Ulaya yaanza kujitayarisha kwa vita vikubwa vinavyoweza kutokea

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na:Cantona Joseph|RFA

NATO inadai kuwa Urusi inaendesha vita vya mseto dhidi ya muungano huo na inajiandaa kwa vita halisi.

Kuongezeka kwa idadi ya matukio yaliyoripotiwa na kuthibitishwa yanayohusisha ukiukaji wa anga ya NATO imesababisha ongezeko la haraka la mivutano barani Ulaya na wasiwasi kuhusu nia ya muda mrefu ya Urusi.

Wataalamu wa Magharibi wanaona kuwa uchumi wa Urusi kwa ujumla unazidi kuhamasishwa kwa mahitaji ya vita, na hii inachangia ukuaji wa jumla wa uwezo wa kijeshi wa Urusi.

Hatahivyo, hakuna dalili dhahiri za kujiandaa kwa uvamizi, kama vile harakati za askari. Kwa hiyo, makadirio mengi yanaonesha muda wa miaka kadhaa, wakati ambapo Urusi inaweza kujiandaa na kuanzisha vita kamili katika Ulaya Magharibi.

Netanyahu afanya mkutano wa usalama leo, huku kukiwa na ripoti zinazokinzana kuhusu msimamo wa Hamas huko Gaza

Wapalestina wakiwa kwenye foleni ili kupata mlo katika jiko la kutoa misaada katika eneo la Mawasi la Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kufanya mkutano maalum siku ya Ijumaa na maafisa wakuu wa usalama.

Channel 14 ya Israel imeripoti kuwa, ajenda ya Netanyahu inajumuisha mada kuu mbili: kutathmini hali ya Gaza, ikizingatiwa nia ya Hamas iliyoripotiwa kukataa mpango wa Marekani, na kuongezeka mashambulizi Ukingo wa Magharibi, ambayo inaweza kusababisha operesheni kubwa sawa na mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi wa BBC Gaza aliripoti kwamba wapatanishi waliwasiliana na mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas huko Gaza, Izz al-Din al-Haddad, ambaye alionesha kutokubaliana kwake na mpango huo mpya wa Marekani wa kusitisha mapigano.

Izz al-Din al-Haddad anaamini mpango huo “unalenga kuiondoa Hamas, iwe vuguvugu hilo linakubali au la,” na ndio maana amedhamiria kuendelea kupigana.

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Mohammed Nazzal aliiambia idhaa ya Al Jazeera ya Qatar Alhamisi jioni kwamba vuguvugu hilo lilipokea mpango wa Trump Jumatatu iliyopita na kuanza mashauriano ya “ndani na nje” kuhusu hilo.

Nazzal aliongeza kuwa vuguvugu hilo lina “angalizo” juu ya mpango huo na litatangaza msimamo wake hivi karibuni, akieleza kuwa vuguvugu hilo liliamua kujadili mpango wa Marekani kwa kuzingatia kanuni ya “kusimamisha vita na mauaji,” kama alivyoweka.

Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas alieleza kuwa vuguvugu hilo litatangaza msimamo wake kuhusu mpango huo hivi karibuni, na “haitachukua muda mrefu.”

Ni nini kilicho nyuma ya visa vya ndege zisizo na rubani kwenye viwanja vya ndege?

Uwanja wa ndege wa Munich

Uwanja wa ndege wa Munich nchini Ujerumani umefunguliwa tena baada ya kuonekana kwa ndege zisizo na rubani kulazimisha kufungwa na kuahirishwa kwa safari zaidi ya kumi na mbili Alhamisi usiku.

Ni hatua ya hivi punde zaidi katika mfululizo wa uvamizi wa hivi karibuni wa ndege zisizo na rubani kote Ulaya.

Haijulikani ni nani aliye nyuma ya matukio haya, lakini Dk Ulrike Franke kutoka Baraza la Umoja wa Ulaya kuhusu Mambo ya Kigeni aliambia kipindi cha Leo cha BBC Radio 4 asubuhi ya leo kwamba tukio la Munich linaweza kusababishwa na “nchi yenye uwezo”.

“Tumekuwa na visa vya ndege kubwa zaidi katika siku na wiki za hivi karibuni na katika visa vingine ndege kubwa zisizo na rubani zenye uwezo wa kurusha droni ndogo, zikiruka karibu na miundombinu muhimu,” alisema.

“Haya ni matukio ambapo tunaweza kuwa na uhakika kwamba hawa si wanagenzi… uwezekano mkubwa ni nchi, kuna uwezekano mkubwa kuwa Urusi.

“Katika kesi ya Munich kwa wakati huu hatuna taarifa za kutosha kuhusu aina ya ndege zisizo na rubani, na jinsi zilivyorushwa, ili kutupa taarifa ni nani alikuwa akiziendesha.” Franke alivitaka viwanja vya ndege kujitayarisha na teknolojia ya kupambana na ndege zisizo na rubani ili kukabiliana na ongezeko la uvamizi wa anga.

Alisema kuwa hadi sasa, maafisa “hawajaona hitaji la kiuchumi” la kuwekeza katika teknolojia.

”Vijana msihadaiwe na wahuni wa kutoka nje kuiharibu nchi’’ -Rais Madagascar

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina
Maelezo ya picha,Rais wa Madagascar Andry Rajoelina

Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, amelaani kile alichokiita jaribio la mapinduzi lililohusishwa na maandamano yanayoendelea nchini humo.

Katika hotuba kwa taifa aliyoitoa kupitia ukurasa wake wa Facebook mapema leo, Rajoelina alisema kuwa maandamano hayo yanayoongozwa na vijana wa kizazi kipya cha Gen Z yamechochewa na watu wenye nia ya kuiangusha serikali kwa nguvu.

Hotuba hiyo pia ilirushwa na televisheni ya taifa, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa ndani.

“Wamechochewa kutekeleza mapinduzi. Ninachotaka kuwaambia ni kwamba kuna watu wanataka kuiharibu nchi,” alisema Rajoelina, kama alivyonukuliwa na shirika la habari la AFP.

Rais alieleza kuwa kulikuwapo na mpango wa kumng’oa madarakani kwa nguvu, ambapo alikumbwa na vitisho vya maisha.

Hata hivyo, amewahakikishia wananchi kuwa yuko salama na serikali iko imara.

Akizungumza akiwa ofisini mwake Rais Rajoelina ameonya kuwa machafuko yanapoendelea, kuna hatari ya kusitishwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Miradi muhimu ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara kuu za kitaifa namba 10 na 13, ipo hatarini kusimama.

Katika hotuba yake pia, Rais amesisitiza kuwa baadhi ya mataifa ya kigeni na mashirika ya kimataifa yanahusika katika njama za kupenya kwenye siasa za ndani kwa lengo la kunufaika na rasilimali za madini za Madagascar.

Akigusia maadamano ambayo yanaendelea kuchacha Rais wa Madagascar ametoa tahadhari kuhusu uwepo wa makundi ya wanamgambo wenye silaha waliopenya kwenye maandamano kwa lengo la kuchochea vurugu na machafuko.

Wakati huo huo, amewasihi vijana na wasanii kutambua adui wa kweli na kutoacha kupoteza dira au malengo yao halisi ya kujenga taifa.

Mnamo Jumatatu, Rajoelina alivunja serikali yake kwa lengo la kupunguza hasira za wananchi, lakini hatua hiyo haikutosha kutuliza hali ya sintofahamu.

Leo hii, polisi wa kutuliza ghasia walifunga sehemu kubwa ya katikati ya jiji la Antananarivo kwa hofu ya maandamano mapya.

Asubuhi ya leo, mamia ya waandamanaji walijaribu kuingia katikati ya jiji lakini polisi waliwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.

Maandamano hayo, yaliyoanza wiki iliyopita siku ya Alhamisi katika mji mkuu, sasa yameenea hadi miji mingine mikuu nchini.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment