Trump ataka mechi za Kombe la Dunia zihamishwe Boston

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuondoa mechi za Kombe la Dunia za mwaka 2026 kutoka eneo la Boston, akidai kuna wasiwasi wa kiusalama na kumshutumu Meya Michelle Wu kwa kushindwa kudhibiti hali ya mji huo.

Trump akiwa na kofia yake inayodai kuwa alikuwa sahihi kuhusu kila kitu.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Na:Cantona Joseph|RFA

Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaweza kuondoa mechi za Kombe la Dunia za mwaka 2026 zilizopangwa kufanyika katika eneo la Boston, akitaja sababu za usalama na kumlaumu meya wa mji huo, Michelle Wu, kwa “uongozi mbaya.”

Akizungumza Jumanne katika Ikulu ya White House, Trump alisema: “Tunaweza kuondoa mechi hizo. Ninawapenda watu wa Boston, lakini meya wao hana uwezo. Ni mwerevu, lakini ana mawazo ya mrengo wa kushoto kupita kiasi.”

Boston imepangiwa kuwa mwenyeji wa mechi saba katika Uwanja wa Gillette, ulioko Foxborough, takriban kilomita 50 kutoka katikati ya jiji, ikiwa ni sehemu ya mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yatakayoshirikisha Marekani, Mexico na Kanada.

Trump aliongeza kuwa anaweza kuzungumza moja kwa moja na Rais wa FIFA Gianni Infantino ili kuhamisha mechi hizo ikiwa ataona hali ya usalama haijaridhisha. “Gianni hatapenda kufanya hivyo, lakini anaweza kukubali kirahisi,” alisema.

Donald Trump na Gianni Infantino watangaza droo ya Kombe la Dunia 2026 – 22.08.2025 Picha: CNP/ADM/Capital Pictures/picture alliance

FIFA yawataka viongozi kuheshimu mamlaka yake juu ya michuano hiyo

Hata hivyo, FIFA imesisitiza kuwa maamuzi ya mwisho kuhusu viwanja vya michuano hiyo yako chini ya mamlaka yake pekee. Makamu wa Rais wa FIFA, Victor Montagliani, alisema: “Ni mashindano ya FIFA, na maamuzi yote ya maeneo ya kufanyia mechi ni ya FIFA.”

Kauli za Trump zimekuja siku chache baada ya tukio la vurugu mjini Boston lililosababisha kukamatwa kwa watu kadhaa. Ofisi ya Meya Wu haijatoa maoni rasmi kuhusu tishio hilo la Rais.

Waandaaji wa mashindano hayo wanasema Boston itafaidika kiuchumi kutokana na wageni na mapato ya utalii, na kwamba tiketi kwa mechi zote tayari zimeuzwa.

Kwa mujibu wa ratiba ya FIFA, mechi ya kwanza katika eneo la Boston inatarajiwa kufanyika Juni 13, 2026, ikiihusisha moja ya timu kutoka Kundi C la mashindano hayo.

Chanzo: APE

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment