Hofu na matumaini kuhusu mustakabali wa AGOA barani Afrika

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Kupitia Mpango wa AGOA, Kenya imeweza kuuza bidhaa zake nchini Marekani bila kutozwa ushuru, ikiwemo maua.

Waajiriwa na viwanda barani Afrika wanakabiliana na waswasi wa kupoteza faida za miongo miwili ya upendeleo wa kibiashara na Marekani kupitia mpango wa fursa za kibiasahra wa AGOA ambao muda wake unamalizika hii leo.

Waajiriwa na wamiliki wa viwanda barani Afrika wanakabiliana na wasiwasi wa kupoteza faida za miongo miwili ya upendeleo wa kibiashara na Marekani kupitia mpango wa fursa za kibiashara wa AGOA, ambao muda wake unamalizika leo Jumanne. Hata hivyo, kuna mwanga wa matumaini baada ya utawala wa Rais Donald Trump kuashiria kuunga mkono kurefushwa kwa mpango huo kwa mwaka mmoja zaidi.

Serikali za Afrika na wawekezaji wameendelea kushinikiza kurefushwa kwa mpango wa AGOA, ambao kwa miaka 25 umekuwa nguzo ya biashara kati ya Marekani na zaidi ya nchi 30 za Afrika. Licha ya jitihada za kupata muda mrefu zaidi kushindikana bungeni Marekani, matumaini mapya yameibuka kutokana na ishara kwamba utawala wa Trump unaweza kuunga mkono kurefushwa kwa muda mfupi.

Mpango wa AGOA, uliopitishwa mwaka 2000, umetoa fursa kwa maelfu ya bidhaa kutoka Afrika kuingia Marekani bila ushuru. Pia umesaidia mamia ya maelfu ya ajira katika sekta za magari, nguo, kilimo na mafuta. Lakini ushuru ulioanzishwa na Rais Trump mwezi Agosti, wa kati ya asilimia 10 na 30, umevuruga biashara na kuzua mashaka juu ya mustakabali wa mpango huu.

Nchini Kenya, sekta ya nguo na mavazi imekuwa miongoni mwa wanufaika wakuu, ikiuza jeans za Wrangler na Levi’s kwa Marekani. Hata hivyo, wiki hii kiwanda kikubwa mjini Nairobi kilitangaza mipango ya kuwafuta mamia ya wafanyakazi kutokana na hali ya kutojulikana mustakabali wa AGOA.

Pankaj Bedi, Mkurugenzi wa United Aryan na mwakilishi wa Shirikisho la wazalishaji bidhaa la Kenya, amesema tayari atapunguza wafanyakazi 1,000 kati ya 10,000, jambo litakalohatarisha maisha ya maelfu ya familia. Amesema viongozi wa Afrika walipewa ishara zisizo rasmi kutoka New York kwamba AGOA itapitiwa upya, lakini uhakika bado ni mdogo.

Mashaka na shinikizo kwa Marekani

Kwa wabunge wa Kenya, hali hii ni tishio kubwa. Akizungumza bungeni, Mbunge wa Tharaka, George Murugara, alisisitiza madhara ya kusitishwa kwa mpango huo.

“Tunajua kuna bidhaa nyingi sana tunazozalisha hapa ambazo zina thamani kubwa kwa watu wa Marekani. Watu wanaofanya kazi katika viwanda na sekta ya kilimo wataathirika. Tuna zaidi ya watu 66,000 wanaofanya kazi hapa na zaidi ya asilimia 75 yao ni wanawake. Mapato yao yanatumika kwa mambo muhimu kama elimu, afya na kupunguza umasikini.”

Lesotho imekumbwa zaidi na ushuru wa juu, ikitozwa asilimia 50 mapema mwaka huu, huku Kenya ikipata kiwango cha chini zaidi cha asilimia 10. Mataifa haya madogo yanategemea kwa kiasi kikubwa AGOA kwa mauzo yake ya nje na ajira kwa maelfu ya wananchi wake.

Wadadisi wanasema kumalizika kwa AGOA kutamaanisha sio tu kupotea kwa soko bali pia kudhoofisha uwekezaji wa kigeni, minyororo ya usambazaji na mapambano dhidi ya umaskini. Wafanyakazi zaidi ya milioni 1.3 barani Afrika, wengi wao wanawake, wamo hatarini ikiwa mpango huu hautarefushwa.

Hali hii imesababisha shinikizo kubwa kwa Marekani, ambapo siasa za ndani zimepunguza umakini kwa mikataba ya kibiashara ya Afrika. Warepublican na Wademocrat bado wanalumbana kuhusu mswada wa matumizi ya dharura, ambao huenda ndiyo njia pekee ya kisheria ya kufanikisha kurefushwa kwa AGOA.

Hofu ya ajira na matumaini ya muafaka

Kwa sasa, viwanda barani Afrika viko katika hali ya taharuki. Wamiliki wa viwanda wanasema wataanza kupunguza wafanyakazi ikiwa mpango wa AGOA hautaendelea, hatua ambayo itazidisha changamoto za ajira na umasikini.

Wafanyakazi katika sekta ya mavazi nchini Kenya, wengi wao wanawake, wanasema maisha yao yanategemea moja kwa moja kazi zinazolindwa na mpango huo. “Kazi hii ndiyo riziki yangu,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda cha Nairobi, “ikipotea, basi maisha yangu pia yamepotea.”

Serikali za Afrika zimekuwa zikijaribu pia kusaka njia mbadala kupitia mikataba ya kibiashara ya pande mbili na Marekani, lakini mchakato huo umekuwa mrefu na mgumu. Rais William Ruto wa Kenya alisema wiki iliyopita kuwa mazungumzo ya makubaliano ya pande mbili yamepiga hatua na huenda yakakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa mikataba ya pande mbili haiwezi kuchukua nafasi ya AGOA kwa kiwango sawa, kwani mpango huo umekuwa jukwaa pana linalounganisha uchumi wa Afrika na soko kubwa zaidi duniani.

Kwa sasa, mustakabali wa mpango huu uko njia panda, ukiakisi mchanganyiko wa hofu na matumaini kwa bara la Afrika, huku macho yote yakielekezwa Washington kwa uamuzi wa mwisho.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment