Israel yazuia msafara wa meli ya misaada kuelekea Gaza

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Msafara wa boti Global Sumud Flotilla unaolenga kufikisha misaada kwa Wapalestina katika ukanda wa Gaza

Jeshi la Israel limezuia msafara wa meli uliokuwa umebeba misaada kuelekea ukanda wa Gaza na kuwakamata wanaharakati waliokuwemo ndani ya msafara huo, akiwemo mwanaharakati wa mazingira kutoka Sweden, Greta Thunberg.

Msafara huo, ujulikanao kama Global Sumud Flotilla (GSF), ulikuwa na takriban meli 45 zilizobeba wanasiasa na wanaharakati, na uliondoka Uhispania mwezi uliopita kwa lengo la kuvunja mzingiro wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza – eneo ambalo Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba linakabiliwa na njaa kali.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imethibitisha kuwa meli kadhaa za GSF zimezuiwa na abiria wake kuhamishwa hadi bandari ya Israel. Serikali ya Tel Aviv ambayo imelitaja jaribio la GSF la kusafirisha misaada kwenda Gaza kuwa ni “uchokozi” imesema “Greta Thunberg na marafiki zake wako salama na wenye afya.”

Wizara hiyo ya mambo ya nje imeongeza kuwa meli hizo ziliagizwa kubadili mwelekeo kwa kuwa zilikuwa zinakaribia “eneo la mapigano.”

Kwa upande wake, GSF imeeleza kuwa hatua ya kuzuiwa kwao ni kinyume cha sheria za kimataifa, na wala sio kitendo cha kujilinda kama inavyodai Israel, bali ni “kitendo cha kukata tamaa kwa dhahiri.”

Kupitia mitandao ya kijamii, msafara huo umeandika: “Hali hii inaonyesha wazi jinsi gani Israel inavyokwenda mbali kuhakikisha Gaza inaendelea kuwa na njaa na kutengwa.”

GSF imetaja meli kadhaa zilizokamatwa, ikiwemo Alma—moja ya meli kuu—pamoja na Surius na Adara. Kabla ya kukamatwa, msafara huo ulidai kuwa jeshi la Israel liliharibu kwa makusudi mawasiliano ya meli ili kuzuia ishara za dharura na kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya ukamataji huo.

Rima Hassan, mbunge wa Bunge la Ulaya mwenye uraia wa Ufaransa na Palestina, ambaye alikuwa sehemu ya msafara huo, ameandika kupitia ukurasa wake wa kijamii wa X kwamba Mamia ya watu wamekamatwa kinyume cha sheria na kuzuiliwa kiholela na Israel.”

Kundi la Hamas ambalo shambulio lake la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel lilichochea vita vya Gaza, limelaani hatua ya kuzuiwa kwa msafara huo katika maji ya kimataifa, na kuitaja hatua hiyo kama uhalifu wa uharamia na ugaidi wa majini.”

Uhispania na Italia, ambazo zilituma meli za kivita kama ulinzi wa raia wao, zilihimiza msafara huo kusimama kabla ya kuingia katika eneo la mzingiro, na kutangaza kuwa meli zao hazitavuka kile walichokiita mstari mwekundu.”

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, amesema wanaharakati hao “hawawakilishi hatari au tishio kwa Israel,” na kutumai kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, “hatawakilisha tishio kwa msafara huo pia.”

Maandamano Italia kufuatia kuzuiwa kwa msafara wa meli ya misaada

Wakati huo huo, maandamano makubwa yamezuka nchini Italia kufuatia hatua ya Israel kuzuia msafara wa meli uliokuwa umebeba misaada kuelekea ukanda wa Gaza.

Mjini Rome, maelfu ya waandamanaji walikusanyika jana jioni nje ya kituo kikuu cha reli mjini humo. Mamlaka zililazimika kufunga kwa muda mlango wa kituo hicho pamoja na kufunga kituo cha karibu cha treni za chini kwa chini kama tahadhari.

Kwa mujibu wa gazeti la La Repubblica, kundi la waandamanaji lilielekea katika ofisi ya Waziri Mkuu Giorgia Meloni, na kuishtumu serikali yake ya mrengo wa kulia kwa kushindwa kuonyesha mshikamano na wanaharakati waliokuwemo ndani ya msafara huo wa meli.

Shirika la Habari la ANSA limeripoti kuwa katika mji wa kusini wa Napoli, waandamanaji waliziba njia za reli katika kituo kikuu cha treni na kulazimisha huduma za usafiri wa treni kusitishwa kwa muda.

Maandamano mengine pia yameripotiwa katika miji ya kaskazini ya Milan na Turin na kuonyesha kuenea kwa hasira ya umma dhidi ya Israel.

Chama kikubwa zaidi cha wafanyikazi nchini Italia, CGIL, kimetangaza mgomo wa kitaifa mnamo siku ya Ijumaa, kama ishara ya kuunga mkono maandamano hayo na kulaani kile kinachoonekana kama ukosefu wa mshikamano na wanaharakati waliokuwemo ndani ya msafara huo wa meli.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment