Trump asifu “siku kubwa kwa Mashariki ya Kati”

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Donald Trump na viongozi wa Mashariki ya Kati wametia saini tamko la Gaza nchini Misri, hatua iliyopelekea kubadilishana kwa mateka na wafungwa kati ya Israel na Hamas, na kuzua matumaini mapya ya utulivu wa eneo hilo.

Trump ametangaza ‘Vita vya Gaza vimeisha’ baada ya kusaini Tamko la Gaza.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Na:Cantona Joseph|RFA

Rais wa Marekani Donald Trump ameongoza kusainiwa kwa tamko jipya la amani linalolenga kudumisha usalama na utulivu katika Ukanda wa Gaza, akilita “siku kubwa kwa dunia na Mashariki ya Kati.” Makubaliano hayo yalisainiwa mjini Sharm el-Sheikh, Misri, yakihusisha viongozi wa Misri, Qatar na Uturuki kama wadhamini wa mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas. Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya pande hizo mbili kubadilishana mateka na wafungwa, hatua iliyopokelewa kwa shangwe katika Tel Aviv, Ramallah na Gaza.

Trump alifanya ziara ya ghafla nchini Israel, ambapo alilihutubia bunge la nchi hiyo na kumpongeza Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa “uongozi wa ujasiri” kabla ya kuelekea Misri kwa mkutano wa kilele wa Gaza. Akizungumza mbele ya zaidi ya viongozi 20 wa dunia, Trump alisema, “Tumefanikisha kile ambacho kila mtu alisema hakiwezekani. Hatimaye, tunayo amani katika Mashariki ya Kati.”

Rais Trump awasili Israel kulihutubia bunge la Knesset

Ahadi ya viongozi kwa Gaza

Kulingana na tamko lililotolewa na Ikulu ya White House, nchi washiriki zimeahidi “kuendeleza dira jumuishi ya amani, usalama na ustawi wa pamoja katika eneo la Mashariki ya Kati.” Hata hivyo, waraka huo haukuweka wazi mustakabali wa suluhisho la taifa moja au mawili, jambo lililozua maswali kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa mpango huo. Trump aliwaambia waandishi wa habari, “Tunazungumza kuhusu kujenga upya Gaza — siyo kuhusu taifa moja au mawili.”

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi alisema makubaliano hayo “yanafunga sura yenye maumivu katika historia ya mwanadamu” na kuweka msingi wa suluhisho la mataifa mawili. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Hamas imewaachia huru mateka 20 wa mwisho waliokuwa wamezuiliwa Gaza kwa zaidi ya miaka miwili, huku Israel ikiwaachia wafungwa 1,968 wa Kipalestina. Wakati familia za Waisraeli zilisherehekea kwa machozi ya furaha, maelfu ya Wapalestina walijitokeza Ramallah na Khan Yunis wakipokea wapendwa wao kwa nyimbo na vilio vya shukrani.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment