 walipovamia Jumanne asubuhi. Genge hilo lilijibu kwa kurusha risasi, kuchoma vizuizi na kurusha mabomu kutoka katika ndege zisizo na rubani.
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema, imeshtushwa na operesheni ya polisi, na kutaka “uchunguzi wa haraka ufanyike.”
Eneo la Favelas karibu na uwanja wa ndege wa Rio linachukuliwa kuwa makao makuu ya mojawapo ya makundi yenye nguvu ya uhalifu nchini Brazil.
Maafisa wa serikali wanasema takriban 50 kati ya waliouawa “wanashukiwa na polisi kuwa wahalifu.”
Makumi ya watu walijeruhiwa, wakiwemo raia walionaswa katika mapigano hayo katika eneo hilo la milima lenye watu wapatao 300,000.
Barabara bado zimefungwa katika eneo lote.
Kikundi cha The Red Command kimekuwa kikipanua eneo lao katika jimbo la Rio, na kuongeza njia za ulanguzi wa dawa za kulevya na udhibiti.
Polisi wa Rio walisema zaidi ya kilo 200 (lb 441) za dawa za kulevya zilinaswa katika uvamizi huo, pamoja na makumi ya bunduki.
Operesheni hiyo ya pamoja ya polisi na jeshi inajiri baada ya uchunguzi wa mwaka mzima.
Makumi ya washukiwa hao wanafikiriwa kuwa wanachama wa kikundi kutoka jimbo la Pará ambao kwa sasa wamejificha huko Rio de Janeiro.
Operesheni kubwa za polisi ni jambo la kawaida nchini Brazili kabla ya matukio makubwa ya kimataifa katika taifa hilo la Amerika Kusini.
Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa COP30 unafanyika katika mji wa kaskazini wa Belem mwezi Novemba.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.