‘Trump anataka kuipindua serikali’ – Afisa wa Venezuela

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na: Cantona Joseph|RFA

Tarek William Saab alisema siku ya Jumapili kwamba wito wa mabadiliko ya utawala nchini Venezuela ni mbinu ya kutaka kunyakua maliasili za nchi yake, ikiwa ni pamoja na akiba ya dhahabu, mafuta na shaba.

‘Trump anataka kuipindua serikali’ – Afisa wa Venezuela

DX

Rais wa Marekani Donald Trump anataka kuigeuza Venezuela kuwa “koloni” la Marekani, Mwanasheria Mkuu wa Venezuela ameiambia BBC.

Tarek William Saab alisema siku ya Jumapili kwamba wito wa mabadiliko ya utawala nchini Venezuela ni mbinu ya kutaka kunyakua maliasili za nchi yake, ikiwa ni pamoja na akiba ya dhahabu, mafuta na shaba.

Mshirika huyo wa karibu wa Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, Saab anasema “hakuna shaka” Marekani inajaribu kuipindua serikali ya Venezuela, akiongeza kuwa ni jaribio la hivi punde katika msururu mrefu wa majaribio kama hayo “yaliyofeli”.

Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo hayamtambui Maduro kama kiongozi halali wa Venezuela, baada ya uchaguzi uliopita wa 2024 kukosolewa na wengi kuwa haukuwa huru na wa haki.

Trump pia amerudia mara kwa mara uwezekano wa kile alichokiita “operesheni za ardhini” nchini Venezuela, na alisema wiki iliyopita kwamba Marekani “inaangalia uwezekano wa operesehani za ardhini” baada ya kupata udhibiti wa eneo la bahari.”

Takriban watu 43 wameuawa katika mashamulizi dhidi ya boti zinazodaiwa kuwa za dawa za kulevya katika pwani ya Amerika Kusini, baada ya utawala wa Trump kuanzisha mashambulizi mapema Septemba kama sehemu ya vita vinavyodaiwa kuwalenga walanguzi wa dawa za kulevya.

Wabunge wa Congress nchini Marekani kutoka pande zote mbili za vyama vya siasa, wameibua wasiwasi juu ya uhalali wa mashambulizi hayo na mamlaka ya rais kutoa amri yafanyike.

Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham aliwaambia waandishi wa habari Jumapili kwamba mashambulizi ya ardhini ni jambo linaloweza kutokea”, na Trump alimwambia kuwa anapanga kuwafahamisha wabunge wa Congress kuhusu operesheni za baadaye za kijeshi atakaporejea kutoka Asia.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuvamiwa kwa ardhi ya Venezuela, Saab ameiambia BBC “haipaswi kutokea, lakini tumejitayarisha.”

Aliongeza kuwa Venezuela “bado iko tayari kuanza tena mazungumzo” na Marekani, licha ya mashambulizi “haramu” dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Marekani imekuwa ikiendelea kujenga kikosi cha meli za kivita, ndege za kivita, wanajeshi wa majini, ndege za kijasusi, na ndege zisizo na rubani katika visiwa vya Caribbean, kama sehemu ya kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya na “magaidi wa mihadarati.”

Wanne wanne wameuawa katika maandamano Cameroon

d

Serikali ya Cameroninasema watu wanne wameuawa wakati wa maandamano ya Jumapili katika mji mkuu wa kiuchumi wa Douala, huku hofu ikiongezeka kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Katika taarifa, Gavana wa mkoa wa Littoral ambao ni kitovu cha uchumi, amesema waandamanaji walishambulia vituo vya polisi na polisi, kwa nia ya kuvichoma moto na vikosi vya usalama vilizuia majaribio haya.

“Katika mapambano hayo, kwa bahati mbaya watu wanne walipoteza maisha,” amesema Gavana Samuel Dieudonné Diboua.

Pia amelaani maandamano hayo ambayo akiyaeleza kuwa ni “vurugu zilizopangwa” ambazo ni shambulio kubwa kwa utulivu wa umma na usalama wa taifa.

Zikiwa zimesalia saa 24 tu kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, mamia ya waandamanaji na wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary walijitokeza mitaani kote nchini na nje ya nchi kukemea kile wanachosema ni udanganyifu wa uchaguzi.

Tchiroma anadai ushindi katika uchaguzi huo, licha ya onyo kutoka kwa serikali.

Misri na Msalaba Mwekundu zaungana kutafuta miili ya mateka Gaza

cdv
Maelezo ya picha,Matrekta ya Misri yanavuka kuingia Ukanda wa Gaza

Timu kutoka Misri na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) zimeruhusiwa kutafuta miili ya marehemu waliotekwa nyara wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, Israel imethibitisha.

Serikali ya Israel imesema timu hizo zimeruhusiwa kutafuta zaidi ya eneo la “mstari wa njano,” amablo linadhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) huko Gaza.

Wakati huo huo, siku ya Jumapili, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba wanachama wa Hamas pia wameruhusiwa kuingia katika eneo linalodhibitiwa na IDF la Gaza kusaidia msako huo, pamoja na timu za ICRC.

Hamas imekabidhi miili ya mateka 15 kati ya 28 wa Israel chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yanayosimamiwa na Marekani. Kundi hilo limesema sasa linashirikiana na mamlaka za Misri.

Donald Trump ameitaka Hamas kurejesha miili “haraka, au nchi nyingine zinazohusika katika mpango huu wa amani zitachukua hatua.”

Msemaji wa Israel alisema timu ya Misri imeruhusiwa kufanya kazi na ICRC kutafuta miili hiyo, na itatumia matreka ya kuchimba na magari makubwa kutafuta miili zaidi ya “mstari wa njano.”

Mstari wa ” njano” unaashiria mpaka wa kaskazini, kusini na mashariki mwa Gaza, eneo ambalo Israeli ilijiondoa, kama sehemu ya hatua ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Baada ya zaidi ya miaka miwili ya mashambulizi makali ya Israel, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa 84% ya eneo la Gaza ni kifusi.

Hamas inasema inajitahidi kadiri iwezavyo kupata miili ya mateka, lakini inakabiliwa na ugumu wa kuipata chini ya vifusi vya majengo yaliyolipuliwa na jeshi la Israel huko Gaza.

Wawili wakamatwa kwa wizi katika jumba la makumbusho Ufaransa

x
Maelezo ya picha,Maafisa wa polisi wa Ufaransa wanachunguza wizi katika Jumba la Makumbusho la Louvre, jijini Paris, Oktoba 19, 2025.

Washukiwa wawili wamekamatwa kwa wizi wa vito vya thamani katika jumba la makumbusho la Louvre jijini Paris, Ufaransa, vyombo vya habari vya nchi hiyo vinasema.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris imesema mmoja wa watu hao ametiwa mbaroni alipokuwa akijiandaa kupanda ndege katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle.

Vito vyenye thamani ya dola za kimarekani milioni 102, viliibiwa katika jumba la makumbusho linalotembelewa zaidi duniani Jumapili iliyopita, wakati wezi wanne waliokuwa na zana za kisasa walipovamia jengo hilo mchana kweupe.

Waziri wa sheria wa Ufaransa amekiri kuwa itifaki za usalama “zilishindwa,” na kuiacha nchi hiyo katika “picha mbaya.”

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris imesema, watu hao walikamatwa Jumamosi jioni, bila kutaja ni watu wangapi wametiwa mbaroni.

Mmoja wa washukiwa alikuwa akijiandaa kusafiri kuelekea Algeria, vyanzo kutoka polisi vimeviambia vyombo vya habari vya Ufaransa, huku ikifahamika kuwa mwengine alikuwa akienda Mali.

Polisi wanaweza kuwazuilia na kuwahoji kwa hadi saa 96.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa siku ya Jumapili, DNA iliyopatikana katika eneo la wizi ilipelekea kutambuliwa kwa mmoja wa washukiwa.

Genge hilo liliacha vitu kadhaa, ikiwa ni pamoja na glavu na koti.

Pia iliripotiwa hapo awali kwamba walidondosha taji ambalo lilikuwa la Empress Eugenie, mke wa Napoleon III.

Mwendesha mashtaka wa Paris alikosoa “kufichuliwa mapema” kwa habari zinazohusiana na kesi hiyo, akiongeza kuwa zinazuia juhudi za kurejeshwa kwa vito hivyo na kuwapata wezi.

Inasemekana wezi hao walifika saa 09:30 (08:30 GMT), muda mfupi baada ya jumba la makumbusho kufunguliwa.

Washukiwa walifika na ngazi ya umeme iliyokuwa kwenye gari na kuikunjua hadi kulifikia dirisha la roshani katika ghorofa ya kwanza ya Gallery ya Apollo.

Wawili kati ya wezi hao waliingia kwa kukata dirishani wakiwa na mashine za kisasa.

Kisha waliwatishia walinzi, ambao walitoka nje ya jengo hilo, na kukata vioo vya masanduku mawili yaliyohifadhi vito.

Ripoti ya awali imefichua kuwa chumba kimoja kati ya vitatu katika eneo la jumba la makumbusho lililovamiwa hakikuwa na kamera za CCTV, kulingana na vyombo vya habari vya Ufaransa.

Polisi wa Ufaransa wanasema wezi hao walikuwa ndani ya jumba kwa dakika nne na kutoroka kwa pikipiki mbili zilizokuwa zikingoja nje saa 09:38.

Wataalamu wameelezea wasiwasi wao kwamba vito hivyo tayari huenda vimevunjwa vunjwa na kuwa vipande vipande.

Dhahabu na fedha zinaweza kuyeyushwa na kukatwa na kuwa vijiwe vidogo ambapo haitawezekana kujua kuwa viliibiwa katika wizi huo, afisa wa upelelezi wa Uholanzi Arthur Brand aliambia BBC.

Hatua za usalama tangu wakati huo zimeimarishwa karibu na taasisi za kitamaduni za Ufaransa.

Kampuni ya Louvre imehamisha baadhi ya vito vyake vya thamani hadi Benki ya Ufaransa kufuatia wizi huo. Sasa vitahifadhiwa katika chumba salama zaidi cha Benki, mita 26 (85ft) chini ya ghorofa katika makao makuu ya benki katikati mwa Paris.

Marekani na China zakubaliana mfumo wa kibiashara kabla ya mkutano wa Trump na Xi

sd
Maelezo ya picha,Donald Trump na mwenzake wa China Xi Jinping wanatarajiwa kufanya mazungumzo nchini Korea Kusini.

Marekani na China zimekubaliana mfumo wa kibiashara ambao utajadiliwa wakati viongozi wao watakapokutana baadaye wiki hii, waziri wa fedha wa Marekani amesema.

Scott Bessent aliiambia CBS, mfumo huo wa makubaliano ni pamoja na “makubaliano ya mwisho” kuhusu shughuli za TikTok Marekani na kulegeza kamba China juu ya udhibiti wake wa rasilimali adimu.

Pia amesema hatarajii ushuru wa 100% kwa bidhaa za China kama Rais wa Marekani Donald Trump alivyotishia, wakati huo huo China itaanza tena ununuzi mkubwa wa soya kutoka Marekani.

China na Marekani zinajaribu kuepusha kuongeza vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

Trump na rais wa China Xi Jinping wanatarajiwa kufanya mazungumzo siku ya Alhamisi nchini Korea Kusini

Bessent alikutana na maafisa wakuu wa biashara wa China kando ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (Asean) nchini Malaysia, ambao Trump pia anahudhuria kama sehemu ya ziara yake Asia.

Beijing imesema kulikuwa na majadiliano mazuri.

Serikali ya China imesema katika taarifa kwamba timu zote mbili za mazungumzo “zilifikia makubaliano juu ya sintofahamu zao.

Maandamano ya vurugu yatokea Cameroon kabla matokeo ya uchaguzi

ds
Maelezo ya picha,Wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary wameandamana katika miji kadhaa nchini Cameroon

Mamia ya waandamanaji wamepambana na vikosi vya usalama katika miji kadhaa kote nchini Cameroon, saa chache kabla ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliokuwa na upinzani mkubwa kutangazwa.

Polisi waliwarushia vitoa machozi na maji ya kuwasha wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary katika ngome yake ya Garoua, mji ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.

Waandamanaji hao walikuwa wakilaani kile walichosema ni mpango wa chama tawala, Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM), “kuiba ushindi” kutoka kwa kiongozi wa upinzani.

Tchiroma Bakary amesisitiza kwamba ameshinda uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 12 Oktoba, akipinga Rais aliye madarakani Paul Biya kwa miaka 43 kuendelea kushikilia madaraka.

Chama cha CPDM kimetupilia mbali madai hayo.

Maandamano hayo yanakuja baada ya Tchiroma Bakary kutoa wito kwa wafuasi wake nchini humo na wale walio njea kuandamana kwa amani “kuikomboa Cameroon.”

Serikali imepiga marufuku mikusanyiko hadi Jumatatu, wakati baraza la katiba la Cameroon litakapopanga kutangaza matokeo.

Huko Garoua, maandamano yalianza kwa amani lakini yakageuka ghasia wakati vikosi vya usalama viliporusha vitoa machozi mitaani ili kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika kumuunga mkono Tchiroma Bakary.

Mwandamanaji mmoja alionekana akiwa amebeba bango la kumtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuwasaidia.

“Tuko hapa kudai ushindi wetu. Tunafanya maandamano ya amani, ambayo ni haki ya kiraia kwa Wacameruni wote – kwa kila mtu,” muandamanaji mwingine alisema.

Wafuasi pia waliingia mitaani katika mji wa kusini-magharibi wa Douala. “Tunamtaka Tchiroma, tunamtaka Tchiroma,” waandamanaji waliimba, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Tchiroma Bakary awali aliambia BBC kwamba hatakubali kuibiwa kura. Alisema timu yake imekusanya taarifa jumla kulingana na matokeo ya vituo vya kupigia kura.

Katika taarifa yake ya video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, Tchiroma Bakary alisema ameshinda uchaguzi huo kwa takriban asilimia 55 ya kura.

Waziri huyo wa zamani wa serikali mwenye umri wa miaka 76 aliachana na Biya mwenye umri wa miaka 92, ambaye anawania muhula mwingine baada ya miaka 43 madarakani.

CPDM imetupilia mbali madai ya ushindi wa Tchiroma Bakary na maafisa kadhaa wameelezea kuwa ni kinyume cha sheria kwa sababu ni baraza la katiba pekee ndilo linaloweza kutangaza matokeo rasmi.

Wafuasi wa upinzani wamedai kuwa uchaguzi wa Oktoba 12 ulikumbwa na dosari, ikiwa ni pamoja na kujazwa kura katika maboksi.

Majaji katika baraza la katiba wametupilia mbali kesi nane, wakisema hazina ushahidi wa kutosha au haina mamlaka ya kubatilisha matokeo.

Tchiroma Bakary alikataa kuwasilisha malalamiko katika baraza hilo, ambalo majaji wake wameteuliwa na Biya, na kuchagua badala yake kujitangaza kuwa “rais halali.”

Mzaliwa wa Garoua, Tchiroma Bakary alikuwa mwanafunzi wa uhandishi nchini Ufaransa kabla ya kurejea Cameron kufanya kazi katika kampuni ya kitaifa ya reli.

1984, alitupwa jela, akishutumiwa kuhusika katika jaribio la kumwondoa madarakani Rais Biya. Licha ya kukana shitaka hilo na hakuwahi kupatikana na hatia, Tchiroma Bakary alikaa jela miaka sita.

Pia aliwahi kuwa waziri wa mawasiliano kuanzia 2009 hadi 2019.

Akiwa msemaji wa serikali, aliitetea serikali ya Biya wakati wa machafuko kama vile uasi wa Boko Haram, na jeshi lilipotuhumiwa kuwaua raia.

Lakini mwezi Juni, miezi minne tu kabla ya uchaguzi mkuu, Tchiroma Bakary alibadilika, akajiuzulu kutoka serikalini na kutangaza kuwa atachuana na Biya kuwania urais.

Marekani kuacha kulipia chakula cha msaada kwa raia wake

l

Msaada wa chakula unaowanufaisha Wamarekani zaidi ya milioni 40 hautatolewa kuanzia Novemba kutokana na kusitishwa shughuli za serikali ya Marekani, kulingana na Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo.

Wizara hiyo imesema hakuna msaada, katika tovuti yake na kuwalaumu wawakilishi wa Democratic katika Seneti kwa mkwamo huo.

Mpango wa Usaidizi wa Lishe (Snap) humnufaisha Mmarekani mmoja kati ya wanane.

Mapema mwezi huu, utawala wa Trump ulikataa kutumia hazina ya dharura ambayo ingeendeleza kutoa msaada huo, ikisema pesa hizo zinahitajika kwa dharura zinazoweza kutokea kama vile majanga ya asili.

Democratic kimemlaani Rais Donald Trump kwa kukataa kutumia hazina ya dharura.

“Pengine hili ni kosa la kikatili na kinyume cha sheria ambalo utawala wa Trump unalifanya,” wabunge katika Congress, Rosa DeLauro na Angie Craig walisema katika taarifa ya pamoja siku ya Ijumaa.

Pia walimkosoa Trump kwa kutoa msaada kwa Argentina na kujenga ukumbi mpya wa White House wakati shughuli za serikali zimefungwa.

Kulingana na taasisi ya fikra tunduizi ya Budget and Policy Priorities (CBPP), hazina ya dharura ingegharamia takriban 60% ya gharama hizo kwa mwezi mmoja.

Snap hufanya kazi kwa kuwapa watu kadi za benki wanazoweza kuzitumia kununua bidhaa muhimu za nyumbani.

Familia ya watu wanne kwa wastani hupokea dola za kimarekani 715 (£540) kwa mwezi, kulingana na CBPP, ambapo ni sawa na dola 6 (£4.50) kwa siku kwa kila mtu.

Majimbo ndio yanasimamia programu hii, huku ufadhili mwingi ukitoka kwa serikali ya shirikisho.

Majimbo kadhaa yameahidi kutumia fedha zao wenyewe kufidia upungufu wowote, hata hivyo serikali ya shirikisho imeonya kuwa fidia hiyo haitarejeshwa.

Baadhi ya majimbo, ikiwa ni pamoja na Massachusetts – ambapo watu milioni moja wanatarajiwa kupoteza msaada huo – wamesema hawana pesa za kutosha kufidia ukosefu wa fedha.

Kufungwa kwa shughuli za serikali ya Marekani kumeingia siku yake ya 26 Jumapili, na kuufanya kuwa ndio ufungaji wa pili kwa ukubwa katika historia.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment