Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakubaliana kuisaidia Ukraine kifedha katika kipindi kingine cha miaka miwili.
Lakini hata hivyo wameshindwa kutoa mamilioni ya fedha za Urusi zilizozuiwa ili kutoa ufadhili wa ulinzi wa nchi hiyo
Katika mkutano wao wa jana viongozi hao waliahirisha uamuzi wao wa kutumia kiasi ya Euro bilioni 140 za mali ya Urusi zinazoshikiliwa nchini Ubelgiji hadi hapo Desemba.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameeleza mkutano huo wa Ubelgiji kwamba hatua hiyo italeta matokeo chanya. ” Ningependa kuwashukuru viongozi wote wa Ulaya kwa mosimamo yao thabiti kupitia vikwazo waliyoweka, alisema.
Mkutano huo wa Brussels ulifanyika jana wakati kukitarajiwa kufanyika mkutano mwingine huko London ambako Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer anatarajiwa kuwahimiza viongozi wa Ulaya kuongeza kupeleka vifaa vya kijeshi nchini Ukraine.
Marekani yazindua mpango wa msamaha kwa wapiganaji wa Gaza watakaoweka silaha chini

Serikali ya Marekani imezindua mpango mpya wa kuanzisha vituo vya ‘mapatano ya hiari’ katika Ukanda wa Gaza, utakaowapa wapiganaji wanaokubali kusalimisha silaha zao fursa ya msamaha na urejeo salama katika maisha ya kiraia.
Ili kufanikisha hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amewasili nchini Israeli siku ya Alhamisi kwa ajili ya kutekeleza mpango wa amani wa vipengele 20 wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Kuwasili kwa Rubio kunafuatia kuondoka kwa Makamu wa Rais J.D. Vance, huku maafisa waandamizi wa Ikulu ya White House pamoja na mkwe wa Rais Trump, Jared Kushner, wakihitimisha ziara zao nchini humo.
Wote wanashiriki katika jitihada za kudumisha usitishaji vita wa siku 13 kati ya Israeli na harakati ya Kipalestina ya Hamas, miaka miwili baada ya vita vilivyoitikisa Mashariki ya Kati.
Katika hatua nyingine, serikali ya Israeli imepitisha kwa kura ya awali mswada wa kutekeleza sheria za Israeli katika Ukingo wa Magharibi hatua ambayo wachambuzi wanaiona kama jaribio la kuinyakua ardhi inayotazamwa na Wapalestina kuwa sehemu ya taifa lao huru la baadaye.
Kabla ya kuondoka kuelekea Israeli, Rubio alionya dhidi ya hatua hiyo ya Knesset, akisema kuwa kupitishwa kwa mswada wowote wa aina hiyo kunaweza kuhatarisha usitishaji vita uliopo Gaza na kuleta matokeo yasiyo na tija kwa pande zote mbili.
Gazeti The Wall Street Journal liliripoti kwamba ongezeko la ziara za maafisa wa Marekani nchini Israeli linalenga kuhakikisha mwendelezo wa makubaliano ya kusitisha vita Gaza na kuzuia kuzuka kwa mivutano mipya ambayo inaweza kudhoofisha juhudi za kidiplomasia zinazoendelea.
Makamu wa Rais Vance alikamilisha ziara yake Alhamisi baada ya kufanya kikao cha ngazi ya juu na makamanda wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Israeli katika makao makuu ya Wizara ya Ulinzi mjini Tel Aviv, ambapo walijadili maendeleo ya uratibu wa shughuli za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Wakati wa mkutano wake na Makamu wa Rais wa Marekani mjini Yerusalemu siku ya Jumatano, Rais wa Israeli Isaac Herzog alisisitiza umuhimu wa kuimarisha matumaini miongoni mwa Waisraeli na Wapalestina, na kuhimiza juhudi za pamoja za kurejesha amani ya kudumu.
Kwa upande wake, Vance alisema kuwa Marekani na Israeli zinaendelea kushirikiana kuimarisha usitishaji vita Gaza na kufungua tena baadhi ya miundombinu muhimu.
Alionyesha matumaini kuwa mpango wa amani wa Rais Trump utaendelea licha ya changamoto zilizopo, na hatimaye kuchangia katika kuimarisha utulivu na amani katika eneo hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli, Gideon Sa’ar, naye alisisitiza dhamira ya serikali yake kuhakikisha mafanikio ya mpango huo wa Gaza, akitoa wito kwa Hamas na Harakati ya Jihad ya Kiislamu kuacha mapigano na kuweka silaha zao chini.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.